050-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Majosho Yaliyo Mustahabbu

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

050-Majosho Yaliyo Mustahabbu

 

Alhidaaya.com

 

1- Kwa ajili ya ‘Iyd mbili

 

Imepokelewa toka kwa Al-Faakih bin Sa'ad kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) alikuwa akikoga wakati wa ‘Iyd el fitr na ‘Iyd el adh-ha. Lakini Hadiyth hii ni Dhwa’iyf sana. [ Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Maajah (1316)].

 

Lakini inaweza kutolewa dalili juu ya kustahabiwa hilo kwa yaliyothibiti toka kwa 'Aliy bin Abi Twaalib na Ibn 'Umar kuwa imepokelewa toka kwa Zaadhaan kuwa mtu mmoja alimuuliza ‘Aliy Allaah Amridhie kuhusu kuoga. Akamjibu akimwambia:

"Oga kila siku ukipenda". Akasema: "Hapana. Kuoga kunakotakikana hasa". Akamwambia: "Siku ya Ijumaa, Siku ya Arafah, Siku ya Kuchinja na Siku ya Fitwr". [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ash-Shaafi'iy katika Musnadi yake (114) na kwa njia yake Al-Bayhaqiy 3/278)].

 

Na imepokelewa toka kwa Naafi'i kwamba ‘Abdullaah bin 'Umar alikuwa akikoga siku ya ‘Iyd el Fitwr kabla ya kwenda sehemu ya kuswalia. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Maalik (426), na kutoka kwake imepokelewa na Ash-Shaafi'iy katika Al-Ummu (1/231)].

 

2- Kuzindukana baada ya kupoteza fahamu

 

Kwani Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) alioga baada ya kupoteza fahamu. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (687) na Muslim (418) katika Hadiyth ndefu iliyopokelewa toka kwa 'Aaishah]. Na hii ilikuwa katika maradhi yake aliyofia.

Na Ijma’a imenukuliwa juu ya kusuniwa hilo, na Maulamaa wanasema kwamba akili kukaa sawa baada ya wendawazimu ni sawa na kupoteza fahamu.

 

3- Kuhirimia Hijjah na ‘Umrah

 

Ni kwa Hadiyth ya Zayd bin Thaabit kwamba yeye alimwona Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) amebadili nguo kwa ajili ya kuhirimia na kisha akakoga.[Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (831). Na tizama Al-Irwaa (149)].

 

Na mwanamke hata kama atakuwa na hedhi au nifasi ataoga, kwani Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) alimwamrisha Asmaa bint 'Umays akoge wakati alipojifungua katika Hijjah. [Hadiyth Swahiyh: Itakuja katika mlango wa Hijjah]. Haya yataelezwa zaidi katika mlango ha Hijjah.

 

4- Kuingia Makkah

 

Ni kwa Hadiyth ya Ibn 'Umar kwamba yeye alikuwa haingii Makkah ila hulala Dhiy Tuwaa mpaka asubuhi, halafu hukoga, kisha huingia Makkah mchana. Inaelezewa kuwa Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) alilifanya hilo.[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1573) na Muslim (1259)].

 

5- Baada ya kila jimai kama atarudiarudia

 

Ni kwa Hadiyth ya Abi Raafi'i kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) aliwazungukia wakeze usiku mmoja huku akikoga kwa huyu na kwa yule. Nikasema: "Ee Rasuli wa Allaah! Kwa nini usikoge mara moja tu"?

Akasema:

 ((هذا أزكى وأطيب وأطهر ))

((Hili ni utakaso zaidi, jema zaidi na twahara zaidi)). [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (216) na Ibn Maajah (560)].

 

6- Baada ya kumwosha maiti (kama Hadiyth ni Swahiyh)

 

Imepokelewa Hadiyth Marfu’u toka kwa Abu Hurayrah:

(( من غسل ميتا فليغتسل ))

((Mwenye kumwosha maiti, basi akoge)).  [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (3162), At-Tirmidhiy (993) na Ibn Maajah (1461). At-Tirmidhiy, Ibn Hajar na Al-Al Baaniy wamesema ni Hasan. Tizama Al-Irwaa (1/174). Lakini inavyoelekea inahitaji ukaguzi hivi, kwani Hadiyth imekosolewa].

 

7- Kwa mwenye damu ya istihaadhwah kwa kila Swalaah

 

Amri ya kukoga kwa mwanamke mwenye damu ya istihaadhwah wakati wa kila Swalaah imekuja katika mjumuiko wa Hadiyth Dhwa’iyf. [Irejee katika Jaami'u Ahkaam An-Nisaa (1/230-237)].

 

Lakini imethibiti toka kwa Aaishah akisema: “Ummu Habiybah alisumbuliwa na damu ya istihaadhwah kwa muda wa miaka saba. Akaja kumuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu Alayhi wa Aaalihi wa Sallam) kuhusiana na tatizo hilo. Rasuli akamwamuru aoge, na akamwambia kwamba huo ni mshipa. Naye akawa anaoga kwa kila Swalaah.”[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (327) na Muslim (334)].

 

Ash Shaafi’iy Allaah Amrehemu anasema: “Alilomwamuru Rasuli ni kuoga na kuswali tu, kwani katika maneno yake hakuna amri yoyote ya kuoga kwa kila Swalaah. [Amri hii ya kuoga ni mutwlaq, haionyeshi kukariri. Huenda Ummu Habiybah alifahamu kwamba ametakiwa kufanya hivyo kwa dalili fulani, hivyo akawa anaoga kila anapotaka kuswali. (Fat-h Al-Baary (1/509)].

 

Na sina shaka yoyote kwamba kuoga kwake kulikuwa ni kwa kupenda kwake mwenyewe kinyume na alivyoamrishwa, na mlango wa hilo uko wazi kwake”. [Sunan Al-Bayhaqy (1/349)].

 

Ninasema: “Hii ni kauli ya Jamhuri ya Maulamaa toka Salafu na waliokuja baada yao kwamba mwanamke mwenye damu ya istihaadhwah si lazima aoge kila Swalaah”.  

 

 

Share