058-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Masuala Yanayohusiana Na Mwenye Janaba

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

058-Masuala Yanayohusiana Na Mwenye Janaba

 

 

- Inajuzu kwa mwenye janaba kuchelewesha kuoga

 

Si lazima kuoga mara tu baada ya kupata janaba ingawa kufanya haraka inakuwa ni bora zaidi na utakasifu zaidi.

 

Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah akisema kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alikutana naye katika njia moja ya Madiynah akiwa na janaba, naye akamhepa asimwone. Kisha alikwenda akaoga. Baadaye alikuja na Rasuli akamwuuliza:

 ((Ulikuwa wapi ee Abuu Hurayrah?))

Akajibu: “Nilikuwa na janaba, nikaona uzito kukaa nawe nikiwa sina twahara”. Akasema:

((سبحان الله، إن المسلم لا ينجس))

((Subhaana Llaah. Hakika Muislamu hanajsi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (283) na Muslim (371)].

 

Na imepokelewa na Anas kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa akiwazungukia wakeze usiku mmoja nailhali wakati huo anao tisa. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (284) na Muslim (309)].

 

Kisha kuharakisha kuoga janaba, bila shaka kwa ngazi ya kwanza kabisa kunakuwa ni kwa ajili ya Swalaah. Na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa mara nyingine akilala kabla ya kuoga kama tutakavyoona baadaye.

 

- Inajuzu kwa mwenye janaba kulala kabla ya kuoga, kama atatawadha

 

Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah akisema:

(( Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa anapotaka kulala hali ya kuwa ana janaba, huosha utupu wake na hutawadha wudhuu wa Swalaah)).[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (288) na Muslim (305)].

 

Na ‘Abdullah bin Qays alimwuuliza akimwambia: “Ni vipi alikuwa akifanya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) akiwa na janaba? Je, alikuwa akioga kabla ya kulala, au akilala kabla ya kuoga?” ‘Aaishah akamjibu:

((Yote hayo alikuwa akiyafanya. Huenda akaoga kisha hulala, na wakati mwingine hutawadha kisha hulala)).

Akasema ‘Abdullaah bin Qays: “Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyefanya wasaa katika jambo”.[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (307)].

 

Na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alimwambia ‘Umar bin Al-Khatwaab alipomuuliza kuhusu janaba inayompata usiku:

((توضأ، واغسل ذكرك، ثم نم))

((Tawadha, osha dhakari yako, kisha lala)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (290) na Muslim (306)].

 

- Hakuna ubaya kwa mwenye janaba kusoma Qur-aan na kugusa Msahafu

 

Haya yamekwishaelezewa kwa ufafanuzi katika mlango wa wudhuu. Basi rejea huko.

 

 

Share