012-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Masharti Ya Kuswihi Swalaah

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

012-Masharti Ya Kuswihi Swalaah

 

 

Sharti ni kile ambacho kukosekana kwake hulazimisha kukosekana chenye kushurutiwa, na kuwepo kwake hakulazimishi kuwepo chenye kushurutiwa au kutokuwepo. Ni kama twahara kwa mfano, kukosekana kwake, hufanya kuswihi kwa Swalaah kukosekane, na kuwepo kwake, hakulazimishi kuwepo kwa Swalaah.

 

Yafuatayo ni baadhi ya masharti ambayo Swalaah haiswihi bila kuwepo pamoja na uwezo:

 

1-    

Kujua kuingia wakati wa Swalaah

 

Allaah Mtukufu Anasema:

((إِنَّ الصَّلَاةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَّوْقُوتًا))

(( Hakika Swalaah kwa Waumini ni fardhi iliyowekewa nyakati maalumu)). [An Nisaa (4:103)].

 

Hadiyth za Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) zimesha ainisha nyakati za Swalaah zote kama ilivyotangulia, na Swalaah ni ‘ibaadah yenye nyakati zilizowekwa ndani ya mpaka wa mabano mawili, haiswihi kuifanya kabla ya wakati wake, wala haiswihi kuifanya baada ya wakati wake, isipokuwa kwa udhuru kwa mujibu wa kauli yenye nguvu ya Ijma’a kama tulivyotangulia kuelezea nyuma.

 

Mafuqahaa wamekubaliana kwamba inatosha kujua kuingia kwa wakati kwa kutopea dhana. [Ibn ‘Aabidiyn (1/247), Ad-Dusuwqiy (1/181), Mughniy Al-Muhtaaj (1/184) na Kash-Shaaf Al Qinaa (1/257)]

 

2-    

Kutwaharika na hadathi mbili pamoja na uwezo wa kujitwaharisha

 

Hii ni sharti ya kuswihi kwa Swalaah kwa dalili zifuatazo:

 

- Neno Lake Ta’alaa:

 

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا قُمْتُمْ إِلَى الصَّلَاةِ فَاغْسِلُوا وُجُوهَكُمْ وَأَيْدِيَكُمْ إِلَى الْمَرَافِقِ وَامْسَحُوا بِرُءُوسِكُمْ وَأَرْجُلَكُمْ إِلَى الْكَعْبَيْنِ ۚ وَإِن كُنتُمْ جُنُبًا فَاطَّهَّرُوا ۚ وَإِن كُنتُم مَّرْضَىٰ أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ أَوْ جَاءَ أَحَدٌ مِّنكُم مِّنَ الْغَائِطِ أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ فَلَمْ تَجِدُوا مَاءً فَتَيَمَّمُوا صَعِيدًا طَيِّبًا فَامْسَحُوا بِوُجُوهِكُمْ وَأَيْدِيكُم مِّنْهُ ۚ مَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيَجْعَلَ عَلَيْكُم مِّنْ حَرَجٍ وَلَـٰكِن يُرِيدُ لِيُطَهِّرَكُمْ وَلِيُتِمَّ نِعْمَتَهُ عَلَيْكُمْ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ))

(( Enyi walioamini!  Mnaposimama kwa ajili ya Swalaah; osheni nyuso zenu na mikono yenu mpaka kwenye visugudi, na panguseni (kwa kupaka maji) vichwa vyenu na (osheni) miguu yenu hadi vifundoni. Na mkiwa na janaba basi jitwaharisheni. Na mkiwa wagonjwa au mko safarini au mmoja wenu akitoka msalani, au mmewagusa wanawake, kisha hamkupata maji; basi tayammamuni (ikusudieni) ardhi kwa juu panguseni kwayo nyuso zenu na mikono yenu. Allaah Hataki kukufanyieni magumu, lakini Anataka kukutwaharisheni na Akutimizieni neema Yake juu yenu ili mpate kushukuru)). [Al-Maaidah (5:6)]

 

- Neno Lake Ta’alaa:

 

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَقْرَبُوا الصَّلَاةَ وَأَنتُمْ سُكَارَىٰ حَتَّىٰ تَعْلَمُوا مَا تَقُولُونَ وَلَا جُنُبًا إِلَّا عَابِرِي سَبِيلٍ حَتَّىٰ تَغْتَسِلُوا ۚ وَإِن كُنتُم مَّرْضَىٰ أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ أَوْ جَاءَ أَحَدٌ مِّنكُم مِّنَ الْغَائِطِ أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ فَلَمْ تَجِدُوا مَاءً فَتَيَمَّمُوا صَعِيدًا طَيِّبًا فَامْسَحُوا بِوُجُوهِكُمْ وَأَيْدِيكُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَفُوًّا غَفُورًا ﴿٤٣﴾

(( Enyi walioamini! Msikaribie Swalaah na hali mmelewa mpaka mjue mnayoyasema, na wala mkiwa mna janaba isipokuwa mmo safarini mpaka muoge josho. Na mkiwa wagonjwa au safarini au mmoja wenu ametoka msalani au mmewagusa wanawake kisha hamkupata maji, basi mtayammam (ikusudieni) ardhi safi ya mchanga, pakeni nyuso zenu na mikono yenu. Hakika Allaah daima ni Mwingi wa kusamehe, Mwingi wa kughufuria)). [An-Nisaa (4:43)]

 

Hadiyth ya Abuu Hurayrah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( Allaah Haikubali Swalaah ya mmoja wenu anapopatwa na hadathi mpaka atawadhe)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (135) na Muslim (225)].

 

- Hadiyth ya Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu Anhumaa) kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Allaah Haikubali Swalaah yoyote bila ya twahara)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (224), At-Tirmidhiy (1), An-Nasaaiy (139), Abuu Daawuud (59) na Ibn Maajah (273)].

 

Hadiyth hizi mbili ziko wazi kwa upande wa shuruti, na Swalaah haiswihi ila kwa kupatikana twahara kutokana na hadathi isipokuwa kwa wale wenye nyudhuru za kisharia kama mwenye kichocho, mwenye tatizo la kuponyokwa upepo na mwanamke mwenye damu ya istihadhwa. Hawa wataswali hata kama watapatwa na hadathi ndani ya Swalaah. Pia aliyekosa maji au mchanga kama mfungwa na mfanowe, huyu ataswali kwa mujibu wa mazingira yalivyo.

 

·       

Je, Ni Sharti Kutwaharika Na Najsi Katika Mwili, Nguo Na Mahala Pa Kuswalia?

 

Kwa upande wa mwili, ni lazima utwaharishwe na najsi kwa dalili zifuatazo:

 

1- Neno Lake Ta’alaa:

((وَثِيَابَكَ فَطَهِّر))

((Na nguo zako toharisha)). [Al-Muddath-thir (74 :4)]

 

Ikiwa kuzitwaharisha nguo ni wajibu, basi kuutwaharisha mwili inakuwa ni wajibu zaidi.

 

2- Hadiyth za kustanji kwa maji na mawe zilizoelezewa kwenye mlango wa twahara, zinatuarifu juu ya ulazima wa kuutwaharisha mwili kutokana na najsi.

 

3- Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameamuru kuiosha dhakari inapoingia madhii.

 

4- Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameamuru kujikinga na mkojo, na akaelezea kuhusu watu wawili waliokuwa wakiadhibiwa ndani ya makaburi yao. Mmoja wao alikuwa hajikingi na mkojo.

 

Dalili zote hizi tumezielezea katika mlango wa twahara.

 

Ama nguo, ni lazima kuzitwaharisha na kuziweka mbali na najsi kwa dalili zifuatazo:

 

1- Neno Lake Allaah Mtukufu:

((وَثِيَابَكَ فَطَهِّر))

((Na nguo zako toharisha)) [Al-Muddath-thir (74 :4)]

 

2- Neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusiana na nguo inayopatwa na damu ya hedhi:

((Ataipikicha, kisha ataikwangua kwa ncha ya vidole na maji, halafu ataisuuza, na kisha atasali nayo)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (227) na Muslim (291)]

 

3- Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alivivua viatu vyake akiwa ndani ya Swalaah baada ya Jibriyl kumjuvya kwamba vina najsi. [Hadiyth Swahiyh: Imeelezewa katika mlango wa kuzitwaharisha najsi].

 

Hili linatutaarifu juu ya wajibu wa kujivua na najsi ya kilichovaliwa wakati wa Swalaah.

Ama mahala pa kuswalia, ni lazima kupatwaharisha mahala hapo kwa dalili zifuatazo:

 

1- Neno Lake Ta’alaa:

 

((وَإِذْ جَعَلْنَا الْبَيْتَ مَثَابَةً لِّلنَّاسِ وَأَمْنًا وَاتَّخِذُوا مِن مَّقَامِ إِبْرَاهِيمَ مُصَلًّى ۖ وَعَهِدْنَا إِلَىٰ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ أَن طَهِّرَا بَيْتِيَ لِلطَّائِفِينَ وَالْعَاكِفِينَ وَالرُّكَّعِ السُّجُودِ))

((Na Tulipoifanya Nyumba (Al-Ka’bah) kuwa ni mahali pa kurejewa na watu na pa amani, na fanyeni mahali pa kusimama Ibraahiym kuwa ni pahala pa kuswalia. Na Tulichukua ahadi kwa Ibraahiym na Ismaa’iyl kwamba: “Itakaseni Nyumba Yangu kwa wanaotufu na wanaokaa i’tikaaf, na wanaorukuu na kusujudu.”)). [Al-Baqarah (2:125)]

 

2-  Kuamuru Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) imiminwe ndoo ya maji kwenye mkojo wa bedui Msikitini. [Hadiyth Swahiyh: Imeelezewa katika mlango wa twahara].

 

Ninasema: “Maulamaa wana kauli mbili kuhusiana na matni zilizotangulia:

 

Ya kwanza: Dalili zilizotangulia zinatutaarifu kwamba ni wajibu kujiepusha na najsi kwenye mwili, nguo na mahala pa kuswalia, na kwamba mtu akiswali mbele ya najsi, au akaibeba, au akakabiliana nayo, basi atapata dhambi lakini Swalaah yake itakuwa ni sahihi. Kwa kuwa matni hizi hazina kinachotutaarifu kukanushika kiini cha dhati ya Swalaah yenyewe, au kuswihi kwake kinyume na kujitwaharisha na hadathi. La wajibu halilazimiki kuwa sharti. [Angalia As-Sayl Al-Jarraar cha Ash-Shawkaaniy (1/157-158)]

 

Ya pili: Matni zote za Aayah na Hadiyth zinaamuru kujiepusha na najsi, na kuamuru kitu ni kukataza kinyume chake. Na ukatazaji kitu ndani ya ‘ibaadah kunahukumia uharibifu wa kitu hicho, na kwa hilo inatolewa dalili juu ya usharuti. Huu ndio msimamo wa Jamhuri ya Maulamaa. [Al-Badaai-’i (1/114), Haashiyatud Dusuwqiy (1/200), Mughnil Muhtaaj (1/188) na Kash-Shaaful Qinaa (1/288)]

 

Kinachotubainikia hapa ni kuwa kauli ya kwanza ndiyo yenye nguvu zaidi. Naam! Inajuzu kutolea dalili juu ya usharuti wa katazo linaloonyesha juu ya uharibifu wenye maana sawa na ubatili. Lakini hii ikiwa katazo la kitu hicho ni kwa dhati yake yenyewe au sehemu yake, si kwa lililo nje ya wigo wake. Na katazo hapa kama inavyoonekana wazi, liko nje ya Swalaah yenyewe. Allaah Ndiye Mjuzi zaidi”.

 

·       

Mwenye Kuswali Akiwa Na Najsi, Naye Hakujua Ila Baada Ya Kumaliza, Je, Atairudia Swalaah?

 

[Mahala pa mas-ala haya panahusiana na kauli ya Jamhuri yenye kushurutisha kutwaharika na najsi ndani ya Swalaah. Ama kwa kauli tuliyoipa nguvu ya uwajibu (bila ushuruti), hapana kitu juu yake kama ilivyo wazi]

 

Maulamaa wamekhitalifiana katika suala hili kwa kauli tatu:

 

Ya kwanza: Swalaah yake ni baatwil. Atalazimika kuswali tena kama atajua kuwa alikuwa na najsi kabla ya wakati wa Swalaah kutoka. Lakini ikiwa amejua baada ya kutoka wakati, hatolipa.

 

Hii ni kauli ya Rabiy-’a, Maalik na Al-Hasan. [Al-Mudawwanah (1/21,22) na Al-Awsatw (2/164)]

 

Ya pili: Swalaah yake ni baatwil, na atalazimika kuilipa tena hata baada ya wakati. Hii ni kauli ya Ash-Shaafi’iy na riwaya ya Ahmad. [Al-Ummu (155), Al-Mughniy (2/65) na Al-Awsatw (2/164)]

 

Wanasema kwamba kwa kuwa amekosa sharti kati ya shuruti za kuswihi Swalaah, basi Swalaah yake ni baatwil na ni lazima aiswali tena.

 

Ya tatu: Swalaah yake ni Swahiyh, na halazimiki kuiswali tena. Wamelisema hili Ibn ‘Umar, ‘Atwaa, Ibn Al-Musayyib, Mujaahid, Abuu Thawr, Is-Haaq, Ash-Sha’abiy, An-Nakh’iy na Al-Awzaa’iy. Ni riwaya ya Ahmad, na Ibn Al-Mundhir kaikubali.  [Al-Awsatw (2/163), Al-Mughniy (2/65) na Al-Majmu’u (3/163)]

 

Dalili yao ni:

 

1- Kwamba alikuwa hajui kama ana najsi, na Allaah Anatuambia:

 

((وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ آمِنُوا كَمَا آمَنَ النَّاسُ قَالُوا أَنُؤْمِنُ كَمَا آمَنَ السُّفَهَاءُ ۗ أَلَا إِنَّهُمْ هُمُ السُّفَهَاءُ وَلَـٰكِن لَّا يَعْلَمُونَ))

((Na wanapoambiwa: “Aminini kama walivyoamini watu.” Husema: “Je, tuamini kama walivyoamini wapumbavu.” Tanabahi! Hakika wao ndio wapumbavu lakini hawajui)). [Al-Baqarah (2:13)]

 

Na katika Hadiyth Swahiyh, ni kuwa Allaah Mtukufu Anasema: ((Hakika Nimeshafanya)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (125)].

 

2- Hadiyth ya Abuu Sa’iyd kuhusiana na kisa cha Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuvua viatu wakati Jibriyl alipomjulisha kwamba vina najsi. Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwa akijua kwamba viatu vina najsi, na Swalaah yake aliikamilisha. Na lau kama Swalaah ingelikuwa baatwil, basi angeiswali tena upya.

 

Ninasema: Tukisema kwamba ni sharti kujiepusha na najsi, basi itatulazimu tuseme kwamba Swalaah ni baatwil, na kama si hivyo, italazimu kwa yule aliyekumbuka kwamba aliswali bila ya wudhuu, asiirejeshe tena Swalaah yake!! Wao hili hawalisemi. Huku ni kuvunja qaida ambazo kati yake ni kuwa shuruti na nguzo hazipomoki kwa kusahau.

 

Ama Hadiyth ya Rasuli kuvua viatu vyake, hiyo ni dalili kwetu kwamba si sharti kujiepusha na najsi ndani ya Swalaah. Dalili hii inaipa nguvu kauli yetu ya uwajibu pasina usharuti. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.”

 

 

Share