024-Majina Ya Allaah Na Sifa Zake: AL-MUSWAWWIRU

 

 

الْمُصَوِّر

AL-MUSWAWWIRU

 

 

 Al-Muswawwir: Muundaji Sura

 

           

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

هُوَ اللَّـهُ الْخَالِقُ الْبَارِئُ الْمُصَوِّرُ ۖ  

Yeye Ndiye Allaah, Muumbaji, Mwanzishi viumbe bila kasoro, Muundaji sura na umbile. [Al-Hashr: 24]

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ndiye Muundaji sura na umbile: Ambaye ameunda sura za viumbe Wake vile Atakavyo, na Akaunda sura za viumbe vyote vilivyomo ulimwenguni, na kuvipanga na Akatoa katika kila kimoja sura maalum na umbile la kipekee ambalo kila kiumbe anatofautika kwa viumbe vingine juu ya  kuwa viumbe vya  Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  ni vingi mno visivyowezekana kuhesabika!  Allaah (Subhaanahau wa Ta'aalaa) Ameumba kila sura na Akitaka kitu husema: Kun! (Kuwa) na kikawa katika wasifu Autakao na sura Aiachaguayo.  Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa): 

 

الَّذِي خَلَقَكَ فَسَوَّاكَ فَعَدَلَكَ ﴿٧﴾

Ambaye Amekuumba Akakusawazisha (umbo sura, viungo) na Akakupima na kukulinganisha sawa.

 

فِي أَيِّ صُورَةٍ مَّا شَاءَ رَكَّبَكَ ﴿٨﴾

Katika sura Aliyotaka Akakutengeneza. [Al-Infitwaar: 7-8]

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameanzisha uumbaji wake katika sura mbali mbali na maumbo mengi yanayotofautiana, urefu, ufupi, dume na jike, kila mmoja na sura na umbile lake. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَلَقَدْ خَلَقْنَاكُمْ ثُمَّ صَوَّرْنَاكُمْ ثُمَّ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ لَمْ يَكُن مِّنَ السَّاجِدِينَ ﴿١١﴾

Na kwa yakini Tumekuumbeni kisha Tukakutieni sura; kisha Tukawaambia Malaika: “Msujudieni Aadam.” Wakasujudu isipokuwa Ibliys hakuwa miongoni mwa waliosujudu. [Al-A’raaf: 7]

 

 

Na Anasema vile vile Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِالْحَقِّ وَصَوَّرَكُمْ فَأَحْسَنَ صُوَرَكُمْ ۖ وَإِلَيْهِ الْمَصِيرُ﴿٣﴾

Ameumba mbingu na ardhi kwa haki, na Akakutengenezeni sura, kisha Akafanya nzuri zaidi sura zenu, na Kwake ndio mahali pa kuishia. [At-Taghaabun: 3]

 

 

Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah; Al-Muswawwiru:

 

 

1-Tafakari na tambua Tawhiyd ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika uundaji Wake katika viumbe Vyake.  Tafakari uundaje Wake wa sura za  wana Aadam na rangi zao, miili yao. Tafakari pia wanyama mbali mbali wa angani, baharini, na ardhini wakiwa katika sura na shepu na rangi mbali mbali wanaopendeza na wanaotisha. Tafakari pia vitu vinginevyo Alivyoviumba vilivyo katika shepu na rangi mbalimbali kama mbingu, jua, mwezi, sayari nyenginezo, bahari, milima na kadhalika.  Tafakari pia miti,  mauwa, matunda, mboga na kadhalika vyote vikiwa katika shepu na rangi mbali mbali vyenye ladha tofauti; tamu, kali chungu. Je kuna Al-Muswawwiru kama Yeye? Ndio Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anawaambia wanamoshirkisha kwamba hivyo ndivyo viumbe na vitu Alivyoviumba Yeye, basi hebu nao waonyeshe ambavyo walivyoviumba wao:

 

 خَلَقَ السَّمَاوَاتِ بِغَيْرِ عَمَدٍ تَرَوْنَهَا ۖ وَأَلْقَىٰ فِي الْأَرْضِ رَوَاسِيَ أَن تَمِيدَ بِكُمْ وَبَثَّ فِيهَا مِن كُلِّ دَابَّةٍ ۚ وَأَنزَلْنَا مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَنبَتْنَا فِيهَا مِن كُلِّ زَوْجٍ كَرِيمٍ ﴿١٠﴾

(Allaah) Ameumba mbingu bila ya nguzo mnaziona, na Akatupa katika ardhi milima isikuyumbieni yumbieni, na Akaeneza humo kila viumbe vinavyotembea. Na Tukateremsha kutoka mbinguni maji, Tukaotesha humo kila aina ya mimea mizuri yenye manufaa.

 

هَـٰذَا خَلْقُ اللَّـهِ فَأَرُونِي مَاذَا خَلَقَ الَّذِينَ مِن دُونِهِ ۚ بَلِ الظَّالِمُونَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿١١﴾

Huu ni uumbaji wa Allaah, basi nionyesheni nini walichokiumba wasiokuwa Yeye. Bali madhalimu wamo katika upotofu bayana. [Luqmaan: 11]

 

 

 

2-Mshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa neema Zake na hikma Yake kubwa kukuumba na kukuunda katika sura nzuri kabisa; kila kiungo Amekiumba mahali pake panapostahiki. Tafakari lau ingelikuwa si Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ndiye Muundaji wa sura za viumbe, basi kungelikuwa na kasoro nyingi katika uuandaji huo wa viumbe. Anasema Allaah (‘Azza wa Jalla):

 

لَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ فِي أَحْسَنِ تَقْوِيمٍ ﴿٤﴾

Kwa yakini Tumemuumba mwana Aadam katika umbile bora kabisa. [At-Tiyn: 4]

 

 

3-Muombe Al-Muswawwiru Aendelee kukuweka katika hali ya ukamilifu ya uundaji Wake kwani kama isemwavyo: “Mwana Aadam hakukamilika mpaka kufa kwake.” Basi wangapi wameumbulika sura na umbo baada ya maafa wakapoteza viungo na sura zao nzuri?

 

 

4-Tumia viungo vya mwili wako katika yale ya kumridhisha Al-Muswawwiru, ikiwa mwanamke umejaaliwa sura nzuri kabisa basi jisitiri na jiepushe na kujishaua kwa kudhirisha sura yako kwa wanaume wasio mahram wako jambo ambalo litapeleka katika maasi, wala usitumie neema hiyo ya kujaaliwa na sura nzuri katika maasi yoyote yale ya Allaah ('Azza wa Jalla) kwasababu  kila kiungo kitashuhudia maovu yatakayotendwa na viungo hivo. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَيَوْمَ يُحْشَرُ أَعْدَاءُ اللَّـهِ إِلَى النَّارِ فَهُمْ يُوزَعُونَ﴿١٩﴾

 

Na Siku watakayokusanywa maadui wa Allaah kwenye moto, nao watakusanywa kupangwa safusafu.

 

حَتَّىٰ إِذَا مَا جَاءُوهَا شَهِدَ عَلَيْهِمْ سَمْعُهُمْ وَأَبْصَارُهُمْ وَجُلُودُهُم بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ﴿٢٠﴾

 

Mpaka watakapoufikia yatashuhudia dhidi yao, masikio yao, na macho yao, na ngozi zao kwa yale waliyokuwa wakiyatenda.

 

 

وَقَالُوا لِجُلُودِهِمْ لِمَ شَهِدتُّمْ عَلَيْنَا ۖ قَالُوا أَنطَقَنَا اللَّـهُ الَّذِي أَنطَقَ كُلَّ شَيْءٍ وَهُوَ خَلَقَكُمْ أَوَّلَ مَرَّةٍ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ﴿٢١﴾

 

Na wataziambia ngozi zao: “Mbona mnashuhudia dhidi yetu?” Zitasema: “Ametutamkisha Allaah Ambaye Ametamkisha kila kitu, Naye Ndiye Aliyekuumbeni mara ya kwanza na Kwake mtarejeshwa.

 

 

وَمَا كُنتُمْ تَسْتَتِرُونَ أَن يَشْهَدَ عَلَيْكُمْ سَمْعُكُمْ وَلَا أَبْصَارُكُمْ وَلَا جُلُودُكُمْ وَلَـٰكِن ظَنَنتُمْ أَنَّ اللَّـهَ لَا يَعْلَمُ كَثِيرًا مِّمَّا تَعْمَلُونَ﴿٢٢﴾

 

“Na hamkuwa mkijisitiri hata yasishuhudie masikio yenu, na wala macho yenu, na wala ngozi zenu; lakini mlidhania kwamba Allaah Hajui mengi katika yale mnayoyatenda. [Fusw-Swilat: 19-22]

 

 

Na Ansema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

يَوْمَ تَشْهَدُ عَلَيْهِمْ أَلْسِنَتُهُمْ وَأَيْدِيهِمْ وَأَرْجُلُهُم بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٢٤﴾

Siku zitakaposhuhudia dhidi yao ndimi zao, na mikono yao, na miguu yao kwa yale waliyokuwa wakiyatenda.  [An-Nuwr: 24]

 

 

5-Ridhika na vile Alivyokuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) wala usilalamike au kujiumbua kwa kubadilisha umbo lako na sura yako ukataka kujiongezea ukubwa au kupunguza udogo katika viungo vya mwili wako. Hii ni katika uchochezi wa shaytwaan ambaye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amemlaani anayejiumbua sura na maumbile yake.  [Rejea An-Nisaa: 117-121]

 

 

6-Unapoona kilema usimcheke bali mshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuwa Amekukamilisha katika kukuunda kwako na pindi unapomuona kilema sema du’aa ya Sunnah kama alivyotufundisha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye amesema:

 

((مَنْ راْ مُبْتَل فَقال: الْحَمْـدُ للهِ الّذي عافاني مِمّا ابْتَـلاكَ بِهِ، وَفَضَّلَـني عَلى كَثيـرٍ مِمَّنْ خَلَـقَ تَفْضـيلا، لَمْ يُصِبْهُ ذالك الْبَلاء))

 

((Atakayemuona aliyepatwa na mtihani akasema:

 

الْحَمْـدُ للهِ الّذي عافاني مِمّا ابْتَـلاكَ بِهِ، وَفَضَّلَـني عَلى كَثيـرٍ مِمَّنْ خَلَـقَ تَفْضـيلا.

Himdi ni za Allaah, Ambaye Ameniepusha na kile Alichokupa mtihani na Akanifanya mimi kuwa bora kuliko wengi miongoni mwa Aliowaumba.”

 

Basi hatofikwa na mtihani huo)) [Hadiyth ya Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) ameipokea At-Tirmidhiy (5/493-4), Ibn Maajah. Angalia: Swahiyh At-Tirmidhiy (3/153)]

 

 

 

7-Jiepushe na kumuiga Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika uundaji Wake kwa kuchora picha za viumbe na kuzitia sura jambo ambalo limeharamishwa katika nususi kadhaa zikiwemo:

 

عَنْ عَائِشَةَ (رَضِيَ اللهُ عَنْهَا) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم) قَال: ((أَشَدُّ النَّاسِ عَذَابًا يَوْمَ القِيَامَةِ الَّذِينَ يُضَاهِئُونَ بِخَلْقِ اللَّهِ))

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللهُ عَنْهَا) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Watakaokuwa na adhabu kali Siku ya Qiyaamah ni wanaomuiga Allaah katika uumbaji Wake)) [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Na pia:

 

عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ ((مَنْ صَوَّرَ صُورَةً فِي الدُّنْيَا كُلِّفَ أَنْ يَنْفُخَ فِيهَا الرُّوحَ وَلَيْسَ بِنَافِخٍ))

Kutoka kwa  Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) Hadiyth Marfuw’: ((Atakayechora picha duniani atalazimishwa aitie roho (Siku ya Qiyaamah), na wala hatoweza)) [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Na pia:

 

عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) :  سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) يَقُولُ: ((كُلُّ مُصَوِّرٍ فِي النَّارِ يُجْعَلُ لَهُ بِكُلِّ صُورَةٍ صَوَّرَهَا نَفْسٌ يُعَذَّبُ بِهَا فِي جَهَنَّمَ))

Kutoka kwa  Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: ((Kila mchoraji picha atakuwa motoni. Kila picha aliyoichora, itatiwa roho nayo itamuadhibu katika Jahannam)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 

Share