051-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Khutbah Ya Ijumaa Na Hukmu Zinazomkhusu Khatibu

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

051-Khutbah Ya Ijumaa Na Hukmu Zinazomkhusu Khatibu

 

Alhidaaya.com

 

 

· Hukmu Yake

 

Jamhuri ya Maulamaa wanasema kwamba khutbah ya Ijumaa ni sharti ya kuswihi Ijumaa. [Al-Badaai-’i (1/262), Ibn ‘Aabidiyn (1/567) na Al-Mughniy (2/74)].

 

Dalili zao ni hizi zifuatazo:

 

1- Ni Neno Lake Ta’alaa:

(( يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نُودِيَ لِلصَّلَاةِ مِن يَوْمِ الْجُمُعَةِ فَاسْعَوْا إِلَىٰ ذِكْرِ اللَّـهِ وَذَرُوا الْبَيْعَ ۚ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ))

(( Enyi walioamini! Inaponadiwa kwa ajili ya Swalaah siku ya Ijumaa, kimbilieni kumdhukuru Allaah na acheni kuuza na kununua. Hivyo ni kheri kwenu mkiwa mnajua)). [Al-Jum-‘ah (62:9)]

 

Na “Dhikr” katika Aayah ni khutbah kwa mambo mawili:

 

(a) Ni kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( فإذا خرج الامام حضرت الملائكة يستمعون الذكر))

((Na imamu anapotoka, Malaika huhudhuria wakasikiliza khutba)). [Hadiyth Swahiyh: Al-Bukhaariy kasema ni “Mu’allaq” (2697) na Muslim (1718) na wengineo wamesema ni “Mawsuwl”].

 

Khutbah imeitwa dhikr. Na juu ya hilo, ikiwa kwenda kwa ajili ya khutbah ni lazima, nayo ni njia, basi khutbah inakuwa ni lazima, nayo ndio lengo.

 

(b) Ni kwamba Allaah Mtukufu Ameamuru kwenda kwenye khutbah tokea pale inapoadhiniwa. Na kwa “Tawaatur” isiyo na shaka, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anakhutubu mara tu baada ya adhana. Na kwa hilo, imejulikana kwamba kwenda kwenye khutbah ni wajibu.

 

2- Ni kudumu Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoa khutbah kila Ijumaa, na kamwe hakuwahi kuswali bila khutbah.

 

3- Kuharamishwa kuzungumza wakati wa khutbah na wajibu wa kuisikiliza khutbah.

 

Ikiulizwa: Dalili hizi hazionyeshi juu ya shurutisho?! Itajibiwa: Swalaah hii imekuwa ni wajibu kwa sifa hii ambayo Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliendelea nayo. Kwa hiyo, mwenye kukusuru kinyume na ilivyokuwa ikifanyika, basi anakuwa hakufanya lililo wajibu juu yake, na hili li wazi katika shurutisho. Na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwenye kufanya amali yoyote isiyohusiana na amri yetu, basi ni batili)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (862), Abu Daawuud (1093), An-Nasaaiy (3/109, 110), At-Tirmidhiy (507) na Ahmad (5/87)].

 

Hili linaonyesha kwamba kama hakukhutubu, ataswali rakaa nne, na Ijumaa si rakaa nne, hivyo inakuwa ni Adhuhuri.

 

· Ni Lazima Akhutubu Khutbah Mbili Kwa Kusimama, Na Akae Kidogo Kati Yake Ila Kama Ana Udhuru

 

Hii ndio kauli ya Jamhuri kinyume na Hanafi. Wajibu wa hili uko wazi –kama ilivyotangulia- kutokana na kudumu kwa kitendo chenye kubainisha sifa ya Swalaah hii ya wajibu, mbali na kutonukuliwa kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitosheka na khutbah moja, na kwamba alikhutubu akiwa amekaa. Imepokelewa toka kwa Jaabir bin Samurah: “Kwamba Rasuli wa Allaah alikuwa anakhutubu kwa kusimama, kisha anakaa, halafu anasimama na kukhutubu. Basi yeyote atakayekueleza kwamba alikuwa anakhutubu kwa kukaa, basi huyo ameongopa. Hakika – Wallaah – niliswali pamoja naye zaidi ya Swalaah elfu mbili”.

 

Katika riwaya nyingine: “Sikumwona ila amesimama”.

 

Imepokelewa toka kwa Ka’ab bin ‘Ajrah kwamba yeye: “Aliingia Msikitini – huku ‘Abdullaah bin Al-Hakam anakhutubu kwa kukaa – akasema: Mwangalieni khabithi huyu anakhutubu kwa kukaa nailhali Allaah Anasema:

وَإِذَا رَأَوْا تِجَارَةً أَوْ لَهْوًا انفَضُّوا إِلَيْهَا وَتَرَكُوكَ قَائِمًا ۚ”

 [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (864), An-Nasaaiy (3/102) na Ibn Abu Shaybah].

 

· Kiasi Kitoshelezacho Khutbah

 

Maulamaa wamekhitalifiana kuhusu kiasi kitoshelezacho khutba. Kiuhakiki ni kusemwa: [Ar-Rawdhwat An-Naddiyyat uk. 137].

 

“Kisha jua kwamba khutbah ya kisharia, ni ile aliyokuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameizoea ya kuwatia watu utashi na kuwatia khofu. Hii kiuhalisia, ndio kiini cha khutbah ambacho kwa ajili yake khutbah imewekwa. Ama kuweka sharti ya kumhimidi Allaah, au kumswalia Rasuli wa Allaah, au kusoma kitu katika Qur-aan, haya yote yako nje ya kusudio kuu la uwepo wa khutbah. Na kukubaliwa mfano wa hayo katika khutbah yake Rasuli, hakuonyeshi kwamba ndio makusudio ya wajibu na sharti la lazima. Na yeyote aliye mwadilifu, atakuwa hana shaka yoyote kwamba kusudio kuu ni mawaidha bila ya yale yanayotokea kabla yake kati ya himdi kwa Allaah na Swalaah kwa Rasuli. Ilikuwa ni katika ada endelevu ya Waarabu kwamba mmoja wao anapotaka kusimama mbele ya hadhira na kusema neno, huanza neno lake kwa kumsifu Allaah na Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ni uzuri na ubora ulioje wa hili!! Lakini, hilo sio kusudio bali kusudio ni yale yanayofuatia. Na bila shaka, yeyote mwenye umbile salama, atapinga na kukataa ikiwa mtu atasimama mbele ya baraza kwa ajili ya kulihutubia, na hotuba yake isiwe na kingine chochote zaidi ya kumhimidi Allaah na kumswalia Rasuli tu.

 

Na tukikubaliana na haya, basi tunajua kwamba mawaidha kwenye khutbah ya Ijumaa ndio dhamira kuu ya mazungumzo, na khatibu akilifanya, anakuwa amefanya jambo la kisharia. Na ikiwa atatanguliza sifa kwa Allaah na kwa Rasuli Wake, au akaingiza ndani ya khutbah yake qaraa za Qur-aan, basi inakuwa ni utimilifu na uzuri zaidi”.

 

Ninasema: “Ni Sunnah kama itakavyokuja mbele”.

 

· Yaliyosuniwa Kwenye Khutbah

 

1- Kuianza kwa kumhimidi Allaah na kumsifu, na kumswalia Rasuli Wake na  kutashahudia

 

Imepokelewa toka kwa Jaabir akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimhimidi Allaah na kumsifu katika khutbah ya Siku ya Ijumaa [kwa Sifa Anazostahiki, kisha anasema: Man Yahdihi Allaahu falaa mudhwilla lahu, waman Yudhwlil falaa haadiya lahu, wakhayrul hadiyth, Kitaabu Allaah]. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (867)].

 

Na katika Hadiyth ya Abu Humayd As Saa’idiy: “Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisimama jioni baada ya Swalaah, akatashahudia, na akamsifu Allaah kwa Sifa Anazostahiki kisha akasema: Ammaa ba’adu”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (926)].

 

Imesuniwa aanze kwa khutbah ya haja. Imepokelewa toka kwa Ibn Mas-’oud akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha katika khutbah ya haja tuseme: “Alhamdu li-Laahi nahmaduhu wa nasta’iynuhu wa nastaghfiruhu, wa na’uwdhu bil Laahi min shuruwri anfusinaa wa sayyiaati a-’amaalinaa. Man Yahdihi Allaahu falaa mudhwilla lahu, waman Yudhwlil falaa Haadiya lahu. Wa ash-hadu an laa ilaaha illa Allaahu wahdahu laa shariyka Lahu, wa ash-hadu anna Muhammadan ‘Abduhu wa Rasuuluhu. [Kisha akasoma Aayah tatu]:

(( يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ حَقَّ تُقَاتِهِ وَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ))  

(( يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ وَخَلَقَ مِنْهَا زَوْجَهَا وَبَثَّ مِنْهُمَا رِجَالًا كَثِيرًا وَنِسَاءً ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ الَّذِي تَسَاءَلُونَ بِهِ وَالْأَرْحَامَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَيْكُمْ رَقِيبًا))

(( يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَقُولُوا قَوْلًا سَدِيدًا يُصْلِحْ لَكُمْ أَعْمَالَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗوَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ فَازَ فَوْزًا عَظِيمًا)) 

[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (2118), At-Tirmidhiy (1105), An-Nasaaiy (6/89) na Ibn Maajah (1892)].

 

Imepokelewa toka kwa Jaabir akisema: “

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapokhutubu, macho yake huwa mekundu, sauti yake huwa juu, na ghadhabu zake hushitadi kana kwamba anaonya watu na jeshi (la uvamizi) akisema: Litawavamieni asubuhi au jioni. Na anasema: ((Nimetumwa mimi, na Qiyaamah kama viwili hivi)), na hukutanisha baina ya kidole chake cha shahada na cha kati. Na husema: ((Ammaa ba’adu. Hakika Maneno yaliyo bora kabisa ni Kitabu cha Allaah, na Uongofu ulio bora kabisa ni Uongofu wa Muhammad, na shari ya mambo ni yale yenye kuzushwa, na kila chenye kuzushwa ni bid-’a, na kila upotevu ni motoni..)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (867), An-Nasaaiy (3/188), Ibn Maajah (45) na Ahmad (3/319)].

 

Na imepokelewa kwa njia sahihi kwamba ‘Umar bin Al-Khattwaab na Ibn Mas-’oud (Radhwiya Allaahu Anhumaa), walikuwa wakifungulia kwa maneno haya khutbah ya Ijumaa na khutbah nyinginezo.

 

2- Kuipa khutbah uzito na kunyanyua sauti

 

Ni kama ilivyotangulia kwenye Hadiyth ya Jaabir isemayo: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapokhutubu, macho yake huwa mekundu, sauti yake huwa juu, na ghadhabu zake hushitadi kana kwamba anaonya watu kuwa watavamiwa na jeshi akisema: Litawavamieni asubuhi au jioni”.

 

3- Kuifupisha khutbah na kuirefusha Swalaah

 

Imepokelewa toka kwa ‘Ammaar bin Yaasir akisema: “Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Hakika mtu kurefusha Swalaah na kufupisha khutbah yake, ni alama ya weledi wake. Basi irefusheni Swalaah hii, na fupisheni khutbah hizi, kwani baadhi ya maneno ni kama uchawi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (869), Ahmad (4/263), Ad-daaramiy (1556) na wengineo].

 

Na imepokelewa toka kwa Jaabir bin Samrah akisema: “Niliswali pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Swalaah yake ilikuwa ni ya wastani, na khutbah yake ni ya wastani”.

 

Na katika riwaya: “Harefushi mawaidha Siku ya Ijumaa, bali yanakuwa ni maneno machache”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (866), Abu Daawuud (1107) na riwaya nyingine ni yake, At-Tirmidhiy (507), An-Nasaaiy (3/110) na Ibn Maajah (1106)].

 

Ninasema: “Kuna faida mbili katika kufupisha khutbah: Kwanza hakumchoshi msikilizaji, na pili kunamfanya aielewe vyema na kuifahamu vizuri zaidi. Lakini weledi na umahiri wa khatibu, unaweza kuifanya kuwa ndefu kwa mujibu wa suala linalozungumziwa. Imethibiti kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anakhutubu kwa kusoma Suwrat “Qaaf” na “Tabaaraka”, na hii ni pamoja na kuzisoma kwa tartiyl na kusimama kwenye kila Aayah. Hili bila shaka lilikuwa likiirefusha khutbah. Makusudio kiujumla, ni kuchunga hali ya watu na haja yao. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.

 

 4- Kusoma Aayah za Qur-aan ndani ya khutbah

 

(a) Imepokelewa toka kwa Jaabir bin Samurah akisema: “ Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikaa baina ya khutbah mbili, na huwakumbusha watu, na husoma Aayah za Qur-aan”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (862) na Abu Daawuud (1094)].

 

(b) Imepokelewa toka kwa Swafwaan bin Ya’alaa toka kwa baba yake: “Kwamba yeye alimsikia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasoma juu ya mimbari "ونادوا يا مالك". [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (3266) na Muslim (871)].

 

(c) Imepokelewa toka kwa Ummu Hishaam akisema: “Sikuihifadhi Suwrat Qaaf isipokuwa toka kwenye kinywa cha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akikhutubu kwayo kila Ijumaa”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (872) na Ahmad (6/463)].

 

5- Kuteremka toka juu ya mimbari anaposoma Aayah ya sijdah

 

Hili limethibiti toka kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab, Abu Muusa Al-Ash-’ariy na ‘Ammaar bin Yaasir. Haya yashaelezwa kwenye mlango wa sijdah ya kisomo.

 

6- Kuwaombea du’aa Waislamu ndani ya khutbah

 

Inasimuliwa toka kwa Samrah: “Kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiwaombea maghfirah Waumini katika kila Ijumaa”. Lakini ni Dhwa’iyf mno, haifai kwa dalili ingawa Maulamaa wanaitumia. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bazzaar katika Al-Majma’a (2/190), na katika Sanad yake, kuna mtu ameachwa].

 

Pamoja na hayo, kuna faida ya kupendeza kuomba du’aa katika khutbah kutokana na Hadiyth ya ‘Ammaarah bin Ra-ayat: “ Ya kwamba yeye alimwona Bishr bin Marwaan juu ya mimbari akinyanyua mikono yake (akiomba) akasema: Allaah Ainyime mikono hii miwili kheri zote. Hakika nilimwona Rasuli wa Allaah haongezi zaidi ya kufanya hivi, na akaashiria kwa kidole chake cha shahada”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (874), An-Nasaaiy (3/108), Abu Daawuud (1104), At-Tirmidhiy (515) na Ibn Maajah (1103)].

 

Katika hili, kuna faida mbili:

 

1- Kuthibitisha kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiomba katika khutbah yake.

 

2- Ukaraha wa imamu kunyayua mikono yake anapoomba juu ya mimbari, na kwamba Sunnah ni kuashiria kwa kidole chake cha shahada. Na hili linatiliwa nguvu na Hadiyth ya Sahl bin Sa’ad aliyesema: “ Sikumwona kamwe Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akinyoosha mikono yake wakati anaomba juu ya mimbari yake wala juu ya mimbari nyingine yoyote, lakini nilimwona akifanya hivi, na akaashiria kidole chake cha shahada, na akakifunga cha kati na gumba”. [Hadiyth Hasan kwa iliyoitangulia: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1105) kwa Sanad laini. Hadiyth iliyotangulia, inaitolea ushuhuda].

 

Na hii ni moja ya mielekeo miwili kwa Hanbali, nao umekhitariwa na Sheikh wa Uislamu. [Al-Ikhtiyaaraat uk. 80].

 

· Zindusho:

 

Kuomba du’aa katika Swalaah ya kuomba mvua, kunatolewa nje ya tuliyoyaeleza, kwani lililothibiti katika Swalaah hiyo ni kunyanyua mikono miwili kama ilivyotangulia katika mlango husika. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

· Mambo Anayoruhusiwa Kuyafanya Khatibu Wakati Wa Khutbah

 

1- Kuegemea fimbo au mfano wake

 

Katika Hadiyth ya Al-Hakam bin Hazan Al-Kalfiyy – katika kisa cha kwenda kwake kwa Rasuli akiwa na wajumbe: “ Tukakaa hapo masiku kadhaa ambapo tulihudhuria Ijumaa pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Akasimama akiegemea fimbo au upinde, akamhimidi Allaah na akamsifu”.  [Hadiyth Swahiyh kwa Hadiyth wenza: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1096), Ahmad (4/212), Abu Ya’alaa (12/204) na Ibn Khuzaymah (1452). Ina Hadiyth wenza].

 

Na katika Hadiyth ya Fatmah bint Qays –kuhusu kisa cha Al-Jassaasah (mnyama mwenye nywele nyingi mwili mzima)..Rasuli wa Allaah akasema: –na akagonga kwa fimbo yake kwenye mimbari– ((Hii ni Twaybah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (2942), Abu Daawuud (4326), At-Tirmidhiy (2253) na Ibn Maajah (4074)].

 

2- Kuzungumza na yeyote amtakaye katika hadhira kwa haja

 

Ni kama kumwamuru aliyeingia aswali rakaa mbili za maamkizi ya Msikiti, au kumwamuru mwenye kuziruka shingo za watu akae, au kumuuliza mtu jambo fulani, au kumjibu anayemuuliza, au kumwamuru mtu aingie na mfano wa hayo.

Hayo yote yamethibiti toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Baadhi yake yashaelezwa nyuma na mengineyo yako njiani.

 

3- Kuwahimiza watu watoe swadaqah kwa masikini wakimwona

 

Imepokelewa toka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriyy akisema: “Alikuja mtu mmoja Siku ya Ijumaa akiwa katika hali mbaya sana (wakati Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anakhutubu). Rasuli wa Allaah akamuuliza: ((Umeswali?)). Akasema: Hapana. Akamwambia: ((Swali rakaa mbili)), na akawahimiza watu kumtolea swadaqah. Wakazikusanya chini nguo zao, na Rasuli akampa nguo mbili kati ya zilizokusanywa”. [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (3/106)].

 

Tanbihi:

 

Kutoa swadaqah kwa masikini wakati wa khutbah, kunaweza kufanyika ikiwa khatibu amenyamaza. Ama desturi iliyozagaa kwenye Misikiti ya kupita mhudumu wa Msikiti na kapu au sanduku kwa Waumini kwa ajili ya kukusanya swadaqah – huku imamu anakhutubu -, hakuna shaka ya kwamba jambo hilo si la kisharia kutokana na ujumuishi wa Hadiyth zenye kuamuru kuisikiliza khutbah, zenye kuharamisha kuzungumza au kufanya vitendo visivyo na maana wakati wa khutbah kama tutakavyokuja kuzungumza.

 

4- Kuikata khutbah ili kulishughulikia jambo lililomtokea kisha arudi kwenye khutbah

 

Kuna Hadiyth nyingi zinazohusiana na hili. Kati ya Hadiyth hizo ni Hadiyth ya Jaabir bin ‘Abdullah –kuhusu kisa cha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuanza kuitumia mimbari baada ya kuwa akikhutubu juu ya kigogo cha mtende- : “Ilipokuwa Siku ya Ijumaa, alisogea juu ya mimbari. Kigogo cha mtende kikapiga ukelele, kama anavyolia mtoto mdogo. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akateremka, akakikumbatia, nacho kinalia kilio cha kunung’unika cha mtoto anayebembelezwa. Kilikuwa kinalia kutokana na khutbah kilichokuwa kikiisikia”.  [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (3584)].

 

Na Hadiyth ya Abu Rifa’at aliyesema: “Nilifika kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa anakhutubu nikasema: “Ee Rasuli wa Allaah! Kuna mtu mgeni amekuja anaulizia kuhusu dini yake, haijua dini yake ni ipi. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akanigeukia, akaacha kukhutubu, akanijia, na akaleta kiti ambacho nadhani miguu yake ni ya chuma. Akakaa na akaanza kunifundisha aliyofundishwa na Allaah. Kisha akarudi kwenye khutbah yake akaikamilisha hadi mwisho wake”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (876) na An-Nasaaiy (8/220)].

 

5- Kutenganisha baina ya khutbah na Swalaah ili kulishughulikia jambo lililomtokezea

 

Imepokelewa toka kwa Anas akisema: “ Hakika nilimwona mtu akimzungumzisha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa amesimama baina yake na Qiblah baada ya kuqimiwa Swalaah. Aliendelea kuzungumza naye, na hakika niliwaona baadhi yetu wakisinzia kutokana na muda mrefu wa kusimama Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na mtu huyo”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (643) na Muslim (376)].

 

 

Share