Wakimbizi Kujiripua (Kukimbilia) Nchi Za Kigeni

 

SWALI:

ASALAM ALYKUM VIPI HALI ZENU ALHIDAAYA HAMJAMBOO? SAMAHANI MIMI NAULIZA MTU AMESHINDWA NA MAISHA NA PENGINE ANAWATOTO SASA AKAAMUA KWENDA LONDAN NA SI KWA NIA MBAYA  ANAMUABUDU ALLAAH KAMA KAWAIDA NA AKIFIKA KULE AKENDA KUJIRIPUA NA AKATUMIA NJIA YA KWANZA KUSEMA UONGO NA UONGO WENYEWE AKASEMA PENGINE ANATOKA NCHI ILIOKUA SIO YAKE  NA LAPILI AKIULIZWA MUME WAKO YUKO WAPI AKISEMA SIMJUI ALIPO, NA HALI UNAJUA YUKO WAPI SASA VIPI ANAPATA DHAMBI KWA YALE ANAYOFANYA,VILE VILE NA HALAFU ILE KITU HAPENDI LKN KWA MATATIZO INABIDI AFANYE  NA HALAFU KATIA NIA KWAMBA NI KWA MUDA TU HALI IKIJIRUDI NA YEYE ANARUDI NAOMBA JIBU HARAKA SAAAAAAAAAAAAAANA NA ILE PESA ANAYOPEWA NI YA HALALI ?.

 


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukran ndugu yetu kwa swali lako hili na kwa hakika swali kama hili tayari tumelijibu kabla, lakini hapana ubaya kulielezea tena. Uislamu ni Dini iliyohimiza na kusisitiza sana kuhusu mas-ala ya ukweli. Zipo fadhila kubwa sana kwa mwenye kuwa na maadili kama hayo. Na yeyote asiyekuwa na tabia hiyo basi anaingia katika unafiki moja kwa moja. Unafiki ambao utampeleka mahali pabaya hapa duniani na kesho Akhera 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Enyi mlioamini! Mcheni Allaah, na kuweni pamoja na wakweli” (9: 119). Amesema tena Aliyetukuka, “Na wasemao kweli wanaume na wanawake” (33: 35). Na ayah katika mas-ala haya ni nyingi sana 

Na Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuhimiza sana kuwa wakweli kwa kutuambia: “Hakika ukweli unamuongoza mtu katika wema na wema unampeleka mtu Peponi. Na hakika mtu huendelea kusema ukweli mpaka akaitwa mkweli mbele ya Allaah. Na hakika uwongo inampeleka mtu katika uchafu na uchafu unampeleka mtu Motoni. Na mtu huendelea kusema uwongo mpaka akaandikwa kuwa ni muongo mbele ya Allaah” (Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud na at-Tirmidhiy).

 Amesema tena: “Nimehifadhi kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ‘Acha lenye kukutia shaka kwa lisilokutia shaka. Hakika ukweli ni utulivu na uwongo unakera” (At-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy na Ahmad na Isnadi yake ni Sahihi).

Na kauli ya Abu Sufyaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwa Hiraql kumuelezea sifa za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Muabuduni Allaah peke yake wala musimshirikishe Yeye na chochote na muache wanayosema wazazi wenu na anatuamuru kusimamisha Swalah na kusema ukweli, kuwa watahirifu na kuunganisha kizazi (kwa kuwasaidia majamaa)” (Ahmad, al-Bukhari na Muslim).

Uwongo una madhara mengi kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Makosa yote yanaweza kupatikana kwa Muumini ila ukosefu wa uaminifu na uongo” (Imaam Ahmad). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa: “Je, Muumini anaweza kuwa muoga?” Akasema: “Ndio”. Akaulizwa tena: “Je, Muumini anaweza kuwa bakhili?” Akajibu: “Ndio”. Akaulizwa tena: “Je, Muumini anaweza kuwa muongo?” Akasema: “Hapana (haiwezekani)” (Imaam Maalik).

Anatuelezea tena Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Watu aina tatu hawawezi kabisa kuingia Peponi. Mzee mkongwe mzinzi, mtu anayesema uwongo na masikini mwenye kiburi” (Al-Bazzaar). Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) ameripoti kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Yeyote anayemuita mtoto akimwambia kuwa atampatia kitu na asimpatie, basi amesema uwongo” (Imaam Ahmad). Anasema tena: “Muumini hawezi kuwa na Imani kamili mpaka aache uwongo katika dhihaka na mijadala japokuwa katika mambo mengine yote” (Imaam Ahmad).

Ibn Mas‘uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) anaripoti kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mtu anaendelea kusema uwongo mpaka doa jeusi linawekwa katika moyo wake na pole pole linaendelea kukua mpaka moyo wote unakuwa mweusi. Wakati huo jina lake linaingizwa katika orodha ya waongo mbele ya Allaah” (Imaam Maalik). Nasi tukiwa tunamuiga Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ambaye ni kielelezo kwetu inatakiwa tuwe na sifa hii ya ukweli katika hali zote na katika hilo Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atatutatulia matatizo na shida zetu kwa njia iliyo nzuri zaidi.

Uislamu umehimiza ukweli na uwongo unampeleka mtu pabaya hapa duniani na kesho Akhera. Hapa duniani ni kuingia mwanzo katika matatizo pamoja na serikali za nchi munazoishi. Mfano ni yule mwanamke wa Kisomali huko Holland mbali na kuwa alikuwa mbunge na kuushambulia Uislamu ilibidi ajiuzulu katika wadhifa wake wa ubunge na hata alikuwa atolewe nchini kwa sababu ya uwongo.

Ikiwa unasema katia nia ya kujirudi pindi hali itakapokuwa sawa sawa, je ikiwa hali haikubadilika? Au amekufa kabla y hali kubadilika kama alivyotarajia? Hakika ni kuwa sisi hatuna dhamana ya uhai wetu wala maisha, huenda tukafariki wakati wowote. Je, ikitokea hivyo tutamlaumu nani? Tuwe wakweli katika hali zote na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atatubariki katika mambo yetu.

Hivyo hakuna kipengele cha wewe kusema uwongo katika mas-ala hayo. Sema ukweli na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atakutolea njia nyengine za riziki. Kwani Yeye Amesema: “Na anayemcha Allaah humtengezea njia ya kutokea. Na Humruzuku kwa njia asiyotazamia. Na anayemtegemea Allaah Yeye Humtosha. Hakika Allaah Anatimiza amri Yake. Allaah Kajaalia kila kitu na kipimo chake

(65: 2 – 3).

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share