32-Wewe Pekee Tunakuabudu: Tawassul Za Shirki Kufru Na Bid’ah: Kutawassal Kwa Vitu Vitukufu Vya Allaah

 

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

Wewe Pekee Tunakuabudu Na Wewe Pekee Tunakuomba Msaada

 

Tawassul Za Shirki Kufru Na Bid’ah

 

32- Kutawassal Kwa Vitu Vitukufu Vya Allaah.

 

 

 

 

Kutawassal kwa kutafuta baraka katika vitu vitukufu vya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kuvifanya au kudhania kuwa ni sababu ya kutakabaliwa mtu du’aa yake haijuzu katika Shariy’ah kwa kuwa inaingia katika shirki.

 

Mfano ni kugusa Msahafu kisha kuomba du’aa au kugusa kuta za Misikiti mitukufu; Masjidul-Haraam au Masjidun-Nabawiy au Ka’bah, au Hajar Al-Aswad  au pia hata kaburi la Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) au kusugulia nguo katika kuta za vitukufu hivyo kisha kujipangusia navyo usoni au mwilini.  

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipofika Makkah kufanya twawaaf hakuashiria kuwa mtu akamate Ka’bah au Ruknul-Yamaani, au Hajar Al-Aswad (jiwe jeusi) kisha ajipangusie nalo kupata baraka zake.

 

Alilofanya ni kulibusu tu Hajar Al-Aswad, na ndio maana ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu 'anhu) alipolifikia na kulibusu alisema:

 

"إِنِّي أَعْلَمُ أَنَّكَ حَجَرٌ لاَ تَضُرُّ وَلاَ تَنْفَعُ وَلَوْلاَ أَنِّي رَأَيْتُ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يُقَبِّلُكَ مَا قَبَّلْتُكَ"

“Hakika mimi natambua kwamba wewe ni jiwe tu, hudhuru wala hunufaishi. Na lau nisingelimuona Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  anakubusu, nisingelikubusu.” [ Al-Bukhaariy, Ibn Maajah na Ahmad]

 

Na ilipomfikia khabari kwamba watu wanapofika Hudaybiyyah katika mti ambao tukio la bay’ah (fungamano) lilitokea chini yake, walikuwa wakiugusa na kuswali hapo n.k., basi aliukatilia mbali kukhofia watu wasiingie katika shirki. [Al-Haafidhw Ibn Hajar fiy Al-Fat-h (7/448)]

 

Pia, Maswahaba walipokuwa wanakwenda vitani, walitaka kuweka silaha zao katika mti kama kutawassal watakabaliwe kupata ushindi. Hawakujua kwamba ni jambo linalowaingiza katika kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).  Hadiyth ifuatayo inaeleza zaidi:    

 

عن أَبِي وَاقٍد اللَّيْثِيِّ (رضي الله عنه) قَالَ: خَرَجْنَا مَعَ النَّبِيِّ (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وآله وَسَلَّمَ) إِلَى حُنَيْنٍ وَنَحْنُ حُدَثَاءُ عَهْدٍ بِكُفْرٍ، وَلِلِمُشْرِكِينَ سِدْرَةٌ، يَعْكُفُونَ عِنْدَهَا وَيُنَوِّطُونَ بِهَا أَسْلِحَتَهُمْ، يُقَالَ لَهَا ذَاتُ أَنْوَاطٍ، فَمَرَرْنَا بِسِدْرَةٍ فَقُلْنَا: يَا رَسُولَ اللهِ اجْعَلْ لَنَا ذَاتَ أَنْوَاطٍ كَمَا لَهُمْ ذَاتُ أَنْوَاط. فَقَالَ النَّبِيُّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم):َ((الله أكبر! هَذَا كَمَا قَالَ قَوْمُ مُوسَى "اجْعَلْ لَنَا إِلَهًا كَمَا لَهُمْ آلِهَةٌ" وَالَّذِي نَفْسِي بِيَدِهِ لَتَرْكَبُنَّ سُنَّةَ مَنْ كَانَ قَبْلَكُمْ))

Imepokewa kutoka kwa Abu Waaqid Al-Laythiyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: “Tulitoka pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwenda (vitani) Hunayn nasi ndio kwanza tumetoka katika ukafiri, na washirikina walikuwa na mkunazi wanaufanyia ‘ibaadah na walikuwa wakitundika silaha zao (kupata baraka). Wakiuita ‘Dhaatu Anwaatw’. Tukapita mbele ya mkunazi tukasema: “Ee Rasuli wa Allaah, tufanyie nasi Dhaata Anwaatw kama walivyokuwa nao (makafiri) Dhaatu Anwaatw.” Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Allaahu Akbar!  (Allaah ni Mkubwa!) Hivi ni kama walivyosema watu wa Muwsaa “Tufanyie nasi muabudiwa kama walivyokuwa nao muabudiwa.” Naapa kwa Ambaye nafsi yangu imo Mikononi Mwake, mtafuata nyendo za walio kabla yenu [za ujahili na kufru].)) [At-Tirmidhiy; Swahiyh At-Tirmidhiy (2180)]

 

Kwa hiyo tawassul kama hizo hazijuzu kabisa.

 

 

 

Share