038-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Swalaah Ya Khofu

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

038-Swalaah Ya Khofu

 

 

  • Taarifu Yake

[Al-Badaai’u (1/243), Haashiyatul ‘Adawiy (1/296), Rawdhwat At-Twaalibiyna (2/49) na Al-Mughniy (2/402)]

 

Khofu ni kutarajia adha kutokana na dalili za kuhisika au zinazoonekana wazi. Na makusudio yake hapa ni kupambana na adui au chochote ambacho kinamtia mtu khofu na taharuki.

 

Swalaah ya Khofu si Swalaah ya kujitegemea yenyewe kama Swalaah ya ‘Iyd au ya Kupatwa Jua na kadhalika, bali ni Swalaah ya kawaida ya faradhi kwa nguzo zake zilezile, masharti yake, Sunnah zake na idadi ya rakaa zake kama inavyokuwa katika hali ya amani. Isipokuwa tu kama itaswaliwa kwa jamaa, itakuwa kwa namna tofauti, na itabeba mambo ambayo haina katika hali ya amani. Na kwa msingi huu, tunaweza kuielezea Swalaah ya Khofu kama ni Swalaah ya Faradhi ambayo wakati wake unaingia na Waislamu wanapambana na adui au wakijilinda na adui.

  • Kujuzu Kwake:

Swalaah ya Khofu imethibiti kutokana na Neno Lake Ta’alaa:

((وَإِذَا كُنتَ فِيهِمْ فَأَقَمْتَ لَهُمُ الصَّلَاةَ فَلْتَقُمْ طَائِفَةٌ مِّنْهُم مَّعَكَ وَلْيَأْخُذُوا أَسْلِحَتَهُمْ فَإِذَا سَجَدُوا فَلْيَكُونُوا مِن وَرَائِكُمْ وَلْتَأْتِ طَائِفَةٌ أُخْرَىٰ لَمْ يُصَلُّوا فَلْيُصَلُّوا مَعَكَ وَلْيَأْخُذُوا حِذْرَهُمْ وَأَسْلِحَتَهُمْ ۗ وَدَّ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْ تَغْفُلُونَ عَنْ أَسْلِحَتِكُمْ وَأَمْتِعَتِكُمْ فَيَمِيلُونَ عَلَيْكُم مَّيْلَةً وَاحِدَةً ۚ وَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِن كَانَ بِكُمْ أَذًى مِّن مَّطَرٍ أَوْ كُنتُم مَّرْضَىٰ أَن تَضَعُوا أَسْلِحَتَكُمْ ۖ وَخُذُوا حِذْرَكُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ أَعَدَّ لِلْكَافِرِينَ عَذَابًا مُّهِينًا))

((Na utapokuwa upo kati yao, ukawaswalisha, basi lisimame kundi miongoni mwao pamoja nawe, na wachukue silaha zao. Watakaposujudu basi wawe nyuma yenu (kuwalinda). Na lije kundi jingine ambalo halikuswali, liswali pamoja nawe, nao washike hadhari na silaha zao. Wale waliokufuru wanatamani kama mtaghafilika na silaha zenu na vifaa vyenu wakuvamieni mvamio mmoja. Na wala si dhambi kwenu ikiwa mna maudhiko kutokana na mvua au mkiwa wagonjwa kuweka (chini) silaha zenu. Na mshike hadhari zenu. Hakika Allaah Amewaandalia makafiri adhabu ya kudhalilisha)). [An-Nisaa (4:102)]

 

Aidha, imethibiti kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliiswali kama tutakavyokuja kulieleza hilo, na Maulamaa wamekubaliana wote juu ya hili, halafu wakakhitalifiana kuhusiana na kujuzu kwake baada ya kufariki Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Jamhuri ya Maulamaa –kinyume na Abu Yuusuf swahibu yake Abu Haniyfah- wanaona kwamba sharia ya Swalaah hii iko mpaka Siku ya Qiyaamah, na kwamba agizo alilopewa Nabiy ni agizo kwa umma wake pia madhali hakuna dalili ya kulihusisha agizo hilo kwake peke yake. [Al-Badaai’u (1/242), Al-Mudawwanah (1/161), Al-Ummu (1/186) na Al-Mughniy (2/400)]

 

Pia, kuhusishwa yeye na agizo hakumaanishi kwamba hukmu inamhusu yeye peke yake mbali na kwamba:

 

1- Kauli yake: ((Swalini kama mnavyoniona nikiswali)), ni jumuishi. [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa mahala pengi].

 

2- Maswahaba wote kwa pamoja wamekubaliana uwepo wa Swalaah hii baada ya kufariki Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) [Al-Haafidh kainukuu Ijma’a kwenye Al Fat-h (2/498) na Ibn Qudaamah kwenye Al-Mughniy (2/400)]…… na kwa waliosimuliwa kuwa wameiswali ambao ni: [Angalia baadhi ya athar zilizopokelewa toka kwao na takhriyj zake katika Irwaa Al-Ghaliyl (3/42-45)]

 

(a) ‘Aliy usiku wa vita vya Swaffayn na Al-Hariyr.

(b) Abu Muusa Al-Ash-’ariy na wenzake huko Asbahaan.

(c) Hudhayfah bin Al-Yamaan na Maswahaba akiwemo Sa’ad bin Abi Waqqaas huko Tubrustan.

 

Ama Al-Mazniy ambaye ni katika wafuasi wa Ash-Shaafi’iy, yeye anaona kwamba Swalaah hii ilikuwepo lakini baadaye iliondoshwa!! Hoja yake ni kuwa katika vita vya Khandaq, zilimpita Rasuli  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Swalaah, na lau kama Swalaah ya Khofu ingelikuwa inajuzu, basi angeiswali. Amejibiwa kwamba hilo lilikuwa kabla ya kuteremka Aayah ya Swalaah ya hofu kama ilivyo katika Hadiyth ya Abu Sa’iyd isemayo: “Tulizingirwa Siku ya Khandaq…. Na hii ni kabla Allaah ‘Azza wa Jalla Hakuteremsha lolote kuhusu Swalaah ya Khofu”. Hadiyth hii ishaelezewa kwenye mlango wa kulipa Swalaah zilizompita mtu.

  • Inavyoswaliwa

Kuna namna nyingi za kuiswali Swalaah ya Khofu zilizothibiti toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zikiwa na usuwli sita. Hakuna makhitalifiano kati ya Maulamaa kuhusiana na namna yoyote, bali kila moja inafaa kwa kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliiswali mara kadhaa, katika siku tofauti na kwa miundo mbalimbali. Katika kila muundo, alikuwa akiangalia namna itakayochunga Swalaah na kuwalinda zaidi na adui. [Al-Badaai-’i (1/342), Mughnil Muhtaaj (1/301), Al-Mughniy (2/412) na Naylul Awtwaar (3/367 na kurasa zinazofuatia)]

 

Picha zake ni tofauti lakini maana yake ni moja. Kati ya miundo hiyo ni:

 

(a) Ikiwa adui hayuko upande wa Qiblah

 

1- Askari watagawanywa vikosi viwili. Kikosi kimoja kitawekwa mkabala na adui na kingine kitajihami nacho kwa namna ambayo mishale haiwezi kukifikia. Imamu ataanza Swalaah na kikosi hiki, na ataswali nao rakaa moja ikiwa Swalaah ni ya rakaa mbili, au rakaa mbili kama Swalaah ni ya rakaa tatu au nne, kisha atabakia amesimama. Halafu maamuma watakamilisha Swalaah wenyewe kisha watakwenda kusimama mkabala na adui. Halafu kitakuja kikosi kilichokuwa awali mkabala na adui, imamu atawaswalisha kwa rakaa zilizobakia, na anapokaa kwa tashah-hudi, wao watasimama kukamilisha rakaa zilizobakia huku yeye akiwasubiri, na wanapokuja kukaa naye, atatoa tasliym kumaliza nao Swalaah. [Haya ndiyo waliyosema Jamhuri ya Maulamaa. Maalik kasema kwamba imamu hatoi tasliym wala hawangojei, bali anapotoa tasliym wao watakamilisha wenyewe rakaa zilizosalia kwa mujibu wa Hadiyth Mawquwf]

 

Asili ya hili ni Hadiyth ya Swaaleh bin Khawwaat kuhusiana na walioswali na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Swalaah ya Khofu Siku ya Dhaat Ar Riqa’a isemayo: “Kikosi kimoja kilisimama safu pamoja naye, na kikosi kingine kilisimama safu mkabala wa adui. Akaswali rakaa moja na kikosi kilichosimama naye, kisha akabaki amesimama, na wao wakakamilisha wenyewe. Walipomaliza walikwenda kusimama mkabala wa adui, na kikosi kilichokuwa mkabala na adui kikaenda kwake, akaswali nao rakaa iliyokuwa imesalia katika Swalaah yake. Halafu alibaki amekaa mpaka wakakamilisha wenyewe, kisha akatoa tasliym pamoja nao”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (4130) na Muslim (842)].

 

Tamshi la Swaaleh bin Khawwaat alilolipokea toka kwa Sahl bin Abi Hatamah linasema kwamba yeye anawangojea akiwa amekaa si amesimama, na ndivyo lilivyo kwenye Swahiyh. Ash-Shaafi’iy na wafuasi wake wanaufuata muundo huu.

 

2- Imamu ataswali rakaa moja na kikosi cha kwanza, na kikosi kingine kitaelekea upande aliko adui. Kisha kikosi alichokiswalisha rakaa moja kitaondoka kiende kusimama upande aliko adui. Halafu kitakuja kile kikosi kingine, atakiswalisha rakaa moja, halafu kila kikosi kitakamilisha chenyewe rakaa moja.

 

Asili ya hili ni Hadiyth ya Ibn ‘Umar aliyesema: “Nilishiriki vita eneo la Najd pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Tulimweka adui mkabala wetu na tukapanga safu mbele yao. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasimama kutuswalisha. Kikosi kimoja kikasimama pamoja naye kuswali na kikosi kingine kikamwelekea adui. Rasuli akakiswalisha kikosi alichonacho rakaa kamili. Kisha wakaondoka kwenda kukamata nafasi ya kikosi ambacho bado hakijaswali, wakaja, Rasuli akawaswalisha rakaa kamili halafu akatoa tasliym. Kisha kila kikosi kikajikamilishia chenyewe rakaa moja”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (943) na Muslim (839)].

 

Mwonekano wa Hadiyth hii ni kuwa wote walikamilisha katika hali moja. Pia yawezekana kwamba kikosi cha pili kilikamilisha baada ya tasliym, halafu wakarejea wale wa mwanzo mahala pao wakakamilisha rakaa. Na hili ndilo lenye nguvu kwa upande wa maana, na kama si hivyo basi ulinzi unaotakikana kuwekwa utakosekana na imamu atabaki peke yake. Riwaya ya Ibn Mas-’oud inalitilia nguvu hili. Inasema: “Kisha akatoa tasliym, na hawa (yaani kikosi cha pili) wakasimama kujikamilishia wenyewe rakaa, wakatoa tasliym kisha wakaondoka. Halafu wakaja wale kwenye sehemu yao wakajikamilishia wenyewe rakaa moja, kisha wakatoa tasliym”. [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Dawuud (1244), At-Twahaawiy (1/184) na Ad-daaraqutwniy. Angalia Al-Irwaa (3/49)].

 

Mahanafi wanaufuata muundo huu isipokuwa Abu Yuusuf.

 

3- Imamu ataswali na kikosi kimoja rakaa mbili na atatoa tasliym, kisha ataswali na kingine na kutoa tasliym.

 

Asili ya hili ni Hadiyth ya Jaabir na Hadiyth ya Abu Bakrah. Jaabir anasema: “Tulikuwa pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huko Dhaat Ar Riqa’a, na Swalaah ikaqimiwa. Akaswali na kikosi kimoja rakaa mbili kisha wakarudi nyuma, halafu aliswali na kikosi kingine rakaa mbili. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawa ameswali rakaa nne, na watu rakaa mbili”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy ikiwa mu’allaq (4136), na mawsuul kwa Muslim (843). Angalia At-Taghliyq (4/120)].

 

Tamshi jingine linasema: “Aliswali na kundi la Maswahaba wake rakaa mbili kisha akatoa tasliym, halafu akaswali na jingine rakaa mbili na kutoa tasliym”. [Isnadi yake ni dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ash-Shaafi’iy (506), An-Nasaaiy (3/178), Ad-daaraqutwniy (186) na Al-Bayhaqiy (3/259)].

 

Abu Bakrah anayatilia nguvu haya akisema kwenye Hadiyth yake: “Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alituswalisha Swalaah ya Khofu. Akaswali rakaa mbili pamoja na baadhi ya Maswahaba wake, kisha akatoa tasliym. Wakarudi nyuma na wakaja wengine wakasimama mahala pao, Nabiy akaswali nao rakaa mbili kisha akatoa tasliym. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawa ameswali rakaa nne, na watu rakaa mbili mbili”. [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (3/179), Abu Dawuud (1248), Al-Bayhaqiy (3/260) na At-Twahaawiy (1/315)].

  • Faida

Hadiyth mbili zinaonyesha kwamba inajuzu kwa mwenye kuswali faradhi kumfuata mwenye kuswali Sunnah. Kwa kuwa rakaa mbili za mwisho zilikuwa ni Sunnah kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na kwa kundi la pili zilikuwa ni faradhi.

 

4- Imamu ataswali rakaa moja na kikosi kimoja – kingine kikiwa kimemwelekea adui – kisha wataondoka, halafu kitakuja kikosi cha pili na ataswali nacho rakaa moja. Kila kikosi kitatosheka na rakaa moja tu na hawataswali rakaa nyingine.

 

Asili ya hili ni Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas asemaye: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali Dhiy Qarad, watu wakapanga safu mbili nyuma yake; safu moja nyuma yake moja kwa moja na nyingine mkabala na adui. Akaswali rakaa moja na safu iliyo nyuma yake moja kwa moja, kisha wakarejea hawa kwenda kwenye safu ya wale wengine. Wale wengine wakaja kwenye safu ya hawa, akaswali nao rakaa moja tu na hawakuswali ya pili”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (3/169), Ibn Hibaan (2871) na Ahmad lakini kwake hakuna “na hawakuswali ya pili”!!]

 

Abu Hurayrah [Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (3035), Ahmad (2/522) na An-Nasaaiy (3/174), na Sanad yake ni Hasan], …Zayd bin Thaabit [Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (3/168) na Ahmad (5/183), na Sanad yake ni Hasan katika Hadiyth wenza],… na Hudhayfah [Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (3/168) na Ahmad (5/183), na Sanad yake ni Hasan katika Hadiyth wenza], …wana Hadiyth kama hii.

 

Hadiyth nyingine ya Ibn ‘Abbaas inayoonyesha kuswihi kutosheka na rakaa moja inasema: “Allaah (Jalla wa ‘Alaa) Aliifaradhisha Swalaah kwa ulimi wa Nabiy wenu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam); mjini rakaa nne, safarini rakaa mbili, na kwenye khofu (vita) rakaa moja”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (687), Abu Daawuud (1247) na Ahmad (1/237)].

 

5- Jeshi litagawanywa vikosi viwili. Kikosi kimoja kitasimama safu nyuma ya imamu na kingine kitatazamana na adui. Vikosi vyote viwili vitafunga Swalaah pamoja na imamu, halafu kikosi kilicho nyuma yake kitarukuu na kusujudu pamoja naye huku kikosi kinachotazamana na adui kikibaki kimesimama. Kisha askari walioswali na imamu rakaa mbili watachukua silaha zao waende kusimama mbele ya adui, na wale waliokuwa mbele ya adui watakwenda nyuma ya imamu, watajiswalia wenyewe rakaa moja huku imamu amesimama, halafu atawaswalisha rakaa ya pili. Kisha watakuja waliokwenda kusimama mbele ya adui, watajiswalia wenyewe rakaa moja huku imamu na kikosi kingine wakiwa wamekaa, kisha imamu atatoa tasliym pamoja nao wote.

 

Asili ya muundo huu ni Hadiyth ya Abu Hurayrah ambaye aliulizwa kuhusu Swalaah ya Khofu akajibu: "Nilikuwa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika vita vile. Nabiy wa Allaah akawagawanya watu makundi mawili. Kundi moja likasimama pamoja naye, na kundi jingine likamwelekea adui nailhali migongo yao imeelekea Qiblah. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akapiga takbiyr na wao wote wakapiga naye takbiyr (walio pamoja naye na waliomwelekea adui). Kisha Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akarukuu rukuu moja, na kundi alilo nalo likarukuu, kisha akasujudu na kundi alilonalo likasujudu huku wale wengine wakiwa wamesimama kuelekeana na adui. Halafu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisimama na watu wa kundi lililoswali naye wakachukua silaha zao, kisha wakaenda kinyumenyume mpaka wakasimama mbele kukabiliana na adui. Halafu likaja kundi lililokuwa mkabala na adui, wakarukuu na kusujudu nailhali Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasimama kama alivyo, kisha wakasimama. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akarukuu rakaa nyingine na wao wakarukuu pamoja naye, akasujudu wakasujudu pamoja naye. Halafu likaja kundi lililokuwa limeelekeana na adui, wakarukuu na wakasujudu nailhali Nabiy wa Allaah amekaa pamoja na alio nao. Kisha ikaja tasliym, na Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatoa tasliym, na wote wakatoa tasliym. Watu wakasimama wakiwa wameshiriki wote Swalaah pamoja naye". [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Dawuud (1241), An-Nasaaiy (3/173) na Ahmad (2/320)].

 

(b) Ikiwa adui yuko upande wa Qiblah

 

6- Imamu atawagawa vikosi viwili, atahirimia Swalaah pamoja nao wote, atasoma, atarukuu na ataitadili pamoja nao wote. Kisha atasujudu na kikosi kimoja huku kingine kikichunga mpaka atakaposimama imamu toka kwenye sijdah, na hapo kikosi kingine kitasujudu, na baada ya kusujudu, watamfata imamu kwenye kisimamo. Katika rakaa ya pili, imamu atafanya hivyo hivyo lakini watakaolinda mara hii ni wale waliosujudu naye katika rakaa ya kwanza. Halafu atakaa nao tashahhudi na kutoa tasliym pamoja nao wote.

 

Asili ya muundo huu ni Hadiyth ya Jaabir aliyesema: “Niliswali pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Swalaah ya vitani. Tulijipanga safu mbili: safu moja nyuma ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huku adui akiwa kati yetu na Qiblah.  Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akapiga takbiyr ya kuhirimia Swalaah, nasi sote tukapiga. Kisha akanyanyua kichwa chake toka kwenye rukuu, nasi sote tukanyanyuka. Akateremka kwenda sijdah pamoja na safu iliyomfuatia, na safu ya nyuma ikasimama mkabala na adui. Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomaliza kusujudu na ikasimama safu inayomfuatia, safu ya nyuma iliteremka kwenda sijdah kisha wakasimama. Kisha safu ya nyuma ikaja mbele na ya mbele ikaenda nyuma, Nabiy akarukuu, nasi sote tukarukuu. Halafu akanyanyua kichwa chake toka kwenye rukuu, nasi sote tukanyanyua, akateremka kwenda sijdah pamoja na safu inayomfuatia ambayo ilikuwa nyuma katika rakaa ya kwanza. Kisha safu ya nyuma ikasimama kumwelekea adui, na Nabiy alipomaliza sijdah pamoja na safu inayomfuatia, safu ya nyuma iliteremka kwenda sijdah wakasujudu, halafu Nabiy akatoa tasliym, nasi sote tukatoa tasliym. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (840) na Abu Dawuud (1241)].

 

Hadiyth mfano wa hii ya Abu ‘Ayyash Az-Zuraqiy iko, nayo ni Hadiyth Swahiyh ambayo imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Dawuud (1236), An-Nasaaiy (3/176), Ahmad (4/59) na wengineo].

 

  • Swalaah Vita Vikiumana

[Al-Badaai-’i (1/244), Rawdhwat At-Twaalibiyna (2/60), Al-Mughniy (2/416) na Kash-Shaaful Qinaa (1/18)]

 

1- Vita vikiumana watu wakashindwa kuswali jamaa kwa miundo iliyotangulia, na wakawa na matarajio ya kutulia hali kabla ya kutoka wakati wa Swalaah, hapo itakuwa vyema kuikawiza.

 

2- Ikiwa muda utabakia wa kuweza kuswali, wataswali kwa kuashiria lakini kama muda hakuna, kila mmoja ataswali peke yake kiasi awezavyo. Wakiweza kurukuu na kusujudu watafanya, au wanaweza kuswali huku wanatembea kwa miguu au kwenye vipando wakiwa wameelekea Qiblah au bila kuelekea. Hawatalipa Swalaah utulivu unaporejea si kwa wakati uliopo kwao wala kwa ujao.

 

Asili ya hili ni Neno Lake Ta’alaa:

((فَإِنْ خِفْتُمْ فَرِجَالًا أَوْ رُكْبَانًا ۖ فَإِذَا أَمِنتُمْ فَاذْكُرُوا اللَّـهَ كَمَا عَلَّمَكُم مَّا لَمْ تَكُونُوا تَعْلَمُونَ))

((Mkikhofu (swalini) huku mnatembea au mmepanda kipando. Mtakapokuwa katika amani mdhukuruni Allaah kama Alivyokufunzeni yale mliyokuwa hamuyajui)). [Al-Baqarah (2:239)]

 

Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar akisema: “Ikiwa kizaazaa kitakuwa zaidi ya hapo, basi wataswali kwa kusimama wakitembea au wakiwa kwenye vipando, wameelekea qiblah au bila kuelekea”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (4535), Ibn Maajah (1258) na Maalik (442)].

 

Al-Bukhaary kaongeza: “Amesema Naafi’i: Simwoni ‘Abdullah bin ‘Umar amelisema hilo isipokuwa toka kwa Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”.

Wakishindwa kurukuu na kusujudu, basi watazifanya kwa ishara, na ishara ya sijdah itakuwa ya chini zaidi kuliko ya rukuu.

 

Ninasema: “Rakaa moja itatosheleza, na Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.

 

3- Ikiwa mapambano na adui yatawashughulisha mpaka wakati wa Swalaah ukatoka, basi hakuna ubaya na Swalaah yao wataiswali pale watakapoweza. Ni kama ilivyotokea kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika vita vya Khandaq. Alishughulishwa yeye na Maswahaba zake hadi Swalaah ya  Alasiri ikawapita wakaja kuiswali baada ya Magharibi. Hadiyth kuhusiana na hili tumeitaja kwenye mlango wa kulipa Swalaah zilizompita mtu.

  • Je, Yafaa Kuswali Swalaah Ya Khofu Mjini?

Mtu akiwa mjini kwake, akakabiliwa na khofu toka kwa adui dhalimu kafiri, auMuislamu katili, au mafuriko, au moto, au mnyama mkali na kadhalika, basi anaruhusiwa kuswali Swalaah ya Khofu. Hii ni kauli ya Maulamaa wengi kama Abu Haniyfah, Maalik, Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Al-Awzaa’iy na Ibn Hazm. [Al-Ummu (1/186), Al-Mudawwanah (1/161), Al-Mughniy (2/302), Twarhu At-Tashriyb (3/141), Naylul Awtwaar (3/377-378) na Al-Muhalla (5/33-43)]

 

Wanasema ni kutokana na Kauli Yake Ta’alaa:

((وَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِن كَانَ بِكُمْ أَذًى مِّن مَّطَرٍ أَوْ كُنتُم مَّرْضَىٰ أَن تَضَعُوا أَسْلِحَتَكُمْ ۖ وَخُذُوا حِذْرَكُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ أَعَدَّ لِلْكَافِرِينَ عَذَابًا مُّهِينًا ))

((Na wala si dhambi kwenu ikiwa mna maudhiko kutokana na mvua au mkiwa wagonjwa kuweka (chini) silaha zenu. Na mshike hadhari zenu. Hakika Allaah Amewaandalia makafiri adhabu ya kudhalilisha)). [An-Nisaa (4:102)]

 

 Na hili halikuhusishwa na safari. [Ila kwa mwenye kusema kwamba makusudio ya Kauli Yake Ta’alaa وإذا ضربتم في الأرض فليس عليكم جناح أن تقصروا من الصلاة ni Swalaah ya Khofu, na si kupunguza Swalaah. Huyo, atajengea kwamba hilo limehusishwa na safari tu]

 

Ikiwa pataulizwa: Je, Hadiyth zote zilizotangulia zinahusiana na safari tu? Patajibiwa kwamba safari ni wasifu usio na kadiri, hauna sharti wala sababu, na kama si hivyo, basi ingelazimu kwamba asiswali isipokuwa wakati wa kutishiwa na adui kafiri!!

  • Faida

Mtu akiswali Swalaah ya Khofu mjini kwake, basi ataiswali kwa idadi kamili ya rakaa zake kwa muundo wowote kati ya miundo iliyoelezewa, na hii ni kwa imamu na maamuma.

 

Lakini je, itafaa kuswali rakaa moja mjini kwa mujibu wa Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas isemayo: “Allaah Jalla wa ‘Alaa Aliifaradhisha Swalaah kwa ulimi wa Nabii wenu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam); mjini rakaa nne, safarini rakaa mbili, na kwenye khofu (vita) rakaa moja?” [Hadiyth Swahiyh: Takhriyj yake tumeitaja nyuma kidogo].

 

Na je, kujuzu kuswali Swalaah ya Khofu kwa kuashiria wakati mambo yanaposhitadi kunaitilia nguvu Hadiyth hii?

Haya ni ya kutafitiwa zaidi. Ibn Hazm kwa mujibu wa mwonekano wa Hadiyth, hakujuzisha kuswali rakaa moja isipokuwa safarini tu. Basi nawe litafiti hili.

 

 

Share