Kuomba Talaka Bila Sababu

 

SWALI:

Subject: Je inajuzu mke kumuomba mumewe talaka bila sababu za kisheria?


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani kwa swali lako hilo ambalo lina pande kadhaa kama tunavyoliona sisi japokuwa hapa limefanyiwa muhtasari. Kwanza, haifai kwa mwanamke kumuomba mumewe talaka bila sababu yoyote ya kisheria. Hii ni kwa kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Llaahu 'alayhi wa sallam) amesema:   "Mwanamke yeyote mwenye kumuomba mumewe talaka pasi na kosa lolote basi Pepo itakuwa haramu kwake wala hatasikia harufu yake" (al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah).

Pili, lau mume atakuwa anamfanyia vitimbi na makuruhi au hampendi lakini anamuweka chini yake ili mke aombe talaka na ilhali yeye ndiye mkosa kwa sababu apate kurudishiwa mahari yake. Hili ni kosa kwa upande wa mume. Katika hali hiyo mke anatakiwa aende kwa Qadhi au msimamizi wa mambo ya Kiislamu (hasa mwanachuoni) ili amuelezee yanayojiri. Hapo Qadhi atachukua jukumu la kumuachisha na mume hatalipwa chochote kwa sababu yeye ndiye mkosa. Kwa hali hii inakuwa ni haramu kwa mume kuchukua chochote wala Khul'u haiswihi hapa kwa kauli ya Aliyetukuka: "Wala msiwazuie (kuolewa na waume wengine kwa kuwa hamuwataki wala hamtaki kuwaacha ila kwa pesa) ili mpate kuwanyang'anya baadhi ya vile mlivyowapa" (4: 19).

 Tatu, mke anamchukia mumewe, hivyo anaitoa nafsi yake kutoka kwake kama mtumwa. Katika hali hiyo mke anamlipa mume mahari yake ili ajitoe katika ndoa. Hii inaitwa Khul'u. Hali hii inajuzu katika sheria kwa dalili zifuatazo:

1- Allaah Aliyetukuka Amesema: "Basi mkiogopa kwamba hamtaweza kusimamisha mipaka ya Allaah, hapo itakuwa hapana dhambi kwao (mme na mke) katika kupokea au kutoa ajikomboleacho mwanamke" (2: 229).

2- Katika Hadiyth Sahihi ni kuwa mke wa Thaabit bin Qays alisema: "Ewe Mtume wa Allaah! Simtolei aibu mume wangu katika maadili yake wala Dini, lakini naogopa ukafiri katika Uislamu (yaani kukanusha kuishi pamoja kwa wema na kutotekeleza wajibu kwa sababu ya chuki kali)". Akasema Mtume wa Allaah (Swalla Llaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Utamrudishia bustani yake?" Akasema: "Ndio". Akasema Mtume wa Allaah (Swalla Llaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Kubali bustani na umtaliki talaka moja" (al-Bukhaariy).

Ndoa ni mapenzi na mahaba baina ya wanandoa ikiwa mahaba kama hayo hayapo basi inaweza kumfanya mmoja kuingia katika madhambi kwa kutoweza kutimiza wajibu wake kwa mwenziwe.

3- Ni Ijmai ya wanazuoni wote kuwa talaka aina hii inasihi na inapita.

Twatumai kwa hayo utakuwa umeelewa vilivyo.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share