06-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Swalaah: Mlango Wa Misikiti

بُلُوغُ الْمَرام

Buluwgh Al-Maraam

 

كِتَابُ اَلصَّلَاةِ

Kitabu Cha Swalaah

 

بَابُ اَلْمَسَاجِدِ

06-Mlango Wa Misikiti

 

 

 

 

 

 

196.

عَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: {أَمَرَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم بِبِنَاءِ اَلْمَسَاجِدِ فِي اَلدُّورِ، وَأَنْ تُنَظَّفَ، وَتُطَيَّبَ}  رَوَاهُ أَحْمَدُ، وَأَبُو دَاوُدَ، وَاَلتِّرْمِذِيُّ، وَصَحَّحَ إِرْسَالَهُ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amsema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliamrisha Misikiti ijengwe katika maeneo ya makazi[1], na kwamba isafishwe na itiwe manukato.” [Imetolewa na Ahmad, Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy, naye aliithibitisha kama Mursal]

 

 

 

197.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  قَالَ : قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَاتَلَ اَللَّهُ اَلْيَهُودَ : اِتَّخَذُوا قُبُورَ أَنْبِيَائِهِمْ مَسَاجِدَ}  مُتَّفَقٌ عَلَيْه

وَزَادَ مُسْلِمُ {وَالنَّصَارَى} 

وَلَهُمَا : مِنْ حَدِيثِ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا : {كَانُوا إِذَا مَاتَ فِيهِمْ اَلرَّجُلُ اَلصَّالِحُ بَنَوْا عَلَى قَبْرِهِ مَسْجِدًا}  وَفِيهِ : {أُولَئِكَ شِرَارُ اَلْخَلْقِ}

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Allaah awalaani Mayahudi, wamefanya makaburi ya Manabii wao kuwa Misikiti.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

Na Muslim akaongeza: “Na Manaswara.”

 

Nao (Al-Bukhaariy, Muslim) wamepokea kuwa: “’Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: Walikuwa akifariki mtu mwema miongoni mwao (Mayahudi na Manaswara) wanajenga juu ya kaburi lake Msikiti.”

 

 

Katika Hadiyth hiyo hiyo iliongezwa: “Hao ni viumbe waovu kabisa katika viumbe[2].”

 

 

 

198.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  قَالَ : {بَعَثَ اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم خَيْلاً، فَجَاءَتْ بِرَجُلٍ، فَرَبَطُوهُ بِسَارِيَةٍ مِنْ سَوَارِي اَلْمَسْجِدِ}  اَلْحَدِيثَ . مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alituma wapanda farasi ambao walirudi na mtu mmoja, kisha wakamfunga[3] katika moja ya nguzo za Msikiti.[4][Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

199.

وَعَنْهُ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ   أَنَّ عُمَرَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  مُرَّ بِحَسَّانَ يَنْشُدُ فِي اَلْمَسْجِدِ ، فَلَحَظَ إِلَيْهِ ، فَقَالَ : "قَدْ كُنْتُ أَنْشُدُ ، وَفِيهِ مَنْ هُوَ خَيْرٌ مِنْكَ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema tena: “’Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) alimkuta Hassan[5] akiimba mashairi Msikitini, akamtazama kwa jicho kali, akasema Nilikuwa naimba Msikitini[6] akiwemo mbora zaidi kuliko wewe (yaani Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ)).” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

200.

وَعَنْهُ قَالَ : قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  مَنْ سَمِعَ رَجُلاً يَنْشُدُ ضَالَّةً فِي اَلْمَسْجِدِ فَلْيَقُلْ : لَا رَدَّهَا اَللَّهُ عَلَيْكَ، فَإِنَّ اَلْمَسَاجِدَ لَمْ تُبْنَ لِهَذَا}  رَوَاهُ مُسْلِم

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mwenye kumsikia mtu anatangaza Msikitini kupoteza kitu, aseme: Allaah Asikurejeshee[7] ulichopoteza, kwani Misikiti haikujengwa kwa ajili ya hilo.” [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

201.

وَعَنْهُ : أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  إِذَا رَأَيْتُمْ مَنْ يَبِيعُ ، أَوْ يَبْتَاعُ فِي اَلْمَسْجِدِ، فَقُولُوا: لَا أَرْبَحَ اَللَّهُ تِجَارَتَكَ}  رَوَاهُ النَّسَائِيُّ ، وَاَلتِّرْمِذِيُّ وَحَسَّنَهُ

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema tena Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mkimuona anayenunua au anauza[8] vitu Msikitini, semeni” “Allaah Asiipe faida biashara yako[9][Imetolewa na An-Nasaaiy na At-Tirmidhiy, naye aliita Hasan]

 

 

 

202.

وَعَنْ حَكِيمِ بْنِ حِزَامٍ قَالَ : قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  لَا تُقَامُ اَلْحُدُودُ فِي اَلْمَسَاجِدِ ، وَلَا يُسْتَقَادُ فِيهَا}  رَوَاهُ أَحْمَدُ، وَأَبُو دَاوُدَ بِسَنَدٍ ضَعِيف

Kutoka kwa Hakiym bin Hizaam[10] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Adhabu hazitekelezwi Msikitini wala kisasi hakilipwi humo.” [Imetolewa na Ahmad, na Abuu Daawuwd, kupitia Isnaad dhaifu]

 

 

 

203.

وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ : {أُصِيبَ سَعْدٌ يَوْمَ اَلْخَنْدَقِ، فَضَرَبَ عَلَيْهِ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم خَيْمَةً فِي اَلْمَسْجِدِ، لِيَعُودَهُ مِنْ قَرِيبٍ}  مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: “Katika siku ya Al-Khandaq (vita vya mahandaki), Sa’d[11] aliumia, Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akamwekea hema Msikitini ili awe karibu[12] kumzuru.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

204.

وَعَنْهَا قَالَتْ : {رَأَيْتُ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم يَسْتُرُنِي، وَأَنَا أَنْظُرُ إِلَى اَلْحَبَشَةِ يَلْعَبُونَ فِي اَلْمَسْجِدِ . . .}  اَلْحَدِيثَ . مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema tena: “Nilimuona Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akinikinga wakati nikiangalia Wahabeshi[13] waliokuwa wanacheza Msikitini[14].” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

205.

وَعَنْهَا : {أَنَّ وَلِيدَةً سَوْدَاءَ كَانَ لَهَا خِبَاءٌ فِي اَلْمَسْجِدِ ، فَكَانَتْ تَأْتِينِي ، فَتَحَدَّثُ عِنْدِي . . .}  اَلْحَدِيثَ. مُتَّفِقٌ عَلَيْه

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema tena: “Mjakazi mmoja mweusi alikuwa na hema Msikitini na alikuwa akinijia na kuongea nami[15].” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

206.

 وَعَنْ أَنَسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم {اَلْبُزَاقُ فِي اَلْمَسْجِدِ خَطِيئَةٌ وَكَفَّارَتُهَا دَفْنُهَا} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Kutema mate Msikitini ni dhambi, na kafara yake ni kuyazika.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

207.

وَعَنْهُ قَالَ : قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم{لَا تَقُومُ اَلسَّاعَةُ حَتَّى يَتَبَاهَى اَلنَّاسُ فِي اَلْمَسَاجِدِ}  أَخْرَجَهُ اَلْخَمْسَةُ إِلَّا اَلتِّرْمِذِيُّ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ خُزَيْمَة

Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema tena Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Qiyaamah hakitasimama hadi watu wajifakharishe (kuhusiana na majengo na mapambo ya) Misikitini[16].” [Imetolewa na Al-Khamsah (An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah, Ahmad) isipokuwa At-Tirmidhiy, na akaisahihisha Ibn Khuzaymah]

 

 

 

208.

وَعَنْ اِبْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم{مَا أُمِرْتُ بِتَشْيِيدِ اَلْمَسَاجِدِ}  أَخْرَجَهُ أَبُو دَاوُدَ ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ حِبَّانَ

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mimi sikuamrishwa kurefusha na kupamba Misikiti[17].” [Imetolewa na Abuu Daawuwd na akaisahihisha Ibn Hibbaan]

 

 

 

209.

وَعَنْ أَنَسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  قَالَ : قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم{عُرِضَتْ عَلَيَّ أُجُورُ أُمَّتِي ، حَتَّى اَلْقَذَاةُ يُخْرِجُهَا اَلرَّجُلُ مِنْ اَلْمَسْجِدِ}  رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ ، وَاَلتِّرْمِذِيُّ وَاسْتَغْرَبَهُ ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ خُزَيْمَةَ

Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Nilionyeshwa malipo ya Ummah wangu, hadi punje ya vumbi anayoiondoa mtu Msikitini.” [Imetolewa na Abuu Daawuwd, na At-Tirmidhiy aliyeipa daraja la Ghaarib (ngeni), na akaisahihisha Ibn Khuzaymah]

 

 

 

210.

وَعَنْ أَبِي قَتَادَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  قَالَ : قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم{إِذَا دَخَلَ أَحَدُكُمْ اَلْمَسْجِدَ فَلَا يَجْلِسْ حَتَّى يُصَلِّيَ رَكْعَتَيْنِ}  مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Abuu Qataadah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mmoja wenu anapoingia Msikitini, asiketi mpaka aswali Rakaa mbili[18].” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

 

[1] Ili mtu aswali karibu na nyumbani kwake.

 

 

[2] “Kugeuza makaburi kuwa Misikiti” kuna maana mbili. Kwanza, matendo ambayo yanatakiwa kufanywa mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى)    ndani ya Misikiti, yanafanywa karibu au juu ya makaburi kwa mfano kusujudu, kuinama, kukalia mapaja, au kusimama huku mikono imekunjwa kama ishara ya heshima. Pili, kujenga Misikiti karibu na makaburi kwa maana yoyote iwayo, kumekatazwa kabisa.

 

 

 

 

 

[3] Maana yake: kwa muda mfupi Msikiti unaweza kutumika kama mahabusu.

 

[4] Hadiyth hii inaonyesha kuwa mtu asiyekuwa Muislamu anaweza kuingia Msikitini kwa kuwa si msafi kiasili bali kidhahiri; lakini haruhusiwi kuingia ndani ya Ka’bah takatifu na hawezi kuhiji.

 

[5] Hassan huyu ndiye Hassan bin Thaabit Al-Answaar Al-Khazraj, aliyekuwa mshairi wa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ). Abuu ‘Ubayda alisema kuwa: “Waarabu wameafiki kuwa Hassan bin Thaabit alikuwa mshairi mzuri kuliko wote.” Alikufa kabla ya mwaka 40 A.H zama za Ukhalifa wa ‘Aliy. Pia inasemekana kuwa alikufa mnamo mwaka 50 A.H. akiwa na umri wa miaka 120 ambayo miaka 60 ya hiyo alikuwa yumo bado katika ujahili, na miaka 60 alikuwa katika Uislaam.

 

[6] Huu ni ushahidi kuwa maadili mema na ushairi wa juu vyaweza kusomwa ndani ya Msikiti. Hassan bin Thaabit alikuwa akisoma mashairi muhimu kujibu mashairi ya makafiri yanayoudhihaki Uislaam, naye Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) daima alikuwa akimsifu Hassan kwa kusema kuwa: “Jibriyl anakusaidia.”

 

[7] Hii ni kuwalaumu wanaosema upuuzi Msikitini. Kwa mfano, itokeapo ng’ombe wamepotea, mwenyewe asiulize ndani ya Msikiti kutoka kwa watu kwa kuwavurugia utulivu wao kwa Allaah (سبحانه وتعالى). Akitaka, asimame kwenye lango la Msikiti aulize.

 

[8] Inamaanisha Misikiti isitumike kama masoko, kwa sababu itaathiri heshima ya Misikiti.

 

[9] Kufanya biashara Msikitini kumekatazwa. Yoyote anayefanya biashara mle, atahesabika kuwa ni mwenye dhambi, lakini mauziano yatakuwa Halaal.

 

[10] Huyu Hakiym bin Hizaam ndiye Abuu Khaalid Al-Qurashi Al-Asadi, kaka yake Khadiyjah “Mama wa Waumini”. Alikuwa miongoni mwa watu watukufu wa Maquraysh, na alizaliwa ndani ya Ka’bah miaka 13 kabla ya tukio la tembo. Alisilimu mnamo mwaka wa kutekwa Makkah, na alikufa Madiynah mnamo mwaka 54 A.H. akiwa na umri wa miaka 120.

 

[11] Sa’d bin Mu’aadh alikuwa kiongozi wa Al- Aws na mmoja wa Swahaba wakuu. Alisilimu kati ya ‘Aqaba ya kwanza na ya Bukhaariy na Muslim pili, na Banu ‘Abdul-Ashhar wakasilimu kwa athari ya Uislaam. Alikuwa anaheshimiwa na anatiiwa sana na watu wake. Alipigwa mshale katika Vita vya Handaki, na kafariki kwa jeraha lile baada ya Vita vya Banu Quraydha mnamo mwezi wa Dhul-Hijjah mwaka wa 5 A.H

 

[12] Hadiyth hii ni ushahidi kuwa kuweka hema ndani ya Msikiti la mtu mgonjwa au aliyejeruhiwa kukaa mle inaruhusiwa.

 

[13] Yaani mwanamke anaweza kumtazama mwanamume bila niyyah maalumu.

 

[14] Mazoezi yanayosaidia katika vita vya Jihaad yaruhusiwa kufanyiwa Msikitini, na wale Wahabeshi walikuwa wakicheza michezo ya kivita.

 

[15] Hadiyth kamili imesimuliwa katika Swahiyh Al-Bukhaariy. Lengo la kuisimulia hapa ni kufahamisha kuwa mwanamke pia anaweza kukaa Msikitini na kuweka hema Msikitini imeruhusiwa.

 

[16] Inamaanisha kuwa, watu watashindana kifahari, na watajivunia upambaji na uzuri wa Misikiti yao. Pia inaweza kumaanisha kuwa watajivunia uku una umaarufu wao ndani ya Misikiti.

 

[17] Inaonyesha kuwa, kwa kuwa ni desturi ya Kiyahudi, imekatazwa kuchora na kuiremba Misikiti.

 

[18] Hii ni wazi kuwa Rakaa hizi mbili ni za Tahiyyatul-Masjid (maamkizi ya Msikiti). Baadhi ya ‘Ulamaa wanazihesabu hizi ni za lazima, wakati wengine wengi wanazihesabu kuwa ni za hiari. Ukichunguza maana ya Hadiyth utaona kuwa ‘Ulamaa wengine wameiruhusu Swalaah hii iswaliwe hata nyakati za makruwh (zinazokatazwa kuswali), ambapo wengine wanakataza isiswaliwe nyakati hizo.

 

Share