049-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Maandalizi Kwa Ajili Ya Swalaah Ya Ijumaa

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

049- Maandalizi Kwa Ajili Ya Swalaah Ya Ijumaa

 

 

Kuoga

 

Ni wajibu kwa mwenye kwenda katika Swalaah ya Ijumaa – katika waliowajibikiwa - aoge kwa mujibu wa kauli mbili sahihi za Maulamaa. Na hii ni kwa mujibu wa dalili tulizokwishazieleza katika mlango wa yenye kuwajibisha ghusl. Kati yake ni Hadiyth ya Abu Sa’iyd ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Kuoga Siku ya Ijumaa ni wajibu kwa kila Muislamu aliyebaleghe)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (879) na Muslim (846)].

 

Na Hadiyth ya Ibn ‘Umar ya kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Akija mmoja wenu Ijumaa, basi aoge)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (877) na Muslim (84)].

 

Linalofahamika kutokana na Hadiyth hizi ni kwamba si wajibu kuoga kwa asiyehudhuria Ijumaa, kwani  hakuna umuhimu huo kwa aliyesameheka kwenda Ijumaa. Haya wameyasema Jamhuri. [Fat-hul Baariy (2/417) na Al-Awsatw (4/48)].

 

· Faida Mbili:

 

1- Aliyepatwa na hadathi ndogo baada ya kuoga

 

Huyu kutamtosheleza kutawadha, kwani hadathi huiathiri twahara ndogo tu na wala haiathiri kusudio la kuoga ambalo ni kuutakasa mwili na kuondosha harufu. Aidha, kuoga huko ni kama kuoga janaba ambako hakutenguliwi na hadathi. [Al-Mughniy (2/99)].

 

2- Aliyepatwa na janaba Siku ya Ijumaa, basi josho moja tu litamtosheleza.

 

Mtu huyu litamtosheleza josho moja kwa janaba na Ijumaa kama atayanuwia yote mawili. Hii na kauli ya Maulamaa wengi ambao wamesema: “Tumekuta kwamba wudhuu mmoja na tayammumi moja, hutosheleza hadathi zote zenye kutengua wudhuu, na josho moja hutosheleza janaba zaidi ya moja, na josho moja hutosheleza hedhi ya masiku kadhaa, na twawafu moja hutosheleza ‘Umrah na Hajji katika qiraan. Hivyo ni lazima iwe hivyo kwa kila lenye kuwajibisha kuoga”.

 

Lakini Ibn Hazm amekwenda kinyume na hili akisema kwamba ni wajibu kila kimoja kiwe na josho lake maalum, na ameikosoa kirefu kauli hiyo ya Jamhuri. [Al-Awsatw (4/43), Al-Majmu’u (4/365), Al-Mughniy (2/99) na Al-Muhalla (2/45)].

 

Yaliyosuniwa Kabla Ya Kwenda Ijumaa

 

1- Kujitia manukato – kama anayo - isipokuwa kwa aliyehirimia na kwa mwanamke

 

Imepokelewa toka kwa Salmaan akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Haogi mtu Siku ya Ijumaa, akajitwaharisha kiasi awezavyo kujitwaharisha, akajipaka mafuta katika mafuta yake, akajitia manukato ya nyumbani kwake, kisha akatoka na asiingie kati ya watu wawili, halafu akaswali aliyoandikiwa, kisha akanyamaza wakati imamu anakhutubu, isipokuwa hughufiriwa yaliyo kati yake na Ijumaa nyingine)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (883), Abu Daawuud (1113), Ad-daaramiy (1541) na Al-Baghawiy (1058)]

 

Ama mwenye kuhirimia, huyo haijuzu kutumia manukato kama itakavyokuja kuelezwa katika mlango wa Hijjah.

 

Ama mwanamke, kuna dalili kochokocho zenye kuthibitisha uharamu wa kutoka akiwa amejitia manukato hata kama ni kwenda Msikitini kwa Swalaah. Kati yake ni Hadiyth ya Zaynab Ath-Thaqafiyyah toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) isemayo: ((Akihudhuria mmoja wenu ‘Ishaa ( Msikiti: katika riwaya nyingine) basi asijitie manukato usiku huo)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (443) na An- Nasaaiy (2/260)].

 

2- Kupiga mswaki

 

Ni kwa Hadiyth Marfu’u ya Abu Sa’iyd: ((Kuoga Siku ya Ijumaa ni wajibu kwa kila aliyebaleghe, apige mswaki na ajitie manukato akipata)). [Hadiyth Swahiyh: Tumeitaja nyuma kidogo].

 

Na kwa ujumla wa neno lake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):  ((Lau si kuchelea uzito juu ya Umma wangu, basi ningeliwaamuru wapige mswaki kila Swalaah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (887) na Muslim (578)].

 

3- Kujipamba kwa nguo maridadi zaidi, na nguo bora zaidi ni nyeupe

 

Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah na Abu Sa’iyd wakisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwenye kuoga Siku ya Ijumaa, akavaa nguo zake zilizo nzuri zaidi, akajitia manukato kama anayo, kisha akaenda Ijumaa, hayo yanakuwa ni kafara kwa yaliyoko kati yake na kati ya Ijumaa ya kabla yake)). [Hadiyth Swahiyh Lighayrihi: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (343), Ahmad (3/81), Al-Haakim (1/283) na Ibn Hibaan (2767)].

 

Na nguo bora zaidi ni nyeupe kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Vaeni katika nguo zilizo nyeupe, kwani hizo ndizo nguo bora zaidi kwenu, na wakafinini kwazo maiti wenu)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (3878), At-Tirmidhiy (994), An-Nasaaiy (8/205), Ibn Maajah (1472) na Ahmad (1/247)].

 

4- Kujiepusha na chenye kukera watu kwa harufu yake

 

Ni kama kula kitunguu maji, kitunguu saumu na mfano wake au kuvuta sigara. Haya tushayaeleza katika mlango wa Swalaah ya Jamaa.

 

Wanayotakiwa Kuyafanya Maamuma Kabla Ya Khutbah

 

1,2- Kwenda mapema Msikitini na kujiweka karibu na imamu

 

Imepokelewa na Abu Hurayrah aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Inapokuwa Siku ya Ijumaa, kunakuwa na Malaika katika kila mlango wa Msikiti wakisajili wa mwanzo na anayefuatia. Imamu anapokaa, hukunja madaftari yao na huja kusikiliza khutbah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (3211) na Muslim (850)].

 

Pia Abu Hurayrah kapokea akisema kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwenye kuoga Siku ya Ijumaa josho la janaba kisha akaenda, basi ni kama ametoa swadaqah ngamia. Na mwenye kwenda katika saa ya pili, basi ni kama ametoa swadaqah ng’ombe. Na mwenye kwenda saa ya tatu, basi ni kama ametoa swadaqah kondoo mwenye pembe. Na mwenye kwenda saa ya nne, basi ni kama ametoa swadaqah kuku. Na mwenye kwenda saa ya tano, basi ni kama ametoa swadaqah yai. Na imamu anapotoka, Malaika huhudhuria kusikiliza khutbah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (881) na Muslim (850)].

 

Na imepokelewa na Samurah bin Jun-dub ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hudhurieni khutbah, na mkurubieni imamu, kwani hakika mtu ataendelea kujiweka mbali mpaka awekwe nyuma peponi hata kama ataingia)). [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1108) na Ahmad (5/10)].

 

3- Kwenda kwa miguu bila kutumia kipando isipokuwa kama atalazimika

 

Imepokelewa toka kwa Aws bin Aws ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwenye kuoga Siku ya Ijumaa na akasafisha kichwa chake, akatoka mwanzo wa wakati na akawahi mwanzo wa khutbah, na akatembea kwa miguu asipande kipando, na akawa karibu na imamu, na akasikiliza na kunyamaza, basi anapata kwa kila hatua amali ya mwaka; Swawm yake na Swalaah yake)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (496), An-Nasaaiy (3/95), Abu Daawuud (345), na Ibn Maajah (1087)].

 

Imepokelewa toka kwa ‘Ubaabah bin Rifaa-’at akisema: “ Abu ‘Absi alinikuta nikienda Ijumaa akaniambia: “Nimemsikia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Mtu ambaye miguu yake itachafuka kwa vumbi katika Njia ya Allaah, basi Allaah Humharamishia moto)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (907)].

 

4- Kuswali Swalaah ya Maamkizi ya Msikiti kabla ya kukaa

 

Imepokelewa toka kwa Jaabir akisema: “Mtu mmoja aliingia Siku ya Ijumaa na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anakhutubu. Rasuli akamuuliza: ((Je, umeswali?)). Akasema: Hapana. Akamwambia: ((Basi swali rakaa mbili)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (930) na Muslim (875)].

 

Na katika tamko jingine: ((Simama uswali rakaa mbili, na uzifupishe)). Hii inamaanisha kwamba ikiwa alikaa bila ya kuswali, basi imesuniwa asimame aziswali – hata kama imamu anakhutubu - na azifupishe. Anaweza kuongeza Sunnah nyinginezo kiasi awezavyo kabla imamu hajapanda mimbari kwa mujibu wa Jamhuri ya Maulamaa. [Sharhu Muslim cha An-Nawawiy (3/385)]. Na hii ni kwa Hadiyth ya Salmaan iliyotajwa mara nyingi nyuma isemayo: ((Kisha akaswali alichoandikiwa, halafu akanyamaza wakati imamu anazungumza, isipokuwa hughufiriwa yaliyo kati yake na Ijumaa nyingine)). [Hadiyth Swahiyh: “Takhriyj” yake ishaelezwa].

 

· Faida:

 

Ijumaa haina Sunnah ya Qabliyyah

 

Adhana inapomalizika, haijuzu kabisa watu kusimama ili kuswali Qabliyyah. [Isipokuwa kama atakuja baada ya kumalizika adhana. Hapo anaweza kuswali Maamkizi ya Msikiti, kisha akae, au kama alisahau kama ilivyotangulia].

 

Hii ndio kauli sahihi zaidi ya Maulamaa. Imesemwa na Hanafiy, Maalik, Ash-Shaafi’iy na wafuasi wake wengi - kinyume na An-Nawawiy na wengineo -. Ni mashuhuri kwa Ahmad. [Al-Fataawaa Al-Kubraa cha Sheikh wa Uislamu (2/351), Zaad Al-Maad (1/433) na Twarhu At-Tathriyb (3/41)].

 

Na hili linathibitishwa na Sunnah, kwani Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anatoka nyumbani kwake, na anapopanda mimbari, Bilaal alikuwa anaanza moja kwa moja kuadhini adhana ya Ijumaa. Anapomaliza, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaanza kukhutubu bila mapumziko. Na hili lilikuwa linashuhudiwa na wote. Hivyo basi, ni wakati gani walikuwa wanaswali Sunnah? Na yeyote anayedhani kwamba walikuwa wote wanasimama kuswali rakaa mbili baada ya Bilaal kumaliza adhana, basi huyo upeo wake wa Sunnah ni mfinyu mno.

 

Linalotilia nguvu haya, ni Hadiyth ya Ibn ‘Umar asemaye: “Niliswali pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) rakaa mbili kabla ya Adhuhuri, na rakaa mbili baada ya Adhuhuri, na rakaa mbili baada ya Magharibi, na rakaa mbili baada ya ‘Ishaa, na rakaa mbili baada ya Ijumaa”. [Hadiyth Swahiyh: “Ishaelezwa kwenye mlango wa Sunnah za Rawaatib].

 

Hii ni matni inayojieleza wazi kwamba Ijumaa kwa Maswahaba, imejitenga kando peke yake mbali na Adhuhuri. Na kwa vile hakuitaja Sunnah ila baada yake, imebainika kwamba haina Sunnah ya kabla yake. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

5- Kutokukusanyika kwa ajili ya darsa kabla ya Ijumaa

 

Ni kwa Hadiyth ya ‘Amri bin Shu’ayb toka kwa baba yake toka kwa babu yake ya kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kununua au kuuza Msikitini, kunadiwa kilichopotea, na kuimbwa mashairi. Na amekataza kukusanyika kwa darsa mfano wa Swalaah Siku ya Ijumaa. [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1079) na wengineo].

 

Kukusanyika huku kunaweza kuwa kwa kukaa kwenye halaqah (mduara) au kukusanyika kwa aina yoyote kwa ajili ya darsa. Na hayo yote yanaingia ndani ya katazo lililopo kwenye Hadiyth. [Angalia Allam-’atu fiy Hukmi Al Ijtimaa liddarsi Qabla Al Jum’at Cha Muhammad Muusa Nasr].

 

Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

 

Share