08-Hadiyth Za Ramadhwaan Na Mafunzo:Swawm Hufuta Madhambi Yatokanayo Na Mtu Kufitinika Na Mkewe Na Mali Yake

 

Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo

 

08-Swawm Hufuta Madhambi Yatokanayo Na Mtu Kufitinika Na Mkewe Na Mali Yake

 

 

 

 

سأل عمر رضي الله عنه قال: من يحفظ حديثًا عن النبي صلى الله عليه وسلم في الفتنة؟  قال حذيفة: أنا سمعته يقول: ((فِتْنَةُ الرَّجُلِ فِي أَهْلِهِ وَمَالِهِ وَجَارِهِ تُكَفِّرُهَا الصَّلَاةُ وَالصِّيَامُ وَالصَّدَقَةُ)).

‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu)  aliuliza: “Nani anahifadhi Hadiyth toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu fitnah?” Hudhayfah akasema: Mimi nimemsikia akisema: ((Kufitinika mtu kutokana na mke wake, mali yake na jirani yake, (dhambi yake) hufutwa na Swalaah na Swawm na swadaqah..)) [Al-Bukhaariy]

 

 

Mafunzo:

 

Maana ya fitnah hapa ni makosa anayoyafanya mtu kutokana na mkewe na watoto kwa kujaribu kuwafurahisha kwa linalomkasirisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), au kuitumia mali yake visivyo akaipeleka kwenye sehemu isipo pake, au akakiuka haki za ujirani mwema kwa kumuudhi jirani yake kimatendo au kimaneno na kadhalika.

 

 

Asili ya neno “fitnah” ni الابتلاء na الاختبار. Kwa maana kuwa hayo yote yanakuwa ni mtihani kwa mtu, na anaposhindwa mtihani huo, basi anakuwa amefitinika “maftuwn”. Allaah ('Azza wa Jalla) Anatuambia:

أَلَا فِي الْفِتْنَةِ سَقَطُوا ۗ  

 Tanabahi! Wamekwishaanguka katika fitnah.  [At-Tawbah: 49]

 

Hivyo basi, mtu anapata mtihani kwa mtoto wake, mke wake, mali yake, jirani yake na wengineo. Kwenye mtihani huu ima afaulu au afeli. Na hii inatupa picha ni namna gani kila mtu anavyokabiliwa na mtihani kama huu ambao bila shaka ni mgumu kwa kila mmoja wetu.

 

Na kwa vile kufeli ni jambo lisiloepukika kwenye mtihani huu, Allaah ('Azza wa Jalla)  kwa Rahmah Zake Ameifanya Swalaah, Swawm na Swadaqah, kuwa ni visafisho vya makosa anayoyafanya mtu na kuanguka kwenye mtihani huo.

 

Swalaah tano anazoziswali Mwislamu kila siku, na Swalaah za Ijumaa anazoziswali wiki baada ya wiki, na Ramadhwaan anayoifunga hadi Ramadhwaan nyingine, hizi zote humtakasa kutokana na makosa hayo ya kuteleza na makosa mengineyo madogo madogo, lakini kwa sharti ya kujiepusha na madhambi makubwa yaliyokemewa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na yale saba yanayoangamiza yaliyotajwa kwenye Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

 

Sharti jingine ni kutofungamana makosa hayo na haki za watu. Ikiwa zitafungamana, basi haki hizo ni lazima awarejeshee wenyewe hapa duniani, na kama hakufanya hivyo, basi atawarejeshea Siku ya Qiyaamah. Hatari ya hili ni kuwa ikiwa haki hizo ni nyingi, basi zinaweza kumaliza mema yake yote, na hatimaye atabebeshwa makosa na madhambi ya walalamikaji, na kisha atatupwa motoni. Na huyo ndio muflis wa kweli kama inavyoeleza Hadiyth iliyopokelewa na Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu):

 

((أَتَدْرُونَ مَنِ الْمُفْلِسُ؟)) قالوا: المفلس فينا من لا درهمَ له ولا دِينار. قال: ((الْمُفْلِسُ مَنْ يَأْتِي يَوْمَ الْقِيَامَةِ بِصَلَاةٍ وَصَدَقَةٍ وَصَوْمٍ، وَيَأْتِي وَقَدْ ضَرَبَ هَذَا، وَشَتَمَ هَذَا، وَقَذَفَ هَذَا، وَأَخَذَ مَالَ هَذَا، فَيُؤْخَذُ مِنْ حَسَنَاتِهِ لِهَذَا،  ولم يبقَ له حسنة،  حَتَّى إِذَا فَنِيَتْ حَسَنَاتُهُ أُخِذَ مِنْ سَيِّئَاتِهِ فَوُضِعَتْ عَلَيْهِ))

Mtume Swalla Allaahu Alayhi wa Sallam aliwauliza: ((Je, mnamjua ni nani muflis?)). Wakasema: “Muflis tunayemjua sisi ni mtu asiye na dirham wala dinari”. Akasema: ((Muflis ni yule atakayekuja Siku ya Qiyaamah na Swalaah, Swadaqah na Swawm. Anakuja akiwa amempiga huyu, amemtusi huyu, amemzushia huyu na amedhulumu mali ya huyu. Fungu la mema yake litachukuliwa apewe huyu, mpaka yanapomalizika mema yake (yaani thawabu za Swalaah zake, Swaum zake na Swadaqah zake), na hakubakiwa na chochote - yatachukuliwa mabaya yake abebeshwe yeye)) [Muslim]

 

 

 

 

Share