079-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Yaliyoharamishwa Kwa Mwenye Hedhi Na Nifasi

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

079-Yaliyoharamishwa Kwa Mwenye Hedhi Na Nifasi

 

Alhidaaya.com

 

 

1-    Kuswali

 

Maulamaa wote wamekubaliana kwamba ni haramu kwa mwenye hedhi au nifasi kuswali, sawasawa ikiwa ni Swalaah ya faradhi au ya Sunnah. Wamekubaliana kwamba ufaradhi wa Swalaah huporomoka, na kuwa hatozilipa atakapotwaharika. [Al-Majmu’u ya An-Nawawiy (2/351) na Al-Muhallaa (2/175) ya Ibn Hazm].

 

Imepokelewa toka kwa Abu Sa’iyd akisema, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( أليس إذا حاضت لم تصل ولم تصم؟ فذلك نقصان دينها))

((Je, si anapopata hedhi haswali wala hafungi? Basi hilo ni upungufu wa Dini yake)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1951), Muslim (80) na wengineo].

 

Na imepokelewa na Mu'aadhah kwamba mwanamke mmoja alimwambia ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha):

"Je, inamtosheleza mmoja wetu Swalaah yake anapotwaharika?" Akamjibu: "Je, wewe ni Mharuriyah? Sisi tulikuwa tukiingia hedhini tukiwa na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na hakuwa akituamrisha, au akasema: Hatuiswali". [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (321) na Muslim (uk. 265)].

 

Mharuriyah”,  ni sifa ya mwenye kufuata madhehebu ya Khawaariji. Baadhi yao walikuwa wakiwajibisha kulipa Swalaah kwa mwenye hedhi.

 

Faida

 

1-   Mwanamke akiingia hedhini muda mfupi kabla ya kuingia Swalaah ya alasiri kwa mfano, na hakuwa ameswali adhuhuri, je itamlazimu alipe Swalaah ya adhuhuri baada ya kutwaharika?

 

Ikiwa kwa mfano itamjia muda mfupi kabla ya alasiri na hakuwa ameswali adhuhuri, basi atailipa Swalaah hiyo ambayo ilimwajibikia kabla ya kupata hedhi wakati anapotwaharika. Hii ndio rai ya Jamhuri ya Maulamaa. Sababu ni kuwa Swalaah ilikuwa imemwajibikia, na ni lazima ailipe madhali wakati wake uliingia hali ya kuwa yuko twahara kwa kiasi cha rakaa.

 

Hii ni kwa Neno Lake Allaah Mtukufu:

((إنَّ الصَّلاةَ كَانَتْ عَلَى المُؤْمِنِينَ كِتَاباً مَّوْقُوتا))

((Hakika Swalaah ina wakati wake maalumu kwa Waumini)). [An-Nisaa (4:103)]

 

Kuna kauli nyingineyo isemayo kwamba haimlazimu kuilipa adhuhuri. Wenye kusema hivi wanatoa dalili inayoashiria kuwa wanawake wakati wa enzi ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), walikuwa wakipata hedhi nyakati zote, lakini haikupokelewa kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwamuru mwanamke yeyote kuswali Swalaah iliyompita kabla ya kupata hedhi anapotwaharika.

 

Shaykh wa Uislamu anasema katika Al-Fataawaa (23/235):

"Dalili yenye nguvu zaidi ni madhehebu ya Abu Haniyfah na Maalik isemayo kuwa halazimiwi na chochote, kwani kulipa kunapasa kwa jambo jipya, na hapa hakuna lolote linalompasa kulipa, mbali na kuwa alichelewesha ucheleweshaji usio wa kuzembea. Ama aliyelala hata kama hakuzembea, basi analolifanya si kulipa, bali huo ni wakati wa Swalaah yake wakati anapoamka na akakumbuka."

 

2-   Anapotwaharika mwenye hedhi muda mfupi kabla ya alasiri kwa mfano, kisha baada ya kuoga wakati wa alasiri ukawa umeshaingia, je, ni lazima aswali adhuhuri?

 

Anapotwaharika na hedhi na nifasi kabla ya kuingia magharibi, itamlazimu aswali adhuhuri na alasiri za siku hiyo. Vile vile, anapotwaharika kabla ya kuchomoza alfajiri, itamlazimu aswali magharibi na ‘ishaa za usiku huo kwa vile wakati wa Swalaah ya pili ndio wakati wa Swalaah ya kwanza katika hali ya udhuru. Katika Al-Fataawa 2/334, Shaykh wa Uislamu anasema:

 

"Na kwa haya, ndivyo yalivyo madhehebu ya Jamhuri ya Maulamaa kama Maalik, Ash-Shaafi'iy na Ahmad, na kwamba mwenye hedhi anapotwaharika mwishoni mwa mchana, atazisali adhuhuri na alasiri. Na anapotwaharika mwishoni mwa usiku, ataswali magharibi pamoja na ‘ishaa. Na hivi ndivyo ilivyonukuliwa toka kwa ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf, Abu Hurayrah na Ibn 'Abbaas, kwa vile wakati ni mmoja kati ya Swalaah mbili katika hali ya udhuru. Hivyo basi, akitwaharika mwishoni mwa mchana, wakati wa adhuhuri hubakia na ataiswali kabla ya alasiri. Na akitwaharika mwishoni mwa usiku, basi wakati wa magharibi hubakia katika hali ya udhuru na ataiswali kabla ya ‘isha. Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.

 

2-   Kufunga

 

Imekubalika kwa Ijma’a ya Maulamaa kuwa mwenye hedhi na nifasi hafungi, lakini atazilipa siku za Ramadhwaan. ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) amesema:

"Hilo lilikuwa likitupata (hedhi) na tunaamrishwa kulipa swawm, lakini hatuamrishwi kulipa Swalaah". [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (265) na Abu Daawuud (263)].

 

Faida

 

1- Mwenye hedhi akitwaharika kabla ya alfajiri na hakuoga, je, atafunga?

 

Ikiwa mwenye hedhi atatwaharika kabla ya alfajiri na akanuia kufunga, basi Swawm yake ni sahihi, kwani kusihi kwa swawm yake hakutegemei kuoga, kinyume na Swalaah. Na hii ni kauli ya Jamhuri.  [Fat-h Al-Baariy (1/192)]

 

2-    Akitwaharika mwenye hedhi kabla ya kuchwa jua, je, atajizuia kula muda uliobakia?

 

Si lazima ajizuie kula mchana uliobakia, kwani alikwishafungua tokea mwanzo, lakini siku hiyo atailipa. Imepokelewa toka kwa Ibn Jaryj akisema: "Nilimwambia 'Atwaa: Mwanamke akiingia hedhini, kisha akatwaharika sehemu ya mchana, je atakamilisha? Akasema: Hapana, bali atalipa". [Isnadi yake ni Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdur Raaziq katika Al-Musannaf (1292) kwa Sanad Swahiyh].

 

 3- Kumwingilia (kumjimai)

 

Maulamaa wote wamekubaliana kwamba haijuzu kumwingilia mwanamke mwenye hedhi katika utupu. [Al-Muhalla (2/162), Majmu’u Al-Fataawaa (21/624) na Tafsiyr At-Twabariy (4/378)]

 

Allaah Mtukufu Ameliharamisha hilo katika Kauli Yake:

((فَاعْتَزِلُوا النِّسَاءَ فِي المَحِيضِ))

((Basi waepukeni wanawake katika hedhi)). [Al-Baqarah (2:222)]

 

Na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

(( اصنعوا كل شيئ إلا النكاح))

((Fanyeni kila kitu isipokuwa kujimai)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (203), Abu Daawuud, An-Nasaaiy, At-Tirmidhiy na Ibn Maajah].

 

Shaykh wa Uislamu katika Al-Fataawaa (21/624) anasema:

"Kumwingilia mwenye nifasi ni kama kumwingilia mwenye hedhi, na hilo ni haramu kwa makubaliano ya Maimam.

 

Faida

 

1- Ikiwa Muislamu ataitakidi kuwa ni halali kumwingilia mwanamke mwenye hedhi katika utupu wake, basi atakuwa ni kafiri aliyeritadi. Na lau kama mtu atalifanya hilo bila kuitakidi kuwa ni halali; ima kwa kusahau au kutojua kuwepo hedhi, au hajui kuwa hilo ni haramu, au akalazimishwa, basi hana makosa, na wala hatoi kafara. Na ikiwa atamwingilia kwa kukusudia akijua kwamba mkewe yuko mwezini na kuwa hilo ni haramu na bila kulazimishwa, basi atakuwa ametenda dhambi kubwa, na ni lazima atubie. [An-Nawawiy katika Sharh Muslim (3/204).

 

Na je, atawajibika kutoa kafara kwa kufanya hivyo?

 

Jamhuri ya Maulamaa – kinyume na Ahmad – wanasema kuwa hapaswi kutoa kafara.

 

Ninasema: "Hili ndilo sahihi. Ama Hadiyth ya Ibn 'Abbaas aliyoipokea toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa anasema kuhusiana na mtu anayemwingilia mkewe akiwa hedhini kwamba ((Anatoa swadaqah dinari moja au nusu dinari)), basi Hadiyth hii ni Dhwa’iyf kwa kauli yenye nguvu, nayo imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (264), An Nasaaiy (1/153), na Ibn Maajah (640).. Na kuchukua mali ya Muislamu ni haramu kiasili, na si halali kuitwaa mali hiyo ila kwa matni.

 

2-    Kinachokatazwa kustarehe na mwenye hedhi ni tupu yake basi. Mume anaruhusiwa kumchezea popote atakapo isipokuwa kuingiza dhakari yake katika utupu.  [Ni madhehebu ya Ath-Thawriy, Ahmad na Is-haaq. Pia Muhammad bin Al-Hasan na Atw-Twahaawiy katika Mahanafi, na baadhi ya wafuasi wa Maalik. Vile vile ni moja ya kauli mbili za Ash-Shaafi'iy. Aidha, limeungwa mkono na Ibn Al-Mundhir na An-Nawawiy (Fa-th Al-Baariy) (1/404). Ni madhehebu ya Ibn Hazm vile vile].

 

Na dalili ya hilo ni Hadiyth ya Anas. Anasema kwamba iliposhuka Kauli Yake Allaah Mtukufu:

((فَاعْتَزِلُوا النِّسَاءَ فِي المَحِيضِ))

((Basi waepukeni wanawake katika hedhi)), hapo Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

((اصنعوا كل شيئ إلا النكاح))

((Fanyeni kila kitu isipokuwa kujimai)). [Tumeitaja milango iliyopita].

 

Na imepokelewa toka kwa baadhi ya wakeze Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakisema:

"Alikuwa anapotaka kitu kwa mwenye hedhi, hutupia nguo juu ya utupu wake". [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (272) kwa Sanad Swahiyh].

 

Ninasema: "Lenye kutilia nguvu zaidi kauli hii ni Hadiyth ya Masruuq. Alimwambia Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha): "Ninataka kukuuliza jambo lakini naona hayaa. Akasema: Mimi ni mama yako, na wewe ni mwanangu. Akasema: Ni jambo lipi ambalo mtu anaweza kulifanya kwa mkewe akiwa hedhini? Akasema: Anaweza kufanya mambo yote, isipokuwa utupu wake". [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Atw-Twabariy katika ((At-Tafsiyr)) (4/378) kwa Sanad Swahiyh, nayo ina njia kadhaa].

 

Na hakuna shaka kuwa Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) ndio mjuzi zaidi wa hukmu ya suala hili, kwa kuwa yeye ndiye mke wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”.

 

Tanbihi

 

Kauli nyingine ya Maulamaa inasema kuwa linalojuzu kwa mwanamume kustarehe na mkewe wakati wa hedhi ni kila kitu, isipokuwa sehemu iliyopo kati ya kitovu na magoti. Kauli hii ina dalili zake, lakini kauli ya kwanza ndiyo yenye nguvu zaidi. Na Allaah Mtukufu Ndiye Ajuaye Zaidi.m [Haya ni madhehebu ya Maulamaa wengi. Angalia kwenye Jaami’u Ahkaamin Nisaa (1/140) na kurasa zinazofuatia ukipenda].

 

3-    Mwanamke anapotwaharika hedhi, haijuzu kwa mumewe kumwingilia mpaka aoge. Allaah Mtukufu Anasema:

 ((ولا تَقْرَبُوهُنَّ حَتَّى يَطْهُرْنَ فَإذَا تَطَهَّرْنَ فَأْتُوهُنَّ مِنْ حَيْثُ أَمَرَكُمُ اللَّهُ))

((Wala msiwakurubie mpaka watwaharike, na wanapotwaharika, basi waingilieni pale Alipowaamrisheni Allaah)). [Al-Baqarah (2:222)]

 

Mujaahid anasema: "Wanawake wana twahara mbili; twahara ya Kauli Yake Allaah Mtukufu: 

 

((حَتَّى يَطْهُرْنَ))

Yaani wanapooga, na hawi halali kwa mumewe mpaka aoge.

Anasema:

((فَأْتُوهُنَّ مِنْ حَيْثُ أَمَرَكُمُ اللَّهُ))

Pale damu inapotoka, na kama hakumwingilia pale Alipoamrisha Allaah, basi si katika wenye kutubia wala wenye kujitwaharisha". [Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdur-Raaziq (1272) na Al-Bayhaqiy (1/310) kwa Sanad Swahiyh hadi kwa Mujaahid].

 

Maulamaa wote wamekubaliana kwamba mwanamke haingiliwi na mumewe – hata kama damu imekatika – mpaka aoge, kinyume na Ibn Hazm.

 

· Ikiwa mke wa Muislamu ni Ahlul-Kitaab, je atalazimishwa kuoga?

 

Atalazimishwa kuoga, na mumewe haruhusiwi kumkurubia mpaka baada ya kuoga, kwani Aayah haimbagui mwanamke Muislamu au asiye Muislamu. [Tafsiyr ya Al-Qurtubiy (3/90)].

 

4-    Ni lazima mwanamke mwenye hedhi amgomee mumewe akitaka kumwingilia, lakini kama atazidiwa nguvu, basi habebi jukumu, bali ataomba maghfirah kwa Allaah Mtukufu. [Jaami’u Ahkaamin Nisaa (1/180)]

 

4- Kutufu

 

Kwa Ijma’a ya Maulamaa, ni haramu kwa mwenye hedhi kutufu. Na dalili ya hili ni Hadiyth ya Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) kwamba alipopata hedhi wakati wa kufanya ‘amali za Hijjah, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia:

(( إفعلي ما يفعل الحاج غير أن لا تطوفي بالبيت حتى تطهري))

((Fanya ayafanyayo mwenye kuhiji, lakini usitufu Nyumba (Ka'bah) mpaka utwaharike)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1650)].

 

Maelezo zaidi yatakuja kuhusiana na hili katika mlango wa Hajji Insha Allaah.

 

 

Share