Imaam Ameswalisha Kwa Kuketi, Je, Nami Niswali Naye Kwa Kuketi?

 

Imaam Ameswalisha Kwa Kuketi, Je, Nami Niswali Naye Kwa Kuketi?

www.alhidaaya.com

 

  

SWALI:

  

Aassalamu aleikum, kwanza kabisa nina mshukuru Allah kwa kila jambo thumma ninawashukuru wote waliojitahidi na kutuwekea ukumbi huu wa maswali na majibu kwa kiswahili ili tuweze kupata faida zaidi na kwa urahisi, asanteni sana. Swali langu ni hili: kuna wakati niliingia msikitini baada ya jamaa kuisha nikampata mzee wa umri mkubwa sana, anasimamisha sala ili asali, nikaja ubavuni mwake kuliani ili nisali nae, tulipo maliza sajda ya kwanza, imam kwa vile ni mzee sana hakusimama,aliendelea kusalisha hali yakuwa ameketi,mimi kwavile ni mara yangu ya kwanza kunitokea jambo kama hilo, sikujua la kufanya, nikawa nimebabaika sijui nisimame wakati imam ameketi au niketi kama yeye, na kwavile imam pia hajaniambia lolote baada ya kumaliza sala na hali ya kuwa mimi pia nimemaliza kwa kuketi kama yeye, na sikupenda kumuuliza kama ni sawa nilivyo fanya, nikishuku yeye pia hajui kama ni sawa au laa. Jee usawa ni vipi? Nifahamisheni JAZAKUM ALLAH KHEIR,

Ndugu yenu 

 

 

 

JIBU 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Wa ‘alaykumus-salaam wa RahmatuLLaahi wa Barakaatuh.

 

Katika mas-ala haya tayari Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa aalihi wa sallam) ametupatia muongozo wake, kwani yeye kuhusu Swalaah anasema: “Swalini kama mulivyoniona mimi nikiswali” [al-Bukhaariy].

 

Imaam yuko mbele ili afuatwe na haifai mtu kumtangulia Imaam. Nabiy (Swalla Llaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:Hakika Imaam amewekwa ili afuatwe” [Ahmad na Abu Dawuud].

 

Lakini hii ni Hadiyth ambayo ina maana ya kijumla.

 

Katika Hadiyth ambayo inalenga swali lako ni ile ya kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Rasuli wa Allah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika Imaam amewekwa ili kufuatwa, hivyo msimtangulie. Anapotoa takbira nanyi leteni takbira, anaporukuu nanyi nendeni katika rukuu na anaposema “Sami‘a Allaahu liman hamidah”, semeni: “Rabbaana Lakal Hamd.” Na anaposujudu nanyi sujuduni na anaposwali akiwa amekaa basi nanyi nyote swalini kwa kuketi” [al-Bukhaariy na Muslim]. Kwa hiyo ulivyofanya kwa kuswali nyuma ya mzee ukiwa umekaa ni sawa kwa mujibu wa Sunnah.

 

Na Allah Anajua zaidi.

 

Share