000-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Swalaah

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

000-Swalaah

 

 

·       

Taarifu Yake:

 

[Mawaahibul Jaliyl (1/277), Al-Majmu’u (3/3) na Kash-Shaaful Qina’a (1/221)]

"Swalaah" kilugha ina maana ya du’aa. Na Swalaah ya kisharia imeitwa hivyo kwa vile inakusanya du’aa. Hivi ndivyo walivyosema mabingwa wengi wa lugha na wahakiki wengineo.

Allaah Mtukufu Anasema:

((وصل عليهم))

Yaani waombee

Na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( إذا دعي أحدكم فليجب، فإن كان صائما فليصل...))

((Anapoalikwa mmoja wenu basi aitikie, na kama amefunga basi amwombee du’aa mwalikaji chakula)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim. Itakuja kuelezewa mbeleni].

 

Ama kiistilahi, Swalaah ni kumfanyia ‘ibaadah Allaah Mtukufu kwa maneno na vitendo maalumu, vikifunguliwa kwa takbiyrah na kuhitimishwa kwa tasliym, pamoja na niya, kwa masharti mahsusi.

 

·       

Cheo Chake Katika Dini

 

1- Swalaah ndio faradhi iliyosisitiziwa na iliyo bora zaidi baada ya shahada mbili na ni moja kati ya nguzo za Kiislamu.

 

Imepokelewa na Ibn 'Umar kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Uislamu umejengewa juu ya (nguzo) tano: Kushuhudia kwamba hapana mungu mwingine isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Rasuli wa Allaah, kusimamisha Swalaah, kutoa Zakaat, kufunga Ramadhwaan na kuhiji)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (8) na Muslim (16)].

 

 2- Allaah Ametoa onyo kali kwa mwenye kuacha Swalaah kufikia mpaka Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumnasibisha mtu huyo na ukafiri, akasema:

((Hakika baina ya mtu na shirki na ukafiri ni kuacha Swalaah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (987), Abu Daawuud (1658), An-Nasaaiy (1/231) na wengineo].

 

Na anasema tena:

((Ahadi iliyopo baina yetu na wao ni Swalaah, mwenye kuiacha basi amekufuru)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (2621), An Nasaaiy (1/231) na Ibn Maajah. Angalia Sanad Zake katika kitabu cha Ta-’adhwiymu Qadri As-Swalaat (uk. 894) nilichokifanyia uhakiki]

 

‘Abdullah bin Shuqayq ambaye ni Taabi’iy amesema: “Maswahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa hawaoni amali ambayo kuiacha kwake ni ukafiri isipokuwa Swalaah”.[Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (2622), na Ibn Naswr katika kitabu cha Ta’adhiymu Qadri As-Swalaat (uk. 948) nilichokifanyia uhakiki]

 

3- Swalaah ndio nguzo ya dini, na dini haisimami ila kwa nguzo hii. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

((Kichwa cha mambo yote ni Uislamu, nguzo yake ni Swalaah, na kilele chake cha juu kabisa ni kufanya jihadi katika Njia ya Allaah)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (2616), na Ibn Maajah (3973)].

 

4- Ni kitu cha kwanza atakachohisabiwa mja. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

((La kwanza atakalohisabiwa mja Siku ya Qiyaamah ni Swalaah. Ikiwa imefaa, basi amefaulu na kufuzu. Na ikiwa imeharibika, basi amepita utupu na amekula hasara)).

 

5- Swalaah ilikuwa ndio kitulizo cha jicho kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika maisha yake. Anasema Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Kitulizo cha jicho langu kiko ndani ya Swalaah)).

 

6- Swalaah ilikuwa ndio wasiya wa mwisho aliousia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) umati wake wakati wa kufariki kwake. Alisema:

((Chungeni Swalaah, na watumwa wenu)).

 

7- Ni ‘ibaadah pekee isiyombanduka aliyebaleghe. Humganda maisha yake yote na wala hasameheki nayo vyovyote hali iwavyo.

 

8- Swalaah ina sifa za kipekee kulinganisha na ‘ibaadah nyinginezo. Kati ya sifa hizo:

 

(a) Allaah Mtukufu Aliifaradhisha Yeye Mwenyewe kwa kuzungumza moja kwa moja na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) usiku wa Mi-’iraaj.

 

(b) Ni faradhi iliyotajwa zaidi katika Qur-aan Tukufu.

 

(c) Ni ‘ibaadah ya kwanza Aliyoifaradhisha Allaah Mtukufu kwa Waja Wake.

 

(d) Imefaradhishwa mara tano mchana na usiku kinyume na ‘ibaadah na nguzo nyinginezo.

 

·       

Vigawanyo Vya Swalaah

 

Swalaah ina vigawanyo viwili. Kuna Swalaah za faradhi na Swalaah za Sunnah

 

1- Swalaah za Faradhi

 

Ni zile ambazo mwenye kuziacha kwa kusudi, huwa amemwasi Allaah Mtukufu, nazo ziko aina mbili:

 

(a) Fardhu ‘Ayn

 

Hizi ni zile ambazo ni lazima kwa kila aliyebaleghe na mwenye akili, mwanamke au mwanamume, aliye huru na mtumwa. Hizi ni kama Swalaah tano.

 

(b) Fardhu Kifaayah

 

Hizi ni zile ambazo baadhi ya watu wakiziswali, basi huwatosheleza wengineo. Ni kama Swalaah ya maiti.

 

2- Swalaah za Sunnah

 

Ni zile ambazo mwenye kuacha kuziswali kwa kusudi, hamuasi Allaah Mtukufu. Ni kama Sunnah zilizozoeleka na nyinginezo zitakazoelezewa katika milango ijayo. Lakini pamoja na hivyo, imesuniwa kuziswali Swalaah za Sunnah, kwani kuziacha ni makruhu.

 

 

Share