016-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Nguzo Za Swalaah

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

016-Nguzo Za Swalaah 

 

 

Nguzo za Swalaah ni maneno na vitendo vinavyounda uhakika na uhalisia wa Swalaah. Ikiwa nguzo moja kati ya nguzo hizi itawachwa, basi Swalaah haiswihi, haizingatiwi kisharia, na haiungwi kwa sijdah ya sahau.

 

Kuacha Nguzo Katika Swalaah

 

[Ibn ‘Aabidiyn (1/297, 318), Ad-Dusuwqiy (1/239, 279) na Kash-Shaaful Qinaa (1/385, 402)]

Mwenye kuacha nguzo katika Swalaah, haachi kuwa ima:

 

(a) Ameiacha makusudi: Mwenye kuacha nguzo yoyote ya Swalaah kwa kusudi, Swalaah yake itabatilika na haitoswihi kwa Ijma’a ya Maulamaa.

 

(b) Au ameiacha kwa kusahau au kwa kutojua: Ikiwa ataweza kuitadaraki na kuitenda, itakuwa ni wajibu, na kama hatoweza kuitadaraki, basi Swalaah yake itaharibika kwa mujibu wa kauli ya Mahanafi. Ama kwa upande wa Jamhuri ya Maulamaa, itafutwa tu rakaa ambayo aliacha nguzo, isipokuwa tu kama aliacha takbiyr ya kuhirimia Swalaah, hapo itabidi aanze Swalaah upya kwa kuwa hajaingia aslani katika Swalaah.

 

Nguzo za Swalaah Ni:

 

1- Kusimama katika Swalaah ya faradhi kwa mwenye kuweza

 

Dalili ya hili ni:

 

(a) Neno Lake Allaah Mtukufu:

((حَافِظُوا عَلَى الصَّلَوَاتِ وَالصَّلَاةِ الْوُسْطَىٰ وَقُومُوا لِلَّـهِ قَانِتِينَ))

((Shikamaneni na Swalaah na khaswa Swalaah ya katikati (Alasiri), na simameni mbele ya Allaah katika hali ya utiifu.)) [Al-Baqarah (2:238)]

 

(b) Neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumwambia ‘Imraan bin Haswiyn:

(( Swali kwa kusimama, ukishindwa swali kwa kukaa, ukishindwa swali kwa ubavu)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1117), Abuu Daawuud (939), na At-Tirmidhiy (369)].

 

(c) Maulamaa wote kwa Ijma’a, wamekubaliana kwamba kusimama ni nguzo katika Swalaah ya faradhi kwa atakayeweza. Pia wamekubaliana kwamba nguzo hii haimhusu mgonjwa kama hawezi kusimama, huyu ataswali kwa kukaa. Pia nguzo hii haimuhusu anayeweza kusimama, ikiwa kusimama huko kunamwia uzito na mashaka makubwa, au anahofia kuzidi maradhi yake, au kukawia kupona.

 

Imepokelewa na Anas akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alianguka toka juu ya farasi akachubuka ubavu wake wa kulia. Tukaenda kumzuru na wakati wa Swalaah ukafika. Alituswalisha kwa kukaa, nasi tukaswali nyuma yake kwa kukaa”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (378) na Muslim (411) na tamko ni lake].

 

Ibn Qudaamah amesema: “Inavyoonekana ni kuwa hakuwa ameshindwa kabisa kusimama, lakini kwa vile ilikuwa ni uzito na tabu, kisimamo kilipomoka kwake na kwa wengine”. [Al-Mughniy (2/571)]

 

·       

Faida

 

(a) Swalaah ya Sunnah inajuzu juu ya kipando katika safari yoyote; ndefu au fupi, lakini haifai mjini. Yameelezwa haya katika masharti ya kuelekea Qiblah.

 

(b) Inajuzu kuswali Swalaah ya Sunnah kwa kukaa (hata bila ya udhuru) lakini thawabu za anayesimama ni kubwa zaidi. Thawabu za anayekaa ni nusu ya thawabu za anayesimama.

 

Imepokelewa toka kwa ‘Imraan bin Haswiyn (Radhwiya Allaahu Anhu) akisema: “Nilimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu Swalaah ya anayeswali kwa kukaa akasema:

((Akiswali kwa kusimama, basi ni bora zaidi, na mwenye kuswali kwa kukaa, atapata nusu ya thawabu za mwenye kusimama, na mwenye kuswali kwa kulala, atapata nusu ya thawabu za mwenye kukaa)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1115), At-Tirmidhiy (371), An-Nasaaiy (3/223) na Ibn Maajah (1231)].

 

Al-Khattwaabiy amesema: “Makusudio hapa ni mtu anayechukulika kuwa mgonjwa anayeweza kujihemeza akasimama kwa tabu, yakafanywa malipo ya mwenye kukaa nusu ya malipo ya mwenye kusimama kwa ajili ya kumtia utashi wa kusimama ingawa anaruhusika kukaa”.

 

Al-Haafidh amesema: “ Ni makisio mazuri”. [Fat-hul Baariy (2/585) chapa ya Al-Ma’arifah]

 

Ninasema: “Nguvu ya makisio haya ipo katika kauli yake Rasuli ((na mwenye kuswali kwa kulala, atapata nusu ya thawabu za mwenye kukaa)), kwa maana kwamba Swalaah ya mwenye kuswali kwa kulala kwa ubavu  bila ya udhuru haifai kwa mujibu wa kauli ya Jamhuri hata kama ni Swalaah ya Sunnah, kwa kuwa haijulikani kabisa kwamba kuna yeyote katika Uislamu aliyeswali kwa kulala ubavu akiwa mzima. Na kama hili lingelikuwepo, basi Waislamu wangelilifanya katika enzi ya Nabii wao (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au baada yake, na angelifanya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ijapokuwa mara moja ili kubainisha kujuzu kwake. [Majmu’u Fataawaa Ibn Taymiyah (23/235)]

 

Anas amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwatokea watu wakiwa wanaswali kwa kukaa (kwa sababu ya ugonjwa) akasema: ((Hakika Swalaah ya mwenye kukaa, ni nusu ya thawabu ya mwenye kusimama)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Maajah (1229) na Ahmad (3/214), na ziada ni yake. Angalia kitabu cha Swifatu Swalaahatin Nabiy ukurasa wa 78].

 

Ninasema: “Hivi ndivyo Al-Khattwaabiy alivyoichukulia Hadiyth ya ‘Imraan kuwa inahusiana na Swalaah ya faradhi na Al-Haafidh akaliridhia hilo. Lakini wengi wameichukulia kuwa inahusiana na Swalaah ya Sunnah sawasawa kwa mwenye udhuru na asiye na udhuru, kwa kuwa inaonyesha kwamba kusimama katika Swalaah ya Sunnah siyo nguzo bali ni mustahabu. Hili linaongezewa nguvu na kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali Swalaah ya Sunnah safarini juu ya mnyama wake lakini si Swalaah ya faradhi. Ama Hadiyth ya Anas, hakuna pingamizi ndani yake, kwa kuwa inaonyesha kwamba inaruhusika kiujumla kuswali kwa kukaa katika Swalaah ya Sunnah. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.

 

Ujumuishi huu unatiliwa nguvu na yale yaliyothibiti kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali Swalaah za Sunnah kwa kukaa kama Hadiyth ya ‘Aaishah isemayo kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipowanda na kupata mwili, alikuwa akiswali Swalaah zake nyingi kwa kukaa. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (732)].

 

Aidha, yaliyothibiti kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akianza Swalaah ya usiku kwa kusimama, kisha hukaa. Hili litazungumziwa karibuni”.

 

·       

Faida mbili

 

Ya kwanza: Thawabu za Swalaah ya mwenye kukaa kwa udhuru hazipungui. Sababu ni kuwa yeye kwa kawaida huswali kwa kusimama, na maradhi au mfano wake ndio yaliyomzuilia, hivyo malipo yake ni kamili kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyo katika Al-Bukhaariy (2996):

((Anayegonjeka au akasafiri, huandikiwa aliyokuwa akiyafanya katika hali ya uzima na ukazi)).

 

Ya pili: Kati ya umahususi maalumu wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kuwa yeye hapunguziwi thawabu hata kama ataswali Swalaah ya Sunnah kwa kukaa bila udhuru. [Sharhu Muslim cha An-Nawawiy na Fat-hul Qadiyr (1/460)]

 

Hii ni kwa Hadiyth ya ‘Abdullah bin ‘Amri aliyesema: “Nilihadithiwa kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Swalaah ya mtu aliyekaa ni nusu ya Swalaah)). Nikamwendea, nikamkuta anaswali kwa kukaa, nikauweka mkono wangu juu ya kichwa chake akaniambia: ((Una nini ee ‘Abdullah bin ‘Amri?)). Nikamwambia: “Nimehadithiwa ee Rasuli wa Allaah kwamba umesema: Swalaah ya mtu aliyekaa ni nusu ya Swalaah, nawe unaswali kwa kukaa!! Akasema: (( Naam, lakini mimi si kama yeyote kati yenu)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (735), An-Nasaaiy (1659), na Abuu Daawuud (950)].

 

(c) Mtu anaweza kufungua kisomo katika Swalaah ya Sunnah kwa kukaa, kisha akasimama kwa mujibu wa makubaliano ya Maulamaa. Na hii ni kutokana na Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu Anha) aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaswali kwa kukaa. Anasoma naye amekaa, na Suwrah anayoisoma inapobakia kiasi cha aya 30 au 40, husimama akasoma kwa kusimama, kisha hurukuu na kusujudu, halafu hufanya hivyo hivyo katika rakaa ya pili”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1119) na Muslim (731)].

 

(d) Mtu anaweza kufungua kisomo katika Swalaah ya Sunnah kwa kusimama, kisha akakaa kutokana na Hadiyth iliyotangulia.

 

(e) Mwenye kuswali kwa kukaa, ni bora akae katika umbo la mkao wa tashah-hud. Atakaa mkao wa “iftiraash” katika hali ya kusimama na kurukuu, kwa kuwa Hadiyth za ‘Imraan na ‘Aaishah zilizotangulia hazikuainisha kikao, na makusudio ya moja kwa moja tunayoyafahamu ya kikao ni kile kilichozoeleka katika Swalaah. Hata hivyo, kikao cha “tarabbu’i” kinajuzu na hasahasa kwa ajili ya udhuru, kwani hili limeripotiwa kufanywa na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  [Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (3/224), Ibn Khuzaymah (2/236) na Al-Bayhaqiy (2/305). Angalia kitabu cha Swifatu Swalaatin Nabiy ukurasa wa 80]

 

Na pia baadhi ya Maswahaba wake.  [Imehadithiwa toka kwa Ibn ‘Umar katika  Muswannaf Ibn Abiy Shaybah (2/220)]

Ama kunyoosha miguu miwili wakati wa kuswali kwa kukaa, hili halifai isipokuwa kwa udhuru.

 

(f) Swalaah ya mwenye kuswali kwa ubavu inajuzu kwa udhuru sawasawa katika Swalaah ya faradhi au ya Sunnah ikiwa hawezi kukaa. Ama katika Swalaah ya Sunnah kama hakuna udhuru, Jamhuri wanaona kwamba haifai kisharia kwa kuwa haikunukuliwa kutoka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala kwa Swahaba yake yeyote kwamba alifanya hivyo angalau kwa mara moja.

 

Ninasema: “Lau kama mtu atashikamana na dhahiri ya Hadiyth ya ‘Imraan iliyotangulia: ((Na mwenye kuswali kwa kulala, atapata nusu ya thawabu za aliyekaa)), je, atakuwa na haki? Jibu sahihi ni kuwa ana haki. Na haya ni madhehebu ya Ibn Hazm katika Al-Muhallaa (3/56) ambayo yameungwa mkono na Ibn ‘Uthaymiyn katika Al-Mumti’i (4/113).”

 

(g) Mwenye kuswali kwa kulala kwa ubavu, imesuniwa alalie ubavu wake wa kulia akielekeza uso wake Qiblah, kwa kuwa imesuniwa kufanya hivyo wakati mtu anapotaka kulala, na kwa Hadiyth ya ‘Aaishah asemaye: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akipendezwa kuanza kwa kulia katika kuvaa viatu, kutembea, kujitwaharisha na katika mambo yake yote”. [Hadiyth Swahiyh: “Takhriyj” yake imetangulia mara nyingi].

 

Na kama hawezi kulala kwa ubavu ila kwa namna maalumu, basi itabidi hivyo hivyo. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

·       

Kusimama Katika Swalaah Ya Faradhi Kwenye Ndege Na Meli

 

Mwenye kuabiri ndege au meli, ni lazima asimame wakati wa kuswali Swalaah ya faradhi kama ataweza. Na kama atahofia kuanguka, kughariki na mfano wake, basi atahesabiwa kuwa hawezi. Hapo ataswali kwa kukaa na ataashiria kwa kichwa katika rukuu na sujudi. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa kuhusu kuswali katika meli akajibu:

((Swali humo kwa kusimama ila tu kama utahofia kughariki)). [Al-Albaaniy ameipasisha kuwa Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bazzaaz (68) na wengineo. Angalia  Swifatu Swalaahatin Nabiy ukurasa 79].

 

·       

Kuegemea Kitu Wakati Wa Kusimama

 

Mwenye kuswali kwa kuegemea ukuta, bakora na mfano wake kwa sababu ya udhuru, hili Maulamaa wamekubaliana kwamba linajuzu kwa kuwa imebidi lifanyike. Allaah Amesema:

 

((فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ وَاسْمَعُوا وَأَطِيعُوا وَأَنفِقُوا خَيْرًا لِّأَنفُسِكُمْ ۗ وَمَن يُوقَ شُحَّ نَفْسِهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ))

((Basi mcheni Allaah muwezavyo, na sikilizeni; na tiini na toeni (kwa ajili ya Allaah) ni kheri kwa ajili ya nafsi zenu. Na yeyote anayeepushwa na ubakhili na tamaa ya uchu wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufaulu)). [At-Taghaabun (64:16)]

 

Imepokelewa toka kwa Ummu Qays binti Muhswin kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipozeeka na kupata mwili, aliweka nguzo katika sehemu yake ya kuswalia ili kuiegemea)). [Al-Albaaniy kaiipasisha kuwa Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (948), Al-Bayhaqiy (2/288) na Al-Haakim (1/264). Angalia Asw-Swahiyhah (319)].

 

·       

Mtu akiswali nyuma ya imamu aliyekaa kwa udhuru, naye ataswali kwa kukaa juu ya kauli sahihi kama itakavyokuja kuelezewa katika mlango wa Swalaah ya jamaa.

 

2- Takbiyr ya kuhirimia

 

Hii ni nguzo kati ya nguzo za Swalaah kwa makubaliano ya Maulamaa wote kutokana na dalili zifuatazo:

 

1- Neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Ufunguo wa Swalaah ni twahara, mlango wake ni takbiyr, na kutoka kwake ni tasliym)). [Al-Albaaniy kaipasisha kuwa Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (61) na At-Tirmidhiy (3). Ameipasisha kuwa Swahiyh katika Al-Irwaa (301)].

 

2- Neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa aliyeswali kwa kukosea:

((Ukisimama kuswali, basi piga takbiyr)). [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa kikamilifu pamoja na “takhriyj” yake]

 

3- Katika tamshi la Hadiyth ya aliyeswali kwa kukosea:

((Hakika haitimu Swalaah ya yeyote katika watu mpaka atawadhe, na atawadhe kama inavyotakikana, kisha aseme: Allaahu Akbar)). [Al-Albaaniy kaipasisha kuwa Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Twabaraaniy (5/38). Angalia Swifatus Swalaahat (uk.86)].

 

Imepokelewa na ‘Aaishah akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifungua Swalaah kwa takbiyr”.[Hadiyth Swahiyhy. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (498)].

 

“Na takbiyr hapa, ni ile ijulikanayo na wote ambayo umma kupitia kizazi hadi kizazi, umeinukuu moja kwa moja toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye yeye alikuwa akiitamka katika kila Swalaah (Allaahu Akbar), na hakusema neno jingine zaidi ya hilo hata mara moja”.  [Tahdhiyb As-Sunan cha Ibn Al-Qayyim (1/49)]

 

Haitojuzu kuingia kwenye Swalaah bila ya kusema (Allaahu Akbar). Hii ndiyo kauli ya nguvu ya Ath-Thawriy, Maalik, Ahmad na Ash-Shaafi’iy [isipokuwa yeye amejuzisha kusema: Allaahu Al-Akbar]. Na hili limeripotiwa toka kwa Ibn Mas-’oud.

 

Lakini Abuu Haniyfah amekwenda kinyume na hao akisema: “Swalaah inafungika kwa kila Jina la Allaah Mtukufu lenye utukuzo kama: Allaahu Al-Adhwiym, au Al-Kabiyr, Au Al-Jaliyl, au Subhaana Allaah, au Al-Hamdulil Laah na kadhalika.” Anasema: “Wote wamesema hivi, kama ilivyo katika khutba ambayo hakuna tamko moja lililoainishwa”!!

 

Hakuna shaka kwamba kipimo hiki hakifai, kwa kuwa amekifanya kwenda kinyume na Hadiyth. Kauli ya Jamhuri ndiyo sahihi.  [Ibn ‘Aabidiyn (1/442), Al-Mudawwanah (1/62), Al-Ummu (1/100), Al-Majmu’u (3/233) na Al-Mughniy (1/333)]

 

·       

Takbiyr Haijuzu Ila Kwa Kiarabu Kwa Mwenye Kuweza

 

Takbiyr haiswihi kwa lugha nyingine isiyo Kiarabu kwa mwenye kuweza kuitamka kwa kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akipiga takbiyr kwa Lugha ya Kiarabu, na wala hakutumia lugha nyingine kamwe. Naye ndiye mwenye kusema: ((Swalini kama mnavyoniona nikiswali)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (631) na Ahmad toka katika Hadiyth ya Maalik bin Al-Huwayrath].

 

Kwa asiyeweza kuitamka takbiyr kwa Kiarabu, itabidi ajifundishe, lakini kama atahofia kupitwa na wakati wa Swalaah kabla hajajifundisha, au hakuweza kabisa kuitamka kwa Kiarabu, basi hapo ataisema kwa lugha yake. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

3- Kusoma Al-Faatihah katika kila rakaa

 

Kusoma Al-Faatihah ni nguzo katika kila rakaa ya kila Swalaah ya Sunnah au ya faradhi, ya kusoma kwa sauti au kwa sauti ya chini. Hii ni kauli ya Ath-Thawriy, Maalik, Ash-Shaafi’iy na Ahmad. Nalo limehadithiwa toka kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab na ‘Uthmaan bin Abul ‘Aasw. [Al-Mudawwanah (1/66), Al-Ummu (1/93), Al-Majmu’u (3/285), Al-Mughniy (1/343) na Al-Awsatw (3/101)]

 

Dalili ya hili ni:

 

1- Hadiyth ya ‘Ubaadah bin Swaamit kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Hakuna Swalaah kwa asiyesoma Faatihahtul Kitaab )). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (756), Muslim (394) na wengineo].

 

2- Hadiyth ya Abuu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Mwenye kuswali Swalaah yoyote bila kusoma Faatihahtul Kitaab, basi Swalaah hiyo ni pungufu, ni pungufu, ni pungufu, haikutimu)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (41), Abuu Daawuud (821), An-Nasaaiy (2/135), At-Tirmidhiy (312) na Ibn Maajah (838)].

 

Swalaah pungufu haiwezi kuitwa kuwa ni Swalaah. Linaloonyesha kwamba upungufu unaokusudiwa hapa ni ule unaoifanya Swalaah isikamilike, ni ukamilisho wa Hadiyth hii kwa Muslim usemao kuwa Abu As- Saaib alisema: “Nilimwambia Abuu Hurayrah: “Wakati mwingine mimi ninakuwa nyuma ya imamu. Abuu Hurayrah akanibonyeza mkono akaniambia: Isome mwenyewe”.

 

3- Riwaya ya Rifa’a bin Raafi’i katika Hadiyth ya aliyeswali kimakosa, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia:

((..kisha soma Ummul Qur-aan, halafu soma Suwrah uitakayo..kisha fanya hivyo hivyo kila rakaa)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (18225). Na neno lake (Soma Ummul Kitaab) si la kawaida, Is-Haaq bin ‘Abdullah kalitumia yeye peke yake. Sheikh wetu Abuu ‘Umayr Allaah Amhifadhi amelihariri katika Shifaaul ‘Ayyi (1/192)]

 

Abuu Haniyfah kwa mujibu wa riwaya toka kwa Ahmad, anasema kwamba si lazima kusoma Suwrat Al-Faatihah, na kwamba inatosha kusoma Aayah yoyote ya Qur-aan. Hoja ya kauli hii ni dalili zifuatazo:

 

1- Neno Lake Ta’alaa:

((فَاقْرَءُوا مَا تَيَسَّرَ مِنَ الْقُرْآنِ ۚ ))

((Basi someni kile kilicho chepesi katika Qur-aan)). [Al-Muzzammil (73:20)]

 

Amejibiwa kwamba makusudio ya Aayah Tukufu ni Al-Faatihah pamoja na Suwrah nyepesi. Pia kuna uwezekano kwamba iliteremka kabla ya kuteremshwa Suwrat Al-Faatihah.

 

2- Katika Hadiyth ya Abuu Hurayrah kuhusiana na kisa cha aliyeswali kwa kukosea, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia mtu yule:

((Soma kilicho chepesi kwako katika Qur-aan)). [Hadiyth Swahiyh: Imekariri mara nyingi nyuma].

 

Anajibiwa kwamba neno lake (kilicho chepesi) ambacho hakikuainishwa ni kipi hasa, kimebainishwa kuwa ni Al-Faatihah katika riwaya isemayo: ((Soma Ummul Qur-aan)) kama itakuwa sahihi!! Kwa kuwa Al-Faatihah, ilikuwa ndiyo Suwrah nyepesi ya kuhifadhiwa na Waislamu. Imesemwa pia kwamba makusudio ya (kilicho chepesi), ni Suwrah nyingine zaidi ya Al-Faatihah kwa kuunganisha dalili tofauti.

 

3- Lau kama Suwrat Al-Faatihah ingelikuwa ni nguzo, basi ingelazimu kujifunza, na wala Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) asingeliruhusu kisomwe kingine mbadala kama ilivyo katika tamko la Hadiyth ya aliyeswali kwa kukosea lisemalo: ((Ikiwa umehifadhi chochote katika Qur-aan (soma), na kama huna basi mhimidi Allaah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (856)].

 

Anajibiwa kwamba hili alilipitisha wakati mtu anapokuwa hajahifadhi chochote katika Qur-aan. Pia linaweza kufungamanishwa na kutoweza mtu kujifundisha Qur-aan kama ilivyo katika Hadiyth ya Ibn Abiy Awfaa kwamba mtu mmoja alisema: “Ee Rasuli wa Allaah! Mimi siwezi kujifunza chochote katika Qur-aan, basi nifundishe kitakachonitosheleza katika Swalaah yangu”. Akamwambia: ((Sema: Subhaanal Laah, walhamdulil Laah, walaailaaha illal Laahu, wal Laahu Akbar, walaahawla walaaquwwata illaa bil Laahi)). [Al-Albaaniy kaipa daraja ya Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (832) na wengineo. Angalia Al-Irwaa (303)].  

 

Ninasema: “Hapana shaka yoyote kwamba kauli ya Jamhuri ndiyo yenye nguvu zaidi, nayo ndiyo inayopasa kufuatwa. Swalaah ambayo haikusomwa ndani yake Suwrat Al-Faatihah haiswihi kwa mwenye kuweza kuihifadhi kutokana na Hadiyth ya ‘ibaadah iliyotangulia ambayo haitiwi doa na lolote katika hayo yaliyotangulia. Kwa kuwa Hadiyth hii (kwa makadirio ya chini kabisa) ina hukmu ya ziada mbali ya ile iliyoko kwenye Aayah pamoja na Hadiyth ya aliyeswali kwa kukosea. Hivyo basi, ni lazima kuitumia.”

 

Kisha ikiwa mwonekano wa Hadiyth hizi utajumlishwa na Hadiyth ya Abuu Qataadah isemayo: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisoma Faatihahtul Kitaab katika kila rakaa”[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (759) kwa maana yake],  ongezea na kauli yake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa aliyeswali vibaya: ((Kisha fanya hivyo katika Swalaah yako yote)), yaani katika kila rakaa, basi hayo yote yanaonesha kwamba kusoma Al-Faatihah katika kila rakaa ni nguzo bila kuwepo tofauti kati ya imamu na maamuma, au kati ya imamu kusoma kwa sauti ya chini au ya juu kwa mujibu wa maelezo yatakayokuja baadaye.

 

·       

Kusoma Basmalah (Bismil Laahi Ar Rahmaan Ar Rahiym) Mwanzoni Mwa Al-Faatihah

 

Maulamaa wamekhitalifiana kuhusiana na hukmu ya kusoma basmalah mwanzoni mwa Suwrat Al-Faatihah kwa mujibu wa mahitilafiano yao kuhusu mas-ala ya: Je, “basmalah” ni Aayah katika Suwrat Al-Faatihah au si Aayah?

 

Lililo sahihi ni kuwa basmalah ni Aayah katika Qur-aan kabla ya kila Suwrah kwa kuwa imethibitishwa katika Msahafu ingawa (kwa mujibu wa kauli yenye nguvu) si Aayah katika Suwrat Al-Faatihah. Hivyo ni lazima kuisoma kabla ya Al-Faatihahh kwa mujibu wa msimamo wa Jamhuri ya Maulamaa. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

·       

Asiyeweza Kuihifadhi Al-Faatihahh

 

Al-Khattwaabiy amesema: [Maalimus Sunan]

 

“Kiasili ni kuwa Swalaah haikamiliki ila kwa kusoma Suwrat Al-Faatihahh, na ni mantiki kwamba kuisoma Suwrat Al-Faatihahh ni kwa mwenye kuimudu, na si kwa asiyeimudu. Na ikiwa mwenye kuswali haimudu lakini anaweza kusoma Aayah zingine za Qur-aan, basi itamlazimu asome kiasi cha Aayah saba za Qur-aan, kwa kuwa dhikri bora zaidi baada ya Al-Faatihahh ni Aayah mfanowe katika Qur-aan. Na kama mtu hana uwezo wa kujifunza chochote katika Qur-aan kutokana na ulemavu wa kimaumbile, au udhaifu wa hifdhi, au matatizo ya ulimi wake, au kilema, basi dhikri bora kwake baada ya Qur-aan itakuwa ni tasbiyh, tahmiyd, tahliyl n.k kama alivyofundisha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”.

 

Ninasema: “Ni neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa asiyeweza kuhifadhi Al-Faatihahh:

((Sema: Subhaanal Laahi, walhamdulil Laahi, walaailaaha illa Laahu, wal Laahu Akbar, walaa hawla walaa quwwata illaa bil Laah)). [Imetangulia karibuni].

 

4, 5- Kurukuu, na kutulizana katika rukuu

 

Kurukuu ni nguzo katika kila rakaa ya Swalaah kwa Ijma’a ya Maulamaa. [Maraatibul Ijma’a cha Ibn Hazm ukurasa wa 26]

 

Dalili zao ni:

 

1- Neno Lake Ta’alaa:

 

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا ارْكَعُوا وَاسْجُدُوا وَاعْبُدُوا رَبَّكُمْ وَافْعَلُوا الْخَيْرَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ))

(( Enyi walioamini! Rukuuni, na sujuduni na mwabuduni Rabb wenu, na fanyeni ya kheri ili mpata kufaulu)). [Al-Hajji (22:77)]

 

2-  Neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa aliyeswali kwa kukosea: ((Kisha rukuu mpaka utulie hali umerukuu)). [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa mara nyingi nyuma].

 

3-  Kudumu Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuifanya rukuu katika kila Swalaah pamoja na kauli yake: ((Swalini kama mnavyoniona nikiswali)). [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa hivi karibuni].

 

Uchache wa kutosheleza rukuu ni kuinama mtu kiasi cha mikono yake kukamata magoti.

Ama kutulizana, ni kwa neno lake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Kisha rukuu mpaka utulie hali umerukuu)).

 

Na kwa neno lake:

((Haikamiliki Swalaah yoyote ambayo mtu hanyooshi uti wake wa mgongo katika rukuu na sujudi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (2/183), At-Tirmidhiy (264), Abuu Daawuud (840) na Ibn Maajah (870)]

 

Kutulizana ni nguzo katika rukuu (na sujudi) kwa mujibu wa Jamhuri ya Maulamaa kinyume na Abuu Haniyfah. [Al-Mabsuutw (1/21), Al-Mudawwanah (1/71), Al-Majmu’u (3/407) na Al-Mughniy (1/360)]

 

Nako hutimu kwa kutulia na kunyamaa viungo vya mtu kama alivyomweleza Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mtu aliyeswali kwa kukosea:

((Haitimu Swalaah ya mmoja wenu mpaka atawadhe wudhuu kamili, kisha arukuu na aweke mikono yake juu ya magoti yake mpaka viungo vyake vitulie na vinyamae)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (859), An Nasaaiy (2/20), At-Tirmidhiy (302) na Ibn Maajah (460)].

 

Imesemwa: Ni kwa kadiri ya dhikri ya wajibu katika rukuu.

 

6, 7- Kuitadili (Kusimama sawa) baada ya rukuu na kutulizana

 

Ni kwa neno lake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa aliyeswali kwa kukosea:

((Kisha nyanyuka mpaka utulizane ukiwa umenyanyuka)).

 

Na katika Hadiyth ya Abuu Humayd (katika Sifa ya Swalaah ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)): ” Na anaponyanyua kichwa chake, hulingamana sawa mpaka irudi kila pingili ya uti wa mgongo (vertebra) mahala pake)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (828)].

 

Na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Swalini kama mnavyoniona nikiswali)).

Kunyanyuka toka kwenye rukuu kunaingia katika nguzo ya kuitadili kwa kuwa kunalazimiana nako.

 

8, 9- Kusuduju na kutulia katika sajdah

 

Kusujudu mara mbili katika kila rakaa, ni nguzo katika nguzo za Swalaah kwa Ijma’a ya Maulamaa. Na dalili yake ni:

 

1- Neno Lake Ta’alaa:

 

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا ارْكَعُوا وَاسْجُدُوا وَاعْبُدُوا رَبَّكُمْ وَافْعَلُوا الْخَيْرَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ))

((Enyi walioamini! Rukuuni, na sujuduni na mwabuduni Rabb wenu, na fanyeni ya kheri ili mpata kufaulu.)) [Al-Hajj (22:77)]

 

2- Neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa aliyeswali kwa kukosea:

((Kisha sujudu mpaka utulie ukiwa umesujudu)).

 

3- Neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Haikamiliki Swalaah yoyote ambayo mtu hanyooshi uti wake wa mgongo katika rukuu na sujudi)). [Hadiyth Swahiyh: Imetangulia hivi karibuni].

 

4- Neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

(( Hana Swalaah mtu ambaye pua yake haigusi sehemu ya ardhi kama kinavyogusa kipaji chake)). [Al-Albaaniy kaipasisha kuwa Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Ad-Daara Qutwniy (1/348). Angalia Sifa ya Swalaahah ukurasa 142].

 

5- Neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Timizeni rukuu na sujudi. Naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu iko Mkononi Mwake, hakika mimi nawaoneni nyuma yangu mnaporukuu na kusujudu)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (418) na Muslim (424) kutoka kwenye Hadiyth ya Abuu Hurayrah].

 

Ni lazima sijdah iwe juu ya viungo saba: Viganja viwili, magoti mawili, nyanyo mbili na kipaji cha uso pamoja na pua kutokana na Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu Anhumaa) kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Tumeamrishwa tusujudu juu ya viungo saba: Kipaji – akaashiria kwa mkono wake kwenye pua – mikono miwili (na katika tamko jingine: viganja viwili), magoti mawili, ncha za miguu miwili, na wala tusiikusanye nguo sehemu moja au nywele)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (812) na Muslim (490)].

 

10, 11- Kikao kati ya sijdah mbili na kutulizana

 

Ni nguzo kati ya nguzo za Swalaah kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa aliyeswali kwa kukosea:

((Kisha sujudu mpaka utulie ukiwa umesujudu, kisha nyanyuka mpaka utulie ukiwa umekaa, kisha sujudu mpaka utulie ukiwa umesujudu)).

 

Imepokelewa na ‘Aaishah amesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa hasujudu mara ya pili anaponyanyua kichwa chake toka kwenye sajdah mpaka alingamane akiwa amekaa”. [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (498) na Ibn Maajah (893)].

 

Ash-Shaafi’iy na Ahmad wamesema kuwa hii ni nguzo, na Maalik hakusema lolote. Ama Abuu Haniyfah, kwake inatosha kunyanyua kichwa kama ncha ya upanga!! [Al-Ummu (1/100), Al-Majmu’u (3/412), Al-Mughniy (1/375), Al-Mudawwanah (1/70) na Ibn ‘Aabidiyn (1/474)]

 

12, 13- Tashah-hudi ya mwisho na kikao chake

 

Ni nguzo kati ya nguzo za Swalaah. Swalaah hubatilika kwa kuiacha kwa kukusudia au kwa kusahau kutokana na dalili zifuatazo:

 

1- Hadiyth ya Ibn Mas-’oud (Radhwiya Allaahu Anhu) aliyesema: “Kabla ya kufaradhishwa kwetu tashah-hudi, tulikuwa tukisema: Assalaamu ‘alal Laahi kabla ‘ibaadihi, assalaam ‘alaa Jibriyl, assalaam ‘alaa Miykaaiyl. Rasuli  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatuambia:

((Msiseme: Assalaamu ‘alal Laahi, lakini semeni: At-Tahiyyaatu lil Laahi…mpaka mwisho wake)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” kwa tamko la: ( قبل أن يفرض علينا ) na An-Nasaaiy (3/40) na Al-Bayhaqiy (2/138). Angalia Al-Irwaa (309) na asili yake ni katika Swahiyh Mbili].

 

Hii ni dalili kwamba tashah-hudi ilifaradhishwa baada ya kuwa si faradhi.

 

2- Hadiyth ya Ibn Mas-’oud kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Anapokaa mmoja wenu katika Swalaah basi aseme: At-Tahiyyaatu lil Laahi…..)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (831) na Muslim (402)].

 

3- Kudumu Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuifanya.

 

Hii ndiyo kauli ya Ash-Shaafi’iy na Ahmad. Maalik anasema kwamba tashah-hudi ni Sunnah na wala si nguzo isipokuwa sehemu inapofanyika tasliym!! Ama Abuu Haniyfah, yeye anaona kwamba kukaa kiasi cha tashah-hudi ndiyo nguzo, ama tashah-hudi yenyewe si lazima!! [Al-Ummu (1/102), Al-Mughniy (1/387), Mawaahibul Jaliyl (2/525), Al-Mabsuutw (1/29)]

 

Wanaosema kwamba tashah-hudi si lazima hawakuleta dalili yoyote isipokuwa wanasema kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakumfundisha Swahaba aliyeswali kwa kukosea. Naam! Hii itafaa kuwa ni hoja na dalili itakapothibiti kwamba Hadiyth ya aliyeswali kwa kukosea ilikuja baada ya kuwajibishwa tashah-hudi. Lakini ikiwa Hadiyth hiyo ilikuja kabla ya kuwajibishwa, basi hakuna pingamizi ya kuja upya wajibu katika mawajibiko ambayo hayakuwemo kabla, kwa kuwa kuyabana mawajibiko yaliyoko kwenye Hadiyth hiyo tu na kuzifumbia macho dalili nyinginezo zilizokuja baada yake zenye kupasisha ulazima wa tashah-hudi, ni kuziba mlango wa sharia na kuyapa mgongo mawajibiko yote mapya yaliyokuja kuhusiana na Swalaah. Na kama historia ya suala haijulikani, basi kusema kuwa ni wajibu ni bora zaidi kwa kuwa yako yenye kuthibitisha wajibu huo. Isitoshe, hakuna chochote cha uhakika chenye kuondosha wajibu huo. Hivyo ni lazima kwa mwenye dalili za wajibu huo, kushikamana na dalili hizo. [As- Saylul Jarraar (1/219) na Naylul Awtwaar (2/309). Chapa ya Al-Hadiyth]

 

·       

Muundo Wa Tamko La Tashah-hudi

 

Imepokelewa toka kwa Ibn Mas-’oud (Radhwiya Allaahu Anhu) akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alinifundisha tashah-hudi viganja vyangu vikiwa kati ya viganja vyake kama anavyonifundisha Suwrah ya Qur-aan:

(( التحيات لله والصلوات لله والطيبات، السلام عليك أيها النبي ورحمة الله وبركاته، السلام علينا وعلى عباد الله الصالحين، أشهد أن لا إله إلا الله وأشهد أن محمدا عبده ورسوله))

((At-Tahiyyaatu lil-Laahi, was- Swalaawaatu lil-Laahi, wat-Twayyibaatu, As- Salaamu ‘alayka ayyuhan-Nabiyyu warahmatul-Laahi wabarakaatuh, as- Salaamu ‘alaynaa wa’ala ‘ibaadil- Laahis- swaalihiyna. Ash-hadu an laailaaha illal-Laahu wa ash-hadu anna Muhammadan ‘Abduhu wa Rasuwluhu)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (6265) na Muslim (402)].

 

Huu ndio muundo sahihi zaidi wa tamko la tashah-hudi. Haya ndiyo waliyoyasema Abuu Haniyfah na masahibu zake, Ath-Thawriy, Ahmad, Is-Haaq, Abuu Thawr na Jamhuri ya Maulamaa. [Al- Awsatw cha Ibn Al-Mundhir (3/207) na Al-Muhallaa (3/207)]

 

Lakini hata hivyo, Maulamaa wamekubaliana kwamba miundo yote ya matamshi ya tashah-hudi iliyothibiti toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inafaa. Baadhi yake itakuja mbeleni.

 

·       

Faida

 

Katika baadhi ya Sanad za Hadiyth hii ya Ibn Mas-’oud, yamekuja baadhi ya yanayolazimia mapishano katika neno lake (As Salaamu ‘Alayka) kati ya wakati wa uhai wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa tamshi la nafsi ya pili (msemeshwa), na kati ya baada ya kufariki kwake kwa tamshi la nafsi ya tatu (mzungumzwa): (As-Salaam ‘alan- Nabiyyi). Katika tamko lililopo kwa Al-Bukhaariy (6265) baada ya kuleta tashah-hudi, Ibn Mas-’oud alisema: “Na yeye akiwa hai nasi, na baada ya kufariki tulisema: As-Salaam, yaani juu ya Rasuli”.

 

Al-Haafidh ameitilia nguvu katika Al-Fat-h (2/366) akisema: “Imesihi bila shaka yoyote, nami nimempata mtu makini aliyeifuatilia. ‘Abdur Raaziq amesema: “Ibn Jariyj ametueleza, amenieleza ‘Atwaa kwamba wakati Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa hai, Maswahaba walikuwa wakisema: As-Salaamu ‘alayka ayyuhan Nabiyyu, na baada ya kufariki walisema: As-Salaam ‘alan Nabiyyi”. Na hii ni Isnadi Swahiyh.

 

Al-‘Allaamah Al-Albaaniy Rahimahul Laahu amesema: “Ni lazima hilo liwe ni kwa matni thabiti toka kwake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hili linatiliwa nguvu na kwamba ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu Anhaa) alikuwa akiwafundisha tashah-hudi katika Swalaah”. [Swifatu Swalaatin Nabiy ukurasa wa 161]

 

14- TASLIYM (KUTOA SALAAM)

 

Jamhuri ya Maulamaa wote isipokuwa Abuu Haniyfah wanasema kwamba tasliym ni nguzo ya Swalaah kwa dalili zifuatazo:

 

1- Neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):)       

((na kutoka kwake ni tasliym)). [Al-Albaaniy kaipa daraja ya Hadiyth Swahiyh. Imeshatajwa nyuma].

2- ‘Aaishah amesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimaliza Swalaah kwa tasliym”. [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (498) na Abuu Daawuud (783)].

 

3- Kudumu Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuifanya.

 

Imesemwa kwamba dalili hizi hazifikii ngazi ya kuipa tasliym hukumu ya kuwa ni nguzo, kwa kuwa tasliym haikutajwa katika Hadiyth ya aliyeswali kwa kukosea mpaka ijulikane kwamba Hadiyth ya ((kutoka kwake ni tasliym)) ilikuja baadaye nyuma. Hivi ndivyo alivyosema Ash-Shawkaaniy. [Naylul Awtwaar (2/352)]

 

Ninasema: “Hapa amekwenda kinyume na yale aliyokuwa ameyakubali  (katika yale niliyoyanukuu kutoka kwake yakieleza kuwa tashah-hudi ni wajibu) ya kwamba kama historia haijulikani, basi kusema ni wajibu kutakuwa na nguvu zaidi kutokana na Hadiyth yenye kuashiria ulazima. Linaloweza kuzozaniwa ni kuwa je Hadiyth ya ((mlango wake ni takbiyr, na kutoka kwake ni tasliym)) ni Swahiyh au la? Anayeona kuwa ni Swahiyh, basi itamlazimu kuizingatia tasliym kuwa ni nguzo.  

 

Jingine linaloonyesha kwamba tasliym ni nguzo ni dalili hizi zingine zifuatazo:

 

4- Hadiyth ya Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( Anapofanya shaka mmoja wenu katika Swalaah yake akawa hajui ameswali rakaa ngapi, je ni tatu au nne, basi aiweke kando shaka yake, kisha ajengee juu ya lile aliloliyakinisha, halafu asujudu sijdah mbili kabla ya kutoa tasliym)). [Hadiyth Swahiyh. Itakuja katika mlango wa sijdah ya kusahau].

 

5- Hadiyth ya Ibn Mas-’oud (kuhusiana na sijdah ya kusahau) : ”…basi alipanie lile analoliona kwamba ni sawa, kisha atoe tasliym, halafu asujudu sijdah mbili za kusahau”. [Hadiyth Swahiyh. Itakuja katika mlango wa sijdah ya kusahau]

 

Katika Hadiyth hizi mbili, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameamuru kutoa tasliym katika kila Swalaah hata ile ambayo mtu amesahau kitu ndani yake. Na amri hii pamoja na dalili nyingine zilizotangulia, zinajulisha kwamba tasliym ni faradhi. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

Ama kwa upande wa Abuu Haniyfah, yeye anasema kwamba tasliym mbili ni jambo la khiyari na wala si katika faradhi za Swalaah, bali ikiwa mtu atakaa kiasi cha tashah-hudi, basi Swalaah yake inakuwa imetimu. Kauli yake hii imetolewa dalili kwa riwaya ya Hadiyth ya Ibn Mas-’oud alipofundishwa tashah-hudi na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kuambiwa:

((Ukisema hivi, basi Swalaah yako imemalizika, ukitaka kusimama simama, na ukitaka kukaa kaa)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Hazm katika Al-Muhalla (3/279) na Al-Bayhaqiy katika Al-Khilaafiyyaat kama ilivyo katika An-Nayl (2/251)].

 

·       

Je, Inatosheleza Tasliym Moja, Au Lazima Tasliym Mbili?

 

Ash-Shaafi’iy, Maalik na Jamhuri ya Maulamaa wanasema kwamba tasliym ya kwanza ndio nguzo, ama ya pili ni Sunnah. Ibn Al-Mundhir kasema:  “Maulamaa wote mashuhuri wamejuzisha Swalaah ya tasliym moja ingawa linalopendeza zaidi ni kufanya tasliym mbili”.

An-Nawawiy kasema: “Maulamaa wakubwa weledi wamekubaliana kwamba haipasi isipokuwa tasliym moja tu!!”

 

Ninasema: “Ahmad bin Hanbali (katika riwaya iliyopokelewa toka kwake) amekwenda kinyume nao kwa kusema kwamba tasliym mbili ni lazima, na haya ndio madhehebu ya Hanbali. Hivi ndivyo pia walivyosema akina Ibn Hazm, Ahlu Dh-Dwaahir, baadhi ya wafuasi wa Maalik na Al-Hasan bin Swaaleh. Dalili zao ni hizi zifuatazo:

 

1- Kudumu Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kufanya tasliym mbili pamoja na Hadiyth yake isemayo: ((Swalini kama mnavyoniona nikiswali)), na hakuna Hadiyth yoyote Swahiyh waliyoipokea kwamba Rasuli alifanya tasliym moja.

 

2- Neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa Maswahaba wake alipowaona wanaashiria kwa mikono yao wakati wa kutoa tasliym:

(( Inamtosha mmoja wenu kuweka mkono wake juu ya paja lake na kumtolea salamu nduguye aliye kuumeni kwake na kushotoni kwake)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (431)].

 

Wamesema: “Kisichotosha, hakitoshelezi”.

 

Jamhuri ya Maulamaa wametoa dalili zifuatazo za kujuzisha kwao tasliym moja:

 

1- Hadiyth isemayo: ((..na kutoka kwake ni tasliym)). Ni kwamba tamko hili si ainishi na linaweza kumaanisha tasliym moja tu.

 

2- Hadiyth ya ‘Abdullaah bin Ubayya Awfaa aliyesema: “Nilimuuliza ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu Anhaa) kuhusiana na Swalaah anayoswali Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) usiku. Kati ya aliyoyasema: “Hakai mpaka anapofika rakaa ya nane, na hapo hukaa kwa ajili ya tashah-hudi, kisha husimama bila kutoa tasliym, na huswali rakaa moja. Halafu hukaa, akasoma tashah-hudi na kuomba du’aa, kisha hutoa tasliym moja akisema: As-Salaam ‘Alaykum kwa sauti ya juu ya kutufanya tuamke”. [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim].

 

Na katika tamko la Muslim (746): “..kisha hutoa tasliym tunayoisikia”. Inawezekana hapa ikawa moja au mbili, isipokuwa tasliym moja imethibiti toka kwa Maswahaba wengi akiwemo Anas na Ibn ‘Umar.

 

·       

Faida Mbili

 

Ya kwanza: Uchache wa tamko linalotosha katika tasliym ni kusema “As-Salaamu ‘Alaykum” kwa mujibu wa kauli sahihi zaidi, lakini ukamilifu na ubora zaidi ni kusema “As-Salaamu ‘Alaykum wa Rahmatul Laahi” kulia na kushoto.

 

Ya pili: Je, kuna nyongeza ya neno “Wa Barakaatuhu” katika tasliym?  [Huu ni muhtasari wa utafiti murua uliofanywa na ndugu yetu Ibrahiym Sheikh – Allaah Amlipe jaza yake – ukiwa na anwani isemayo: “Matamko ya Tasliym katika Swalaah”. Utafiti huu ulitolewa utangulizi na Sheikh wetu Mustwafa Al-‘Adawiy (Allaah Ainyanyue hadhi yake)]

 

La sahihi lililothibiti toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika tasliym ni kusema “As-Salaamu ‘Alaykum wa Rahmatul Laahi” kulia na kushoto. Hili limepokelewa toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa Sanad Swahiyh katika Hadiyth ya Jaabir bin Samrah, Ibn ‘Umar na Ibn Mas-’oud.

 

Ama nyongeza ya “Wa Barakaatuhu”, hii haikuja ikiwa marfu’u kwa isnadi isothabiti isipokuwa kupitia kwa Muusa bin Qays toka kwa Salamah bin Kuhayl toka kwa ‘Al-Qamah toka kwa Waail bin Hajar. Ad-daaraqutwniy ameikosoa riwaya hii, na baadhi ya Maulamaa wamezungumzia shaka yao kuhusiana na ‘Al-Qamah kuisikia toka kwa baba yake. Haikuja ikiwa Mawquwf kwa Isnadi Swahiyh isipokuwa toka kwa Al-Aswad bin Yaziyd.

 

Ili kuiweka ziada hii katika hali ya usahihi na kutanua wigo wa ijtihada na uhakiki zaidi, tunasema kuwa kwa yule anayeona kuwa riwaya ni Swahiyh, basi atachukulia kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiisema mara chache sanakatika tasliym ya kwanza. [Kafanya hivi Al’Allaamah Al-Albaaniy – Allaah Aitakase roho yake – katika kitabu cha Swifatus Swalaat]

 

Ama yule anayeichukulia kwamba ni Dhwa’iyf, basi aiache lakini asimshambulie mwenye kukhalifiana naye ambaye anaisema kwa nadra. Ama kudumu nayo kama wanavyofanya baadhi ya wanaodai kuwa ni wana Sunnah, huko ni kwenda kinyume kabisa na Sunnah.

Ijulikane kwamba wanachoona Jamhuri ya Maulamaa ni kufupisha na kusema: “As-Salaamu ‘Alaykum wa Rahmatul Laahi, As-Salaamu ‘Alaykum wa Rahmatul Laahi”.

 

15- Kufuatisha kimpangilio nguzo baada ya nyingine

 

Hii ni kutokana na yaliyothibiti kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), alikuwa akiswali kwa kuzifuatisha nguzo hizi kuongezea na neno lake: ((Swalini kama mnavyoniona nikiswali)). Aidha, alimfundisha aliyeswali kwa kukosea aswali kimpangilio kwa kusema: ((kisha..kisha)).

 

Na kwa vile Swalaah ni ‘ibaadah inayobatilika kwa hadathi, mpangilio umekuwa ni nguzo ndani yake kama ‘ibaadah nyinginezo. [Ad-Dusuwqiy (1/241), Mughnil Muhtaaj (1/158), Kash-Shaaful Qinaa (1/389) na Al-Mumti’i (3/426)]

 

 

Share