06-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Twahaarah: Mlango Wa Kubatilika Wudhuu

بُلُوغُ الْمَرام

Buluwgh Al-Maraam

 

كِتابُ الطَّهارَة

Kitabu Cha Twahaarah

 

بَابُ نَوَاقِضِ اَلْوُضُوءِ

06-Mlango Wa Kubatilika[1] Wudhuu

 

 

 

 

61.

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ ‏ رضى الله عنه ‏ قَالَ: {كَانَ أَصْحَابُ رَسُولِ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏‏عَلَى عَهْدِهِ‏ يَنْتَظِرُونَ اَلْعِشَاءَ حَتَّى تَخْفِقَ رُؤُوسُهُمْ، ثُمَّ يُصَلُّونَ وَلَا يَتَوَضَّئُونَ} أَخْرَجَهُ أَبُو دَاوُدَ، وَصَحَّحَهُ اَلدَّارَقُطْنِيُّ

وَأَصْلُهُ فِي مُسْلِمٍ

Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Maswahaba wa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ), katika zama zake (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) walikuwa wakingojea Swalaah ya ‘Ishaa hadi wanainamisha chini vichwa vyao (kwa kusinzia)[2], kisha wanaswali bila kutawadha upya[3].” [Imetolewa na Abuu Daawuwd na akaisahihisha Ad-Daaruqutwniy]

[Chanzo chake ni Hadiyth ya Muslim]

 

 

 

62.

وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: {جَاءَتْ فَاطِمَةُ بِنْتُ أَبِي حُبَيْشٍ إِلَى اَلنَّبِيِّ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏فَقَالَتْ: يَا رَسُولَ اَللَّهِ! إِنِّي اِمْرَأَةٌ أُسْتَحَاضُ فَلَا أَطْهُرُ، أَفَأَدَعُ اَلصَّلَاةَ؟ قَالَ: "لَا.‏ إِنَّمَا ذَلِكَ عِرْقٌ، وَلَيْسَ بِحَيْضٍ، فَإِذَا أَقْبَلَتْ حَيْضَتُكِ فَدَعِي اَلصَّلَاةَ، وَإِذَا أَدْبَرَتْ فَاغْسِلِي عَنْكِ اَلدَّمَ، ثُمَّ صَلِّي} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

وَلِلْبُخَارِيِّ: {ثُمَّ تَوَضَّئِي لِكُلِّ صَلَاةٍ}

وَأَشَارَ مُسْلِمٌ إِلَى أَنَّهُ حَذَفَهَا عَمْدًا

Kutokwa kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: Faatwimah bint Abiy Hubaysh[4] alikuja kwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akauliza: “Ee Rasuli wa Allaah! Mimi ni mwanamke nakuwa na istihaadhwah (damu[5] ya haikatiki hata baada ya muda wa hedhi kumalizika) hivyo huwa sitohariki, je, niache kuswali?” Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: “Hapana kwani huo ni mshipa wa damu, wala si hedhi, hivyo, ukiingia katika hedhi, sitisha kuswali, na hedhi ikiisha, osha damu huko iliko, kisha uswali.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

Na katika Riwaayah ya Al-Bukhaariy ameongezea: “Kisha tawadha kwa kila Swalaah[6].”

Na Muslim alitaja kuwa ameiondoa nyongeza hii kwa maksudi.

 

 

 

63.

وَعَنْ عَلِيِّ بْنِ أَبِي طَالِبٍ ‏ رضى الله عنه ‏ قَالَ: {كُنْتُ رَجُلاً مَذَّاءً، فَأَمَرْتُ اَلْمِقْدَادَ بْنَ اَلْأَسْوَدِ أَنْ يَسْأَلَ اَلنَّبِيَّ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏فَسَأَلَهُ  فَقَالَ: "فِيهِ اَلْوُضُوءُ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ، وَاللَّفْظُ لِلْبُخَارِيِّ

Kutoka kwa ‘Aliy bin Abuu Twaalib (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Nilikuwa mtu wa kutokwa na madhiy[7] (majimaji yatokayo katika dhakari), nikamuamrisha Miqdaad bin Al-Aswad[8] amuulize Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ), akamuuliza.” Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: “Anapaswa atawadhe.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

[Na tamshi hili ni la Al-Bukhaariy]

 

 

 

64.

وَعَنْ عَائِشَةَ، رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا، {أَنَّ اَلنَّبِيَّ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏قَبَّلَ بَعْضَ نِسَائِهِ، ثُمَّ خَرَجَ إِلَى اَلصَّلَاةِ وَلَمْ يَتَوَضَّأْ} أَخْرَجَهُ أَحْمَدُ، وَضَعَّفَهُ اَلْبُخَارِيُّ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alimbusu[9] mmoja wa wake zake, na akaenda kuswali bila kutawadha upya.” [Imetolewa na Ahmad, na akaidhoofisha Al-Bukhaariy]

 

 

 

65.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ ‏ رضى الله عنه ‏ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏{إِذَا وَجَدَ أَحَدُكُمْ فِي بَطْنِهِ شَيْئًا، فَأَشْكَلَ عَلَيْهِ: أَخَرَجَ مِنْهُ شَيْءٌ، أَمْ لَا؟ فَلَا يَخْرُجَنَّ مِنْ اَلْمَسْجِدِ حَتَّى يَسْمَعَ صَوْتًا، أَوْ يَجِدَ رِيحًا} أَخْرَجَهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mmoja wenu akipata kinachomtia shaka katika tumbo lake kuwa anatokwa kitu au la, basi asitoke Msikitini hadi amesikia sauti yake au ahisi harufu[10] yake.” [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

66.

وَعَنْ طَلْقِ بْنِ عَلِيٍّ ‏ رضى الله عنه ‏ قَالَ: {قَالَ رَجُلٌ: مَسَسْتُ ذَكَرِي أَوْ قَالَ اَلرَّجُلُ يَمَسُّ ذَكَرَهُ فِي اَلصَّلَاةِ، أَعَلَيْهِ وُضُوءٍ ؟ فَقَالَ اَلنَّبِيُّ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏"لَا، إِنَّمَا هُوَ بَضْعَةٌ مِنْكَ"} أَخْرَجَهُ اَلْخَمْسَةُ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ حِبَّانَ

وَقَالَ اِبْنُ اَلْمَدِينِيِّ: هُوَ أَحْسَنُ مِنْ حَدِيثِ بُسْرَةَ.‏

Kutoka kwa Twalq bin ‘Aliy[11] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Mtu mmoja alisema: “Nimeigusa dhakari yangu” au aliuliza: “Mtu aliyegusa dhakari yake wakati wa Swalaah, Je ni lazima kutawadha?” Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: “Hapana, hiyo ni sehemu ya mwili wako.” [Imetolewa na Al-Khamsah: Ahmad, Abuu Daawuwd, At-Tirmdhiy, An-Nasaaiy na Ibn Maajah  na akaisahihisha Ibn Hibbaan]

 

[Na Ibn Al-Madiyniyy amesema: “Hii ni bora kuliko Hadiyth ya Busrah.”]

 

 

 

67.

وَعَنْ بُسْرَةَ بِنْتِ صَفْوَانَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا، {أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏قَالَ: "مَنْ مَسَّ ذَكَرَهُ فَلْيَتَوَضَّأْ"} أَخْرَجَهُ اَلْخَمْسَةُ، وَصَحَّحَهُ اَلتِّرْمِذِيُّ، وَابْنُ حِبَّانَ

وَقَالَ اَلْبُخَارِيُّ: هُوَ أَصَحُّ شَيْءٍ فِي هَذَا اَلْبَابِ.‏

Kutoka kwa Busrah bint Swafwaan[12] (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Atakayegusa dhakari[13] yake basi na atawadhe.” [Imetolewa na Al-Khamsah, na akaisahihisha At-Tirmidhiy na Ibn Hibbaan]

 

[Na Al-Bukhaariy amesema: “Hadiyth hii ni sahihi zaidi kuliko zote katika mlango huu.”]

 

 

 

68.

وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا، أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صَلَّى عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: {مَنْ أَصَابَهُ قَيْءٌ أَوْ رُعَافٌ، أَوْ قَلَسٌ، أَوْ مَذْيٌ فَلْيَنْصَرِفْ فَلْيَتَوَضَّأْ، ثُمَّ لِيَبْنِ عَلَى صَلَاتِهِ، وَهُوَ فِي ذَلِكَ لَا يَتَكَلَّمُ} أَخْرَجَهُ اِبْنُ مَاجَه

وَضَعَّفَهُ أَحْمَدُ وَغَيْرُهُ.‏

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Yeyote atakayetapika au kutokwa na damu puani[14] kutokwa na madhiy, atoke atawadhe kisha aendelee na Swalaah yake[15] (kwa kuendelea kutokea pale alipoiachia hiyo Swalaah), kwa sharti kwamba  asizungumze katika wakati wa harakati hiyo.” [Imetolewa na Ibn Maajah]

 

Na akaidhoofisha Ahmad na wengine.

 

 

 

69.

وَعَنْ جَابِرِ بْنِ سَمُرَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا، {أَنَّ رَجُلاً سَأَلَ اَلنَّبِيَّ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏أَتَوَضَّأُ مِنْ لُحُومِ اَلْغَنَمِ ؟ قَالَ: إِنْ شِئْتَ قَالَ: أَتَوَضَّأُ مِنْ لُحُومِ اَلْإِبِلِ  ؟ قَالَ: نَعَمْ} أَخْرَجَهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa Jaabir bin Samurah[16] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) anasema kuwa: “Mtu mmoja alimuuliza Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ): “Je! Nitawadhe kwa kula nyama ya kondoo?” Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: “Ukipenda.” Akauliza: “Je nitawadhe kwa kula nyama ya ngamia[17]?” Akasema: “Ndiyo.” [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

70.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ ‏ رضى الله عنه ‏ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏{مَنْ غَسَّلَ مَيْتًا فَلْيَغْتَسِلْ، وَمَنْ حَمَلَهُ فَلْيَتَوَضَّأْ} أَخْرَجَهُ أَحْمَدُ، وَالنَّسَائِيُّ، وَاَلتِّرْمِذِيُّ وَحَسَّنَهُ

وَقَالَ أَحْمَدُ: لَا يَصِحُّ فِي هَذَا اَلْبَابِ شَيْءٌ.

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Aliyemuosha maiti[18] na aoge na aliyembeba atawadhe.” [Imetolewa na Ahmad na An-Nassaiy, na ameifanya ‘Hasan’ At-Tirmidhiy]

 

[Na Ahmad amesema: “Hakuna Hadiyth yoyote iliyosihi katika mlango huu]

 

 

 

71.

وَعَنْ عَبْدِ اَللَّهِ بْنِ أَبِي بَكْرٍ رَحِمَهُ اَللَّهُ، {أَنَّ فِي اَلْكِتَابِ اَلَّذِي كَتَبَهُ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏لِعَمْرِو بْنِ حَزْمٍ: أَنْ لَا يَمَسَّ اَلْقُرْآنَ إِلَّا طَاهِرٌ} رَوَاهُ مَالِكٌ مُرْسَلاً، وَوَصَلَهُ النَّسَائِيُّ، وَابْنُ حِبَّانَ، وَهُوَ مَعْلُولٌ.‏

Kutoka kwa ‘Abdullaah bin Abiy Bakr[19] (رَحِمَهُ اَللَّهُ) amesema kuwa: Katika barua ya Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliyomwandikia “’Amr bin Hazm[20]: “Asiiguse Qur-aan[21] isipokuwa aliyekuwa kwenye twahaarah.” [Imetolewa na Maalik Mursalaa, na Mawswul (wameiunganisha) An-Nasaaiy na Ibn Hibbaan, nayo ina dosari]

 

 

 

72.

وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: {كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏يُذْكُرُ اَللَّهَ عَلَى كُلِّ أَحْيَانِهِ} رَوَاهُ مُسْلِمٌ، وَعَلَّقَهُ اَلْبُخَارِيُّ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akimdhukuru Allaah nyakati zake[22] zote.” [Imetolewa na Muslim, na Al-Bukhaariy akaipa daraja la Mu’alaq]

 

 

 

73.

وَعَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ ‏ رضى الله عنه ‏ {أَنَّ اَلنَّبِيَّ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏اِحْتَجَمَ وَصَلَّى، وَلَمْ يَتَوَضَّأْ} أَخْرَجَهُ اَلدَّارَقُطْنِيُّ، وَلَيَّنَهُ

Kutoka kwa Anas bin Maalik (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alifanya hijaamah[23] (kuumikwa au kupigwa chuku) akaswali wala hakutawadha.” [Imetolewa na Ad-Daaruqutwniy, aliyeipa daraja la Dhaifu]

 

 

 

74.

وَعَنْ مُعَاوِيَةَ ‏ رضى الله عنه ‏ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏{الْعَيْنُ وِكَاءُ السَّهِ، فَإِذَا نَامَتْ اَلْعَيْنَانِ اِسْتَطْلَقَ اَلْوِكَاءُ} رَوَاهُ أَحْمَدُ، وَالطَّبَرَانِيُّ وَزَادَ {وَمَنْ نَامَ فَلْيَتَوَضَّأْ}

وَهَذِهِ اَلزِّيَادَةُ فِي هَذَا اَلْحَدِيثِ عِنْدَ أَبِي دَاوُدَ مِنْ حَدِيثِ عَلِيٍّ دُونَ قَوْلِهِ: {اِسْتَطْلَقَ اَلْوِكَاءُ} وَفِي كِلَا الْإِسْنَادَيْنِ ضَعْفٌ

وَلِأَبِي دَاوُدَ أَيْضًا، عَنْ اِبْنِ عَبَّاسٍ مَرْفُوعًا: {إِنَّمَا اَلْوُضُوءُ عَلَى مَنْ نَامَ مُضْطَجِعًا} وَفِي إِسْنَادِهِ ضَعْفٌ أَيْضًا

Kutoka kwa Mu’aawiyah[24] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Jicho lililo macho ni kamba na kizuizi cha kutoka upepo, na macho yote mawili yakilala, hiyo kamba hufunguka (na upepo hutoka bila hisia[25]).” [Imetolewa na Ahmad na Atw-Twabaraaniy]

 

Na Atw-Twabaraaniy aliongezea: “Kila aliyelala atawadhe upya.”

 

Pia imetolewa na Abuu Daawuwd kwa Hadiyth ya ‘Aliy bila maneno: “Kamba hufunguka” [Isnaad zote mbili ni dhaifu]

 

Na kutoka kwa Abuu Daawuwd vile vile kutoka kwa Ibn ‘Abbaas ikiwa ni Hadiyth Marfuw’aa: “Hakika wudhuu ungalipo kwa aliyelala kwa makalio yake.” [Katika Isnaad yake kuna udhaifu pia]

 

 

 

75.

وَعَنِ اِبْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا، أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏قَالَ: {يَأْتِي أَحَدَكُمُ الشَّيْطَانُ فِي صَلَاتِهِ، فَيَنْفُخُ فِي مَقْعَدَتِهِ فَيُخَيَّلُ إِلَيْهِ أَنَّهُ أَحْدَثَ، وَلَمْ يُحْدِثْ، فَإِذَا وَجَدَ ذَلِكَ فَلَا يَنْصَرِفُ حَتَّى يَسْمَعَ صَوْتًا أَوْ يَجِدَ رِيحًا} أَخْرَجَهُ اَلْبَزَّارُ

وَأَصْلُهُ فِي اَلصَّحِيحَيْنِ مِنْ حَدِيثِ عَبْدِ اَللَّهِ بْنِ زَيْدٍ

وَلِمُسْلِمٍ: عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ نَحْوُهُ.

وَلِلْحَاكِمِ.‏ عَنْ أَبِي سَعِيدٍ مَرْفُوعًا: {إِذَا جَاءَ أَحَدَكُمُ الشَّيْطَانُ، فَقَالَ: إِنَّكَ أَحْدَثْتَ، فَلْيَقُلْ: كَذَبْتَ}

وَأَخْرَجَهُ اِبْنُ حِبَّانَ بِلَفْظِ: {فَلْيَقُلْ فِي نَفْسِهِ}

Kutokwa kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesimulia kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Shaytwaan huja kwa mmoja wenu ndani ya Swalaah, na humpulizia upepo makalioni mwake naye hudhani amepata hadath nae hajapata hadath. Hivyo, akihisi hivyo asiondoke hadi asikie sauti au ahisi harufu[26].” [Imetolewa na Al Bazzaar]

 

[Asili yake ni katika Swahiyh mbili, Al-Bukhaariy na Muslim kuwa ilisimuliwa na ‘Abdullaah bin Zayd]

 

[Na Muslim amepokea Hadiyth ya Abuu Hurayrah vivyo hivyo]

 

Na Al-Haakim amemnukuu Abuu Sa’iyd katika Hadiyth Marfuw’aa (yenye upokezi wa wazi): “Endapo shaytwaan atamjia mmoja wenu na kumwambia: “Wewe umetengua wudhuu wako kwa kutoa upepo”, basi aseme: “Umesema uongo.”” [Imetolewa na Al-Haakim]

 

Na Ibn Hibbaan pia amepokea Hadiyth hiyo pamoja na tamshi: “Na aseme moyoni mwake.”

 

 

[1] Mazingira yote yanayobatilisha wudhuu na kutawadha kwa maji, pia hubatilisha wudhuu wa kutayammam (kutawadha kwa udongo safi itokeapo maji hakuna).

 

[2] Hii inathibitisha kwamba, kusinzia hakubatilishi au hakutangui wudhuu.

 

[3] Hili suala la iwapo usingizi unabatilisha wudhuu au laa, lina utata sana. Katika kadhia hii, maamuzi ya mwisho ni kuwa, endapo usingizi utakuwa ule mzito, basi wudhuu unabatilika, vinginevyo hautenguki.

 

[4] Faatwimah bint Abiy Hubaysh ni Swahabiyyah kutoka Quraysh na tena Asad. Babake ni Qays bin ‘Abdil-Mutwalib bin Asad bin ‘Abdil-‘Uzza bin Quswayy. Alikuwa Muhajira (mhamiaji kutoka Makkah) maarufu, na aliolewa na ‘Abdullaah bin Jahsh.

 

[5] Damu za mwanamke ziko za namna tatu:
a) Hedhi ni damu ya kila mwezi mmoja wa hedhi, ambayo huanza mwanamke akiwa baleghe. Damu ya aina hii husimama wakati mwanamke yu mjamzito.

b) Nifaas, yaani damu ya mwanamke imtokayo akisha kuzaa, ambayo haidumu zaidi ya siku 40.

c) Istihaadhwah, yaani damu inayoweza kutoka kwa sababu zisizokuwa hizo mbili. Hapa inamaanisha inayotajwa mwishoni.

 

[6] Hii inamaanisha kuwa, damu ya Istihaadhwah hubatilisha wudhuu, ndiyo maana Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akaamuru kutawadha upya kabla ya kila Swalaah.

 

[7] Madhiy ni majimaji meupe kama mafuta ambayo hutoka bila kuzuilika wakati mtu ana ashki ya jimai. Ute huu hubatilisha wudhuu, lakini hauhitaji kuoga rasmi.

 

[8] Miqdaad bim ‘Amr bin Tha’labah Al-Bahraan alipewa jina la utani la Abul-Aswad au Abuu ‘Amr, na anajulikana kwa jina la Al-Miqdaad bin Al-Aswad. Al-Aswad bin Yaghuwth Az-Zuhr alimlea na wakafanya mkataba wa kujihami na Miqdaad zama za ujaahiliyyah (kabla ya ujio wa Uislaam). Alikuwa ni mmoja wa Swahaba wenye taqwah, wenye busara, na maarufu. Alikuwa wa sita kusilimu, alihama hijrah zote mbili, na alishiriki vita zote kuu. Alikuwa mpanda farasi katika vita vya Badr, na alishiriki katika kuiteka Misri. Alifariki akiwa na miaka 70 mnamo mwaka 33 A.H kule Al-Jawf, maili tatu kutoka Al-Madiynah. Kwa hivyo mwili wake ulipelekwa Al-Madiynah. ‘Uthmaan akasalisha Swalaah yake ya Janaazah, na kuzikwa Al-Baqi’.

 

[9] Hadiyth hii inathibitisha kwamba, wudhuu haubatiliki kwa kumgusa mwanamke, ukimtamani au usimtamani. Hii inaungwa mkono na ripoti ya Al-Bukhaariy iliyosimuliwa na ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) “Alikuwa akisali gizani, nami nilikuwa nimepumzika wakati miguu yangu ilining’inia hadi kule ambako Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikokuwa akisujudia juu ya msala wake. Kila anaposujudu alikuwa akigusa miguu yangu, nami nikawa naiondosha.”

 

[10] Hadiyth hii inataja msingi wa maana kwamba kila kitu hubaki katika amri ya awali, mpaka kitokee kitu dhahiri dhidi yake. Dhana peke yake si ya kuzingatia ukiwa umo ndani ya Swalaah au laa.

 

[11] Huyu Twalq ni Abuu ‘Aliy Twalq bin ‘Amr Al-Hanaf As-Siheim Al-Yamaam. Alimzuru Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) mara alipofika Al-Madiynah, na akafanya naye kazi katika kuujenga Msikiti wa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ).

 

[12] Busrah bint Swafwaan bin Naefal bin Asad bin ‘Abdil-‘Uzza Al-Quraishiyyah Al-Asadiyyah alikuwa ni Swahaba miongoni mwa Waislaam wa kwanza, alihajiri (alihama) mapema, na akaishi hadi katika Ukhalifa wa Mu’aawiyah.

 

[13] Hadiyth hiyo hapo juu ya Twalq bin ‘Aliy inaelekea inapingana na hii, lakini sivyo hivyo. Kama kiungo hicho kitaguswa bila kufunikwa nguo au kwa nia ya matamanio hapo wudhuu utakuwa umebatilika; vinginevyo haubatiliki.

 

[14] Hadiyth hii ni dhaifu, na hakuna Hadiyth Swahiyh juu ya kadhia hii.

 

[15] Hii inamaanisha kwamba, iwapo mtu alishaswali rakaa  mbili na Imaam, na ikatokezea kwamba wudhuu wake umebatilika, ataicha Swalaah, na baada ya kutawadha upya, ajiunge na jamaa katika sehemu ile ile alipoachia, kisha amalizie Swalaah na Imaam.

 

[16] Jaabir ni Swahaba maarufu na ni mtoto wa dada wa Sa’d bin Abiy Waqqaas. Alilowea Kufa akajenga nyumba kule. Alifariki mnamo mwaka 66 au 74 A.H. Baba yake Samurah bin Junada As-Sawai Al-‘Aamir naye pia ni Swahaba.

 

[17] Watu wengine wanasema hii inamaanisha kutawadha kamili na wengine wanasema kusukutua mdomo tu. Fikra hii ya mwisho ni sahihi, kwa kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alitaja sababu ya amri hii kuwa ni mafuta, na mafuta huganda mdomoni tu.

 

 

[18] Kuhusu kadhia hii, hakuna Hadiyth Swahiyh. Wengine wanasema kuwa kuoga ni lazima kwa yule anayeogesha maiti, wengine wanasema ni vizuri, na wengine wanasema kutawadha ni lazima, na wengine wanasema hata hii siyo lazma.

 

[19] Huyo ni ‘Abdullaah bin Abiy Bakr bin ‘Amr bin Hazm Al-Answaar Al-Madani Al-Qadi. Taabi’ wa daraja la 5. Alifariki mnamo mwaka 135 A.H akiwa na miaka 70.

 

[20] Huyu ‘Amr bin Hazm ni Mkhazraj, Mnajaar aliyepewa jina la utani la Abuu Ad-Dhwahhaak. Alishiriki kwanza katika vita ya Khandaq, na Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alimtuma Najran kuwafundisha watu dini na kukusanya swadaqah. Aliwaandikia kitabu chenye matendo ya lazima na ya hiari, swadaqah na hiki ndicho kitabu kilichotajwa katika Hadiyth hii. Alifariki Madiynah akiwa na miaka hamsini na kitu.

 

[21] Hadath Akbar: (hadathi au najisi kubwa, yaani majimaji ya kijinsia yanayotoka kwenye sehemu za siri), na Hadath Aswghar: (Hadathi ndogo kutoa upepo, mkojo au kinyesi), vyote hivi vinahitaji kutawadha. Lakini ikiwa hiyo Hadath inatokana na kujamiiana, basi imeafikiwa na wote kuwa huna ruhusa kuigusa Qur-aan, lakini kuna maoni tofauti kuhusu kufanya hivyo bila kutawadha.

 

[22] Nyakati za kuenda haja kubwa, kukojoa na za kujamiiana, hazimo. Katika kunajisika kwa kujamiiana, dhikr au kutamka jina la Allaah kunaruhusiwa, lakini kuigusa au kuisoma Qur-aan hakuruhusiwi.

 

[23] Hadiyth hii inaweka wazi kwamba, kutokwa na damu nje ya sehemu mbili kama katika hali hii ya kufanyiwa hijaamah (ukeni na sehemu ya kutolea kinyesi) hakubatilishi wudhuu. Hadiyth za daraja hilo zimesimuliwa pia na Ibn ‘Umar Ibn ‘Abbaas na Abuu Aufa (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ).

 

[24] Mu’aawiyah huyu pamoja na babake, Abuu Sufyaan Sakhr bin Harb, walisilimu ilipotekwa Makkah. ‘Umar alimteuwa akawa Gavana wa Shaam, baada ya kifo cha kaka yake Yaziyd bin Abuu Sufyaan na alibakia hivyo hadi ‘Aliy alivyojitokeza ili apate kumuondosha kwa nguvu, na akaapishwa kuwa Khalifa wakati wa Al-Hasan alipojiuzulu kwa kumuachia yeye cheo mnamo mwaka wa 40 H. Alifariki mnamo mwezi wa Rajabu mwaka 60 A.H akiwa na miaka 78.

 

[25] Hii inamaanisha kuwa usingizi ni chanzo cha hadathi (uchafu), lakini siyo uchafu wenyewe.

 

[26] Hii maana yake ni kwamba, kulala na sambamba na kilalio hupelekea kubatilika kwa wudhuu, ambapo kwenye Hadiyth ya juu inaelezea kuwa usingizi peke yake wowote unabatilisha wudhuu. Kulala sambamba na kilalio ni ishara ya kulala usingizi mzito, wakati viungo vyote vya mwili vinapumzika na kunawezesha upepo kutoka bila kizuizi, ambapo katika usingizi mwepesi au kusinzia, mtu huwa hajapoteza fahamu zote.

 

Share