070-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Anayeamka Usingizini Muda Wa Swalaah Ukawa Mfinyu, Je Atayammamu Ili Auwahi Wakati?

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

070-Anayeamka Usingizini Muda Wa Swalaah Ukawa Mfinyu, Je Atayammamu Ili Auwahi Wakati?

 

Alhidaaya.com

 

 

Kuna mielekeo miwili katika suala hili mfano wa ile ya suala lililotangulia: [Al Awsatw (2/30), Al Muhalla (2/117), na Majmuu Al-Fataawaa (22/35-36)]

 

Wa kwanza:

 

Atatayammamu na ataswali ndani ya wakati. Hili limesemwa na Maalik, Al-Awzaa’iy, Ath-Thawriy na Ibn Hazm.

 

Wa pili:

 

Ataoga na ataswali na hata baada ya kutoka wakati. Huu ni msimamo wa Jamhuri, na Shaykh wa Uislamu ameukhitari. 

 

Msimamo huu ndio wenye nguvu zaidi, kwani wakati kwa mwenye kulala ni pale anapoamka.

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi wa Aalihii wa Sallam) amesema:

((أما إنه ليس في نوم تفريط، إنما التفريط على من لم يصل الصلاة حتى يجئ وقت الصلاة الأخرى، فمن فعل ذلك فليصلها حين ينتبه بها))

((Ama hakika, hakuna uzembe usingizini, bali uzembe ni kwa yule ambaye hakuswali mpaka ukaingia wakati wa Swalaah nyingine. Mwenye kufanya hivyo, basi aiswali anapoikumbukia)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (1532) na Abuu Daawuud (437).

 

Na imekuja katika Swahiyh Mbili katika Hadiyth Marfu’u iliyopokelewa na Abuu Hurayrah: “

((من نسي صلاة فليصلها إذا ذكرها لا كفارة لها إلا ذلك))

((Aliyeisahau Swalaah, basi aiswali anapoikumbuka, hakuna kafara yake ila hilo)).

 

Na katika tamshi la Muslim katika Hadiyth ya Anas:

((من نسي صلاة أو نام عنها فكفارتها أن يصليها إذا ذكرها))

((Aliyeisahau Swalaah, au akalala ikampita, basi kafara yake ni kuiswali anapoikumbuka))].

 

Ibn Taymiyah amesema (22/35):

 

“Na kama ni hivyo, kama ataamka kabla ya kuchomoza jua na hakuweza kuoga na kuswali ila baada ya kuchomoza, basi anakuwa ameiswali Swalaah katika wakati wake na wala hazingatiwi kuwa ameipitisha. Ni kinyume na yule aliyeamka mwanzoni mwa wakati. Huyu wakati wake ni kabla ya kuchomoza jua, atahadhari asiuache wakati wa Swalaah ukamtoka".

 

 

Share