04-Hadiyth Za Ramadhwaan Na Mafunzo: Swawm Ni Taqwa

 

Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo

 

04-Swawm Ni Taqwa

 

 

 

 

عَنْ ابْنِ عُمَرَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : (( بُنِيَ الإِسْلامُ عَلَى خَمْسٍ شَهَادَةِ أَنْ لا إِلَهَ إِلا اللَّهُ وَأَنَّ مُحَمَّدًا رَسُولُ اللَّهِ وَإِقَامِ الصَّلاةِ وَإِيتَاءِ الزَّكَاةِ وَالْحَجِّ وَصَوْمِ رَمَضَانَ)) " 

Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) akisema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema: ((Uislamu umejengwa juu ya matano: Kushuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki illa Allaah na kwamba Muhammad ni Rasuli wa Allaah, kusimamisha Swalaah, kutoa Zakaah, kuhiji na Swawm ya Ramadhwaan)) [Imesimuliwa na Al-Bukhaariy (8) na Muslim (16)]

 

 

Mafunzo:

 

Hadiyth hii inatujulisha kuwa kufunga mwezi wa Ramadhwaan ni wajibu kwa kila Mwislamu asiye na udhuru, na kwamba Swawm ni moja kati ya nguzo tano za Uislamu ambayo Allaah (‘Azza wa Jalla) Ameifaradhisha kwa Waja Wake kwa hikma adhimu, na siri kubwa ambayo ameijua aliyeijua na amejingikiwa aliyejingikiwa.

 

 

Makusudio makuu ya Swawm ni kuizuia nafsi na matamanio, kuiweka mbali na mambo iliyoyazoea, na kuzidhibiti nguvu zake za kimatamanio ili Mwislamu aweze kulifikia lengo halisi la Swawm ambalo ni taqwa.

Allaah (‘Azza wa Jalla) Anatuambia:

 

أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ ﴿١٨٣﴾

Enyi walioamini! Mmefaridhishwa Swiyaam kama ilivyofaridhishwa kwa walio kabla yenu mpate kuwa na taqwa. [Al-Baqarah: 183]

 

Aayah hii inaelezea wazi sababu ya kufaradhishiwa sisi Swawm kama Waislamu wenzetu waliotutangulia katika umma zilizopita. Swawm inakuwa ni kama zoezi la kumwandaa Mwislamu kuwa na uwezo wa kujizuia na makatazo kwa kuacha matamanio yake halali ya kimaumbile kwa ajili tu ya kutekeleza agizo la Allaah (‘Azza wa Jalla) na kutarajia malipo Yake. Irada yake inaleleka kutokana na Swawm hii kuwa na uwezo wa kuacha matamanio na kujipamba kwa subra ambayo malipo yake yanakuwa hayana hisabu au mpaka maalum, na hakuna ajuaye malipo yake isipokuwa Allaah (‘Azza wa Jalla) Peke Yake.

 

Swawm ina athari ya ajabu katika kuvilinda na kuvihifadhi viungo vya nje na nguvu za ndani ya mwili. Mfungaji Swawm wa kweli, hujikuta moyo wake ukichukia kila lile lenye kumkasirisha Allaah (‘Azza wa Jalla) na kulipenda kila lile lenye kumfurahisha huku akitaraji malipo makubwa kabisa toka kwa Allaah (‘Azza wa Jalla) kutokana na subra anayoifanya ya kufuata amri Yake na kujizuia na matamanio yote ya mwili.

 

Imaam As-Sa’diy katika Tafsiyr yake amenukuu yafuatayo kuhusu maana ya  taqwa katika Aayah ya Swawm. Akasema kuwa Swawm ni sababu kuu ya taqwa (kumcha Allaah) kwa kuwa ni kutekeleza amri za Allaah na kujiepusha na yaliyokatazwa.

 

Kwa hiyo katika Swawm yanapatikana:

 

 

1. Taqwa ya asw-swaaim (anayefunga swawm) huacha yote Aliyoyakataza Allaah; kula, kunywa, kujimai na kama hayo, na yote yanayoelemea nafsi yake kuyatamani; hapo basi hujikurubisha kwa Allaah kwayo akitaraji thawabu kwa kujiepusha nayo. Haya yote ni kutokana na taqwa. 

 

2.  Na Swawm pia inamfunza mtu kumcha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) basi hujiepusha na hawaa ya nafsi yake, kwa (kutegemea) Uwezo Wake (Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kuwa anatambua kwamba Allaah Anamuona (ayatendayo yote).

 

 

3. Swawm pia inamzuia mtu na shaytwaan, kwani hakika shaytwaan anatembea katika mwili wa binaadam kamba damu inavyotembea katika mishipa. Kwa hiyo Swawm inamvunja nguvu shaytwaan (na uchochezi wake), hivyo madhambi hupunguka. 

 

 

4.  Swawm pia aghalbu humfanya mtu azidishe utiifu na utiifu ni katika sifa za taqwa.

 

 

5.  Swawm pia inamfanya tajiri anaposhikwa na njaa inayombidi imshike (kwa kuwa ni fardhi kwake, huwafikiria na) huwahurumia  masikini na mafuqara na hii ni miongoni mwa sifa za taqwa.  

 

 

Hali kadhaalika taqwa ni kuacha kila aina ya maovu na khasa kuzuia ulimi kutokunena maovu kama kusema uongo, uzushi, kushuhudia uongo, ghiybah (kusengenya), namiymah (kufitinisha au kuchongesha baina ya watu), kutukana, kumfanyia mtu kejeli na kadhaalika kwa kuwa maovu katika Swawm humaharibia mtu Swawm yake kwa dalili zifuatazo:

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: (( مَنْ لَمْ يَدَعْ قَوْلَ الزُّورِ وَالْعَمَلَ بِهِ فَلَيْسَ لِلَّهِ حَاجَةٌ فِي أَنْ يَدَعَ طَعَامَهُ وَشَرَابَهُ))

 Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Asiyeacha kusema uongo (kutoa ushahidi wa uongo, na maasi yote ya ulimi)  na vitendo vibaya  basi ajue kuwa Allaah hana haja na Swawm yake katika kuacha chakula chake na kinywaji chake)) [Al-Bukhaariy]

 

 

Kwa maana: Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Hataikubali Swawm yake.

 

Bila shaka Swawm ina faida nyinginezo mbali ya hilo la kufikia kilele cha taqwa. Hadiyth kadhaa zimetufahamisha kuwa mwenye kutekeleza ya wajibu na ya faradhi, na akaacha maharamisho, basi huyo ni katika watu watakaofuzu na kuingia Peponi:

 

عَنْ طَلْحَةَ بْنَ عُبَيْدِ اللَّهِ، يَقُولُ جَاءَ رَجُلٌ إِلَى رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم فَإِذَا هُوَ يَسْأَلُهُ عَنِ الإِسْلاَمِ، فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: ((خَمْسُ صَلَوَاتٍ فِي الْيَوْمِ وَاللَّيْلَةِ)) ‏ فَقَالَ: هَلْ عَلَىَّ غَيْرُهَا؟ قَالَ: ((لاَ، إِلاَّ أَنْ تَطَّوَّعَ‏))‏ فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: ((وَصِيَامُ رَمَضَانَ))‏ قَالَ: هَلْ عَلَىَّ غَيْرُهُ ؟ قَالَ: ((لاَ، إِلاَّ أَنْ تَطَّوَّعَ)) ‏قَالَ: وَذَكَرَ لَهُ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم الزَّكَاةَ‏.‏ قَالَ: هَلْ عَلَىَّ غَيْرُهَا؟ قَالَ: ((لاَ، إِلاَّ أَنْ تَطَّوَّعَ)) ‏ ‏ فَأَدْبَرَ الرَّجُلُ وَهْوَ يَقُولُ: "وَاللَّهِ لاَ أَزِيدُ عَلَى هَذَا وَلاَ أَنْقُصُ‏".‏ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: ((أَفْلَحَ إِنْ صَدَقَ))

Imepokelewa kutoka kwa Twalhah bin ‘Ubaydillaah (Radhwiya Allaahu 'anhu)  kwamba: Mtu mmoja alimwendea Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  na kuanza kumuuliza kuhusu Uislamu. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Swalaah tano usiku na mchana)). Akauliza: “Je, liko jingine zaidi ya hilo linalonipasa?” Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema ((Hakuna, ila kama utafanya lililosuniwa)). Halafu Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamkamilishia na kumwambia: ((Na Swawm ya Ramadhwaan)). Akauliza: “Je, liko jingine zaidi ya hilo linalonipasa?” Akasema: ((Hakuna, ila kama utafanya lililosuniwa)). Akasema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamtajia kuhusu Zakkaah. Akauliza: “Je, liko jingine zaidi ya hilo linalonipasa?” Akasema: ((Hakuna, ila kama utafanya lililosuniwa)) Hapo yule mtu akaondoka zake huku akisema: “Wa-Allaahi sitozidisha juu hayo wala sitoyapunguza.” Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Ikiwa kasema ukweli basi atafuzu)) [Al-Bukhaariy]

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Share