Imaam Ibn Baaz: Kaweka Nadhiri Kwa Imaam Kisha Akatambua Kuwa Haipasi Je, Atekeleze Kafara?

 

Kaweka Nadhiri Kwa Imaam Kisha Akatambua Kuwa Haipasi Je, Atekeleze Kafara?

 

Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Imenitokea mushkila nikaweka nadhiri kwa ajili ya mmojawapo wa ma-Imaam, kisha nikaja kutambua kuwa haifai kuweka nadhiri kwa asiyekuwa Allaah. Tambua kuwa sehemu aliyoko huyo Imaam iko mbali, je, inajuzu nilipize nadhiri hii kwa mafakiri au niifanyie kafara?

 

 

JIBU: 

 

Nadhiri hiyo ni baatwil, kwa sababu ni ‘ibaadah kwa asiyekuwa Allaah.  Inakupasa utubie kwa Allaah kwayo na urudi Kwake kwa kutubia na kuomba maghfirah na kujuta kwani nadhiri ni ‘ibaadah, Anasema Allaah Ta’aalaa:  

 

وَمَا أَنفَقْتُم مِّن نَّفَقَةٍ أَوْ نَذَرْتُم مِّن نَّذْرٍ فَإِنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُهُ ۗ

Na chochote mtoacho (kwa ajili ya Allaah) au mkiwekacho nadhiri, basi Allaah Anakijua. Na madhalimu hawana wa kuwanusuru. [Al-Baqarah: 270]

 

Yaani: Atakulipeni kwayo. Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

من نذر أن يُطِيعَ اللهَ فلْيُطِعْهُ، ومن نذرَ أن يعصِيَه فلا يَعْصِه

((Aliyeweka nadhiri kumtii Allaah amtii, na aliyeweka nadhiri kumuasi Allaah, basi asimuasi))  

 

Kwa hiyo nadhiri hiyo ni baatwil, na ni kumshirikisha Allaah (‘Azza wa Jalla) kama vile nadhiri kwa ajili ya ma-Imaam na waliokufa ni nadhiri baatwil na ni kumshirkisha Allaah, basi nadhiri haijuzu isipokuwa kwa ajili ya Allaah Pekee, kwa sababu ni ‘ibaadah kama vile Swalaah, na kuchinja na nadhiri, na kufunga Swiyaam na du’aa zote ni kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kama Anavyosema (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ ﴿٥﴾

Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada.

 

Na Anasema (Subhaanahu):

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ  

Na Rabb (Mola) wako Amehukumu kwamba: “Msiabudu (yeyote) isipokuwa Yeye Pekee [Al-Israa: 23

Na Anasema:

فَادْعُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ وَلَوْ كَرِهَ الْكَافِرُونَ ﴿١٤﴾

Basi mwombeni Allaah wenye kumtakasia Dini japokuwa wanachukia makafiri. [Ghaafir: 14]

Na Anasema (‘Azza wa Jalla):

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا﴿١٨﴾

Na kwamba Misikiti ni kwa ajili ya Allaah, basi msiombe yeyote pamoja na Allaah. [Al-Jinn: 18]

 

Basi ‘ibaadah ni haki ya Allaah, na nadhiri ni ‘ibaadah, na Swawmi ni ‘ibaadah, na Swalaah ni ‘ibaadah, na du’aa ni ‘ibaadah basi inawajibika kuisafisha kwa ajili ya Allaah Pekee. Kwa hiyo nadhiri hiyo ni baatwil, na haikupasi kufanya chochote, si kwa mafukara wala wengineo, bali inakupasa utubie tu na huna haja ya kuilipizia nadhiri hiyo kwa vile ni baatwil na ni shirki, ila tu utubie tawbah ya kikweli na kufanya matendo mema, Allaah Akuwafikie na Akuongoze katika yanayomridhisha na Akujalie ufanye tawbah ya kikweli.

 

 

http://www.binbaz.org.sa/fatawa/4776

 

 

Share