023-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Kutawadha Kwa Maji Yanayochuruzika Toka Viungo Vya Wudhuu

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

023-Kutawadha Kwa Maji Yanayochuruzika Toka Viungo Vya Wudhuu

 

Alhidaaya.com

 

 

Maji yanayochuruzika toka kwenye viungo vya mwenye kutawadha na mfano wake, huitwa “maji yaliyotumika”. Na bila shaka Maulamaa wamehitalafiana kuhusu maji hayo kama yanapoteza sifa ya kuwa ni yenye kutwaharisha au la. 

 

Rai yenye nguvu ni kuwa maji hayo yanabakia ni yenye kutwaharisha madhali hayajapoteza jina la maji “mutwlaq na wala hayajachanganyika na najsi ikaathiri moja kati ya sifa zake.

 

Haya ndio madhehebu ya ‘Aliy bin Abi Twaalib, Ibn ‘Umar, Abuu Umaamah na watangu wema wengi. Ni mashuhuri pia katika madhehebu ya Maalik. Aidha, ni moja kati ya riwaya mbili zilizopokelewa toka kwa Ash-Shaafi’iy na Ahmad. Pia ni madhehebu ya Ibn Hazm na Ibn Al-Mundhir. Mwelekeo huu pia umekhitariwa na Shaykh wa Uislamu (Ibnu Taymiyah).  [Al-Mughny (1/31), Al-Majmuu (1/205), Al-Muhallaa (1/183), Majmuu Al-Fataawaa (20/519) na Al-Awswat (1/285)].

 

Kauli hii inatiliwa nguvu na dalili zifuatazo:

 

1- Kwamba asili ni kuwa maji ni twahara wala hayanajsiwi na chochote. Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema

((الماء طهور لا ينجسه شيئ))                                        

((Maji ni twahara, hayanajsiwi na chochote)).[Hadiyth Hasan. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (266), At-Tirmidhy (66) na An-Nasaaiy (1/173)].

 

Isipokuwa kama sifa yake moja itabadilika au yakapoteza jina la maji “mutwlaq” kwa kuchanganyika na kitu twahara.

 

2- Imethibiti kwamba Maswahaba walikuwa wakitumia mabaki ya maji aliyotawadhia Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). (Hii ni kwa dalili zifuatazo):

 

 

(a) Imepokelewa toka kwa Abuu Juhayfah akisema:

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitutokea mchana wa jua kali, akaja na maji ya kutawadhia kisha akatawadha. Hapo watu wakaanza kuchukua mabaki ya maji aliyotawadhia na kujipangusa nayo”.[Hadiyh Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (187)].

 

Al-Haafidh katika “Al-Fat-h” (1/353) anasema: “Inawezekana kuwa walichukua yale yaliyochuruzika toka kwenye viungo vya wudhuu vya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na hii ni dalili wazi kuwa maji yaliyotumika ni twahara.

 

 

(b) Na katika Hadiyth ya Al-Masuur bin Makhramah: “…na anapotawadha Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), walikuwa wakikaribia kupigana kugombea maji aliyotawadhia”.[Hadiyh Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (189)].

 

 

(c) Imepokelewa na Abuu Musa Al-Ash’ary kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliagizia bilauri ya maji. Akaoshea mikono yake na uso wake humo na akatema. Kisha akamwambia yeye (Abuu Muusa) na Bilaal: 

(( إشربا منه، وأفرغا على وحوهكما ونحوركما))                               

((Kunyweni humo, na yamiminieni kwenye nyuso zenu na shingo zenu)).[Hadiyh Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (188)].

 

 

3- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar akisema: “Katika enzi ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), wanaume na wanawake walikuwa wakitawadha wote pamoja”. [Hadiyh Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (193), Abuu Daawuud (79), An-Nasaaiy (1/57), na Ibn Maajah (381). Riwaya baada yake ni ya Abuu Daawuud kwa Sanad Swahiyh].

 

Na katika riwaya: Katika enzi ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), tulikuwa sisi na wanawake tukitawadha katika chombo kimoja tukiingiza mikono yetu ndani”.

 

 

4- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiogea kwa mabaki (ya maji) ya Maymunah. [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (323). Iko kwenye Swahiyh Mbili kwa tamko lisemalo: “Walikuwa wakiogea chombo kimoja”].

 

 

5- Imepokelewa toka kwa Al-Rubayi’i bin Mu’awwadh kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipangusa kichwa chake kwa mabaki ya maji yaliyokuwa mkononi mwake. [Hadiyth Hasan. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (130) na Ad Daaraqutwny (1/87)].

 

 

6- Ibn Al-Mundhir katika Al-Awswaat (1/288) amesema: “Na katika Ijma’a ya Maulamaa ni kwamba matone tone yaliyobakia katika viungo vya mwenye kutawadha au mwenye kuoga, na yale maji yaliyotona kwenye nguo zao, hayo yote ni twahara. Na hii ni dalili kuwa maji yaliyotumika ni twahara. Na kama ni twahara, basi hakuna maana kuzuia kutawadhia maji hayo bila ya hoja wanayoirejelea wale wenye rai tofauti na kauli”.

 

Inafaa kueleza hapa kwamba kundi la baadhi ya Maulamaa wamesema: “Haijuzu kutawadhia maji yaliyotumika”. Yamesemwa haya na Maalik, Al-Awzaa’iy, Ash-Shaafi’iy – katika riwaya moja kati ya mbili – na Abuu Haniyfah na wenzake. [Al-Istidhkaar (1/253), At-Tamhyid (4/43), Al-Mughny (1/19), na Al-Awswat (1/285)].

 

Maulamaa hawa hawana dalili yakinifu za kuridhisha. Mwenye kutaka, azirejee katika rejea tajwa.

 

 

 

 

Share