Yajue Mambo Anayopaswa Kufanyiwa Mtu Akifariki

 

Yajue Mambo Anayopaswa Kufanyiwa Mtu Akifariki

 

Abuu 'Abdillaah

 

Alhidaaya.com

 

 

Yampasa Muislam ajiandae kufikiwa na mauti kwa kukithirisha (kufanya sana) matendo mema na kujiepusha na makatazo (vilivyoharamishwa). Vilevile mauti yawe akilini mwake, kwa maneno ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Zidisheni kukumbuka kiondoshacho ladha (yaani mauti)” 

 

[Hadiyth hii imepokewa na Imaam at-Tirmidhiy na akaithibitisha usahihi wake Imaam Al-Albaaniy katika kitabu chake Irwaaul-Ghaliyl uk. 682]

 

 

Anapofariki Muislam yampasa yule au wale waliopo pale karibu na maiti kumfanyia mambo yafuatayo:

 

 

1. Kuyafumba macho ya maiti huyo kwani Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyafumba macho ya Abu Salamah alipofariki kisha akasema: 

 

“Hakika macho yanafuata roho inapotolewa”. [Imesimuliwa na Imaam Muslim]

 

2. Avilainishe viungo vya maiti ili visikakamae.

 

3. Aifunike maiti hiyo kwa nguo ambayo itasitiri mwili mzima kwa kauli ya mama wa waumini ‘Aaishah:

 

“Hakika alipofariki Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifunikwa kwa nguo iliyomsitiri kote.” 

 

[Imesimuliwa na Imaam Al-Bukhaariy na Imaam Muslim]

 

4.  Waharakishe kuiandaa maiti, kuiosha, kuikafini, kuiswalia na kuizika. Kwani Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  

 

“Liharakisheni jeneza…”  [Imesimuliwa na Imaam Al-Bukhaariy na Imaam Muslim]

  

5.  Waizike katika mji au eneo alilofia kwa vile katika vita vya Uhud Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamrisha mashahidi wa vita wazikwe pahala pale walipofia wala wasihamishwe”. [Imepokewa na Ahlus Sunan: Ma-Imaam Abuu Daawuwd, An-Nasaaiy, At-Tirmidhiy, Ibn Maajah; na ameithibitisha usahihi wa Hadiyth hiyo Imaam Al-Albaaniy katika kitabu chake cha Ahkaamul Janaaiz uk. 14]

 

Share