11-Hadiyth Za Ramadhwaan Na Mafunzo: Fadhila Za Suhuwr (Daku)

 

 

Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo

 

11-Fadhila Za Suhuwr (Daku)

 

 

 

عن انس بن مالك رضي الله عنه قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((تَسَحَّرُوا فَإِنَّ فِي السَّحُورِ بَرَكَةً))

Imepokelewa toka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Kuleni suhuwr (daku), kwani kuna barakah katika daku)) [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

Mafunzo:

 

 

‘Ulamaa wanasema kwamba barakah katika suhuwr (daku) inapatikana kwa njia tofauti.

 

Kwanza: Barakah hupatikana kwa kuifuata Sunnah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Pili: Barakah inapatikana kwa kukhalifiana na Ahlul-Kitaab.

 

 

Tatu: Barakah inapatikana kwa kumpatia Mwislamu nguvu ya kufunga Swawm na kufanya kazi zake nyinginezo mchana.

 

 

Nne: Barakah inapatikana kwa kumfanya mwenye Swawm kuwa mbali na hali ya hamaki hamaki itokanayo na njaa.

 

 

Tano: Barakah inapatikana kwa sababu ya kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kuomba du’aa wakati huo ambapo inakuwa yakini kujibiwa kabla ya mwisho wa usiku ambapo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anateremka katika wingu wa dunia.

 

Aidha, barka hiyo inaweza kuambatana na mambo ya Aakhirah, kwani kusimamisha Sunnah, humpatisha Muumini malipo ya Aakhirah.

 

Na kubwa zaidi ya hayo, ni kuwa Allaah ‘Azza wa Jalla) pamoja na Malaika Wake, Huwatakia rahmah wote wenye kula daku. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : ((السُّحُورُ أَكْلَةٌ بَرَكَةٌ فَلا تَدَعُوهُ وَلَوْ أَنْ يَجْرَعَ أَحَدُكُمْ جَرْعَةً مِنْ مَاءٍ فَإِنَّ اللَّهَ وَمَلائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى الْمُتَسَحِّرِينَ)) رواه أحمد (11003) وحسنه الألباني في صحيح الجامع (3683) . 

Imepokelewa toka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Suhuwr (Daku) chakula chake ni barakah, basi msikiache hata kumeza mmoja wenu funda la maji. Kwani Allaah na Malaika Wake, wanawatakia rahmah wenye kula daku)) [Ahmad (11003) na ameipa daraja la Hasan Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Jaami’ (3683)]

 

 

Na kwa ajili ya kufaidika zaidi na barakah hizo, inakuwa vyema kwa walaji daku wautumie vyema muda huo kwa kutawadha na kuswali angalau rakaa mbili, kukithirisha du’aa, kusoma Qur-aan Tukufu na kuleta nyiradi. Pia kuwakirimu majirani kwa kuwapelekea daku na hata kwa wasiojiweza.

 

 

Tunarudi tukisema: “Je, amri hii ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwetu “تسحروا” (kuleni daku), ni amri ya wajibu?

 

‘Ulamaa wanasema kuwa si amri ya wajibu, bali ni amri ya Sunnah au Mustahabb (inapendekezwa). Na dalili ni kuwa yeye Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alifanya الوصال pamoja na Maswahaba. الوصال ni kufunga Swawm siku mbili mfululizo bila kufuturu au kula daku.

 

 

 

Share