14-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Biashara: Mlango Wa Qiraadhw

 

بُلُوغُ الْمَرام

Buluwgh Al-Maraam

 

كِتَابُ اَلْبُيُوعِ

Kitabu Cha Biashara

 

بَابُ اَلْقِرَاضِ

14-Mlango Wa Qiraadhw[1]

 

 

 

 

 

765.

عَنْ صُهَيْبٍ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ أَنَّ اَلنَّبِيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ قَالَ: {ثَلَاثٌ فِيهِنَّ اَلْبَرَكَةُ: اَلْبَيْعُ إِلَى أَجَلٍ، وَالْمُقَارَضَةُ، وَخَلْطُ اَلْبُرِّ بِالشَّعِيرِ لِلْبَيْتِ، لَا لِلْبَيْعِ} رَوَاهُ اِبْنُ مَاجَهْ بِإِسْنَادٍ ضَعِيفٍ

 Kutoka kwa Swuhayb[2] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mambo matatu ndani yake kuna Baraka: kuuza kwa muda maalumu, Muqaaradhwah na kuchanganya ngano na shayiri[3] kwa matumizi ya nyumbani si kwa kuuza.” [Imetolewa na Ibn Maajah kwa Isnaad dhaifu]

 

 

 

766.

وَعَنْ حَكِيمِ بْنِ حِزَامٍ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ {أَنَّهُ كَانَ يَشْتَرِطُ عَلَى اَلرَّجُلِ إِذَا أَعْطَاهُ مَالًا مُقَارَضَةً: أَنْ لَا تَجْعَلَ مَالِي فِي كَبِدٍ رَطْبَةٍ، وَلَا تَحْمِلَهُ فِي بَحْرٍ، وَلَا تَنْزِلَ بِهِ فِي بَطْنِ مَسِيلٍ، فَإِنْ فَعَلْتَ شَيْئًا مِنْ ذَلِكَ فَقَدَ ضَمِنْتَ مَالِي} رَوَاهُ اَلدَّارَقُطْنِيُّ، وَرِجَالُهُ ثِقَاتٌ 

وَقَالَ مَالِكٌ فِي " اَلْمُوَطَّأِ " عَنْ اَلْعَلَاءِ بْنِ عَبْدِ اَلرَّحْمَنِ بْنِ يَعْقُوبَ، عَنْ أَبِيهِ، عَنْ جَدِّهِ: {أَنَّهُ عَمِلَ فِي مَالٍ لِعُثْمَانَ عَلَى أَنَّ اَلرِّبْحَ بَيْنَهُمَا} وَهُوَ مَوْقُوفٌ صَحِيحٌ 

Kutoka kwa Hakiym bin Hizaam (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa: “Alikuwa anampa mtu masharti anapompa mali kwa Muqaaradhwah akimuambia: Usifanyie biashara mali yangu katika viumbe vyenye uhai, wala usiibebe baharini, wala usiteremke nayo maporomoko ya mito; utakapofanya hivyo utaidhamini mali yangu.” [Imetolewa na Ad-Daaraqutwniyy na wapokezi wake ni madhubuti]

Maalik amesema katika kitabu chake “Al-Muwatwa” kutoka kwa Al-‘Alaa[4] bin ‘Abdir-Rahmaan bin Ya’quwb naye kutoka kwa baba yake[5] kutoka kwa babu yake[6]: “Kwamba yeye alifanyia biashara mali ya ‘Uthmaan kwa sharti ya kugawana faida baina yao.”[7] Hadiyth hii ni Mawquwf.

 

[1] Qiraadhw na Muqaaradhw yote ni majina ya kitu kimoja; ni mtu ampe mwenzie mali afanyie biashara na mwingine atatoa nguvu za kufanyia kazi, faida itakayopatikana watagawana, kama washirika. Kama kutakuwa na hasara, itaangukia katika rasilimali aliyotoa muekezaji. Kwa jina lingine huitwa Mudhwaarabah.

 

[2] Huyu ni Abuu Yahya Swuhayb bin Sinaan bin Maalik Ar-Rumi, Abuu Yahya. Alikuwa mwarabu wa kabila la An-Nimir bin Qaasitw bin Waail ambaye alichukuliwa mateka na Waroma na ndipo alipopata jina Ar-Rumi, akakulia kwao, na akawa miongoni mwao. Inasemekana kuwa alipobaleghe na kuwa mkubwa alikimbia na kurudi Makkah na akawa katika wafuasi wa ‘Abdullaah bin Jad’an. Inasemekana kuwa mmoja katika watu wa kabila la Baniy Kalb alimnunua na akamleta Makkah. ‘Abdullaah bin Jad’an akamnunua. Swuhayb alikuwa Swahaba mkubwa ambaye alisilimu mapema, alipata mateso kwa ajili ya dini yake. Alihamia Madiynah na kufariki Madiynah mwaka wa 38 Hijriyyah.

 

[3] Shayiri: nafaka inayofanana na ngano inayotumika kwa chakula.

 

[4] Huyu ni Abuu Sibli Al-‘Alaa bin ‘Abdir-Rahmaan bin Ya’quwb Al-Juhani, muachwa huru wa Al-Huraaqa Al-Madaniy. Alikuwa katika Taabi’iyna maarufu wa kizazi cha tano. Alikuwa ni mkweli lakini alikuja kuchanganyikiwa kuhusu Hadiyth. Ahmad na wengineo wanaithibitisha uaminifu wake. Al-Waaqidi anasema kuwa alikufa wakati wa ukhalifa wa Al-Manswuwr.

 

[5] ‘Abdur-Rahmaan bin Ya’quwb Al-Juhani alikuwa miongoni mwa Taabi’iyna na alikuwa katika kizazi cha tatu. Alichukua Hadiyth za Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) kutoka kwa baba yake, Abuu Hurayrah na Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy.

 

[6] Ya’quwb Al-Juhani alikuwa ni muachwa huru wa Al-Huraaqa na alikuwa kiongozi katika kizazi cha pili katika Taabi’iyna. Aliishi wakati wa ‘Umar bin Al-Khatwaab na miongoni mwa wapokezi wachache wa Hadiyth

 

[7] Al-Mudhwaarabah au Al-Qiraadhw ni aina za mikataba. Ambayo fidia inasamehewa kwa watu. Kama hasara inatokana na uzembe au makossa ya mfanyakazi, atawajibika kwa hilo. Vinginevyo, hawajibiki. Hivyo hivyo, kutekeleza kinyume na maagizo au maelekezo ya muekezaji, mshirika katika biashara atawajibika na hasara iliyotokea.

Share