16-Hadiyth Za Ramadhwaan Na Mafunzo: Fadhila Za I’tikaaf

 

Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo

 

 16-Fadhila Za I’tikaaf

 

 

 

 

 عَنْ عَائِشَةَ رضى الله عنها قَالَتْ: "كَانَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم يَعْتَكِفُ فِي الْعَشْرِ الأَوَاخِرِ مِنْ رَمَضَانَ، فَكُنْتُ أَضْرِبُ لَهُ خِبَاءً فَيُصَلِّي الصُّبْحَ ثُمَّ يَدْخُلُهُ"

Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) akisema:  Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikaa I’tikaaf katika kumi la mwisho la Ramadhwaan. Nilikuwa nikimtengenezea kijihema, akaswali Alfajiri, kisha akaingia humo)) [Al-Bukhaariy (4/346)]

 

 

 

Mafunzo:

 

 

Maana ya I’tikaaf ki Shariy’ah  ni kukaa Msikitini kwa lengo la kufanya ‘ibaadah kwa ajili ya Allaah (‘Azza wa Jalla) Peke Yake. ‘Ibaadah hii tukufu imesuniwa kwa wanaume na wanawake kutokana na yaliyothibiti toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa alikuwa akikaa I’tikaaf katika kumi la mwisho pamoja na baadhi ya wakeze, na wake zake hao waliendelea kukaa I’tikaaf baada ya yeye kufariki.

 

 

Mahala pa kufanyia I’tikaaf hii ni kwenye Msikiti unaoswaliwa jamaa, na ikiwa I’tikaaf itapitiwa na Ijumaa, basi inakuwa ni bora zaidi.

 

I’tikaaf haina muda maalumu kwa mujibu wa kauli sahihi zaidi za ‘Ulamaa, na pia haina sharti kuwa lazima mtu awe amefunga (Swawm), lakini akiwa amefunga inakuwa bora zaidi.

 

Muda mzuri zaidi wa kukaa I’tikaaf ni katika kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhwaan kwa kumfuata Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  ambaye alikuwa akikaa I’tikaaf katika kumi hili na kutoka moja kwa moja baada ya kumalizika. Alikuwa akiianza Alfajiri ya tarehe 21 ya Ramadhwaan hadi mwisho.

 

 

Mwenye kukaa I’tikaaf anaruhusiwa kutenga kijieneo chake ndani ya Msikiti ili aweze kupumzika na kulala wakati anapohitajia kufanya hivyo. Na wakati ‘ibaadah yake inaendelea, anatakikana akithirishe kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kusoma Qur-aan, kuomba maghfirah, na kuomba du’aa badala ya kujishughulisha na mambo ya kidunia ambayo aslani ameyasusa kwa ajili ya I’tikaaf yake.

 

 

Hakuna ubaya kutembelewa na watu kama watahitaji kufanya hivyo na kuzungumza naye. Wakeze Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  walikuwa wakimtembelea na kuzungumza naye. Mara moja mkewe Swafiyyah alimtembelea, akazungumza naye, na wakati alipoondoka, alikwenda naye mpaka kwenye mlango wa Msikiti. Na hili linaonyesha kuwa hakuna ubaya kufanya hivyo.

 

 

Masharti ya I’tikaaf:

 

 

1- Kuwa Mwislamu.

 

 

2- Kuwa na akili.

 

 

3- Kuweka niyya ya kujikurubisha kwa Allaah (‘Azza wa Jalla) kama zilivyo amali nyinginezo.

 

 

4- Wakati wa I’tikaaf uwe muda ambapo Swawm inasihi. Haijuzu kukaa I’tikaaf siku ya ‘Iyd Al-Fitwr au ‘Iyd Al-Adhw-haa kwa kuwa ni haramu kuwa katika Swawm.

 

 

5-  Ifanyike ndani ya Msikiti mkubwa ambapo watu huswalia jamaa. Kwa maana hiyo, haifai I’tikaaf kwenye Msikiti mdogo wa zawiya au nyumbani. Hii ni kutokana na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَلَا تُبَاشِرُوهُنَّ وَأَنتُمْ عَاكِفُونَ فِي الْمَسَاجِدِ ۗ

Na wala msiwaingilie hali ya kuwa nyinyi wenye kukaa i’tikaaf Misikitini. [Al-Baqarah: 186]  

 

 

6- Msikiti uwe ni mmoja tu. Haifai kufanyia I’tikaaf moja kwenye Misikiti miwili kwa kukaa kwenye Msikiti mmoja baadhi ya siku na kumalizia zingine kwenye Msikiti mwingine.

 

 

7- Asitoke Msikitini ila kwa dharura tu.

 

 

 

 

Share