19-Hadiyth Za Ramadhwaan Na Mafunzo: Sifa Za Laylatul-Qadr

 

Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo

 

19-Sifa Za Laylatul-Qadr

 

 

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَة رَضِيَ اللَّه عَنْهُ قَالَ : لَمَّا حَضَرَ رَمَضَان قَالَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ  ((قَدْ جَاءَكُمْ شَهْرُ رَمَضَان شَهْرٌ مُبَارَكٌ اِفْتَرَضَ اللَّهُ عَلَيْكُمْ صِيَامَهُ تُفْتَح فِيهِ أَبْوَاب الْجَنَّة وَتُغْلَق فِيهِ أَبْوَابُ الْجَحِيم وَتُغَلُّ فِيهِ الشَّيَاطِين فِيهِ لَيْلَة خَيْرٌ مِنْ أَلْف شَهْر مَنْ حَرُمَ خَيْرهَا فَقَدْ حُرِمَ)) وَرَوَاهُ النَّسَائِيّ

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Huraryah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba ilipofika Ramadhwaan, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Umekujieni mwezi wa Ramadhwaan, ni mwezi wa Baraka.  Imefanywa Swawm kwenu kuwa ni fardhi, milango ya Jannah hufunguliwa na milango ya moto hufungwa na mashaytwaan hufungwa. Katika mwezi huu, kuna usiku ulio bora kuliko miezi elfu.  Atakayenyimwa kheri zake, basi hakika amenyimwa!)) [An-Nasaaiy]

 

Mafunzo:

 

 

Ni vipi Mwislamu ataujua usiku huo? Kuna baadhi ya alama zilizothibitishwa na Hadiyth za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Kati ya hizo ni:

 

 

1-Mwezi kuwa na umbo la nusu sinia kutokana na Hadiyth:

 

عَنْ أَبِي حَازِمٍ، عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ،  رضى الله عنه  قَالَ تَذَاكَرْنَا لَيْلَةَ الْقَدْرِ عِنْدَ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم فَقَالَ: ((أَيُّكُمْ يَذْكُرُ حِينَ طَلَعَ الْقَمَرُ وَهُوَ مِثْلُ شِقِّ جَفْنَةٍ)) مسلم

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Haazim, kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyesema: “Tulitajiana Laylatul-Qadr kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  naye akasema: ((Yupi kati yenu ana kumbuka wakati ulipochomoza mwezi ukiwa mithili ya nusu sinia?)) [Muslim]

 

Na hapa kuna ishara kuwa usiku wa Laylatul Qadr unakuwa katika kumi la mwisho, kwa kuwa mwezi hauwi katika picha hiyo, isipokuwa katika kumi la mwisho la mwezi wa Hijriyyah.

 

 

2-Ni usiku wake kuwa na nuru, na utulivu, na hali ya hewa ya wastani. Ni kwa Hadiyth isemayo:

 

وَهِيَ لَيْلَةٌ طَلْقَةٌ بَلْجَةٌ لَا حَارَّةٌ وَلَا بَارِدَةٌ ،

((Nao ni usiku mwangavu, uliotulia, usio na joto wala baridi)) [Hadiyth Marfuw’ kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Ibn Khuzaymah (2190)]

 

 

Zingine ni kama Mwislamu kujisikia hali nzuri ya kisaikolojia, uchangamfu wa mwili, khushuu ya moyo na kadhalika.

 

 

La muhimu kwa Mwislamu ili aweze kuupata usiku huo, ni kujitahidi kuanzia mwanzo wa mwezi hadi mwisho kufanya ‘ibaadah kwa nguvu zake zote, na ahakikishe kuwa hakuna usiku wowote wa Ramadhwaan unaompitia bila kufanya ‘ibaadah ila kwa udhuru.

 

 

 

 

Share