20-Wewe Pekee Tunakuabudu: Tawassul Zinazokubalika: Kutawassal Kwa Kutaja Hali Na Kutaja Sababu

 

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

Wewe Pekee Tunakuabudu Na Wewe Pekee Tunakuomba Msaada

 

Tawassul Zinazokubalika

 

20-Kutawasali Kwa Kutaja Hali Na Kutaja Sababu

 

 

 

 

Inafaa kutawassal kwa kutaja hali au sababu ya jambo unaloliombea du'aa. Ikiwa jambo unaloliomba ni kwa ajili ya manufaa ya dunia, basi  liwe ni jambo lenye kumridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na linalokubalika katika shariy’ah. 

 

Mifano mingi imo katika Qur-aan waliyoomba Manabii. Mifano michache ifuatayo:

 

Nabiy Nuwh ('Alayhis-Salaam):  

 

Aliomba nusra baada ya kushindwa kuwalingaia watu wake miaka mia tisa na khamsini. [Al-‘Ankabuwt 29: 14].

 

Katika Suwratul-Qamar Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:  

كَذَّبَتْ قَبْلَهُمْ قَوْمُ نُوحٍ فَكَذَّبُوا عَبْدَنَا وَقَالُوا مَجْنُونٌ وَازْدُجِرَ ﴿٩﴾

Walikadhibisha kabla yao kaumu ya Nuwh, wakamkadhibisha mja Wetu, wakasema: “Majnuni.” Na akakaripiwa. [Al-Qamar: 9]

  

Nabiy Nuwh ('Alayhis-Salaam) akaomba:

فَدَعَا رَبَّهُ أَنِّي مَغْلُوبٌ فَانتَصِرْ ﴿١٠﴾

Basi akamwita Rabb wake kwamba: “Hakika mimi nimeshindwa nguvu basi Nusuru.” [Al-Qamar: 10]

 

Hapo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akamtakabalia du’aa yake Akamuokoa Akawaangamiza madhalimu kama Anavyosema:

فَفَتَحْنَا أَبْوَابَ السَّمَاءِ بِمَاءٍ مُّنْهَمِرٍ ﴿١١﴾

Tukafungua milango ya mbingu kwa maji yanayofoka na kumiminika kwa nguvu.

 

وَفَجَّرْنَا الْأَرْضَ عُيُونًا فَالْتَقَى الْمَاءُ عَلَىٰ أَمْرٍ قَدْ قُدِرَ ﴿١٢﴾

Na Tukazibubujua ardhi chemchemu; basi yakakutana maji kwa amri iliyokwisha kadiriwa.

 

وَحَمَلْنَاهُ عَلَىٰ ذَاتِ أَلْوَاحٍ وَدُسُرٍ ﴿١٣﴾

Na Tukambeba kwenye ile (jahazi) yenye mbao na misumari.

 

تَجْرِي بِأَعْيُنِنَا جَزَاءً لِّمَن كَانَ كُفِرَ ﴿١٤﴾

Inatembea chini ya Macho Yetu, ni jazaa kwa yule aliyekuwa amekanushwa.

 

وَلَقَد تَّرَكْنَاهَا آيَةً فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ ﴿١٥﴾

Na kwa yakini Tumeiacha iwe ni Aayah (ishara, zingatio) je, basi yuko yeyote mwenye kuwaidhika?

 

فَكَيْفَ كَانَ عَذَابِي وَنُذُرِ ﴿١٦﴾

Basi vipi ilikuwa adhabu Yangu na maonyo Yangu? [Al-Qamar: 11-16]

 

 

Nabiy Ibraahiym ('Alayhis-Salaam):   

 

Alitaja hali yake ilivyo ya kuacha ahli yake baada ya kujenga Ka’bah, sehemu ambako kulikuwa bado hakuna mazao wala chochote. Akataja na sababu  ya kuomba Allaah Awaruzuku mazao ili watu waweze kuishi hapo na  kutekeleza ‘ibaadah na ili watu wapate kumshukuru Allaah (‘Azza wa Jalla). Akaomba:

 

رَّبَّنَا إِنِّي أَسْكَنتُ مِن ذُرِّيَّتِي بِوَادٍ غَيْرِ ذِي زَرْعٍ عِندَ بَيْتِكَ الْمُحَرَّمِ رَبَّنَا لِيُقِيمُوا الصَّلَاةَ فَاجْعَلْ أَفْئِدَةً مِّنَ النَّاسِ تَهْوِي إِلَيْهِمْ وَارْزُقْهُم مِّنَ الثَّمَرَاتِ لَعَلَّهُمْ يَشْكُرُونَ ﴿٣٧﴾

 “Rabb wetu! Hakika mimi nimewaweka baadhi ya dhuria wangu katika bonde lisilokuwa na mmea wowote, kwenye Nyumba Yako Tukufu. Rabb wetu, ili wasimamishe Swalaah na Ujaalie nyoyo za watu zielekee kwao na Uwaruzuku mazao ili wapate kushukuru.” [Ibraahiym: 37]

 

Aayah zinazofuatia baada ya hiyo zinaendelea kutaja du’aa ya Ibraahiym ('Alayhis-Salaam). [Ibraahiym: 38-41]

 

 

Nabiy Zakariyyaa ('Alayhis-Salaam):

 

Aliomba mtoto akiwa katika hali ya uzee na mkewe pia alikuwa tasa. Akataja kwanza mifupa kuwa dhaifu na nywele kugeuka mvi. Kisha akataja sababu kwamba alikhofu baada ya kufariki kwake kubakia kizazi kiovu, hivyo aliomba mtoto ili awe Nabiy baada yake atakayeongoza watu katika Dini. Imetajwa katika Qur-aan:

ذِكْرُ رَحْمَتِ رَبِّكَ عَبْدَهُ زَكَرِيَّا ﴿٢﴾

 (Huu ni) Ukumbusho wa rahmah ya Rabb wako kwa mja Wake Zakariyyaa.

 

إِذْ نَادَىٰ رَبَّهُ نِدَاءً خَفِيًّا ﴿٣﴾

Alipomwita Rabb wake mwito wa siri.

 

 

قَالَ رَبِّ إِنِّي وَهَنَ الْعَظْمُ مِنِّي وَاشْتَعَلَ الرَّأْسُ شَيْبًا وَلَمْ أَكُن بِدُعَائِكَ رَبِّ شَقِيًّا ﴿٤﴾

Akasema: “Rabb wangu! Hakika mimi mifupa imeninyong’onyea na kichwa kimeng’aa mvi, na wala sikuwa mwenye kunyimwa katika kukuomba du’aa, ee Rabb wangu.

 

وَإِنِّي خِفْتُ الْمَوَالِيَ مِن وَرَائِي وَكَانَتِ امْرَأَتِي عَاقِرًا فَهَبْ لِي مِن لَّدُنكَ وَلِيًّا ﴿٥﴾

 “Nami nakhofia jamaa zangu nyuma yangu, na mke wangu ni tasa. Basi Nitunukie kutoka kwako mrithi.”

 

يَرِثُنِي وَيَرِثُ مِنْ آلِ يَعْقُوبَ ۖ وَاجْعَلْهُ رَبِّ رَضِيًّا ﴿٦﴾

Anirithi na arithi kizazi cha Ya’quwb, na Mjaalie Rabb wangu awe mwenye kuridhisha”. [Maryam: 2-6]

 

Hapo Jibriyl ('Alayhis-Salaam) akamjia na kumbashiria mtoto:  

 

يَا زَكَرِيَّا إِنَّا نُبَشِّرُكَ بِغُلَامٍ اسْمُهُ يَحْيَىٰ لَمْ نَجْعَل لَّهُ مِن قَبْلُ سَمِيًّا ﴿٧﴾

 (Akaambiwa): “Ee Zakariyyaa! Hakika Sisi Tunakubashiria ghulamu jina lake Yahyaa, Hatukupata kabla kumpa jina hilo yeyote.” [Maryam: 7]

 

 

Nabiy Muwsaa ('Alayhis-Salaam):

 

Baada ya kumkimbia Fir’awn aliyetaka kumuua baada ya kufikwa na mtihani wa kumuua mtu bila ya kusudio mjini. Akakimbia hadi kufika mji wa Madyan akiwa amechoka, mwenye njaa hadi kufika kula majani njiani. Rejea Suwrah: Al-Qaswasw: (28: 15-21).

 

Alipofika mtoni ambako walikuweko watu wakichota maji, alikuta pembeni yake mabinti wawili wameakaa kando wakisubiri wachungaji Wanyama wachote maji kisha ndio wao wasogee kuchota. Endelea kurejea Al-Qaswasw (28: 22-23)

 

Nabiy Muwsaa ('Alayhis-Salaam) alipotambua kwamba mabinti hao hawakuwa na uwezo wa kuchota maji kwa sababu ya mzongano wa watu wanaochota maji,  aliwatekea maji kisha akakaa kivulini na akamwomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kwa kumtajia hali yake kuwa ni  mhitaji wa neema Zake. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

فَسَقَىٰ لَهُمَا ثُمَّ تَوَلَّىٰ إِلَى الظِّلِّ فَقَالَ رَبِّ إِنِّي لِمَا أَنزَلْتَ إِلَيَّ مِنْ خَيْرٍ فَقِيرٌ ﴿٢٤﴾

Basi akawanyweshea, kisha akageuka kwenda kivulini, akasema: “Rabb wangu! Hakika mimi ni mhitajia wa kheri yoyote Utakayoniteremshia.” [Al-Qaswasw 28: 24]

 

Hapo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akampa faraja na akaruzukiwa mke katika mmoja wa hao mabinti kama Anavyosema:

 

فَجَاءَتْهُ إِحْدَاهُمَا تَمْشِي عَلَى اسْتِحْيَاءٍ قَالَتْ إِنَّ أَبِي يَدْعُوكَ لِيَجْزِيَكَ أَجْرَ مَا سَقَيْتَ لَنَا ۚ فَلَمَّا جَاءَهُ وَقَصَّ عَلَيْهِ الْقَصَصَ قَالَ لَا تَخَفْ ۖ نَجَوْتَ مِنَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿٢٥﴾

Basi akamjia mmoja kati ya wanawake wawili akitembea kwa kuona hayaa; akasema: “Baba yangu anakwita ili akulipe ujira wa kutunyweshea.” Basi alipomfikia na akamsimulia visa vyake; alisema: “Usikhofu, umeokoka na watu madhalimu.”

 

قَالَتْ إِحْدَاهُمَا يَا أَبَتِ اسْتَأْجِرْهُ ۖ إِنَّ خَيْرَ مَنِ اسْتَأْجَرْتَ الْقَوِيُّ الْأَمِينُ ﴿٢٦﴾

Mmoja wao akasema: “Ee baba yangu, muajiri! Hakika mbora uwezaye kumwajiri ni mwenye nguvu mwaminifu.”

 

 

قَالَ إِنِّي أُرِيدُ أَنْ أُنكِحَكَ إِحْدَى ابْنَتَيَّ هَاتَيْنِ عَلَىٰ أَن تَأْجُرَنِي ثَمَانِيَ حِجَجٍ ۖ فَإِنْ أَتْمَمْتَ عَشْرًا فَمِنْ عِندِكَ ۖ وَمَا أُرِيدُ أَنْ أَشُقَّ عَلَيْكَ ۚ سَتَجِدُنِي إِن شَاءَ اللَّـهُ مِنَ الصَّالِحِينَ ﴿٢٧﴾

Akasema: “Mimi nataka nikuozeshe mmoja wapo wa binti zangu hawa wawili kwa sharti kuwa unitumikie miaka minane; ukitimiza kumi, basi ni kutoka kwako. Na wala sitaki kukutia mashakani; utanikuta In Shaa Allaah miongoni mwa Swalihina.”

 

قَالَ ذَٰلِكَ بَيْنِي وَبَيْنَكَ ۖ أَيَّمَا الْأَجَلَيْنِ قَضَيْتُ فَلَا عُدْوَانَ عَلَيَّ ۖ وَاللَّـهُ عَلَىٰ مَا نَقُولُ وَكِيلٌ ﴿٢٨﴾

 (Muwsaa) Akasema: “Hayo ni baina yangu na baina yako. Muda wowote kati ya miwili nitakaoutimiza basi hakuna uadui juu yangu. Na Allaah juu ya yale tunayoyasema ni Mdhamini.” [Al-Qaswasw: 25-28]

 

 

Na baada ya hapo ndipo alipofikia kuzungumza na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika bonde tukufu la Twuwaa, akajaaliwa kupewa Unabiy na kuwa Rasuli. Rejea Aayah zinazoendelea katika Suwrah hiyo ya Al-Qaswasw.

 

 

 

 

Share