031-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Swalaah Ya Tawbah

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

031-Swalaah Ya Tawbah

 

 

Mwenye kuteleza akatenda dhambi, ni lazima aharakie kutubia na kurejea kwa Allaah Mtukufu, kwani Allaah ni Mwenye Kughufiria madhambi na Mwenye Kukubali toba.

 

Swalaah kwa ajili ya toba ya madhambi imesuniwa katika madhehebu yote manne. [Ibn ‘Aabidiyn (1/462), Ad-Dusuwqiy (1/314), Asnal Matwaalib na Kash-Shaaful Qinaa (1/443)]

 

Na hii ni kutokana na Hadiyth ya Abu Bakri (Radhwiya Allaahu Anhu) aliyesema: “Nimemsikia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

(( Hakuna mtu yeyote anayetenda dhambi, kisha akasimama, akatawadha na kuswali, halafu akaomba maghfirah kwa Allaah isipokuwa Allaah Humghufiria)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (406), Abu Daawuud (1521) na Ibn Maajah (1395). Katika Sanad yake yuko Asmaa bin Al Hakam. Al-Haafidh kasema: “Ni mkweli asiye na shaka”. Ninasema: “Bali hajulikani”] Kisha akasoma Aayah hii:

(( وَالَّذِينَ إِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً أَوْ ظَلَمُوا أَنفُسَهُمْ ذَكَرُوا اللَّـهَ فَاسْتَغْفَرُوا لِذُنُوبِهِمْ وَمَن يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلَّا اللَّـهُ وَلَمْ يُصِرُّوا عَلَىٰ مَا فَعَلُوا وَهُمْ يَعْلَمُونَ ))

Sanad ya Hadiyth hii ni Dhwa’iyf, lakini Aayah inatilia nguvu maana yake. Baadhi ya Maulamaa wameipasisha kuwa ni Hadiyth Swahiyh.

 

· Kuswali Rakaa Mbili Baada Ya Kutufu Al-Ka’abah

 

Jamhuri ya Maulamaa wanasema kwamba imesuniwa kuswali rakaa mbili nyuma ya Maqaamu Ibraahiym baada ya Kutufu. Katika rakaa hizo mbili, atasoma baada ya Al-Faatihahh (Qul yaa ayyuhal kaafiruwna) na (Qul Huwa Allaahu Ahad). Na hii ni kutokana na kitendo chake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hijjah yake kama ilivyo katika Hadiyth ndefu ya Jaabiritakayoelezewa kikamilifu katika mlango wa Hijjah. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (1218). Itaelezewa kikamilifu katika mlango wa Hijjah]

 

Abu Haniyfah anasema kwamba rakaa hizo mbili ni wajibu.

 

Rakaa hizi mbili huswaliwa wakati wowote hata katika wakati usioruhusiwa kuswali kutokana na Hadiyth ya Jubayr bin Mutwim kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Enyi ukoo wa ‘Abdi Manaaf! Msimzuie yeyote aliyetufu Nyumba hii na akaswali wakati wowote aupendao mchana au usiku)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (869), An-Nasaaiy (5/223) na Ibn Maajah (1254)].

 

 

Share