06-Hadiyth Za Ramadhwaan Na Mafunzo:Malipo Ya Swawm Siku Moja Kwa Ajili Ya Allaah

 

Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo

 

06-Malipo Ya Swawm Siku Moja Kwa Ajili Ya Allaah

 

 

 

 

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ رضي الله عنه قَالَ : قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: مَنْ صَامَ يَوْماً فِي سَبِيلِ اللَّهِ بَعَّدَ اللَّهُ وَجْهَهُ عَنْ النَّارِ سَبْعِينَ خَرِيفًا .

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayefunga  (Swawm) siku moja kwa ajili ya Allaah, Allaah Ataubaidisha uso wake na moto masafa ya miaka sabini)) [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

Mafunzo:

 

 

‘Ulamaa wametofautiana kuhusiana na maana ya “Fiy SabiyliLLaah.”

 

Kauli ya kwanza inasema kuwa kinachofahamika kwa hisia ya kwanza katika Hadiyth hii tukufu, ni kuwa kinachokusudiwa hapa ni kufunga Swawm wakati wa vita ambapo mfungaji anakusanya ‘ibaadah ya Swawm, ‘ibaadah ya jihaad katika Njia ya Allaah, na ‘ibaadah ya kufanya subra wakati anapokuwa amekabiliana na mazito na mashaka na hususan katika taharuki ya vita ambapo mtu huhofia nafsi yake kuuawa au kujeruhiwa, na huhofia watoto wake na nduguze Waislamu kiujumla.

 

 

Kauli ya pili, ni kwamba  makusudio ya “Fiy SabiyliLlaah” ni Dini ya Allaah ('Azza wa Jalla)  na Shariy’ah Yake. Hivyo itakuwa na maana ya mwenye kufunga kwa ajili ya Radhi za Allaah ('Azza wa Jalla) tu, na kuzitafuta thawabu Zake, na si vinginevyo. Kwa maana hii, anatoka nje ya wigo hapa mwenye kufunga kwa ajili ya riyaa na umashuhuri, au kutaka kusifiwa kutokana na Swawm yake au kwa lengo jingine lolote la maslaha yake binafsi.

 

Hivyo basi, kwa mujibu wa kauli hii, yeyote mwenye kufunga kwa ajili ya Allaah ('Azza wa Jalla)  tu akiwa mjini kwake, au akiwa safarini, basi huyo anaingia katika wigo wa “Fiy SabiyliLLaah” na hivyo kustahiki malipo haya makubwa ya kuwekwa mbali na moto wa Jahannam umbali wa miaka 70. Hii ni kwa vile SabiyliLLaah inajumuisha kila tendo analolifanya Mwislamu kwa ajili ya kuitumikia Dini yake, na kuwatumikia Waislamu kwa ajili ya kuiweka juu Dini ya Allaah ('Azza wa Jalla).   

 

 

Kujenga madrasa kwa ajili ya kuhifadhisha watoto Qur-aan na kuwafundisha ilmu ya Dini, kuwalipia ada na karo za shule, kuwanunulia wagonjwa madawa na kuwalipia matibabu, hayo yote yanaingia ndani ya wigo wa Fiy SabiyliLlaah.

 

 

Ama kuwekwa mbali na moto huo kama wanavyosema ‘Ulamaa, ni kwamba mfungaji huyu atabaidishwa umbali wa mwendo wa miaka 70 asiweze kusikia mngurumo wake wala sauti yake, na hivyo pia atakuwa ameepushwa nao, na hatoweza kuingia humo. Wameeleza maana ya neno “khariyf” kama ni miaka ingawa maana yake hasa ni msimu kati ya misimu ya mwaka ambao ni “autumn”. Msimu huu huja mara moja kila mwaka, na hivyo ukija mara sabini ni sawa na miaka 70. Miaka hii sabini si sawa na miaka ya hapa duniani, bali ni kwa vipimo Vyake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), kwani siku moja Kwake ni kama miaka 1000 ya hapa duniani kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَيَسْتَعْجِلُونَكَ بِالْعَذَابِ وَلَن يُخْلِفَ اللَّـهُ وَعْدَهُ ۚ وَإِنَّ يَوْمًا عِندَ رَبِّكَ كَأَلْفِ سَنَةٍ مِّمَّا تَعُدُّونَ ﴿٤٧﴾

Na wanakuhimiza kwa adhabu, na Allaah Hakhalifu ahadi Yake. Na hakika siku moja kwa Rabb wako ni kama miaka elfu katika yale mnayoihesabu. [Al-Hajj: 47]

   

 

Tunarudi tukisema kwamba kwa mujibu wa tafsiyr ya kwanza ya ‘Ulamaa kuhusu “Fiy SabiyliLLaah” ni kuwa hapo Swawm itakuwa na sifa mbili muhimu. Sifa ya wakati na sifa ya mahala.

 

Sifa ya wakati ni kuwa wakati wa mapambano na vita, ni wakati wa kujibiwa zaidi du’aa. Ama sifa ya mahala, ni kuwa eneo panapopiganiwa vita na Mwislamu, linakuwa ni eneo lililo karibu zaidi na Jannah yake, kwani akiuawa tu kishahidi, basi huingia moja kwa moja Jannah. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

  ((‏وَاعْلَمُوا أَنَّ الْجَنَّةَ تَحْتَ ظِلاَلِ السُّيُوفِ))‏‏

((Jueni kwamba Janna iko chini ya vivuli vya panga)) [Hadiyth ya ‘Abdullaah bin Awfaa imesimuliwa na Al-Bukhaariy]

 

 

Na hii ni kwa ajili ya kuwahamasisha na kuwaraghibisha kuipigania Dini ya Allaah ('Azza wa Jalla) kwa nguvu zao zote. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

وَلَا تَحْسَبَنَّ الَّذِينَ قُتِلُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ أَمْوَاتًا ۚ بَلْ أَحْيَاءٌ عِندَ رَبِّهِمْ يُرْزَقُونَ ﴿١٦٩﴾ 

Na wala usiwadhanie kabisa wale waliouawa katika njia ya Allaah ni wafu, bali wahai, kwa Rabb wao wanaruzukiwa. [Al-Baqarah: 169]

 

 

 

 

 

 

 

Share