01-Hadiyth Za Ramadhwaan Na Mafunzo: Ikhlaasw Katika Swawm

 

Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo

 

01-Ikhlaasw Katika Swawm

 

 

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: (( مَنْ صَامَ رَمَضَانَ إِيمَانًا وَاحْتِسَابًا غُفِرَ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ)) 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu)    akisema: Amesema Rasuli wa Allaah Swalla Allaahu Alayhi wa Sallam: ((Mwenye kufunga Ramadhwaan kwa iymaan na kutaraji malipo, hughufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Imesimuliwa na Al Bukhaariy 38 na Muslim]

 

 

Hadiyth hii ni dalili wazi juu ya fadhila ya mwezi mtukufu wa Ramadhwaan. Mwezi huu ni sababu ya Muislamu kughufuriwa madhambi yake na kufutiwa makosa yake. Lakini hilo halifanyiki isipokuwa kwa masharti matatu kama Hadiyth inavyoeleza:

 

La kwanza: Ni kuwa na iymaan kamili kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Ndiye Aliyeifaradhisha Swawm na Yeye Ndiye Atakayewalipa wafungaji malipo makubwa kwa kutii amri Yake.

 

La pili: Kufunga kwa ajili ya kumtakasia niyyah Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Peke Yake. Swawm anayofunga mtu kwa ajili ya riyaa tu, au kufuata desturi au mkumbo tu, basi haina malipo.

 

La tatu: Mwenye swawm kujiepusha na madhambi makubwa. Madhambi haya ni yale yote yaliyowekewa adhabu hapa duniani, au kutolewa laana, au makamio makali na adhabu za Aakhirah kama shirki, kula ribaa, kula mali ya yatima, kuzini, kufanya uchawi, kuwaasi wazazi wawili, madhambi saba yanayoangamiza na kadhalika. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)    Anatuambia:

 

إِن تَجْتَنِبُوا كَبَائِرَ مَا تُنْهَوْنَ عَنْهُ نُكَفِّرْ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَنُدْخِلْكُم مُّدْخَلًا كَرِيمًا ﴿٣١﴾

  Mkijiepusha na madhambi makubwa mnayokatazwa Tutakufutieni madhambi yenu madogo na Tutakuingizeni katika mahali patukufu. [An-Nisaa (4:31)]

 

 

Hivyo mja akifunga Swawm yake ya Ramadhwaan kama inavyotakikana, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Atamghufuria madhambi yake madogo na makosa aliyoyafanya kama atajilinda na madhambi hayo makubwa.

 

Hivyo basi, Muislamu anatakikana katika mwezi huu aharakie kufanya tawbah kwa madhambi yake yote makubwa na madogo ili awe na uhakika zaidi wa kupata maghfirah.

 

 

Na yeyote atakayechafua maisha yake kwa maasia na madhambi, basi amejipotezea mwenyewe nafasi ya kujitakasa na kusamehewa. Huyo hastahiki kupata maghfirah yaliyoahidiwa, bali huenda yakampata maapizo ya du’aa ya Jibriyl ('Alayhis-Salaam) iliyoitikiwa “aamiyn” na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama anavyoeleza Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu)  kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alipanda mimbari akasema: “Aamiyn, Aamiyn, Aamiyn”. Mtu mmoja akamwambia: Ee Rasuli wa Allaah! Umepanda mimbari ukasema: “Aamiyn, Aamiyn, Aamiyn”. Akasema: ((Hakika Jibriyl ('Alayhis-Salaam)  alinijia akaniambia: Aliyeupata mwezi wa Ramadhwaan, naye asighufiriwe, na akaingia motoni, basi Allaah Amtupilie mbali, akasema: Aamiyn, nami nikasema Aamiyn)) [‘Allaamah Al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) amesema: Hadiyth Hasan Swahiyh]  

 

Muislamu mwenye swawm anatakikana awe na shime ya kuzitafuta nyenzo zote za kupatia maghfirah na Radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kwa kuilinda Swaum yake na kuwajibika ipasavyo na mawajibiko yote, na ajiweke mbali kabisa na visababishi vyote vya kumkosesha Radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

   

Kati ya nyenzo hizo kama alivyokuwa akifanya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), ni kukithirisha aina mbalimbali za ‘ibaadah, kutoa swadaqah kwa wingi, kufanya ihsaan, kusoma Qur-aan, kufanya I’tikaf na kadhalika.

          

 

 

 

Share