Mume Hapendi Kustarehe Na Mimi Anastarehe Nje Na Wanawake Nje

Mume Hapendi Kustarehe Na Mimi Anastarehe Nje Na Wanawake Nje

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

 

Assalamu alykum 

 

Nakushukurukuruni sana kwa majibu yenu na nimefahamu na in Shaa-Allah nitajitahidi kusikiliza mawaidha   yenu In Sha-Allah Allaah atusaidie amin.

 

Mtanisamehe mimi nimo katika mtihani mkubwa na najitahidi na ninamuomba Allaah anipe moyo huu nisije nikavuka mipaka yake amin.

 

Sababu yakumtajia mume wangu talaka ni hii mimi mume wangu tuko pamoja  na  tunaishi pamoja lkn mume wangu hana  starehe namie wala hamu na hata  mimi nikiwa na hamu nikimuendea  bc simalizi hamu yangu na namhisi hana raha sasa nakua naona dhiki sana lkn  sina la kufanya nikimuliza mume wangu kuna kitu hupendi kwangu au sikuridhishi unachopenda,  hanijibu, halafu huku ana mambo hayo  anakwenda na wanawake. Sasa mimi ndugu zangu nimfanye nini ili mume wangu aridhike kwangu na awe na hamu na mimi tunaweza kukaa hata mwezi hajanigusa na mimi nikimuendea bc anakua hawezi kustarehe na mimi. Namuomba Allaah usiku na mchana  anikinaishe nisije nikavuka mipaka  na kwa sababu namuogopa Allaah ndio maana sitaki kuvuka mipaka sina ziada ila mtanisamehe  kwa masuala hayo lkn In Shaa-Allaah mtanipa jawabu ya kuniridhisha na kunistahmilisha. Maasalama.

 

 

 

JIBU:

 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani kwako dada yetu kwa kunufaika na mawaidha pamoja na nasaha ambazo tulikutunukia ili kuweza kukimu ndoa yako. Tatizo hili la kijamii katika jamii yetu limekuwa sugu, hivyo ni muhimu wazazi, Mashaykh, Maustaadh, kaka na dada wachukue jukumu lao ili kuweza kuwaweka wasichana na vijana chini na kuwaandaa vizuri kabla ya kuingia katika ndoa.

 

 

Mara nyingi zile taswira zetu za ndoa zinakwenda kinyume na matarajio yetu, hivyo kuleta shida kwa wanandoa. Kuna msemo kuwa ‘Marriage is not a bed of roses’ (ndoa si kitanda cha mawaridi) lakini sisi huchukulia kinyume na hayo. Sababu kubwa ni kuwa huwa tunaleta taswira ya starehe, raha, mapenzi yenye kudumu na mengineo. Hatuelewi wala kueleweshwa kuwa watu wawili wanaposihi kunaweza kutokea matatizo, magomvi n.k., hivyo tunapaswa kuyajua hayo ili tuweze kukabiliana nayo kama familia moja bila hivyo tutakuwa ni kama zima moto. Kwa sababu ya maumbile ya mwana-Aadam ambayo yaeleweka na Muumba Wake kuwa wanandoa watakuwa na matatizo Aliweka njia na mbinu za kutatua matatizo hayo kwa njia muruwa kabisa. 

 

 

Matatizo ya wanandoa yanatokea kwa sababu ya wawili hao kutoelewa haki na majukumu yao au kuwa wanaelewa lakini wakashindwa kuyatimiza au kutotaka kuyatimiza kabisa. Katika hali hizo mizozano na migongano huwa haimaliziki. Likitatuliwa moja huzuka na kuibuka jengine mpaka ndoa hiyo ikawa ni yenye kuvunjika.

 

 

Kueleza wazi tatizo linapotokea ni njia moja muafaka ya kuweza kulitatua. Katika mas-ala ya Dini hasa ya Kiislamu hakuna samahani katika kuuliza wala hakuna hayaa katika hilo. Kwa ajili hiyo ndio tumeweza kujua mengi katika maingiliano baina ya mume na mke kwa sababu wanawake wa Kianswari hawakuwa ni wenye kuona hayaa katika kuuliza mambo ya Dini yao. Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Anatuambia:

 

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَسْتَحْيِي أَن يَضْرِبَ مَثَلًا مَّا بَعُوضَةً فَمَا فَوْقَهَا ۚ  

Hakika Allaah Haoni hayaa kupiga mfano wa mbu na ulio zaidi yake (kwa udogo).   [Al-Baqarah: 26]

 

Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

  وَاللَّـهُ لَا يَسْتَحْيِي مِنَ الْحَقِّ ۚ  

Allaah Hasitahi (kubainisha) haki.   [Al-Ahzaab (33:53)]

 

 

Kwa mujibu wa swali lako pamoja na maelezo yako inaonyesha dada yetu haujafanya (wewe na mume wako) bidii ya kutaka kujua tatizo liko wapi. Unaweza kuwa unasikia uchungu kwa mume wako kutoweza kukustarehesha kimapenzi na una haki ya hilo. Kwa maoni yetu tunaona ni vyema kabla ya kukasirika na kutaka talaka kutambua na kufahamu tatizo lenyewe. Maswali yafuatayo yanaweza kutusaidia kujua tatizo:

 

 

1. Tatizo la mumeo kutoweza kukustarehesha limeanza karibuni au tangu akuoe?

 

2. Je, mumezaa watoto katika ndoa yenu?

 

3.  Je, mumeoana kijamaa/ kindugu au mko mbali kinasaba?

 

4. Je, yeye aliridhika nawe, nawe kuridhika naye kabla ya ndoa au alilazimishwa au ulilazimishwa au mlilazimishwa na wazazi?

 

5. Je, mliwahi kuwa katika mapenzi kabla ya kuoana?

 

6. Je, mlikutanishwa kabla ya kufungwa nikaah?

 

7. Je, mmekaa pamoja kama mume na mke kwa muda gani?

 

8. Je, awali uhusiano wenu ulikuwa ndio hivi hivi au ulikuwa mzuri?

 

9. Je, unaishi na mumeo pamoja na wazazi wake au wako au mnaishi wenyewe?

 

 

Mara nyingine wanaume wanakuwa na tatizo la kutoweza kukamilisha tendo la ndoa kwa sababu moja au nyingine. Ikiwa ni mraibu wa mirungi au miraa basi huvunja maume yake na hivyo kutoweza kukamilisha mahusiano ya kimwili. Ikiwa ni mtu wa kuangalia filamu za ngono au wanawake wakiwa uchi au kujichua basi uume wake unapungua nguvu, hivyo kutoweza kufanikisha tendo hilo. Pia inawezekana kuwa hana mambo yote hayo na akawa uwezo wake ni mdogo sana katika suala hilo. Kwa hiyo, haina haja yako kukasirika bali ni kutafuta njia ya kumtibu na kumuondolea tatizo hilo ili maisha yenu ya ndoa yawe mazuri. Udhaifu huu huweza kutibika katika hospitali na madaktari waliobobea katika fani hiyo.

 

 

Jambo ambalo ni muhimu kabla ya kutaka talaka ni kukaa wewe na mumeo mkazungumza kama mume na mke. Katika mazungumzo hayo kila mmoja atoe alichonacho ili kutibu tatizo au ugonjwa huo. Ikiwa mtakutana lakini ikawa kila mmoja hawezi kutapika au kutoa dukuduku lake basi tatizo litaendelea kuwepo hivyo kuhatarisha ndoa yenu.

 

 

Ikiwa mmeshindwa kufikia muafaka au maamuzi basi jaribu kuwashirikisha wazazi wenu au Mashaykh wanaoweza kuwasikiliza nyote wawili baada ya hapo kuwapatia ufumbuzi wa tatizo lenu hilo. Ikiwa kweli niyyah ni sulhu basi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Atawafikishia kama Aanvyosema:

 

وَإِنْ خِفْتُمْ شِقَاقَ بَيْنِهِمَا فَابْعَثُوا حَكَمًا مِّنْ أَهْلِهِ وَحَكَمًا مِّنْ أَهْلِهَا إِن يُرِيدَا إِصْلَاحًا يُوَفِّقِ اللَّـهُ بَيْنَهُمَا ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيمًا خَبِيرًا ﴿٣٥﴾

Na mkikhofu mafarikiano baina yao wawili, basi pelekeni mwamuzi kutoka watu wa mume na mwamuzi kutoka watu mke. Wakitaka sulhu Allaah Atawawafikisha baina yao.  Hakika Allaah daima ni Mjuzi wa yote, Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [An-Nisaa: 35]

 

 

Kuwa na busara dada yetu ili uweze kuokoa ndoa yako, na kwa sababu ya ikhlaasw yako na niyyah nzuri basi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Atakusahilishia hilo. Kisha umezungumzia kuwa mumeo anakwenda kwa wanawake bila ya kufafanua lolote. Je, anakwenda kwao ili kutimiza uchu wake wa kimapenzi au vipi? Je, umemshudia hilo au umesikia kwa waja? Ikiwa umesikia kwa waja, uhusiano wako na wao ni upi? Waliokuambia ni wanaume au wanawake? Ikiwa umesikia kwa watu usianze kuchukua dhana, kwani watu mara nyingi wanaeneza uvumi na umbeya jambo ambalo limekatazwa na Uislamu. Inatakiwa uwe na hakika na hilo kwa sababu ikiwa huna hakika na yakawa ni mambo ya kusikia tu, utakuwa na dhambi mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) na kama kungekuwa na dola ya Kiislamu ungekuwa ni mwenye kutiwa adhabu kama vile mume kumsingizia mkewe kuwa amezini bila ya kuleta mashahidi wanne. Kwa hiyo, jihadhari na hilo ikiwa huna uhakika nalo.

 

 

In Shaa Allaah kwa niyyah yako safi ya kutaka kukaa katika hali ya utwaharifu na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Hatakuacha katika hali hilo bali Atakutolea njia njema ya kuweza kuishi katika maisha ya kumridhisha Yeye.

 

 

Endelea kumuomba Allaah, kufanya Ibaadah kwa wingi haswa Swalaah ya usiku ya Tahajjud, zidi kumuomba kwa dua kwa wingi. Hakika ni kuwa mwenye kujitahidi katika kufanya ya kheri Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anamsaidia kuepukana na mambo ya shari na kumsogezea mambo mema. Hakuna mtu yeyote anayeacha kitu kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) isipokuwa Yeye Humsaidia katika kufikia malengo yake na kumpatia badali ya hilo.

 

 

Tuna Iymaan kuwa kwa niyyah yako nzuri na njema ya kutaka kutekeleza mambo mema na mazuri Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Hatakuacha mkono wala Hatakutupa bali Atakusaidia kwani Yeye Anasema:

 

فَإِنَّ مَعَ الْعُسْرِ يُسْرًا ﴿٥﴾ إِنَّ مَعَ الْعُسْرِ يُسْرًا ﴿٦﴾

 

Basi hakika pamoja na kila ugumu kuna wepesi. Hakika pamoja na kila ugumu kuna wepesi. [Ash-Sharh: 5 – 6]

 

 

Kwa hiyo fuata wasiya wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  pale Anaposema:

 

وَاسْتَعِينُوا بِالصَّبْرِ وَالصَّلَاةِ ۚ وَإِنَّهَا لَكَبِيرَةٌ إِلَّا عَلَى الْخَاشِعِينَ ﴿٤٥﴾

Na tafuteni msaada kupitia subira na Swalaah; na hakika hilo ni kubwa isipokuwa kwa wanyenyekevu. [Al-Baqarah: 45]

 

 

Nasi tunakutakia kila la kheri pamoja na du’aa zetu kwako Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Akuondolee matatizo yako pamoja na wengine wenye matatizo kama yako au makubwa zaidi, Akusahilishie na Akupe subira pamoja na kukuimarisha katika Dini hii tukufu, Uislamu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share