054-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Kuoga Mwanamke Janaba

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

054-Kuoga Mwanamke Janaba

 

Alhidaaya.com

 

 

Anavyooga mwanamke janaba ni sawa na anavyooga mwanamume. Na mwanamke kama amesuka nywele zake, basi haimlazimu kuzifumua bali  atalazimika tu kuhakikisha kuwa maji yanafika hadi kwenye mizizi ya nywele. Hii ni kutokana na Hadiyth ya Maymuuna aliyesema:

“Ee Rasuli wa Allaah! Mimi ni mwanamke ninayependa sana kusuka nywele zangu. Je, nizifumue kwa ajili ya kuoga janaba?”

Rasuli akamwambia:

(( Hakika yakutosha kumwagia kichwa chako mateko matatu ya maji, kisha utajimiminia maji, na hapo unakuwa umetwaharika)). [Hadiyth Swahiyh: Imeshatajwa sana nyuma.]

 

Na imepokelewa na ‘Aaishah aliyesema:

“Tulikuwa tukioga tukiwa na “adh-dhimaad” nailhali tuko na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) sawasawa tukiwa tumehirimia au hatujahirimia”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (254) na Al-Bayhaqiy (2/182)].

 

Adh-dhimaad ni dawa ya kupaka kwenye nywele. Inazifanya zishikamane na zinyooke kama zilizonatishwa na gundi na kuwa kama rasta.

 

Na ‘Aaishah alimshambulia ‘Abdulaah bin ‘Amri kwa kuwaamuru wanawake kufumua nywele zao wakati wa kuoga. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (331), An-Nasaaiy (1/203) na Ibn Maajah (604)].

 

 

Share