Kwa Nini Nguruwe Na Mbwa Haraam?

 

 

SWALI:

Na naomba unipe maelezo yanayofanya mbwa na nguruwe wawe haramu...just i need points that lead them to be haram to islam society


JIBU:

 

Sifa zote njema anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla AAllaahu ‘alayhi wa aalihi wasallam) na Swahaba zake (Radhiya AAllaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Mas-ala ya halali na haramu ni haki ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala) peke Yake. Hakuna mwengine yeyote ambaye ana jukumu kama hilo. Hii ni kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala) Ambaye Ametuumba sisi binaadamu Ndiye Mwenye kujua vilivyo vizuri kwetu na vile ambavyo ni madhara kwetu sisi. Sisi viumbe Vyake hatuna haki ya kumsaili wala kumuasi Yeye. Kwa kuwa Yeye ni Mwingi wa Rehema kwa waja Wake, Anahalalisha na kuharamisha kwa sababu na hekima, kwa kutilia maanani maslahi ya mwanadamu. Hivyo, Alivyohalalisha ni safi na vizuri na Ameharamisha vile ambavyo ni vichafu na vibaya.

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Hakika Allaah Aliyetukuka ni Mzuri na Hakubali ila zuri. Na hakika Allaah Aliyetukuka Amewaamrisha Waumini yale Aliyowaamrisha Mitume. Akasema Allaah Aliyetukuka: 'Enyi Mitume! Kuleni vizuri na fanyeni mema' (23: 51). Na Akasema tena Allaah Aliyetukuka: 'Enyi Mlioamini! Kuleni vizuri Tulivyowaruzuku' (2: 172). Kisha akamtaja mtu anayekwenda safari ndefu, nywele zake zimechafuka na kujaa vumbi ainua mikono yake mbinguni akisema: 'Ewe Mola! Ewe Mola' – na ilhali chakula chake ni cha haramu, kinywaji chake ni cha haramu, kivazi chake ni cha haramu, amelishwa haramu! Je, atatakabaliwaje?" (Muslim kutoka kwa Abu Hurayrah).

 

 

Ni kweli kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala) Aliharamisha baadhi ya vitu vizuri kwa Mayahudi kama adhabu ya ukaidi wao na kuvuka mipaka iliyowekwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala). Lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala) Alipomtuma Mtume Wake wa mwisho na Akaikamilisha Dini kwa wanaadamu Aliwarehemu watu kwa kuondosha vikwazo hivyo. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:

"Anayewaamrisha mema na Anawakanya maovu, na Anawahalalishia vizuri, na Anawaharimishia viovu, na Anawaondolea mizigo yao na minyororo iliyo kuwa juu yao" (7: 157).

 

 

Kulingana na Uislamu vitu vinaharamishwa kwa sababu nyingi; ima kwa hekima, au bila hekima ikiwa ni sehemu ya mitihani na kupimwa viumbe utiifu wao, na kwa hekima mfano ni vichafu au vina madhara. Ikiwa kitu chochote kina madhara kinakuwa haramu; na kikiwa kina manufaa kinakuwa halali; na kikiwa madhara yake ni makubwa kuliko manufaa kitakuwa ni haramu; ilhali madhara yake yakiwa ni kidogo kuliko manufaa kinakuwa ni halali. Kanuni hii imeelezwa katika Qur-aan kuhusiana na pombe na kamari:

"Wanakuuliza juu ya ulevi na kamari. Sema: Katika hivyo zipo dhambi kubwa na manufaa kwa watu. Lakini dhambi zake ni kubwa zaidi kuliko manufaa yake" (2: 219).

Kwa mantiki hiyo hiyo, ikiwa itaulizwa, ni kitu gani ambacho ni halali katika Uislamu, jibu ni vitu vizuri. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:

"Wanakuuliza wamehalalishiwa nini? Sema: Mmehalalishiwa kila vilivyo vizuri" (5: 4).

 

 

Muislamu haitajiki kujua kwa uhakika uchafu au madhara ya Alivyoharamisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala); inaweza kuwa imefichikana naye au madhara yake hayajavumbuliwa. Kinachohitajika kwa Muislamu ni kusema: "Nimesikia na nimetii".

 

 

Lakini leo kwa hivi vitu ambavyo vimekatazwa upo uvumbuzi wa sayansi ambao unamyakinishia Muislamu hekima ya katazo hilo na kumuongezea yeye Imani.

 

 

Tukizama kwa makini tutaona ya kwamba Dini zote zimeharamisha nguruwe. Mfano tazama katika Biblia (Agano la Kale), Kitabu cha Walawi: "Na nguruwe msimle; ana kwato zilizogawanyika lakini hachuei; kwenu huyo ni najisi. Kwa sababu wanyama hao ni najisi msile nyama zao wala msiguse mizoga yao" (11: 7 - 8). Na katika Kitabu cha Isaya: "Mwenyezi Mungu asema hivi: 'Wapo watu waaojitakasa na kutawadha wapate kuingia katika bustani za ibada za sanamu; wanafanya maandamano na kahini akiwa kati yao. Watu hao hula nguruwe, panya na vyakula vingine haramu'" (66: 17).

Na katika agano jipya, Yesu anasema: "Msidhani kuwa nimekuja kutangua sheria na mafundisho ya manabii. Sikuja kutangua bali kukamilisha" (Mathayo 5: 17).

 

 

Na Qur-aan ipo wazi kabisa kuwa nyama ya nguruwe haifai kuliwa. Allaah Anasema:

"Yeye Amekuharimishieni mzoga tu na damu na nyama ya nguruwe na kilichotajiwa, katika kuchinjwa kwake, jina la asiyekuwa Mwenyezi Mungu" (2: 173).

 

 

Nguruwe pamoja na kuwa anakula vinyesi na vitu vichafu pia ina matatizo mengi ambayo watafiti wamegundua kuwa nguruwe hata akilishwa lishe safi, bado:

(i) Ni wanyama wachafu katika mambo mengine na nyama ya wanyama wachafu ikiliwa inamuathiri mlaji.

(ii) Nyama ya nguruwe ina mafuta mengi zaidi kuliko nyenzo za kujenga misuli.

(iii) Ina uwezakano wa kupata magonjwa kuliko aina nyengine yoyote ya nyama (Abdallah Yusuf Ali, The Holy Qur'an, Revised and edited by the Presidency of Islamic Researches, IFTA, Call and Guidance, uk. 69).

 

 

Athari ya madhara ya nyama hiyo sasa inajulikana vilivyo na kila mmoja. Asidi ya Uric, inapatikana kwa kila mnyama, na mwili wa mwanadamu pia ina nasibu yake, ambayo inatolewa nje ya mwili na mafigo kwa 90% ya asidi ya uric inatolewa kwa njia hii, lakini chemia ya nguruwe ni kuwa inatowa nje ya mwili 2% ya asidi yake ya uric pekee. Iliyobaki inabakia ndani ya mwili wake. Hii ni sababu ya kupatikana kwa kiwango kikubwa ugonjwa wa baridi yabisi (rheumatism) wa nguruwe na wale wenye kula nyama yake (Maulana Wahiduddin Khan, God Arises, uk. 209 – 210).

 

 

Dkt. Simpson ana haya ya kusema kuhusu nyama hiyo: "kwa sababu ya kuwa na mafuta mengi, nyama ya nguruwe ina tatizo kubwa kusagwa katika vyakula vyote. Mnyama huyo anaweza kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na lava wa Taenia solium hivyo kufanya "tegu (surua ya nguruwe)" na hii tegu inaleta aina ya tegu, T. solium. Inaathiriwa zaidi na Trichinella spiralis ambayo inaleta maradhi ya "Trichinosis" (Imenukuliwa na Yousef Saleem, Pork, A Bad Diet Prohibited by Islam, al-Islam, March/April, 1980, p. 29).

 

 

Trichinosis ni ugonjwa ambao unaletwa na kiinitete cha Trichinella spiralis wakati vinapohama kutoka kwa utumbo wa mwanadamu mpaka kwenye misuli. Katika wiki ya kwanza baada ya kuvamiwa mtu anaanza kutapika, kuhara na kusikia kichefuchefu. Ugonjwa unapoendelea inaleta matatizo ya kumeza, kuzungumza na kupumua.

 

 

Njia moja ya kuzuia ugonjwa ni kuipima nyama kwa tegu. Lakini Leavell na Clark wameandika: "Kwa vile cysts wa Trichinella ni wadogo sana kuonekana na macho, uchunguzi huo haufalii kitu. Wajerumani rasmi walikuwa wakifanya uchunguzi kwa hadubini kwa lengo hilo lakini ilikuwa ni ghali sana. Njia bora ya kuepukana na trichinosis ni kupika bidhaa za nguruwe barabara" (Imenukuliwa na Yousef Saleem, Pork, A Bad Diet Prohibited by Islam, al-Islam, March/April, 1980, p. 29).

 

 

Jambo jengine muhimu ni kuwa nguruwe ana shingo ndogo sana (kwa ndani, ingawa nje inaonekana pana), hivyo kuwa shida kuchinjwa. Hivyo, mwanzo anapigwa na chuma na baada ya kuzirai ndio anachinjwa. Hii ina matatizo kwa sababu Uislamu umeweka aina yake ya kuchinja ambayo inamfanya mnyama atoe kiwango kikubwa cha damu. Kama tunavyojua ni kuwa damu ni chombo cha kubeba viini vya ugonjwa na kemikali ambavyo vina madhara na hasa kwa mwanadamu. Kubakia ndani ya mnyama damu huenda kukaleta madhara makubwa kwa mlaji. Na kwa kuwa nguruwe hachinjwi kama wanyama wengine, damu nyingi hubakia ndani ya mwili badala ya kutoka nje.

 

 

Mwisho, nyama ya nguruwe ni chakula duni. Charles Annondale ameandika, "Nyama freshi ya nguruwe, japokuwa kwa wengine inachukuliwa kuwa chakula kitamu, hasa anapouliwa akiwa mchanga, ni lishe duni ukilinganisha na nyama ya ng'ombe au mbuzi na inatumika kwa uchache" (Imenukuliwa na Yousef Saleem, Pork, A Bad Diet Prohibited by Islam, al-Islam, March/April, 1980, p. 29).

 

 

Tunayopata katika maagizo na shari’ah ya Kiislamu kuhusu mbwa ni kuwa yeye ni najisi na pia ni haramu kuliwa. Hivyo, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuagizia kuwa ikiwa mbwa ataramba chombo chochote basi chombo hicho kioshwe mara saba moja wapo ikiwa ni kwa mchanga. Na utafiti wa sasa unaonyesha kuwa katika umaji maji wake vipo viini ambavyo ni hatari haviwezi kuuliwa wala kuondoshwa isipokuwa kwa mchanga, kwani mchanga una vitu ambavyo vinaua viini hivyo. Kwa kuwa maslahi ya mwanaadamu anayeyajua ni Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala). Na pia mbwa kama carnivorous (walaji nyama) wengine wanakula vitu vingi hivyo kuliwa na binadamu inamtoa katika ule ustaarabu na unaweza kumletea maradhi mengi kwa ajili ya hilo.

 

 

Wa Allaahu A'alam

 

Share