004-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Je, Pombe Ni Najsi?

 

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

004-Je, Pombe Ni Najsi?

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Wanazuoni wamehitilafiana juu ya hukmu ya pombe katika kauli mbili:

 

Kauli ya kwanza:

 

Pombe ni najsi.

Huu ni mwelekeo wa Jamhuri ya Maulamaa wakiwemo Maimamu wanne. Shaykh wa Uislamu yupo katika kundi hili. Na hoja yao ni Neno Lake Subhaanah:

 

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالأَنصَابُ وَالأَزْلاَمُ رِجْسٌ مِّنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ فَاجْتَنِبُوهُ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ))

((Enyi walioamini! Bila shaka ulevi, kamari, kuabudu masanamu na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya shaytwaan. Basi jiepusheni navyo ili mpate kufanikiwa)). [Al Maaidah 5:90].

Wanasema kwamba uchafu "rijsu" ni najsi, na kwa hivyo, wamehukumu kuwa pombe yenyewe ni najsi ya kihisia.

 

Kauli ya pili:

 

Pombe ni twahara.

Rai hii wameisema akina Rab-y'a, Al-Layth, Al-Muzany na watangu wema wengineo. Na imetiliwa nguvu na Ash-Shawkaany, As Swan-’aaniy, Ahmad Shaakir na Al-Albaaniy (Allaah Awarehemu). Kauli hii ndio yenye nguvu kwa dalili zifuatazo:

 

1- Ni kwamba katika Aayah hakuna dalili juu ya unajsi wa pombe. Na hii ni kwa njia zifuatazo:

 

(a) Ni kwamba neno uchafu "rijsu", ni katika visawe, kwani linabeba maana tofauti. [Angalia kitabu cha An-Nihaaya cha Ibn Al-Athyr pamoja na Lisaan Al-‘Arab, Mukhtaar As-Swihaah na Tafsiyr mbalimbali]. Kati ya maana hizo ni kitu kichafu, kitu kilichoharamishwa, kitu kibaya, adhabu, laana, ukafiri, shari, dhambi, najsi na kadhalika.

 

(b) Ni kwamba "sisi hatujakuta" au kugundua kauli ya mwanasalafi yeyote aliyefasiri "Ar-Rijsu" katika Aayah hii kwa maana ya najsi, bali Ibn 'Abbaas amesema kuwa "Ar-Rijsu" ni hasira, wakati Ibn Zayd amesema kwamba "Ar-Rijsu” ni shari.

 

(c) Kwamba neno "rijsu", mbali na Aayah hii, limekuja katika Kitabu cha Allaah katika pahala patatu, na hakuna pahala popote kati yake ambapo "rijsu" ina maana ya najsi. Katika Neno Lake Subhaanah: 

((كَذَلِكَ يَجْعَلُ اللّهُ الرِّجْسَ عَلَى الَّذِينَ لاَ يُؤْمِنُون))

Hivyo ndivyo Allaah Anavojaalia unajisi (na adhabu) juu ya wale wasioamini. [Al-An’aam: 125]

neno "Ar-Rijsu" hapa, maana yake ni adhabu.

Na katika neno Lake Subhaanah kuhusu wanafiki:

إِنَّهُمْ رِجْسٌ ۖ وَمَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ

hakika wao ni najsi, na makazi yao ni Jahannam. Ni jazaa kwa yale waliyokuwa wakiyachuma. [At-Tawbah: 95]

 

..makusudio ni kuwa vitendo vyao ni vichafu, yaani vibaya.

 

Na katika Neno Lake Subhaanah:

((فَاجْتَنِبُوا الرِّجْسَ مِنَ الْأَوْثَانِ))

Basi jiepusheni na uchafu wa (kuabudu) masanamu [Al-Hajj: 30]

 

..masanamu yameitwa uchafu kwa vile yenyewe ndio  sababu ya makamio na adhabu, na wala makusudio sio najsi ya kukamatika, kwani mawe yenyewe na masanamu si najsi.

(d) Na ilipotuka katika Aayah kuwa pombe ipo sanjari na masanamu na upigaji ramli, hilo limekuwa ni kielelezo chenye kuengua maana ya uchafu kupelekea katika unajsi usio wa kisharia. Na ndivyo hivyo hivyo katika Kauli Yake Subhaanah:

((إِنَّمَا الْمُشْرِكُونَ نَجَسٌ ))

((Hakika washirikina ni najsi)). [At Tawbah (9:28)]

 

..zilipokuja dalili sahihi zinazothibitisha kuwa miili ya washirikina si najsi.

 

 

(e) Kwamba kuharamishwa pombe, hakuwajibishi kuwa ni najsi, kwani tunaona ni haramu kuvaa hariri na dhahabu ingawa vyenyewe ni twahara ikiwa ni udharura wa kisharia na kwa makubaliano ya wote.

 

(f) Kwamba neno "Ar-Rijsu" katika Aayah limeainishwa (muqayyad) kuwekwa ndani ya (kazi ya shaytwaan). Kwa hiyo ni uchafu wa kivitendo, kwa maana ya kuwa ni kitu kibaya au kilichoharamishwa au dhambi, na wala si uchafu wa kiini cha kitu wa kuvifanya vitu hivi kuwa ni najsi.

 

2- Na kati ya vinavyotolewa ushahidi juu ya utwahara wa pombe ni aliyoyasema Anas katika kisa cha kuharamishwa pombe. Anasema: "…Na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwamrisha mwenye kunadi atangaze: Jueni kwamba pombe imeharamishwa,…". Akasema: "Nikatoka nikaimwaga, ikatiririka katika barabara za Madiynah” [Swahiyh Al-Bukhaariy (2332), na Muslim (1980)].

 

 

3- Na katika kisa cha mtu aliyekuwa na mapipa mawili ya pombe

 

((…Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Hakika Allaah Aliyeharamisha kuinywa, Ameharamisha kuiuza)). Mtu yule akayafungulia mapipa mawili mpaka vikamalizika vilivyomo ndani yake…).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa ‘ikhraaj” na Muslim, na Maalik (1543)].  

 

Na lau kama tembo ingelikuwa najsi, basi Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) angeliamrisha kumwagia maji juu ya ardhi ili kuitwaharisha kama alivyoamrisha kumwagia maji juu ya mkojo wa bedui, na angeliwaamuru kujikinga nayo.

 

4- Kwamba asili yake ni twahara, na hanukui kuhusu utwahara huo ila mnukuzi sahihi. Na kwa kuwa hakuna dalili yoyote inayothibitisha unajsi wake, pombe inabakia katika asili yake.

 

 

Share