24-Wewe Pekee Tunakuabudu: Tawassul Za Shirki Kufru Na Bid’ah: Kutawassal Kwa Waja Wema Waliofariki

 

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

Wewe Pekee TunakuabuduNa Wewe Pekee Tunakuomba Msaada

 

Tawassul Za Shirki, Kufru Na Bid’ah

 

24-Kutawassal Kwa Waja Wema Waliofariki

 

 

 

 

Haijuzu kutawasali kwa waja wema waliokwishafariki. Ingelikuwa inafaa kutawasali kwa waliofariki, basi ingelikuwa ni awlaa kutawassal kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na tumeshabainisha dalili yake katika makala iliyotangulia.

 

Kutawassal kwa asiyekuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni shirki bali ni kufru inayomtoa mtu nje ya Uislamu kwa dalili ya kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَمَن يَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ لَا بُرْهَانَ لَهُ بِهِ فَإِنَّمَا حِسَابُهُ عِندَ رَبِّهِ ۚ إِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الْكَافِرُونَ ﴿١١٧﴾

Na yeyote yule anayeomba du’aa (au kuabudu) pamoja na Allaah muabudiwa mwengine hana ushahidi wa wazi wa hilo; basi hakika hesabu yake iko kwa Rabb wake. Hakika hawafaulu makafiri. [Al-Muuminuwn: 11]

 

 

Miongoni mwa tawassul za shirki ya aina hii ni kuwaomba waja wema makaburini mwao kwa madai kuwa hawaabudiwi bali wanawakurubisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa sababu ya wema wao na hali Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anakusha hayo kama Anavyosema:

 

 وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ ۚ قُلْ أَتُنَبِّئُونَ اللَّـهَ بِمَا لَا يَعْلَمُ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ ۚ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ﴿١٨﴾

Na wanaabudu pasi na Allaah ambavyo haviwadhuru wala haviwanufaishi na wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.” Sema: “Je, mnamjulisha Allaah kwa yale Asiyoyajua katika mbingu na ardhini?” Subhaanah! (Utakasifu ni Wake) na Ametukuka kwa ‘Uluwa kwa yale yote wanayomshirikisha. [Yuwnus: 18]

 

Na Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ

na wale waliojichukulia badala Yake walinzi (wakisema): “Hatuwaabudu isipokuwa ili wapate kutukurubisha kwa Allaah tumkaribie” [Az-Zumar 39: 3]

 

Kisha hao waliokwishariki wala hawawezi kusikia wito au ombi la mtu wala hawawezi kumnufaisha mtu kwa lolote lile wala wao wenyewe hawana uwezo wa kujisaidia lolote lile. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

إِن تَدْعُوهُمْ لَا يَسْمَعُوا دُعَاءَكُمْ وَلَوْ سَمِعُوا مَا اسْتَجَابُوا لَكُمْ ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكْفُرُونَ بِشِرْكِكُمْ ۚ وَلَا يُنَبِّئُكَ مِثْلُ خَبِيرٍ ﴿١٤﴾

Mkiwaomba, hawasikii maombi yenu, na hata wakisikia, hawatakuitikieni.  Na Siku ya Qiyaamah watakanusha ushirikina wenu, na wala hakuna atakayekujulisha vilivyo kamaMwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [Faatwir: 14] 

 

Na pia Anasema Allaah ('Azza wa Jalla):

 

إِنَّ الَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ عِبَادٌ أَمْثَالُكُمْ ۖ فَادْعُوهُمْ فَلْيَسْتَجِيبُوا لَكُمْ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ﴿١٩٤﴾

Hakika wale mnaowaomba badala ya Allaah ni waja kama nyinyi. Hebu waiteni wakuitikieni ikiwa nyinyi ni wakweli. [Al-A’raaf: 194] 

 

Na Anasema pia Allaah ('Azza wa Jalla):

 

 إِنَّمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ أَوْثَانًا وَتَخْلُقُونَ إِفْكًا ۚ إِنَّ الَّذِينَ تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ لَا يَمْلِكُونَ لَكُمْ رِزْقًا فَابْتَغُوا عِندَ اللَّـهِ الرِّزْقَ وَاعْبُدُوهُ وَاشْكُرُوا لَهُ ۖ إِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿١٧﴾

 “Hakika mnaabudu badala ya Allaah masanamu, na mnaunda uzushi. Hakika wale mnaowaabudu badala ya Allaah hawakumilikiini riziki; basi tafuteni riziki kwa Allaah, na mwabuduni Yeye na mshukuruni, Kwake mtarejeshwa. [Al-‘Ankabuwt: 17]

 

Na Anasema pia Allaah ('Azza wa Jalla):

 

 وَمَنْ أَضَلُّ مِمَّن يَدْعُو مِن دُونِ اللَّـهِ مَن لَّا يَسْتَجِيبُ لَهُ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ وَهُمْ عَن دُعَائِهِمْ غَافِلُونَ﴿٥﴾

 “Na nani aliyepotoka zaidi kuliko ambaye anayeomba asiyekuwa Allaah ambaye hamuitikii mpaka Siku ya Qiyaamah; nao wala hawatambui  maombi yao.” [Al-Ahqaaf: 5]

 

Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَلَا تَدْعُ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَنفَعُكَ وَلَا يَضُرُّكَ ۖ فَإِن فَعَلْتَ فَإِنَّكَ إِذًا مِّنَ الظَّالِمِينَ﴿١٠٦﴾

Na wala usiombe badala ya Allaah visivyokufaa wala visivyokudhuru. Na ukifanya, basi hakika utakuwa miongoni mwa madhalimu.

 

 

وَإِن يَمْسَسْكَ اللَّـهُ بِضُرٍّ فَلَا كَاشِفَ لَهُ إِلَّا هُوَ ۖ وَإِن يُرِدْكَ بِخَيْرٍ فَلَا رَادَّ لِفَضْلِهِ ۚ يُصِيبُ بِهِ مَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ ۚوَهُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿١٠٧﴾

Na Allaah Akikugusisha dhara, basi hakuna wa kuiondosha isipokuwa Yeye. Na Akikutakia kheri, basi hakuna wa kurudisha fadhila Zake, Anasababisha kumfikia kwayo (fadhila Yake) Amtakaye katika waja Wake. Naye ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Yuwnus: 106-107]

 

Kwa hiyo hata kama mtu aliyefariki alikuwa ni mwema mno haifai kutawassal kwake kwani juu ya kuwa ni kufru na shirki, pia ni upotofu mkubwa. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

يَدْعُو مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُ وَمَا لَا يَنفَعُهُ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الضَّلَالُ الْبَعِيدُ ﴿١٢﴾

Humwomba badala ya Allaah ambavyo visivyomdhuru na wala visivyomnufaisha. Huo ndio upotofu wa mbali.

 

يَدْعُو لَمَن ضَرُّهُ أَقْرَبُ مِن نَّفْعِهِ ۚ لَبِئْسَ الْمَوْلَىٰ وَلَبِئْسَ الْعَشِيرُ ﴿١٣﴾

Humwomba yule ambaye dhara yake iko karibu kuliko manufaa yake. Bila shaka ni mlinzi muovu kabisa, na bila shaka ni rafiki muovu kabisa. [Al-Hajj: 12-13]

 

 

 

Share