019-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Kupiga Mswaki

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

019-Kupiga Mswaki

 

 

 

Maana Yake Na Usharia Wake

 

Ni neno linalotokana na kitenzi (ساك) anaposugua. Ama maana ya kiistilahi ni kutumia kijiti au mfano wake kwenye meno ili kuondosha unjano na mabaki mengineyo.[Nayl Al-Awtwaar (1/102)].

 

Inapendeza zaidi kutumia mswaki nyakati zote kutokana na Hadiyth ya ‘Aaishah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( السواك مطهرة للفم، مرضات للرب))

((Mswaki ni utwaharisho kwa mdomo, na maridhio ya Mola)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (1/50), Ahmad (6/47, 62) na wengineo.]

 

Kupiga mswaki kunakuwa ni mustahabu zaidi katika nyakati zifuatazo:

 

 

1-     Wakati wa kutawadha

 

Ni kutokana na Hadiyth ya Abu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

 ((لَوْلَا أَنْ أَشُقَّ عَلَى أُمَّتِي لَأَمَرْتُهُمْ بِالسِّوَاكِ مع الوُضُوءٍ))

((Lau kama si kuuonea uzito umma wangu, basi ningeliwaamuru kupiga mswaki sambamba na wudhuu)).[Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad, nayo iko katika Swahiyh Al-Jaami’i (5316)].

 

 

2-     Wakati wa kuswali

 

Ni kutokana na Hadiyth ya Abu Hurayrah kwamba Rasuli  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

((لَوْلَا أَنْ أَشُقَّ عَلَى أُمَّتِي لَأَمَرْتُهُمْ بِالسِّوَاكِ عند كل صلاة))

((Lau kama si kuuonea uzito umma wangu, basi ningeliwaamuru kupiga mswaki kila wakati wa Swalaah)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (6813), na Muslim (252)].

 

 

3-     Wakati wa kusoma Qur-aan

 

Ni kutokana na Hadiyth ya ‘Aliyy anayesema: “Tumeamrishwa kupiga mswaki. Amesema (yaani Rasuli): ((Mja anaposimama katika Swalaah, humjia Malaika akasimama nyuma yake huku akiisikiliza Qur-aan na kumsogelea. Huendelea kusikiliza na kumjongelea hadi anakiweka kinywa chake kwenye kinywa chake. Na hapo mja hasomi Aayah yoyote, isipokuwa huingia ndani ya kinywa cha Malaika huyo)). [Al-Al Baaniy kasema ni Swahiyh. Al-Bayhaqy ameifanyia “ikhraaj” (1/246). Angalia kitabu cha Asw Swahiyhah (1213).

 

 

4-     Wakati mtu anapoingia nyumbani kwake

Ni kutokana na Hadiyth ya Al Miqdaam bin Shurayh toka kwa baba yake. Anasema:

“Nilimuuliza Aa’ishah: Ni jambo gani la kwanza alilokuwa akilifanya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anapoingia nyumbani? Akasema: Ni kupiga mswaki”.

 

5-     Wakati wa kuamka kwa ajili ya Swalaah ya Usiku

 

Ni kutokana na Hadiyth ya Hudhayf anayesema:

((Rasuli Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam alikuwa akiyasafisha meno yake kwa mswaki wakati anaposimama kuswali tahajjudi)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (246) na Muslim (255)].

 

Ni vizuri zaidi kutumia mswaki wa miti (Al Araak) wakati wa kupiga mswaki. Na kama haukupatikana, basi utatosheleza mswaki wa aina nyingine wenye uwezo wa kusafisha kinywa na kung’arisha meno. Ni kama miswaki ya brashi pamoja na dawa maalum za meno. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi

 

 

Share