013-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Baadhi Ya Adabu Za Kustanji

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

013-Baadhi Ya Adabu Za Kustanji

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Kati ya adabu ambazo inatakikana mtu ajipambe nazo wakati wa kustanji ni:

 

1- Asistanji kwa mkono wa kulia

 

Ni kutokana na Hadiyth ya Abuu Qataadah, amesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( لا يمسكن احدكم ذكره بيمينه وهو يبول، ولا يتمسح من الخلاء بيمينه، ولا يتنفس في الاناء))

((Asikamate kabisa mmoja wenu dhakari yake kwa mkono wake wa kulia wakati anakojoa, wala asijisafishe haja kwa mkono wake wa kuume, wala asipumulie ndani ya chombo)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy ( 153) Muslim (267) na wengineo].

 

Na imepokelewa toka kwa Salmaan, amesema: “Mtu mmoja aliniambia: “Hakika mwenzenu huyu anawafundisheni hata kwenda haja kubwa”. Akasema (Salmaan): “Ndiyo. Ametukataza kuelekea Qiblah wakati wa kukidhi haja kubwa au ndogo, ametukataza kustanji kwa mikono yetu ya kulia, au kustanji kwa chini ya vijiwe vitatu”.[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (262), Abuu Daawuud (7), At-Tirmidhiy (16) na An-Nasaaiy (1/16).  

 

 

2- Asiuguse utupu kwa mkono wake wa kulia

 

Ni kwa Hadiyth ya Abuu Qataadah iliyotangulia.

 

3- Ausugue mkono wake kwenye udongo, au auoshe kwa sabuni na mfano wake baada ya kustanji

 

Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah, amesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akiingia msalani, nilikuwa nikimpelekea maji katika kijidoo kidogo, halafu hustanji na kisha huupangusa mkono wake juu ya ardhi”. [Hadiyth Hasan Lighayrihi. Imefanyiwa “ikhraaj” na …(45), Ibn Maajah (678) na An-Nasaaiy (1/45). Angalia Kitabu cha Al-Mishkaat (360)].

 

Hili linatiliwa nguvu na Hadiyth ya Maymuunah isemayo: “Kisha Rasuli alijimwagia maji juu ya utupu wake, akauosha kwa mkono wake wa kushoto, kisha akaupiga mkono wake juu ya ardhi, halafu akauosha”.[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (266) na Muslim (317)].

 

4- Aunyunyizie utupu wake maji pamoja na nguo yake baada ya kukojoa ili kuondosha shaka na wasiwasi

 

Imepokelewa na Ibn ‘Abbaas kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitawadha mara moja, halafu akaunyunyizia maji utupu wake. [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Ad-daaramiy (711) na Al-Bayhaqiy (1/161). Al-Albaaniy amesema katika kitabu cha Tamaam Al-Minnah (uk. 66) kwamba Sanad yake ni Swahiyh juu ya sharti ya Masheikh wawili].

 

 

Share