13-Hadiyth Za Ramadhwaan Na Mafunzo: Fadhila Za Kuwahi Kufuturu

 

Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo

 

13-Fadhila Za Kuwahi Kufuturu

 

 

 

عَنْ سَهْلِ بْنِ سَعْدٍ، أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ : ((لاَ يَزَالُ النَّاسُ بِخَيْرٍ مَا عَجَّلُوا الْفِطْرَ)) متفق عليه

Imepokelewa toka kwa Sahl bin Sa’d As Saa’idiy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Watu wataendelea kudumu kwenye kheri, madhali wanaharakia kufungua Swawm)) [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

Mafunzo:

 

 

Hadiyth hii ina mambo kadhaa ndani yake:

 

 

Kwanza: Ni Sunnah mtu asicheleweshe kufungua Swawm yake, bali afungue mara tu baada ya kuhakikisha kuwa jua lishazama. Na hii ni Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na madhali Waislamu wataishikilia Sunnah hii, basi wataendelea kuwa ndani ya kheri.

 

 

Pili: Ni Sunnah mwenye Swawm afungue kwa “rutwab” na kama hatopata, basi kwa “tamr”, na kama hakupata, basi afungue kwa maji. Hili limesuniwa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth yake nyingine.

 

 

“Rutwab” na “tamr” vinameng’enyeka haraka tumboni kutokana na mada zake za kisukari.

 

Rutwab = Tende freshi, mpya safi ziloiva ambazo zimajimaji.  

 

 

Tamr =   Tende zinazobadilika hali baada ya hatua ya rutwb kwa kuanikwa juani, hivyo huwa ni kavu kiasi fulani. 

 

 

Tatu: Uharakiaji kufungua Swawm unabeba hukmu zifuatazo:

 

 

(a) Kuharakia huko ni kulitii Agizo la Allaah (‘Azza wa Jalla) kama Muumini alivyoitikia agizo la kufunga Swawm.

 

 

(b)  Ni kuwa mbali na uchupaji mipaka “ghuluwwi” na kujiingiza katika jambo ambalo halikuamrishwa.

 

 

(c) Mwislamu anaitumia vyema rukhsa aliyopewa inayoingia ndani ya wigo wa kuwepesishiwa na kusahilishiwa maarisho ya Dini.

 

 

(d)  Kutojishabihisha na Ahlul- Kitaab. Hao huchelewesha kufungua Swawm kama alivyosema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 

((لا يَزَالُ الدِّينُ ظَاهِرًا مَا عَجَّلَ النَّاسُ الْفِطْرَ لأَنَّ الْيَهُودَ وَالنَّصَارَى يُؤَخِّرُونَ ‏))

((Dini itaendelea kuwa shindi na juu madhali watu wataharakia kufungua Swawm, kwa kuwa Mayahudi na Manaswara huchelewesha)) [Sunan Abiy Daawuwd (2353) na Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan]

 

 

(e)  Mfungaji hupata nguvu ya kuendelea na ‘ibaada zingine kama Swalaah za faradhi na za Sunnah zinazofuatia baada ya kufungua Swawm.

 

 

 

 

 

 

 

 

Share