09-Sifa Kumi Na Fadhila Zake: Wanaume Na Wanawake Wanojihifadhi Tupu Zao

 

Sifa Kumi Na Fadhila Zake

 

09-Wanaume Na Wanawake Wanojihifadhi Tupu Zao

 

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

إِنَّ الْمُسْلِمِينَ وَالْمُسْلِمَاتِ وَالْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ وَالْقَانِتِينَ وَالْقَانِتَاتِ وَالصَّادِقِينَ وَالصَّادِقَاتِ وَالصَّابِرِينَ وَالصَّابِرَاتِ وَالْخَاشِعِينَ وَالْخَاشِعَاتِ وَالْمُتَصَدِّقِينَ وَالْمُتَصَدِّقَاتِ وَالصَّائِمِينَ وَالصَّائِمَاتِ وَالْحَافِظِينَ فُرُوجَهُمْ وَالْحَافِظَاتِ

Hakika Waislamu wanaume na wanawake, na Waumini wanaume na wanawake, na watiifu wanaume na wanawake, na wasemao kweli wanaume na wanawake, na wanaosubiri wanaume na wanawake, na wanyenyekevu wanaume na wanawake, na watoao swadaqah wanaume na wanawake, na wafungao Swawm wanaume na wanawake, wanaojihifadhi tupu zao wanaume na wanawake, [Al-Ahzaab: 35]

 

 

Kuhifadhi tupu kujiepusha na yote Aliyoyaharamisha Allaah ('Azza wa Jalla) kama zinaa, liwaat (wanaume kwa wanaume) na pia wafanyao uchafu baina ya wanawake kwa wanawake.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ametahadharisha kutokukaribia zinaa Anaposema:

 

وَلَا تَقْرَبُوا الزِّنَىٰ ۖ إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاءَ سَبِيلًا ﴿٣٢﴾

Na wala msiikaribie zinaa. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya kabisa. [Al-Israa: 32]

 

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametahadharisha pia katika Hadiyth kadhaa zikiwemo:

 

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((لاَ يَنْظُرُ الرَّجُلُ إِلَى عَوْرَةِ الرَّجُلِ، وَلاَ الْمَرْأَةُ إِلَى عَوْرَةِ الْمَرْأَةِ، ولاَ يُفْضِي الرَّجُلُ إِلَى الرَّجُلِ فِي ثَوْبٍ وَاحِدٍ، وَلاَ تُفْضِي الْمَرْأَةُ إِلَى الْمَرْأَةِ فِي الثَّوْبِ الْوَاحِدِ)) مسلم

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Sa’iyd (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Mwanamme asitazame uchi wa mwanamme, wala mwanamke asitazame uchi wa mwanamke, wala mwanamme asilale na mwanamme mwenzie katika nguo moja, wala mwanamke asilale na mwanamke mwenzie katika nguo moja)). [Muslim]

 

 

Na pia:

 

 

عَنْ عُقْبَةَ بْنِ عَامِرٍ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((إِيَّاكُمْ وَالدُّخُولَ عَلَى النِّسَاءِ)) فَقَالَ رَجُلٌ مِنْ الأَنْصَارِ: يَا رَسُولَ اللَّهِ أَفَرَأَيْتَ الْحَمْوَ؟ قَالَ:  ((الْحَمْوُ الْمَوْتُ))  متفق عليه

Imepokelewa kutoka kwa ‘Uqbah bin ‘Aamir (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Tahadharini na kuingia kwa wanawake!)) Mtu mmoja katika Answaariy akauliza: “Ee Rasuli wa Allaah! Nieleze akiwa ni shemeji?” Akamwambia:  ((Shemeji ni mauti!)). [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Na pia:

 

 

Kutoka kwa 'Umar  (رضي الله عنه)  kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Hachanganyiki mwanamume na mwanamke ila shaytwaan huwa ni watatu wao)). [At-Tirmidhiy]

 

Na pia:

 

Hadiyth  kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه)   kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Allaah Ameandika kila sehemu ya zinaa ambayo humuingiza mtu katika shauku. Hakutokuwa na kuikwepa. Zinaa ya macho ni kutazama, ya masikio ni kusikiliza, ulimi ni kunena maneno, mkono ni kuunyoosha, mguu ni hatua zake, na moyo hupata matamanio, na tupu husadikisha [hutenda] au hukadhibisha [huacha])). [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Waumini wenye kuhifadhi tupu zao ni wale ambao hawamkaribii yeyote isipokuwa wale waliohalalishwa nao na wale iliyomiliki mikono yao ya kuume kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ﴿٢٩﴾

Na ambao wanahifadhi tupu zao.

 

إِلَّا عَلَىٰ أَزْوَاجِهِمْ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ﴿٣٠﴾

Isipokuwa kwa wake zao, au wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume, basi hao si wenye kulaumiwa.

 

فَمَنِ ابْتَغَىٰ وَرَاءَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْعَادُونَ﴿٣١﴾

Basi yeyote yule atakayetaka kinyume ya hayo, basi hao ndio warukao mipaka. [Al-Ma'aarij: 29-31]

 

 

Sifa hii vile vile ni miongoni mwa sifa Alizozitaja Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuwa pindi Muislamu akizimiliki, ataingizwa Jannah ya Al-Firdaws kama ilivyotajwa katika Suwratul-Muuminuwn:

 

وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ ﴿٥﴾

Na ambao wanazihifadhi tupu zao.

 

إِلَّا عَلَىٰ أَزْوَاجِهِمْ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ ﴿٦﴾

Isipokuwa kwa wake zao, au kwa iliyowamiliki mikono yao ya kuume basi hao hawalaumiwi.

 

 

فَمَنِ ابْتَغَىٰ وَرَاءَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْعَادُونَ ﴿٧﴾

Lakini atakayetaka kinyume ya hayo; basi hao ndio wapindukao mipaka. [Al-Muuminuwn 5-8]

 

Zinaendelea Aayah mpaka kauli Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 

أُولَـٰئِكَ هُمُ الْوَارِثُونَ ﴿١٠﴾

Hao ndio warithi.

 

الَّذِينَ يَرِثُونَ الْفِرْدَوْسَ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿١١﴾

Ambao watarithi (Jannah) ya Al-Firdaws, wao humo ni wenye kudumu. [Al-Muuminuwn: 1-11]

 

 

Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pia ametubashiria Jannah kwa wenye kuhifadhi tupu zao aliposema:

 

((مَنْ يَكْفُل لِي مَا بَيْن لَحْيَيْهِ وَمَا بَيْن رِجْلَيْهِ أَكْفُل لَهُ الْجَنَّة)) البخاري

((Atakayenipa dhamana (ya kuhifadhi) baina  ya ndevu (ulimi) zake na miguu yake (tupu) basi atadhaminiwa Jannah)) [Al-Bukhaariy]

 

 

 

Muislamu pindi akiinamisha macho yake na wanawake wakitii amri ya Allaah ('Azza wa Jalla) kuhusu kutimiza hukmu za hijaab, basi wataweza kujilinda na hayo yaliyotahadharishwa.  Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anaamrisha:

 

قُل لِّلْمُؤْمِنِينَ يَغُضُّوا مِنْ أَبْصَارِهِمْ وَيَحْفَظُوا فُرُوجَهُمْ ۚ ذَٰلِكَ أَزْكَىٰ لَهُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا يَصْنَعُونَ ﴿٣٠﴾

Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao. Hivyo ni utakaso zaidi kwao. Hakika Allaah ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika kwa yale wayatendayo. 

 

 

وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا ۖ وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ ۖ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ أَوِ التَّابِعِينَ غَيْرِ أُولِي الْإِرْبَةِ مِنَ الرِّجَالِ أَوِ الطِّفْلِ الَّذِينَ لَمْ يَظْهَرُوا عَلَىٰ عَوْرَاتِ النِّسَاءِ ۖ وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِن زِينَتِهِنَّ ۚ وَتُوبُوا إِلَى اللَّـهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٣١﴾

Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao, na wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika. Na waangushe khimaar (shungi) zao mpaka vifuani mwao, na wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa kwa waume zao, au baba zao, au baba za waume wao, au wana wao wa kiume, au wana wa kiume wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kiume wa kaka zao, au wana wa kiume wa dada zao, au wanawake wao (wa Kiislamu), au wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume, au wafuasi wanaume wasio na matamanio ya jimai miongoni mwa wanaume au watoto ambao hawatambui kitu kuhusu sehemu za siri za wanawake. Na wala wasipige miguu yao yakajulikana yale wanayoyaficha katika mapambo yao. Na tubuni kwa Allaah nyote, enyi Waumini mpate kufaulu. [An-Nuwr: 30-31]

 

 

Wanawake wasiotimiza hijaab, wameharamishwa Jannah na hawatasikia hata harufu yake:

 

 

  عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((صِنْفَانِ مِنْ أَهْلِ النَّارِ لَمْ أَرَهُمَا: قَوْمٌ مَعَهُمْ سِيَاطٌ كَأَذْنَابِ الْبَقَرِ يَضْرِبُونَ بِهَا النَّاسَ، وَنِسَاءٌ كَاسِيَاتٌ عَارِيَاتٌ مُمِيلاَتٌ مَائِلاَتٌ رُءُوسُهُنَّ كَأَسْنِمَةِ الْبُخْتِ الْمَائِلَةِ، لاَ يَدْخُلْنَ الْجَنَّةَ وَلاَ يَجِدْنَ رِيحَهَا، وَإِنَّ رِيحَهَا لَيُوجَدُ مِنْ مَسِيرَةِ كَذَا وَكَذَا)) مسلم

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah(رضي الله عنه)  kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه  وآله وسلم ) amesema: ((Aina mbili za watu wa motoni sijawaonapo [hawapo katika zama zangu]: Watu walio na mijeledi mfano wa mikia ya ng’ombe wanawapiga watu kwa mijeledi hiyo [kwa dhulma], na wanawake waliovaa nguo na ilhali wako uchi, wakitembea kwa maringo huku wakiyanyonga mabega yao na wakiwafunza wengineo kutenda kama hivyo, vichwa vyao ni kama nundu za ngamia-bukhti wanaodemadema. Hawatoingia Jannah wala hawataisikia harufu yake, na kwa hakika harufu yake husikika umbali kadha wa kadhaa)). [Muslim]

 

  

Hadiyth hiyo ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inatudhihirikia uhakika wake kwani tunawaona baadhi ya dada zetu wanaovaa nguo wakidhani wamejisitiri kumbe wako uchi.  Utamuona mwanamke amejifunika kichwa tu akidhania ndio maana ya hijaab lakini mwili wake wote haukusitirika kwa sababu vazi lake halikutimiza masharti yake ya hijaab ambayo ni mwanamke kujigubika jilbaab limfunike mwili mzima (pamoja na khilafu iliyopo kati ya Wanachuoni kuhusu suala la uwajibu wa kuufunika uso na kutoufunika).  Jilbaab hilo lifuate masharti yafuatayo: 

 

 

1. Jilbaab liwe refu la kukufunika mwili mzima mpaka miguu, na kama halikufunika miguu basi mwanamke avae soksi.  

 

 

2.  Jilbaab liwe pana na sio lenye kuonyesha umbo, yaani lisiwe lenye kubana popote mwilini.  

 

 

3.  Jilbaab liwe zito na si jepesi la kuonyesha mwili.

 

 

4.  Jilbaab lisiwe na marembo yoyote yale ya kuvutia.

 

 

5. Jilbaab halitakiwi lifanane na mavazi ya makafiri.

 

 

6.  Jilbaab halitakiwi liwe ni katika mavazi ya fakhari.

 

 

7. Wanawake kutokuvaa nguo zinazofanana na nguo za kiume.

 

  

8.    Kutotia manukato.

 

 

Dada zetu wa Kiislamu watakapotimiza haya watakuwa wamekamilisha hijaab zao na watakuwa katika stara pamoja na kusitiri jamii na ndipo watakapokuwa wamejitahidi kujihifadhi waweze kuingia katika sifa hiyo ya kuhifadhi tupu zao.  

 

 

Kisa cha Zahrah na safari yake ya kuvaa hijaab. 

 

 

"Safari yangu ya hijaab au labda niseme "hijaab inayopasa ki-shariy’ah” ni ndefu na ya pole pole na sio ya tamthilia.   

 

Nilikuwa na umri wa miaka 14 nikienda shule pamoja na kaka yangu na dada zangu. Baba yangu alikuwa akitupeleka na kuturudisha shuleni. Kwa vile baba yangu alikuwa ana kazi nyingi sana na wakati wake ulikuwa wa dhiki, aliamua kutuwekea teksi kwa muda wa wiki mbili.  Dereva wa teksi alikuwa mtu mwema na mchangamfu. Alikuwa akitutolea visa na vichekesho wakati tunaelekea shuleni na kurudi. Tukaanza kumpenda na kumheshimu kama vile ni mjomba wetu. Hakuwa anajua Kiingereza, lakini siku moja alitupa tafsiyr ya Qur-aan ya Marmaduke Pickthall.

 

Siku moja wakati anaturudisha nyumbani, mara ghafla akasema: "Wasichana wa Kiislamu ni lazima wavae hijaab." Maneno yake yakawa yananigonga masikioni siku nzima! Sikupata kuvaa hijaab kabla, na karibu nisba ya 99% ya wasichana darasani mwangu hawakuwa wanavaa hijaab, wala sikupenda fikra hiyo ya kuvaa hijaab mwenyewe. Lakini sikuweza kupinga aliyoyasema dereva huyo ingawa sikuwa na pendekezo nalo jambo hili, na sikuweza kukanusha kwamba wanawake wa Kiislamu wanapaswa kuvaa hijaab.

 

Nikaanza kuvaa kitambaa cha kichwa siku ya pili na nakiri kwamba nilianza kuvaa kwa sababu ya heshima niliyo kuwa nayo ya dereva huyo bila ya kufikiri kwamba ni makosa kwani nilitakiwa nimkumbuke Mola wangu kwanza. Na sikuwa na sababu ya kunizua kuvaa hijaab. Wazazi wangu walifurahia uamuzi wangu.

 

 

Siku za mwanzo, nilianza kuvaa kitambaa cha kichwa kwa kujifunika nusu na huku baadhi ya nywele zikionekana! Nilitambua kuwa hivyo sivyo ilivyopasa kuvaliwa. Baada ya hapo nikatamuba unafiki wangu nikaanza kuivaa vizuri na kufunika nywele zote. Haikuwa wepesi ingawa nilikuwa naishi katika nchi ya Kiislamu na marafiki zangu walikuwa wakiniuliza: "Kwa nini unafanya hivyo? Unaonakana kama mzee!”

 

Kwao wao, jambo hilo lilikuwa ni kama tendo la watu wazima tu. Na sisi tulio vijana tukiwa bado shuleni tunatakiwa tuwe na uhuru wa mavazi. Lakini AlhamduliLLaah sikuwasikiliza maneno yao kwani hijaab ilinifanya nionekane mtu makini na heshima zaidi. Nikaamua kuivaa moja kwa moja. Nikaanza kuvaa nguo zilizofunika mikono yote, na zilizokuwa pana kila mahali nilikokwenda hadi ilipofika mwezi wa Septemba nikajifunza kwamba jilbaab ni lazima nikaanza kuvaa jilbaab.

 

Nikitazama nyuma nawaza kwamba hijaab imenisaidia sana kuniunda kama mwanamke hasa wa Kiislam. Nilipoanza kuivaa hata sikuwa nadumisha Swalaah zangu tano. Lakini  AlhamduliLLaah hatua baada ya hatua hijaab yangu imenisaidia kufunga milango yote ya shari na mambo yasiyopasa ya Kiislamu yaliyonizunguka katika mazingira yangu. Nimeunda picha fulani katika macho yangu na ya wengine, hivyo ikanibidi niishi katika kigezo hicho cha picha hiyo; picha ya staha.”

 

 

 

Share