Sa'ad Ibn Abiy Waqqaas (رضي الله عنه)

 

Sa’ad Ibn Abiy Waqqaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu)

 

Alhidaaya.com

 

 

Alikuwa kijana mfupi na aliyejengeka kimwili na nywele nyingi. Watu wa Makkah walimfananisha na simba mtoto. Nae pia anatoka katika ukoo wa kitajiri na kuheshimika. Ni mtu wa karibu sana kwa wazazi wake na alimpenda sana mama yake. Muda wake mwingi aliupoteza kutengeneza mishale na pinde na kufanya sana mazoezi ya kurusha mishale kama kwamba anajiandaa na vita vikubwa.

 

 

Sa’ad hakuwa na furaha katika mfumo mzima wa maisha ya Maquraysh wa Makkah. Alihisi kwamba iymaan zao na miungu wanayoiabudu ina upungufu aina fulani bila ya kuujua hasa ni upi. Tabia za Maquraysh nazo pia hazikumpendeza wala kumridhisha.

 

Siku moja alitembelewa na Abu Bakr As-Swidiyq (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na kuzungumza naye. Abu Bakr alimfahamisha kuhusu Muhammad ibn ‘AbdiLLaah mtoto wa dada yake kwa mjomba na shangazi, Aaminah bint Al-Wahhaab kwamba ameteremshiwa Wahy na kutumwa kutangaza Dini ya haki na uongofu.

 

 

Baadae Abu Bakr alienda naye kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Ilikuwa ni jioni na Rasuli ndio kwanza amemaliza kuswali. Baada ya kusikia wito na yeye mwenyewe tangu mwanzo kuwa na wasi wasi na iymaan ya kiquraysh alikubali hapo hapo na kutamka shahada.

 

Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifurahishwa sana na kusilimu kwa Sa’ad kwani tokea utotoni wake alama za kuwa mtu wa busara tayari zilijitokeza. Vile vile kusilimu kwake kungepelekea vijana wengine pia nao kuja katika uislaam.

 

 

Ingawa Rasuli (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifurahishwa sana na kitendo cha Sa’ad kuingia katika uislaam, kuna watu wengine walichukizwa sana na tendo hilo akiwemo mama yake Sa’ad. Sa’ad (Radhiya Allaahu ‘anhu) anasimulia:

 

'Wakati mama yangu alipopata habari kwamba nimesilimu aliingiwa na hasira na alikuja kwangu huku ameghadhibika na kunikaripia, 'Ee Sa’ad mwanangu, nini kimekusibu kuacha dini ya baba na mama yako na kufuata dini gani hii? Naapa ima uachane na dini yako hii mpya au nitajifungia kula na kunywa mpaka nife.

Moyo wako utaemewa kwa huzuni na majuto kukukumba na watu kukuapiza milele kwa jinsi ulivyomtendea mama yako.'

 

Sa’ad akajibu, "usifanye hivyo, ee mama yangu, hakuna kitu chochote kitakachonifanya niachane na dini yangu." Hata hivyo, mama yake hakumsikiliza na kuanza mgomo wake wa kutokula wala kunywa. Akaanza kudhoofika na Sa’ad alijitahidi kumbembeleza na kumsihi mama yake huku akimletea chakula. Mama yake alikataa kata kata na kurudia usemi wake ule ule, "achana na dini yako na mimi nitakula, bila hivyo, niache nife."

 

 

Sa’ad akamwambia, "ee mama yangu nina mapenzi makubwa kwako kama mama yangu ulienizaa, lakini mapenzi yangu kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na Rasuli Wake ni makubwa zaidi. WaLLaahi, lau hata roho elfu moja na moja zitaondoka (kwa kunitaka nirudi dini yangu ya zamani) kamwe sitorudi dini yangu." Mama yake kuona msimamo wa mwanawe haujatetereka wala kuyumba licha ya kitisho kizito alichomtisha akaona hakuna haja tena ya kuendelea na mgomo na kuanza kula.

 

Katika tukio hili ‘adhiym la msimamo wa Sa’ad kwa mama yake katika Suwraah Luqmaan:14-15

وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ حَمَلَتْهُ أُمُّهُ وَهْنًا عَلَىٰ وَهْنٍ وَفِصَالُهُ فِي عَامَيْنِ أَنِ اشْكُرْ لِي وَلِوَالِدَيْكَ إِلَيَّ الْمَصِير﴿١٤﴾وَإِن جَاهَدَاكَ عَلَىٰ أَن تُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا ۖ وَصَاحِبْهُمَا فِي الدُّنْيَا مَعْرُوفًا ۖ وَاتَّبِعْ سَبِيلَ مَنْ أَنَابَ إِلَيَّ ۚ ثُمَّ إِلَيَّ مَرْجِعُكُمْ فَأُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿١٥﴾

Na Tumuemuusia insani (kuwafanyia wema) wazazi wake wawili. Mama yake ameibeba mimba yake (akimzidishia) udhaifu juu ya udhaifu, na (kumnyonyesha na) kuacha kwake ziwa katika miaka mwili; ya kwamba, unishukuru Mimi, na wazazi wako; Kwangu ndio mahali pa kuishia. Lakini (wazazi wako) wakikufanyia juhudi kwamba unishirikishe na yale usiyokuwa na elimu nayo, basi usiwatii. (Lakini) Suhubiana nao kwa wema duniani, na fuata njia ya anayerudi (kutubia) Kwangu. Kisha Kwangu ndio marejeo yenu, na Nitakujulisheni yale mliyokuwa mkiyatenda. [Luqmaan: 14-15]

 

Katika siku za mwanzo wa Uislaam, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwausia waislam kuwa na tahadhari sana na Maquraysh wasije wakakasirika kwani bado Uislaam haukuwa na nguvu za kuweza kuhimili vishindo vyao. Wakati huo walikuwa wakitoka vikundi kwenda kando kando ya mji wa Makkah kufanya ‘ibaada. Siku moja baadhi ya makafiri waliwaona waislaam wakiswali na wakawabughudhi na kuwafanyia ‘inaad.

 

 

Subira ya waislaam ilifika kikomo na wakavamiana nao na kuanza kupigana. Sa’ad alikamata bufuru la ngamia na kumpiga mmoja wao na kumjeruhi. Ilikuwa ni damu ya kwanza kumwagika kati ya vita vya waislaam na makafiri vita ambavyo ilikuja kuwa kubwa na kujaribu iymaan za waumini na kuwatia katika mitihani.

 

Hata hivyo, baada ya tukio hili, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) bado alisisitiza pale pale kuwa na subira na uvumilivu na kuwakumbusha kuwa hiyo ilikuwa ni amri ya Allaah Aliyetukuka na wakati bado haujawa muafaka. Allaah Anasema katika Suwrah Al- Muzamiyl 10:11

 

وَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا يَقُولُونَ وَاهْجُرْهُمْ هَجْرًا جَمِيلًا﴿١٠﴾وَذَرْنِي وَالْمُكَذِّبِينَ أُولِي النَّعْمَةِ وَمَهِّلْهُمْ قَلِيلًا﴿١١﴾

Na subiri juu ya yale wayasemayo, na wahame, mhamo mzuri. Na Niache Mimi na wanaokadhibisha walioneemeka; na uwape muhula kidogo. [Al-Muzzammil: 10-11]

 

 

Alipigana vita vya Badr pamoja na mdogo wake ‘Umayr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye aliomba aruhusiwe kuungana na jeshi japokuwa alikuwa na umri mdogo. Sa’ad (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alirudi peke yake Madiynah kwani ‘Umayr ni mmoja katika mashahidi kumi na wanne waliouwawa.

 

 

Katika vita vya Uhud, Sa’ad (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alichaguliwa pamoja na Zayd (Radhwiya Allaahu ‘anhu), Saib ibn Úthmaan bin Ma’azun kwani walikuwa warusha mishale stadi. Alipigana kwa moyo na nguvu zake zote katika kumlinda Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) hasa pale baadhi ya waislam waliopangwa milimani kuondoka sehemu zao.
Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimpa moyo huku akimwambia:

ارمي يا سعد. فداك ابي وأمي

"Rusha, rusha yaa Sa’ad, Fidaaka Abiy wa Ummiy".

 

‘Alliy ibn Abi Twaalib anasema hajawahi kumsikia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiahidi kulipa kwa mtu yoyote isipokuwa Sa’ad (Radhwiya Allaahu ‘anhu). Katika historia ya Kiislaam Sa’ad (Radhwiya Allaahu ‘anhu) atakumbukwa kuwa Swahaba wa kwanza kurusha mishale kwa ajili ya kuuhami Uislaam na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuombea Du’aa:

 

"Ee Rab Uongoze mshale wake na umkubalie Du’aah zake"

 

 

Na’aam! Sa’ad (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alijaaliwa utajiri na hakuwa maarufu kwa ushujaa tu bali pia alikuwa mkarimu. Wakati wa Hijjatul Widaa (Hijja ya kuaga) akiwa pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliugua. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaja kumtazama.

 

 

Hadiyth ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inasimulia haya:

 

وعن أبي إسحاقَ سَعدِ بنِ أبي وَقَّاصٍ مالِكِ بنِ أُهَيْب بنِ عبدِ منافِ ابنِ زُهرَةَ بنِ كلابِ بنِ مُرَّةَ بنِ كعبِ بنِ لُؤيٍّ القُرشِيِّ الزُّهريِّ رضي الله عنه أَحَدِ العَشَرَةِ المشهودِ لهم بالجنةِ رضي الله عنهم قَالَ: جاءنِي رسولُ اللهِ صلى الله عليه وسلم يَعُودُنِي عَامَ حَجَّةِ الوَدَاعِ مِنْ وَجَعٍ اشْتَدَّ بي، فقُلْتُ: يَا رَسُولَ اللهِ! إنِّي قَدْ بَلَغَ بي مِنَ الوَجَعِ مَا تَرَى، وَأَنَا ذُو مالٍ وَلا يَرِثُني إلا ابْنَةٌ لي، أفأَتَصَدَّقُ بِثُلُثَيْ مَالِي؟ قَالَ: ((لا))، قُلْتُ: فالشَّطْرُ يَا رَسُولَ اللهِ؟ فقَالَ: ((لا))، قُلْتُ: فالثُّلُثُ يَا رَسُولَ اللهِ؟ قَالَ: ((الثُّلُثُ، والثُّلُثُ كَثيرٌ- أَوْ كبيرٌ- إنَّكَ إنْ تَذَرْ وَرَثَتَكَ أغنِيَاءَ خيرٌ مِنْ أنْ تَذَرَهُمْ عَالَةً يتكفَّفُونَ النَّاسَ، وَإنَّكَ لَنْ تُنفِقَ نَفَقَةً تَبْتَغي بِهَا وَجهَ اللهِ إلا أُجِرْتَ عَلَيْهَا حَتَّى مَا تَجْعَلُ في فِيِّ امْرَأَتِكَ))، قَالَ: فَقُلتُ: يَا رسولَ اللهِ، أُخلَّفُ بعدَ أصْحَابي؟ قَالَ: ((إِنَّكَ لَنْ تُخَلَّفَ فَتَعملَ عَمَلًا تَبتَغي بِهِ وَجْهَ اللهِ إلا ازْدَدتَ بِهِ دَرَجةً ورِفعَةً، وَلَعلَّكَ أنْ تُخَلَّفَ حَتّى يَنتَفِعَ بِكَ أقْوَامٌ وَيُضَرَّ بِكَ آخرونَ. اللَّهُمَّ أَمْضِ لأصْحَابي هِجْرَتَهُمْ ولا تَرُدَّهُمْ عَلَى أعقَابهمْ، لكنِ البَائِسُ سَعدُ بْنُ خَوْلَةَ)). يَرْثي لَهُ رَسُولُ اللهِ صلى الله عليه وسلم أنْ ماتَ بمَكَّة. مُتَّفَقٌ عليهِ.

Abu Is-haaq Sa’ad bin Abi Waqqaas Maalik bin Uhaib bin ‘Abdi-Manaaf bin Zuhrah bin Kilaab bin Murah bin Ka’ab bin Lu-ayyi Al-Qurashiyy Az-Zuhriyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu), ambaye ni mmojawapo kati ya watu waliobashiriwa Jannah (Pepo), amesimulia: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alinitembelea mwaka wa Hajjatul-Wadaa’a kutokana na ugonjwa ambao uliokuwa umenishitadi.
Nikamwambia: “Eee Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ugonjwa umenifikisha kama unionavyo, nami ni mwenye mali nyingi, wala hakuna atakayenirithi ispokuwa bint yangu (mmoja tu). Je, nizitoe swadaqa thuluthi mbili za mali yangu?” Akasema: “Hapana.” Nikasema: “Basi nitoe nusu yake ee Rasuli wa Allaah?” Akasema: “Hapana”. Nikasema: “Je, thuluthi (moja)?” Akasema: “Thuluthi (unaweza kutoa)”. Na hiyo thuluthi ni nyingi – kwa hakika uwaache wenyekukurithi ni wenyekujiweza, ni bora kulikoni kuwaacha wawe mafukara wakiomba watu. Na hakika hutatoa gharama ya matumizi ukawa unataka radhi za Allaah kwa matumizi hayo, ispokuwa utapewa ujira kwayo; hata unachokitia katika kinywa cha mkeo.” Nikamwambia: “Ee Rasuli wa Allaah, nitaachwa (niishi muda mrefu) baada ya wenzangu?” Akasema: “Hakika hutoachwa ukafanya ‘amali kwa ajili ya kutafuta radhi ya Allaah kwa ‘amali hiyo, ispokuwa utazidi daraja na utukufu kwa ‘amali hiyo. Na (huenda) ukaachwa (uishi) mpaka watu wanufaike kwa sababu yako, na wengine wadhuriwe kwa sababu yako. Ee Rabb! Wakamilishie Swahaba wangu Hijrah yao, wala usiwarejeshe nyuma kwa visigino vyao. Lakini masikini ni Sa’ad bin Khawlah!” Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamsikitikia kwa kuwa amekufa Makkah.” [
Al-Bukhaary na Muslim.]

 

Sa’ad alijaaliwa kupona ugonjwa na kubarikiwa na watoto wengine wengi tu. Alikuwa maarufu zaidi kama kamanda wa jeshi la kiislaam lililotumwa na Khalifah ‘Umar ibn Khattwaab kwenda kupigana na waajemi (Persians) katika vita vya Qadisiyyah. Khalifah alitaka kuung’oa utawala wa Sasania (Ctesphon) uliokuwa ukitawala kwa karne nyingi.

 

Kazi hii haikuwa rahisi kwani waajemi walikuwa wapiganaji stadi na wenye nidhamu ya hali ya juu. Hivyo lilihitajika jeshi lililotimia katika maeneo yote. Khalifa akatuma wajumbe katika miji ya waislaam iliyokombolewa kutangaza wito wa Jihaad na kukusanya wale wote wenye uwezo, utaalamu, mbinu na mikakati kujiandaa na vita hivi ‘adhim.

 

 

Na’aam! Wanajihadi wakaitikia wito na kukusanyika Madiynah kutoka kila kona ya miji ya waislaam. Kutokana na ukubwa wa jeshi la kiislam na uzito wa kazi yenyewe, Khalifah ‘Umar ibn Khatwaab ikambidi afanye shura kuhusu nani atakuwa kiongozi wa jeshi.

Ushauri wake Khalifah ulikuwa kuliongoza yeye mwenyewe kwani kazi ilikuwa nzito na kama ni Amiril Muuminin ni wajibu wake kuwaongoza waislaam. ‘Alliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) hakuunga mkono wazo hilo na kumfahamisha Amiyr kwamba waislaam walikuwa wanamuhitaji sana Khalifah kubaki Madiynah kuliko kwenda kuhatarisha maisha yake vitani.

Baada ya kupita shura, Sa’ad akachaguliwa. Mmoja katika Swahaba wakongwe Abdur-Rahmaan bin ‘Awf akampongeza Khalifah na kusema, “Umejua kuchagua! nani mwengine zaidi ya Sa’ad?"

Amiyril Muuminiyn ‘Umar akasimama na kulitakia kila la khayr jeshi la kiislaam na kumpa nasaha Sa’ad kwa kumwambia:

 

"Ee Sa’ad! Usikubali maneno yoyote yatakayosemwa kwamba (umechaguliwa kwa sababu) ni mjomba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au ni Swahaba wa mjumbe wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) haondoshi jambo baya kwa ubaya bali huondosha baya kwa jambo jema"

"Ee Sa’ad! Hakuna mahusiano yoyote kati ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na mtu yoyote isipokuwa kwa kumtii Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Kwa mtazamo wa Allaah watu wote ikiwa ni mheshimiwa au mtu wa kawaida, ni sawa sawa. Rabb ni Mola wao, wote ni waja Wake wanaotafuta kunyanyuliwa kwa Taqwa na kutii. Mkumbuke Rasuli wa Allaah(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokuwa akiwafanyia waislaam na wewe ufanye hivyo hivyo!"

Amirul Muuminiyn aliweka bayana kwamba vita hivi si kwa ajili ya mtu kupata umaarufu wala kutawala bali ni kulifanya neno la Allaah “ لا إله إلا الله ” kuwa juu.

 

 

Watu elfu thelathini wakaanza safari kuelekea Qadisiyyah wakiwemo tisini na tisa waliopigana vita vya Badr na zaidi ya mia tatu walioshuhudia suluhu ya vita vya Hudaybiya, pia wakiwemo takriban mia tatu wengine waliokuwamo katika jeshi la kuifungua Makkah (Fat-hu Makkah). Wakiwemo watoto wa Swahaba na wanawake waliokwenda kuwashajiisha na kama wauguzi.

 

 

Walipiga kambi Qadisiyyah katika mji wa Hiraa, Waajemi walijiandaa na vita hivi na jeshi la watu laki moja na ishirini elfu wakiongozwa na kamanda wao shujaa Rustum.

Amirul Muuminiyn alimuagiza Sa’ad kumpelekea habari kwa kila kitakachotokea kwa waislaam na makafiri. Sa’ad akamwandikia Amirul Muuminiyn juu ya ukubwa wa jeshi la makafiri na zana walizonazo.

Amirul Muuminiyn akajibu, “Usitishike wala kushtushwa na utakayoyasikia kuhusu jeshi lao na mbinu watakazozitumia dhidi yenu. Omba msaada kwa Allaah na uwe na iymaan. Peleka ujumbe wa watu wenye busara, hikmah na walio madhubuti wamlinganie kuingia Uislaam na jitahidi kuniandikia kila siku.”

 

 

Sa’ad alifanya kama alivyoagizwa na kutuma ujumbe mzito kwanza kwa Yazdaqird na baadaye kwa Rustum, wote kuwataka kuingia katika uislaam na kulipa jizyah (ushuru) ili wahakikishiwe usalama wao na kuishi kwa amani vyenginevyo wachague vita baina yao.

Ujumbe wa mwanzo wa waislaam ulibezwa na kudharauliwa na kiongozi wa Waajemi, Yazdaqird. Uliongozwa na Bin Nuum ibn Muqarrin. Ujumbe wa pili ukiongozwa na Rubiiy ibn Aamir kwa Rustum, ulikwenda moja kwa moja kambi ya Rustum. Huku akiwa na mkuki mkononi, Rubiiy akampa ujumbe na Rustum akauliza:

"Rubiiy! Nini mnnataka kutoka kwetu?” mkiwa mnataka utajiri, tutakupeni, mkitaka chakula tutakulisheni mpaka mkinai. "Aliendelea kusema,

"Tutakupeni nguo na kukufanyeni muwe matajiri na wenye furaha, tazama Rubriiy! Nini unaona kwenye majlis yangu hii?. Hapana shaka huoni alama za utajiri, mazulia ya fahari, mapazia ya kupepea, kuta zilizonakishiwa dhahabu, huna hata hamu basi tukikutunukia vyote hivi tulivyonavyo!"

 

Rubiiy alitulia na kumsikiliza Rustum akijifakharisha na kumwambia, "Sikiliza, Allaah Ametuchagua sisi na kutoka kwetu sisi kizazi chake ambacho mwenyewe Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) amemtaka ili kututoa katika kuabudu masanamu kwenda kwenye Tawhiyd (kumpwekesha Allaah)na kututoa kutoka kwenye wale wote wanaojishughulisha na dunia (kusahau Aakherah), na kututoa katika watawala dhalimu dhidi ya Uislaam." Aliendelea kusema,

"Na yeyote atakayetukubalia wito wetu tuko tayari kumkaribisha kwa mikono miwili na yoyote atakayeamua kupigana nasi, sisi tutapigana nae mpaka ahadi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) itakapotimia.

Rustum akauliza,

"Kitu gani amekuahidini Rabb wenu?"

"Pepo kwa wataokufa shaahid na ushindi kwa watakaoishi." Alijibu Rubiiy.

Hata hivyo, Rustum kwa kujiona wao ni bora zaidi hakuwa tayari kuzingatia maneno haya hasa kwa mtu mwenyewe anayesema kuonekana dhalili na kwa kuwa karne nyingi watu hawa walikuwa wakiwatawala na kuwajua kama walikuwa makatili na wajinga.

 

 

Vita hivyo vikawa vinanukia, Sa’ad alitokwa na machozi kwani kupindi hiki alikuwa mgonjwa hata kushindwa kusimama sawa sawa. Aliona dalili zote kwamba vita hivi vitakuwa vikubwa, hatari na damu nyingi itamwagika. Akawa akisema moyoni Lau...., lakini hapo hapo akaikumbusha nafsi yake kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amefundisha waislaam kutosema Lau…, kwani humaanisha ukosefu wa dhati na azma ya kufanya na kuona kwamba lau hali ingelikuwa hivi n.k. Hii si tabia ya kiislaam.
Akajikongoja na kusimama mbele na kuanza kuwahutubia wanajihaad, katika Qur-aan Suuwratu Al-Anbiyaa, ayaa ya 105.

وَلَقَدْ كَتَبْنَا فِي الزَّبُورِ مِن بَعْدِ الذِّكْرِ أَنَّ الْأَرْضَ يَرِثُهَا عِبَادِيَ الصَّالِحُونَ

Na kwa yakini Tuliandika katika Az-Zabuwr (Vitabu viloteremshwa mbinguni) baada ya Adh-Dhikri (Lawhun Mahfuudhw) ya kwamba: Ardhi (ya Jannah) watairithi waja Wangu wema.

 

 

Baada ya kumaliza khutbah ya kuhuisha nyoyo na kuwatia mori wanajihaad, wakaswali swala ya adhuhr jamaa na kuwageukia tena baada ya swala na kuwapa amri ya kupigana kwa kutamka kilio cha kivita,

“الله أكبر, الله أكبر, الله أكبر, الله أكبر” mara nne na kuamrisha washambulie huku akiwatia moyo kwa kusema, "حيّ على بركات", (haya wavamieni kwa baraka za Allaah).

 

 

Kwa siku nne mfulululizo vita vilipigwana huku Sa’ad akiwa kwenye hema lake akiongoza mashambulizi na kupanga mikakati na kuwatia mori wanajihaad,

 

"الله أكبر, لا حول ولا قوّة اِلا بالله"

 

 

Waislaam walipigana kwa moyo wao wote na ufundi wakijua ima ni ushindi au shahaada tu. Baadhi ya wanajihadi mashujaa walitafuta mbinu mpaka kuweza kumfikia kamanda Rustum kwenye ngome yake. Hapo ikazuka piga nikupige ya aina yake kwani ni vumbi tu lililokuwa likitimka ndilo lililoonekana na paa la ngome ya Rustum kutupwa ndani ya mto. Kuona patashika hiyo Rustum alijaribu kukimbia lakini hakufika mbali na alikamatwa na kuuwawa.

Baada ya kuuwawa kwa kamanda wao majeshi ya Kiajemi yalianza kusambaratika na kukimbia huku na kule wasijue la kufanya na huku wanajihaad wa kiislaam wakiwashambulia.

 

 

Vita hivi viliweka historia ya damu nyingi sana kumwagika kwani kwa siku nne tu zilizopiganwa vita hivi takriban watu elfu thelathini waliuwawa, na katika siku moja tu waislam elfu mbili walikufa shaahidi na makafiri elfu kumi kupoteza maisha yao.

Vita vya Qadisiyyah vilileta ushindi mkubwa sana kwa waislaam. Vilimaliza kabisa na kuondoa utawala wa kisasania kama vilivyokuwa vita vita vya Yarmuk kuumaliza utawala wa Kibizantini.

 

 

 

Miaka miwili baadaye na kuwa na hali nzuri ya kiafya Sa’ad alikwenda kuutwaa mji mkuu wa Sasan – Ctesiphon, waliweza kuutwaa mji huu baada ya kuuvuka mto Tigris wakati wa mafuriko.

Shujaa wa Qadisiyyah kama alivyojulikana baada ya vita hivi, Sa’ad (Radhwiya Allaahu ‘anhu), aliishi na kufariki akiwa na umri wa miaka themanini. Kabla ya kufariki alimwita mwanawe na kumuomba afungue sanduku ambalo alikuwa amelihifadhi mwenyewe muda wote. Ndani yake kulikuwa na juba la sufi na kumuusia mwanawe, “Nitakapokufa nikafinini kwa juba hili kwani ndilo nililokuwa nimevaa nilipokutana na makafiri siku ya vita vya Badr na ningependelea kukutana na Allaah nikiwa nalo.”

 

 

 

Share