07-Du'aa Za Ruqyah Na Tafsiri Zake: Kuomba Uongofu, Taqwa, Utakasifu na Utajiri wa Moyo

 

 

Du’aa Za Ruqyah (Kinga): Faida Na Sharh Zake

 

07-Kuomba Uongofu, Taqwa, Utakasifu na Utajiri wa Moyo

 

www.alhidaaya.com

 

   

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alikuwa akimwomba Allaah ('Azza wa Jalla)    akisema:

 

((اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ الْهُدَى، وَالتُّقَى، وَالْعَفَافَ، وَالْغِنَى))

((Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba hidaayah, taqwa, utakasifu, na utajiri)). [Imekharijiwa na Muslim 2721]

 

 

Faida Na Sharh:

 

Du’aa hii adhimu, imekusanya maombi manne makubwa na yenye shani ya juu kabisa ambayo kila mja anayeelekea kwa Allaah ('Azza wa Jalla)  anayapupia kutokana na umuhimu wake kwa hapa duniani na kesho Aakhirah.

 

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  ameanza kwa Al-Hudaa au  Hidaayah. Bila shaka hili ni ombi kubwa zaidi kwa mja.

 

الْهُدَى Al-Hudaa ni neno jumuishi linalohusiana na kila ambalo linahitajia uongofu katika mambo ya dunia na Aakhirah kati ya itikadi safi, utengenefu wa amali, kauli na tabia.

 

 

التُّقَى At-Tuqaa ambalo ni sawa na At-Taqwaa (taqwa), ni jina jumuishi la utendaji wa yote Aliyoyaamuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  na kuyaacha yote Aliyoyakataza. Na asili ya neno hili ni ngao au kizuizi, kwa maana kwamba Muislamu anaweka ngao kati yake na adhabu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) kwa kuwajibika na yale yote yatakayomwepushia ghadhabu za Allaah ('Azza wa Jalla) . Hivyo kumwomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  ngao hii, ni muhimu sana kwa Muislamu.

 

 

الْعَفَافَ  Al-'Afaaf  ni kusafika na mambo yote yasiyofaa, na kujizuia na matamanio na tamaa za kidunia.  Al-‘Afaaf inajumuisha kuwa mbali kwa mfano na aina zote za zinaa kama zinaa ya kuangalia, zinaa ya kugusa, zinaa ya kusikiliza, zinaa ya utupu, kujihisi au kujiona bora kuliko wengine na mengineyo yanayofanana na hayo kama chumo la haramu na kadhalika. [Sharhu Riyaadhw Asw-Swaahiliyna, Al ‘Allaamah Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu-Allaah) 2/333]

 

 

 

الْغِنَى Alghinaa, ni utajiri na uliokusudiwa hapa ni utajiri wa moyo. Ni mtu kukinai kile alichonacho na kutovikodolea macho wanavyovimiliki watu wengine. Sifa hii Anaipenda Allaah (‘Azza wa Jalla).

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   amrsema:

 

((إِنَّ اللَّهَ يُحِبُّ الْعَبْدَ التَّقِيَّ، الْغَنِيَّ، الْخَفِيَّ))

((Hakika Allaah Anampenda mja mwenye taqwa, tajiri wa moyo, asiyejitangaza)). [Swahiyh Muslim 2965]

 

 

Al-‘Allaamah ‘Abdur-Rahmaan bin Naaswir As-Sa'diy (Rahimahu-Allaah) akiizungumzia du’aa hii ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alisema:  "Du’aa hii ni du’aa kusanyifu zaidi na yenye manufaa makubwa zaidi. Inakusanya maombi ya kheri za dunia na za Aakhirah, kwani Al-Hudaa ni elimu yenye manufaa, At-Tuqaa ni kufanya amali njema chanya na kuacha aliyoyakataza Allaah na Rasuli Wake. Kwa haya, Dini inatengenea, kwani Dini ni elimu yenye manufaa, na maarifa ya kweli ndio hidaayah. Na kumtii Allaah na Rasuli Wake ndio At-Tuqaa, na Al-Afaaf na Al-Ghinaa kunajumuisha kutowategemea viumbe, kutoufungamanisha moyo nao, kumtegemea Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Peke Yake katika rizk na kutosheka na kinachopatikana. Kwa haya, furaha ya dunia na Aakhirah inatimu, na utulivu wa moyo unapatikana. Na haya ndio maisha mema bora. Na mwenye kuruzukiwa hidaayah, taqwa, utwaharifu na utajiri wa moyo, basi kapata furaha mbili, kapata kila linalotakiwa, na ameokoka na kila linaloogopwa. [Kitabu cha Bahjat-Quluwbil Abraar uk. 249]

 

 

 

Share