022-Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake أسماء الله الحسنى وصفاته: AL-KHAALIQ, AL-KHALLAAQ

 

أسماء الله الحسنى وصفاته

Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake

 

Alhidaaya.com

 

 

الْخالِقُ-الْخَلاَّق

 

AL-KHAALIQ

AL-KHALLAAQ

 

 

 

Al-Khaaliq: Muumbaji.

 

Al-Khallaaq: Mwingi wa kuumba Atakavyo

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

هُوَ اللَّـهُ الْخَالِقُ الْبَارِئُ الْمُصَوِّرُ ۖ  

Yeye Ndiye Allaah, Muumbaji, Mwanzishi viumbe bila kasoro, Muundaji sura na umbile. [Al-Hashr: 24]

 

Al-Khaaliq au Al-Khallaaq maana yake ni kukiunda kitu kisichokuwa na mfano wake hapo kabla. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ ثُمَّ جَعَلَ مِنْهَا زَوْجَهَا وَأَنزَلَ لَكُم مِّنَ الْأَنْعَامِ ثَمَانِيَةَ أَزْوَاجٍ ۚ يَخْلُقُكُمْ فِي بُطُونِ أُمَّهَاتِكُمْ خَلْقًا مِّن بَعْدِ خَلْقٍ فِي ظُلُمَاتٍ ثَلَاثٍ ۚ  

Amekuumbeni kutokana na nafsi moja, kisha Akamfanya humo mkewe na Akakuteremshieni katika wanyama wa mifugo jozi nane. Anakuumbeni matumboni mwa mama zenu umbo baada ya umbo, katika viza vitatu.  [Az-Zumar: 6]

 

Yaani; Amekuumbeni tone, kisha kipande cha nyama, kisha mfupa kama Anavyosema pia:

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن سُلَالَةٍ مِّن طِينٍ ﴿١٢﴾

Kwa yakini Tumemuumba insani kutokana na mchujo safi wa udongo.

 

ثُمَّ جَعَلْنَاهُ نُطْفَةً فِي قَرَارٍ مَّكِينٍ ﴿١٣﴾

Kisha Tukamjaalia kuwa tone la manii katika kalio makini.

 

ثُمَّ خَلَقْنَا النُّطْفَةَ عَلَقَةً فَخَلَقْنَا الْعَلَقَةَ مُضْغَةً فَخَلَقْنَا الْمُضْغَةَ عِظَامًا فَكَسَوْنَا الْعِظَامَ لَحْمًا ثُمَّ أَنشَأْنَاهُ خَلْقًا آخَرَ ۚ فَتَبَارَكَ اللَّـهُ أَحْسَنُ الْخَالِقِينَ ﴿١٤﴾

Kisha Tukaumba tone la manii kuwa pande la damu linaloning’inia, Tukaumba pande la damu hilo linaloning’inia kuwa kinofu cha nyama, Tukaumba kinofu cha nyama hiyo kuwa mifupa, Tukavisha mifupa hiyo nyama, kisha Tukamuanzisha kiumbe kingine. Basi Tabaaraka-Allaah, Amebarikika Allaah Mbora wa wenye kuumba. [Al-Muuminuwn: 12-14]

 

 

Na maana ya pili ni kukikadiria kitu na kukinyoosha. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

إِنَّمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ أَوْثَانًا وَتَخْلُقُونَ إِفْكًا ۚ  

“Hakika mnaabudu badala ya Allaah masanamu, na mnaunda uzushi. [Al-‘Ankabuwt: 17]

 

 

Yaani mnakadiria na kutayarisha, nayo ni uongo, kama ilivyo kauli yake Ta’aalaa:

مَا سَمِعْنَا بِهَـٰذَا فِي الْمِلَّةِ الْآخِرَةِ إِنْ هَـٰذَا إِلَّا اخْتِلَاقٌ ﴿٧﴾

“Hatukusikia haya katika mila ya mwisho, haya si chochote isipokuwa ni jambo lilozushwa tu.  [Swaad: 7]

 

 

Tofauti kati ya Al-Khaaliq na Al-Khallaaq:

 

Al-Khaaliq ni Ambaye Anakiunda kitu ambacho hakikuwepo.

 

Al-Khallaaq ni Ambaye Anayeumba  kwa kwingi zaidi,  na uumbaji Wake wa  aina mbali mbali. Anaumba Atakavyo, Apendavyo Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

إِنَّ رَبَّكَ هُوَ الْخَلَّاقُ الْعَلِيمُ ﴿٨٦﴾

Hakika Rabb wako Ndiye Mwingi wa kuumba Atakavyo, Mjuzi wa yote. [Al-Hijr: 86]

 

  يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ ۚ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴿١٧﴾

Anaumba Atakacho. Na Allaah juu ya kila kitu ni Muweza. [Al-Maaidah: 17]

Na Anasema pia:

 

ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمْ ۖ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ فَاعْبُدُوهُ ۚ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ وَكِيلٌ ﴿١٠٢﴾

Huyo kwenu Ndiye Allaah, Rabb wenu. Hapana muabudiwa wa haki ila Yeye Muumbaji wa kila kitu, basi mwabuduni Yeye Pekee. Naye juu ya kila kitu ni Mdhamini Anayetegemewa kwa yote.  [Al-An’aam: 102]

 

 

Al-Khaaliq Anathibitisha Mwenyewe (‘Azza wa Jalla) Tawhiyd ya Ar-Rubuwbiyyah, kwamba Yeye Ndiye Muumbaji, basi je, wale mapagani (Wanaokanusha kuweko kwa Allaah, Al-Khaaliq) wanalo la kujibu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anaposema?

أَمْ خُلِقُوا مِنْ غَيْرِ شَيْءٍ أَمْ هُمُ الْخَالِقُونَ ﴿٣٥﴾

Au wameumbwa pasipo na kitu chochote au wao ndio waumbaji?

 

أَمْ خَلَقُوا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۚ بَل لَّا يُوقِنُونَ ﴿٣٦﴾

Au wameumba mbingu na ardhi? Bali hawana yakini. [Atw-Tuwr: 35-36]

 

 

Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah; Al-Khaaliq, Al-Khallaaq:

 

1. Tafakari uumbaji wa Allaah na jinsi uumbaji Wake ulivyokuwa hauna kasoro. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

الَّذِي خَلَقَ سَبْعَ سَمَاوَاتٍ طِبَاقًا ۖ مَّا تَرَىٰ فِي خَلْقِ الرَّحْمَـٰنِ مِن تَفَاوُتٍ ۖ فَارْجِعِ الْبَصَرَ هَلْ تَرَىٰ مِن فُطُورٍ﴿٣﴾

Ambaye Ameumba mbingu saba matabaka, hutoona katika uumbaji wa Ar-Rahmaan tofauti yoyote. Basi rejesha jicho je, unaona mpasuko wowote ule?

 

ثُمَّ ارْجِعِ الْبَصَرَ كَرَّتَيْنِ يَنقَلِبْ إِلَيْكَ الْبَصَرُ خَاسِئًا وَهُوَ حَسِيرٌ ﴿٤﴾

Kisha rejesha jicho tena na tena litakupindukia jicho likiwa limehizika na lenye kunyong’onyezwa.  [Al-Mulk 3-4]

 

 

2. Kuwa miongoni mwa wenye kumshukuru na kumwabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kutafakari uumbaji Wake. Hii ni aina ya ‘ibaadah iliyo nzito kwa thawabu mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na  ambayo ni dalili ya kuamini Tawhiyd ya Rubuwbiyyah, na kwamba Allaah (‘Azza wa Jalla) Hakuumba Alivyoviumba kuwa ni bure bila ya lengo! Ametaja Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) hayo katika Suwrah na Aayah kadhaa, miongoni mwazo ni Aayah za mwisho katika Suwratul-‘Imraan ambazo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliamka usiku mmoja akaswali tahajjud kisha akalia mpaka ndevu zake zikarowa, kisha akasujudu na kulia mpaka akaifanya ardhi irowe, kisha akalala kwa upande wa kulia mpaka akaja Bilaal, akamuuliza: “Ee Rasuli wa Allaah  jambo gani linakuliza na hali Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amekwishakufutia madhambi yako yaliyotangulia na yanayokuja?” Akasema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Je, nisiwe mja anayeshukuru? Nimeteremshiwa Aayah… Ole wake, yule anayezisoma lakini hazitafakari…

 

إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لَآيَاتٍ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ ﴿١٩٠﴾ 

Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi, na mabadiliko ya mfuatano wa usiku na mchana; bila shaka ni Aayaat kwa wenye akili.

 

الَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِهِمْ وَيَتَفَكَّرُونَ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَـٰذَا بَاطِلًا سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ ﴿١٩١﴾ 

Ambao wanamdhukuru Allaah kwa kusimama, na kwa kukaa na kwa kulala ubavuni mwao na wanatafakari katika kuumbwa mbingu na ardhi (wakisema): “Rabb wetu, Hukuumba haya bure, Subhaanak! Utakasifu ni Wako, tukinge na adhabu ya moto

[Aal-‘Imraan: 190 – mpaka 199 – Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa - Taz. As-Silsilah Asw-Swahiyhah (1/147), Swahiyh At-Targhiyb (1468)]

 

3. Tafakari uumbaji wa Al-Khallaaq Anayeumba Atakavyo; tafakari kwanza viumbe wasioonekana kwetu kama Malaika na majini. Kisha tafakari uumbaji wa wana Aadam jinsi tunavyotofautiana umbo, rangi na wingi wetu ulimwenguni. Kisha tafakari  viumbe vingapi vipya vipya vinagundulikana? Tafakari aina za wanyama wa nchi kavu unapoishi na mbali walioko katika majangwa na misitu ya ulimwengu mzima! Mfano mzuri mwengine wa kutafakari ni pale mpiga mbizi baharini anapokutana huko na aina mbali mbali za samaki wa kila rangi na kila maumbile. Pia angalia mabilioni yaliyoumbwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa aina mbali mbali na sura za kila aina katika wanyama, wadudu, ndege, samaki, miti, na viumbe vinginevyo tusivyoviona au kuvijua, lakini Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anavijua vilivyo kwani Anasema:

أَلَا يَعْلَمُ مَنْ خَلَقَ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ﴿١٤﴾

Kwani Hajui Yule Aliyeumba! Na hali Yeye ni Mwenye kudabiri mambo kwa ulatifu, Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [Al-Mulk 14]

 

4. Weka Iymaan thabiti moyoni kuhusu Tawhiyd ya Allaah na kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Hafanani na kiumbe chochote na wala Yeye Hakuumbwa. Basi tahadhari na shaytwaan asikutie wasiwasi kuhusu hilo, imetahadharishwa katika Hadiyth:

 

عن أبي هُرَيْرَةَ ـ رضى الله عنه قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: ((يَأْتِي الشَّيْطَانُ أَحَدَكُمْ فَيَقُولُ: مَنْ خَلَقَ كَذَا، مَنْ خَلَقَ كَذَا، حَتَّى يَقُولَ: مَنْ خَلَقَ رَبَّكَ، فَإِذَا بَلَغَهُ فَلْيَسْتَعِذْ بِاللَّهِ، وَلْيَنْتَهِ))

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Shaytwaan humjia mmoja wenu aseme: “Nani ameumba kadhaa, nani ameumba kadhaa, mpaka mwisho husema: Nani amemuumba Rabb wako? Basi itakapofika hivyo, ajikinge kwa Allaah na aachilie mbali [mawazo hayo])) [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

5. Mshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kukuumba ukiwa umekamilika viungo na uvitolee swadaqah kwa kuswali rakaa mbili za Adhw-Dhwuhaa.

 

عن أبي ذَرٍّ رضي الله ُ عنه، عن النـَبي ِّ صلـَّى الله عليه وسلم قال: ((يـُصـْبـِحُ عـَلى كـُلِّ سـُلامى مـِنْ أحـَدِكـُمْ صـَدَقةُ: فـَكُل تـَسْبـِيحـَةِ صـَدَقةٌ، وَ كُل تـَحمِيدة صـَدَقةٌ، وكُلُ تـَهْـليْلةٌ صـَدَقـَةٌ، وكُلُّ تـَكْبِيْرةِ صـَدقةٌ، وأمرٌ بالمـَعرُوف صـَدقةٌ، ونـَهىٌ عـَنِ المـُنْكرِ صـَدقةٌ ويـُجْزئ مـِنْ ذلكَ رَكـْعتـَانِ يـَركَعُهُما مـنَ الضـُّحى)) رواه مسلم

 

Kutoka kwa Abuu Dharr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) amesema: ((Kila kiungo katika mwili wenu hupambaukiwa kikihitaji kutolewa swadaqah, kwa hiyo kila tasbiyh - Subhaana-Allaah ni swadaqah, na kila tahmiyd - AlhamduliLLaah ni swadaqah, na kila tahliyl - La Ilaaha Illa Allaah ni swadaqa  na kila takbiyr - Allaahu Akbar ni swadaqah, na kuamrisha mema ni swadaqah na kukataza maovu ni swadaqah na itamtosheleza (mtu) kwa rakaa mbili za Dhwuhaa)) [Muslim]

 

6. Msabbih Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kila mara kwani ni haki Yake kumsabbih kwa kuwa Ndiye Aliyetuumba. Anasema:

سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الْأَعْلَى ﴿١﴾

Sabbih Jina la Rabb wako Mwenye ‘Uluwa Ametukuka kabisa kuliko vyote.

 

الَّذِي خَلَقَ فَسَوَّىٰ ﴿٢﴾

Ambaye Ameumba (kila kitu) kisha Akasawazisha. [Al-A’laa: 1-2]

 

7. Usijfanye wewe muumbaji, nayo ni kuchora viumbe, au kutundika picha za viumbe, kwa sababu ukifanya hivyo utakuwa miongoni mwa watu waovu kabisa Siku ya Qiyaamah na adhabu zake ni kali mno!

 

عَنْ عَائِشَةَ (رَضِيَ اللهُ عَنْهَا) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم) قَال: ((أَشَدُّ النَّاسِ عَذَابًا يَوْمَ القِيَامَةِ الَّذِينَ يُضَاهِئُونَ بِخَلْقِ اللَّهِ))

Imepokelewa kutoka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Watakaokuwa na adhabu kali Siku ya Qiyaamah ni wanaomuiga Allaah katika uumbaji Wake)) [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما): سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) يَقُولُ: ((كُلُّ مُصَوِّرٍ فِي النَّارِ يُجْعَلُ لَهُ بِكُلِّ صُورَةٍ صَوَّرَهَا نَفْسٌ يُعَذَّبُ بِهَا فِي جَهَنَّمَ))

Imepokelewa  kutoka kwa Ibn ‘Abbaas  (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwamba: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Kila mchoraji picha atakuwa motoni. Kila picha aliyoichora, itatiwa roho nayo itamuadhibu katika Jahannam)) [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

8. Tafakari kuwa tunaomba du’aa zinazotaja uumbaji katika nyiradi za kulala na asubuhi na jioni. Tunapolala tunatakiwa tuombe:

 

اللّهُـمَّ إِنَّـكَ خَلَـقْتَ نَفْسـي وَأَنْـتَ تَوَفّـاهـا لَكَ ممَـاتـها وَمَحْـياها، إِنْ أَحْيَيْـتَها فاحْفَظْـها، وَإِنْ أَمَتَّـها فَاغْفِـرْ لَـها. اللّهُـمَّ إِنَّـي أَسْـأَلُـكَ العـافِـيَة

Allaahumma Innaka Khalaqta nafsiy wa Anta Tawaffahaa. Laka mamaatuhaa wamahyaahaa. In-Ahyaytahaa fahfadhw-haa wain amattahaa faghfir lahaa. Allaahumma inniy as-alukal ‘aafiyah.

 

Ee Allaah, hakika Wewe Umeiumba nafsi yangu Nawe Utaifisha. Ni Wewe Unaumiliki umauti wake na uhai wake. Ukiipa uhai basi Ihifadhi, na Ukiifisha basi Ighufurie. Ee Allaah, hakika mimi nakuomba Al-‘Aafiyah

[Hadiyth ya ‘Abdullaah bin ‘Umar  (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) - Muslim (4/2083) [2712], na Ahmad kwa tamshi lake (2/79)]

 

Al-‘Aafiyah ni neno linalojumuisha  Allaah (عزّ وجلّ)  kumjaalia mja Wake salama na kumpa amani, na kumlinda na maradhi, balaa, majanga, madhara, misukosuko, na kila aina za shari za wanaadam na majini na kubakia salama katika Dini yake na Aakhirah yake.

 

 

9. Tafakari kuwa baadhi ya viumbe Alivyoviumba Allaah (’Azza wa Jalla) ni viumbe vyenye shari na hivyo tunaomba kujikinga navyo tunaposoma:

 

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ ﴿١﴾

Sema: “Najikinga na Rabb wa mapambazuko.

 

مِن شَرِّ مَا خَلَقَ ﴿٢﴾

Kutokana na shari ya Alivyoviumba.  [Al-Falaq: 1-2]

 

 

Na pia du’aa katika nyiradi za asubuhi na jioni:

 

أَعُوْذُ بِكَلِماتِ اللَّهِ التَّامَّتِ مِنْ شَرِّ مَا خَلَقَ

A’uwdhu bikalimaatiLLaahit-ttaammati minsharri maa khalaq (mara 3 jioni na asubuhi).

 

Najikinga kwa maneno ya Allaah yaliyotimia kutokana na shari Aliyoiumba.

 

[Hadiyth ya Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) - Ahmad (2/290), An-Nasaaiy katika ‘Amal Al-Yawm wal-Laylah [590], Ibn As-Sunniy [68]. Angalia: Swahiyh At-Tirmidhiy (3/187), Swahiyh Ibn Maajah (92/266), Tuhfat Al-Akhyaar  (uk.. 45). Na Taz.  katika   Swahiyh Al-Jaami’ [6427]. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayesema mara tatu jioni hatodhuriwa na mdudu wa sumu usiku huo).

 

 

 

Share