014-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Sehemu Ya Mwili Inayopasa Kusitiriwa

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

014-Sehemu Ya Mwili Inayopasa Kusitiriwa 

 

 

Ijulikane mwanzo kabisa kwamba uhakiki(nao ni muhtasari wa yaliyohakikiwa na Sheikh wa Uislamu Ibn Taymiyah Rahimahul Laahu katika Al-Fataawaa (22/113-120)) unasema: “Hakuna mafungamano ya kimahusiano kati ya uchi nyeti na uchi wa Swalaah, bali istilahi ya “kusitiri uchi” wanayoizingatia Mafuqahaa kwamba ni sharti ya kuswihi Swalaah, si katika matamshi ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Hakuna katika Quraan wala Hadiyth linaloeleza kwamba sehemu anayoisitiri mwenye kuswali ni uchi, bali Allaah Mtukufu Anasema:

 

((يَا بَنِي آدَمَ خُذُوا زِينَتَكُمْ عِندَ كُلِّ مَسْجِدٍ وَكُلُوا وَاشْرَبُوا وَلَا تُسْرِفُوا ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُسْرِفِينَ))

((Enyi wana wa Aadam! Chukueni mapambo yenu katika kila Masjid; na kuleni na kunyweni; na wala msifanye israfu. Hakika Yeye (Allaah) Hapendi wanaofanya israfu)). [Al-A’araaf (7 :31)]

 

Uchi wa kuangaliwa, ni uchi wa kutamanika kimwili. Ama kujisitiri kwenye Swalaah, hiyo ni kwa Haki ya Allaah Mtukufu. Haifai kwa yeyote kuzunguka Al-Ka’abah au kuswali akiwa uchi hata kama yuko peke yake. Hivyo imejulikana kwamba kujisitiri kwenye Swalaah si kwa ajili ya kujisitiri na watu. Hivyo basi, hii ni aina, na hii ni aina nyingine.

 

Na wakati huo, wakati wa Swalaah, mwenye kuswali anaweza kusitiri sehemu inayojuzu kuiacha wazi wakati usio wa Swalaah, na wakati wa Swalaah anaweza kuiacha wazi sehemu anayoisitiri watu wasimwone. Kwa mfano, Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza mtu kuswali na nguo moja bila kuwa na chochote juu ya mabega yake. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Al-Bukhaariy (359) na Muslim (516)].

 

Na hii ni kwa upande wa haki ya Swalaah, lakini inajuzu kwa wanaume kuyawacha wazi mabega nje ya Swalaah. Kadhalika, mwanamke katika Swalaah hujitanda ushungi, lakini hajitandi kwa mumewe wala kwa maharimu zake.

 

Na kinyume cha hivyo kwa uso, mikono miwili na miguu miwili, hairuhusiwi kuvionyesha kwa ajanibu kwa mujibu wa kauli mbili zilizo Swahiyh. Ama kuvisitiri viungo hivi wakati wa Swalaah, si wajibu kwa itifaki ya Waislamu, bali inajuzu kwake kuonyesha uso wake na viganja vyake katika Swalaah kwa rai ya Jamhuri. Pia, miguu miwili kwa mujibu wa rai ya Abuu Haniyfah, na rai hii ndiyo yenye nguvu zaidi. Tukilijua hili, tunasema:

 

·       

Kinachopasa Akisitiri Mwanamume Katika Swalaah

 

- Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kutufu Al Ka’abah uchi. [Hadiyth Swahiyh: Itakuja katika mlango wa Hajji].

 

Hivyo basi kujisitiri kwenye Swalaah ni bora zaidi.

 

- Na amesema kuhusu nguo moja: ((Kama ni pana, jizungushie, na kama inabana, jifunge nayo chini)). [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa katika mlango tulionao].

 

Hivyo basi, haitoshelezi sitara isiyoweza kusitiri sehemu ya chini ya mwili.

 

- Na amesema Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Sehemu iliyo kati ya kitovu na magoti ni uchi)). [Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (495, 496). Angalia Al-Irwaa (1/226)].

 

Na imepokelewa na Buraydah akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza mwanamume kuswali na nguo ya kujitanda bila kujifunga nayo, na amekataza mwanamume kuswali na sirwali bila kuwa na nguo ya kufunika juu” [Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (636). Angalia Swahiyh Abuu Daawuud (636)].

 

Hii inaonyesha kuwa ni lazima kuisitiri sehemu ya juu ya mwili wakati wa Swalaah.

-Rasuli amekataza mtu kuswali na nguo moja bila kuwa na chochote juu ya mabega yake. [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa katika mlango tulionao].

 

Hadiyth hii inaonyesha kwamba mwanamume anaamuriwa asitiri uchi katika Swalaah yake kama paja na viungo vinginevyo hata juu ya kuwepo kauli isemayo kwamba paja si uchi, bali uchi ni utupu wa mbele na nyuma tu. (Hili limetiliwa nguvu kama itakavyokuja kuelezwa baadaye katika mlango wake hata kama ataswali peke yake nyumbani kwake bila kuwepo amwonaye, itamlazimu hilo).

 

Ama yule mwenye kujengea kwamba uchi ni tupu mbili, [ juu ya moja ya riwaya mbili toka kwa Ahmad na Ibn Hazm ] na kwamba inajuzu kuswali mapaja wazi, basi huyo amekosa, na wala hilo Ahmad (Rahimahul Laahu) hakulisema. Vipi Ahmad aamuru kusitiri mabega mawili, halafu aruhusu kuwacha wazi mapaja mawili?!

 

Kikhulaswa, tunasema kwamba mwanamume katika Swalaah ameamuriwa asitiri mwili wake kuanzia mabega mawili hadi magoti yake mawili. Na kama hana nguo ya kumtosha, hapo atajifunga nayo chini na sehemu ya juu ya mwili ataiacha wazi kama ilivyotangulia katika Hadiyth ya Jaabir.

 

·       

Faida

 

Ni lazima kusitiri sehemu zinazopasa kusitiriwa katika Swalaah kwa nguo isiyoonyesha rangi ya ngozi ya mwili kama ni nyeupe, au nyekundu au nyeusi. Ama ikiwa nguo ni nzito lakini inabana na kuonyesha muundo wa kiungo bila rangi yake, basi ni karaha kuswali nayo, lakini Swalaah inakuwa ni sahihi.  [Sheikh Wahiyd Hafidhahul Laah ametupatia faida kwa haya katika kitabu cha Al-Ikliyl (1/311)]

 

·       

Kinachopasa kusitiriwa na mwanamke katika Swalaah

 

[Nimenukulu toka kitabu changu cha Fiqhus Sunnat Lin-Nisaa (kurasa 81,82 na 83)]

 

1- Mwanamke akiswali mbele ya watu wasio maharimu wake (ajanibu), ni lazima asitiri mwili wake wote isipokuwa uso na viganja viwili kwa mujibu wa rai ya Jamhuri. [Kuna makhitalifiano baina ya Maulamaa kuhusiana na suala la kufunua uso na viganja viwili. Litaelezewa kwa uchambuzi katika mlango wake]

 

2- Ikionekana sehemu yoyote inayolazimu kusitiriwa mbele ya wanaume wasio maharimu, basi atapata madhambi lakini Swalaah yake haibatiliki kwa mujibu wa kauli sahihi ya Maulamaa, kwa kuwa hakuna dalili yoyote ya kubatilika Swalaah yake kwa hilo.

 

3- Kama anaswali peke yake au mbele ya mumewe au maharimu zake, basi inajuzu kufunua uso wake na viganja vyake. Hii ndio kauli ya Maulamaa wengi.

 

Ama kwa upande wa nywele za mwanamke, imekuja Hadiyth isemayo:

((Allaah Haikubali Swalaah ya mwanamke aliyebaleghe ila kwa khimari)). [Imefanyiwa "ikhraaj" na Abuu Daawuud (641), At-Tirmidhiy (377) na wengineo. Maulamaa zaidi ya mmoja wameikosoa. Angalia Jaami'i Ahkaamun Nisaa (1/310)].

 

Hadiyth hii ingawa ni Dhwaíyf, lakini At-Tirmidhiy alisema baada yake: "Wanavyoitumia Maulamaa ni kuwa ikiwa mwanamke anaswali na huku sehemu ya nywele zake inaonekana, basi Swalaah yake haijuzu. Na hii ni kauli ya Ash-Shaafi'iy aliyesema: "Haijuzu Swalaah ya mwanamke ikiwa sehemu ya mwili wake iko wazi".

 

Na kwa mujibu wa rai ya Maulamaa wengi wakiwemo Abuu Haniyfah na Ahmad, Swalaah ya mwanamke inakuwa ni Swahiyh na wala hairejeshi ikiwa sehemu ndogo ya nywele zake na mwili wake itaonekana. Lakini kama ni sehemu kubwa, basi ataswali tena katika wakati wake kwa mujibu wa rai ya Maulamaa wote, Maimamu wanne na wengineo.  [Majmu'u Al-Fataawaa cha Ibn Taymiyah (22/123). Angalia Al-Mughniy cha Ibnu Qudaamah (1/601)]

 

·       

Mguu Wa Mwanamke Katika Swalaah

 

Imepokelewa Hadiyth ya Ummu Salamah kwamba alimuuliza Rasuli  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Je, mwanamke anaweza kuswalia diraa na khimar bila nguo ya chini?” Akamjibu: ((Ikiwa diraa ni pana inafunika mgongo wa miguu yake)). Hadiyth hii ni Dhwaíyf. [Imefanyiwa "ikhraaj" na Abuu Daawuud (640) na Al-Bayhaqiy (2/232) kwa Sanad Dhwaíyf ikiwa mawquuf na Marfu’u].

 

Ash-Shaafi'iy katika Al-Ummu (1/77) anasema: "Mwili wote wa mwanamke ni uchi (yaani katika Swalaah) isipokuwa uso wake, viganja vyake na miguu yake”. Na At-Tirmidhiy amenukulu kauli yake: "Imesemwa kwamba ikiwa mgongo wa miguu yake uko wazi, basi Swalaah yake inajuzu". Na haya ni madhehebu ya Abuu Haniyfah kama alivyonukulu Ibn Taymiyyah katika Al-Fataawaa (22/123).

 

Maalik na Ahmad, wao wanaona kwamba mwili wote wa mwanamke ni uchi, na Ahmad amevuka zaidi ya hapo kwa kusema: "Mwanamke aswali na kisionekane chochote cha mwili wake hata ukucha".

 

Ninasema: "Ninaloliona lina nguvu ni kuwa inajuzu kuswali hata kama mgongo wa mguu wake utakuwa wazi lakini si mbele ya wasio maharimu zake ingawa kusitiri miguu yake itakuwa ni akiba zaidi. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi."

 

4- Ni mustahabu mwanamke aswali kwa kuvaa nguo inayositiri mwili, na bora zaidi ni ile yenye kumsitiri zaidi. Na kwa ajili hiyo, Ash-Shaafi’iy amesema: “Wote wamekubaliana juu ya diraa na khimar, na yenye kuzidi ni bora na sitara zaidi. [Diraa inafanana na kanzu, lakini yenyewe ni ndefu hadi kufunika miguu miwili. Khimaar hufunika kichwa na shingo. Ama jilbabu, hii hutandiwa juu ya diraa. Imepokelewa kwa njia Swahiyh toka kwa ‘Umar, Ibn ‘Umar, Ibn Siyriyn na wengineo kwamba wamesema: “Mwanamke huswali kwa nguo tatu: Diraa, khimaar na jilbabu”]

 

Na kwa vile ikiwa amejitanda jilbabu, ataitanua wakati wa kurukuu na kusujudu ili nguo yake isionyeshe makalio yake na sehemu nyingine za mwili”. [Al-Mughniy (1/602), Al-Muhadh-Dhab (3/172) na Jaami’u Ahkaamin Nisaa (1/335)]

 

5- Ama ikiwa mwanamke ni kijakazi, hukumu yake ni kama ya mwanamke muungwana isipokuwa inajuzu aswali bila kufunika nywele zake kwa makubaliano ya Maulamaa wote isipokuwa Al-Hasan na ‘Atwaa.

 

6- Binti mdogo ambaye bado hajabaleghe, si lazima afunike nywele zake wakati wa Swalaah. ‘Abdur Raaziq katika Al-Muswannaf (3/113) kwa Sanad Swahiyh toka kwa Jariyj anasema: “Nilimwambia ‘Atwaa: Vipi kuhusu msichana ambaye hajavunja ungo anaposwali?” Akasema: “Inamtosha izari yake”.

 

·       

Faida Mbalimbali

 

(a) 

Mwenye Kufunukwa Uchi Wakati Wa Swalaah Bila Kukusudia, Je Swalaah Itabatilika?

 

Jamhuri ya Maulamaa wanasema kwamba mtu ambaye sehemu ya uchi wake itafunuka wakati wa Swalaah hata bila kukusudia, basi Swalaah yake itabatwilika kama hakuifunika hapo hapo. Mahanafi wameweka mpaka wa robo kiungo, kiasi cha kutekeleza nguzo!! [Ibn ‘Aabidiyn (1/273), Al-Mawaahib (1/498) na Al-Majmu’u (3/166)]

 

Mahanbali nao wanaona kwamba Swalaah haibatiliki kwa kufunuka uchi kwa kitambo kidogo kama vile upepo kupeperusha nguo uchi ukaonekana, au pia kama uchi wake utaonekana kidogo hata kwa muda mrefu. [Kash-Shaaf Al-Qinaa (1/269)]

 

Na hii ni kwa Hadiyth ya ‘Amri bin Salamah anayesema: “ Baba yangu aliondoka na ujumbe wa watu wake kuelekea kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), naye Rasuli akawafundisha namna ya kuswali. Akawaambia: Imamu wenu atakuwa yule mwenye kujua zaidi kusoma, nami nilikuwa ndiye mwenye kujua zaidi kusoma wakati nilipokuwa nikihifadhi, nao wakanitanguliza kuwa imamu. Nilikuwa nikiwaswalisha nikiwa nimevaa burdah yangu ndogo ya njano, nikisujudu, inanivuka. Mwanamke mmoja akasema: “Tusitirieni uchi wa msomaji wenu”. Wakaninunulia kanzu ya Kiomani, nami sikufurahishwa na kitu chochote baada ya kusilimu kwangu kama nilivyofurahishwa na kanzu hii.” [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (4302) na Abuu Daawuud (585), na tamko ni lake].

 

Haikusikika kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), alilipinga hilo au Swahaba yeyote.

 

Ninasema: “Hili ndilo Swahiyh. Lakini ni lazima aufunike uchi wake kama ataweza ikiwa amejua kwamba umefunuka”.

 

(b)

 Swalaah Ya Asiyeweza Kujisitiri Uchi

 

[Ibn ‘Aabidiyn (1/275), Ad-Dusuwqiy (1/216), Al-Majmu’u (3/142, 182) na Kash-Shaaf Al-Qina’a (1/270)]

 

Maulamaa wote wamekubaliana kwamba Swalaah haipomoki kwa mtu asiyepata kitu cha kujisitiri nacho, lakini wamekhitalifiana namna ya kuswali kwake. Jamhuri wanasema kwamba ikiwa hakupata isipokuwa nguo yenye najsi, au nguo ya hariri (kwa mwanamume), basi ni lazima avae. Na kama hakupata chochote, basi ataswali uchi kwa Neno Lake Allaah Mtukufu:

(( فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ وَاسْمَعُوا وَأَطِيعُوا وَأَنفِقُوا خَيْرًا لِّأَنفُسِكُمْ ۗ وَمَن يُوقَ شُحَّ نَفْسِهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ))

(( Basi mcheni Allaah muwezavyo, na sikilizeni; na tiini na toeni (kwa ajili ya Allaah) ni kheri kwa ajili ya nafsi zenu. Na yeyote anayeepushwa na ubakhili na tamaa ya uchu wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufaulu)). [At-Taghaabun (64:16)].

 

Kisha Mahanafi na Mahanbali wakasema kuwa atachaguzwa kati ya kuswali kwa kukaa au kusimama, na wamependezesha aashirie wakati wa kurukuu na kusujudu, kwani ni sitara zaidi. Lakini Maalik na Mashafii wanasema kwamba ni lazima aswali kwa kusimama, na haijuzu kuswali kwa kukaa.

 

Na je atailipa Swalaah kama atapata cha kujisitiria? La sawa na sahihi ni kuwa hatoilipa Swalaah kama walivyosema Mashafii na Mahanbali. Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.

 

(c) 

Kujipamba Na Kujiweka Maridadi Kwa Swalaah

 

Inajuzu kuswali kwa nguo moja kama ilivyotangulia. Lakini inapendeza mtu kuswalia na zaidi ya nguo moja, kujipamba na kujiweka maridadi kiasi awezavyo kutokana na Neno Lake Ta’alaa:

(( خذوا زينتكم عند كل مسجد))

 

Yaani kwa kila Swalaah. Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Anaposwali mmoja wenu, basi avae nguo zake mbili, kwani Allaah Anastahiki zaidi kupambiwa )). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bayhaqiy (2/236). Angalia Al-Majmu’u (2/54)].

 

1-    

Kuelekea Qiblah na kuwa na uwezo wa kufanya hivyo

 

Ni sharti ya kuswihi Swalaah kwa Ijma’a ya Maulamaa. [Maraatibul Ijma’a cha Ibn Hazm (uk 26)]

Ni kwa dalili hizi zifuatazo:

 

1- Neno Lake Ta’alaa:

(( فَوَلِّ وَجْهَكَ شَطْرَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِۚ وَحَيْثُ مَا كُنتُمْ فَوَلُّوا وُجُوهَكُمْ شَطْرَهُ ))

((Basi elekeza uso wako upande wa Al-Masjidil-Haraam. Na popote mtakapokuwepo (mkataka kuswali), basi elekezeni nyuso zenu upande wake)). [Al-Baqarah (2:144)]

 

2- Hadiyth ya Ibn ‘Umar: “Watu wakiwa Qubaa katika Swalaah ya Alfajiri, aliwajia mtu akawaambia: Hakika Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameteremshiwa usiku Quraan akaamuriwa aelekee Al-Ka’abah, basi nanyi elekeeni. Walikuwa wameelekeza nyuso zao Sham, wakageuka kuelekea Al-Ka’abah”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (4491), Muslim (526) na An-Nasaaiy (2/61)].

 

3- Hadiyth mashuhuri ya aliyeswali vibaya iliyopokelewa na Abuu Hurayrah kwamba mtu mmoja aliingia Msikitini na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekaa pembeni mwa Msikiti. Aliswali kisha alikwenda kwa Rasuli kumsalimia. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: ((Waalaykas Salaam. Rudi ukaswali, kwani hukuswali)). Kisha mara ya pili au iliyofuatia, mtu yule akasema: “Nifundishe ee Rasuli wa Allaah”. Akamwambia:

((Ukisimama kuswali, tawadha wudhuu kikamilifu, halafu elekea Qiblah upige takbiyr. Kisha soma chepesi ulichonacho katika Quraan, halafu rukuu mpaka utulie katika rukuu, kisha nyanyuka mpaka usimame wima sawasawa, halafu sujudu mpaka utulie katika sijdah, kisha nyanyuka mpaka utulie katika kikao, halafu sujudu mpaka utulie katika sijdah, kisha nyanyuka mpaka utulie katika kikao, halafu fanya hivyo katika Swalaah yako yote)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (6251) na Muslim (397)].

 

·       

Kuelekea Kuko Namna Mbili:

 

Mwenye kuswali ima awe anaiona Al Ka’abah au haioni. Anayeiona, ni lazima aielekee Al Ka’abah yenyewe kwa mwili wake wote. Akiwa ndani ya Al Haram na anaiona Al Ka’abah, haitomtosheleza kuelekea sehemu ya Msikiti bila ya Al-Ka’abah.

 

Ama kwa asiyeiona, huyu ni lazima aelekee upande wake iliko na si yenyewe hasa, kwa kuwa huo ndio upeo wa mwisho anaouweza. Na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Msikielekee Qiblah au kukipa mgongo kwa haja ndogo au haja kubwa, lakini elekeeni mashariki au Magharibi)). [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa katika mlango wa Twahara].

 

Hadiyth hii inaonyesha kwamba sehemu iliyopo kati ya mashariki na Magharibi, inazingatiwa kuwa ni Qiblah kwa watu wa Madiynah. Ama kwa watu wa Misri, mwelekeo wa Qiblah kwao ni kati ya mashariki na kusini.

 

Qiblah kinaweza kujulikana kwa mihrabu zilizoko ndani ya Misikiti ya Waislamu, au kwa kutumia dira na vinginevyo.

 

·       

Ni Wakati Gani Kuelekea Qiblah Husameheka?

 

Umejua kwamba kuelekea Qiblah ni sharti ya kuswihi Swalaah. Lakini kuna hali zisizo za kawaida ambazo Swalaah itajuzu bila ya kuelekea Qiblah. Hali hizo ni:

 

1-    

Asiyeweza kuelekea Qiblah:

 

Ni kama mgonjwa asiyeweza kujigeuza na hana wa kumgeuzia Qiblah. Huyu atasamehewa kwa Neno Lake (Subhaanahu wa Ta’alaa): ((Mcheni Allaah muwezavyo)), na Neno Lake: ((Allaah Hamkalifishi mtu isipokuwa kwa uwezo wake)).

 

2-    

Asiyejua Qiblah kilipo, akajitahidi kukisia lakini akaswali na kuelekea kwingine.

 

Asiyejua Qiblah kilipo, ni lazima amuulize mtu aonyeshwe, na kama hakumpata, atajitahidi kukiainisha kilipo. Ikiwa atajitahidi, akaswali, kisha akalibaini kosa lake wakati anaendelea kuswali, ni lazima azunguke kukielekea huku Swalaah ikiendelea kama ilivyo katika Hadiyth ya ‘Ibn ‘Umar tuliyoitaja hivi karibuni ambayo sehemu yake inasema: “Wakageuka kuelekea Al-Ka’abah”. Na ikiwa kosa atalijua baada ya kumaliza Swalaah, basi Swalaah yake ni Swahiyh na wala hatoiswali tena kwa kauli yenye nguvu. Hii ni kwa Hadiyh ya ‘Aamir bin Rabiy’a (Radhwiya Allaahu Anhu) aliyesema: “Tulikuwa pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) safarini katika usiku wa giza. Hatukujua Qiblah kilipo, na kila mmoja wetu aliswali kuelekea upande wake. Tulipopambaukiwa, tulimweleza Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na hapo ikashuka:

 

(( وَلِلَّـهِ الْمَشْرِقُ وَالْمَغْرِبُ ۚ فَأَيْنَمَا تُوَلُّوا فَثَمَّ وَجْهُ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ وَاسِعٌ عَلِيمٌ))

((Na Mashariki na Magharibi ni ya Allaah; basi popote mnapogeuka kuna Wajihi wa Allaah. Hakika Allaah ni Mwenye wasaa, Mjuzi wa yote)) [Al-Baqarah (2:115)].

 

Haya ni madhehebu ya Ath-Thawriy, Ibn Mubaarak, Ahmad na Is-Haaq.

 

3- Wakati inaposhitadi hofu ya kushambuliwa na adui au jinginelo:

 

Allaah Anasema:

 

((حَافِظُوا عَلَى الصَّلَوَاتِ وَالصَّلَاةِ الْوُسْطَىٰ وَقُومُوا لِلَّـهِ قَانِتِينَ •  فَإِنْ خِفْتُمْ فَرِجَالًا أَوْ رُكْبَانًا ۖ فَإِذَا أَمِنتُمْ فَاذْكُرُوا اللَّـهَ كَمَا عَلَّمَكُم مَّا لَمْ تَكُونُوا تَعْلَمُونَ ))

(( Shikamaneni na Swalaah na khaswa Swalaah ya katikati (Alasiri), na simameni mbele ya Allaah katika hali ya utiifu • Mkikhofu (swalini) huku mnatembea au mmepanda kipando. Mtakapokuwa katika amani mdhukuruni Allaah kama Alivyokufunzeni yale mliyokuwa hamuyajui )). [Al-Baqarah (2:238 na 239)].

 

Na katika Hadiyth ya Ibn 'Umar kuhusiana na Swalaah ya hofu: "Na ikiwa hofu ni kubwa kuliko hivyo, waliswali wakienda kwa miguu au wamepanda, wakiwa wameelekea Qiblah au hawakuelekea". [Hadiyth Swahiyhi: Imefanyiwa "ikhraaj" na Al-Bukhaariy (4535) na Maalik (396)].

 

Na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Wanapopambana, basi ni takbiyr na kuashiria kwa kichwa)). [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bayhaqiy (3/255)].

 

4- Katika Swalaah ya Sunnah kwa mpandaji anapokuwa safarini

 

Inajuzu kwa msafiri aswali Swalaah ya Sunnah akiwa juu ya mnyama wake (au kwenye gari, ndege, au meli), na si lazima aelekee Qiblah kama itakuwa ni uzito kwake. Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar kwamba yeye alikuwa akiswali juu ya mnyama wake usiku akiwa safarini, hajali popote pale atakapoelekea. Na amesema: “Rasuli wa Allaah Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam alikuwa anaswali juu ya mnyama wake kuelekea upande wowote ule, na huswali juu yake witri, lakini alikuwa haswali juu yake Swalaah ya faradhi”. [Hadiyth Swahiyhi: Imefanyiwa "ikhraaj" na Al-Bukhaariy (1098) na Muslim (700)]

 

Na imepokelewa toka kwa ‘Aamir bin Rabiy’a akisema: “Nilimwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akiswali juu ya mnyama wake; anaashiria kwa kichwa chake upande wowote anapoelekea, na hakuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) analifanya hilo katika Swalaah ya faradhi”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1098)].

 

Na imepokelewa na Jaabir (Radhwiya Allaahu Anhu) akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali juu ya mnyama wake popote pale anapoelekea, na anapotaka kuswali Swalaah ya faradhi, huteremka akaelekea Qiblah”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa "ikhraaj" na Al-Bukhaariy (400)].

 

Lakini; ikiwa ataweza kuanza Swalaah yake kwa kuelekea Qiblah, kisha akaelekea na mnyama wake kule anakokwenda, basi ni bora. Na hii ni kwa yale yanayohadithiwa kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapotaka kuswali Swalaah ya Sunnah juu ya mnyama wake, anaelekea naye Qiblah akapiga takbiyr, kisha huswali kuelekea kule msafara unakoelekea” [Al-Albaaniy kaipa daraja ya Hasan. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (1225) na wengineo. Angalia Swifatu Swalaatin Nabiyyi ukurasa wa 75].

 

Mas-ala: Ikiwa msafiri amepanda gari ambalo yeye si dereva baada ya Swalaah ya Adhuhuri, na akajua kwamba hatoswali ila baada ya Magharibi, je anaweza kuswali Swalaah ya Alasiri ndani ya gari? Au ataiswali pamoja na Magharibi?

 

Linaloonekana kuwa na nguvu hapa ni kuwa ni lazima aswali Alasiri katika wakati wake ndani ya gari hata kwa kukaa na hata bila kuelekea Qiblah, kwa kuwa wakati ni muhimu zaidi kwa Swalaah za faradhi kama ilivyoelezewa nyuma, na hupewa kipaumbele zaidi kuliko sharti ya kuelekea Qibla. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

 

 

Share