054-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Swalaah Ya ‘Iyd Mbili

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

054-Swalaah Ya ‘Iyd Mbili

 

 

· Hikma Ya Kuwekwa ‘Iyd Mbili

 

Ni kwamba kila watu wana siku yao maalumu ambapo hujipamba na kutoka majumbani mwao wakiwa na mapambo yao. [Hujjat Allaah Al-Baalighah cha Ad-Dahlawiy (2/23)].

 

Imepokelewa toka kwa Anas (Radhwiya Allaahu Anhu) akisema: “ Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuja, na watu wa Madiynah wana siku mbili wanazozisherehekea katika ujahilia, naye akasema: ((Nimewajieni, nanyi mna siku mbili mnazozisherehekea katika ujahilia. Na hakika Allaah Amewabadilishieni kwa siku nyingine bora zaidi kuliko hizo: Siku ya Kuchinja, na Siku ya Fitwri)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1134), An-Nasaaiy (3/179), Ahmad (3/103), Al-Baghawiy (1098) na wengineo].

 

“Yaani, kwa kuwa siku za Fitwr na kuchinja zimewekwa na Allaah Mtukufu, na ndizo Alizozichagua kwa Waja Wake, na kwa kuwa huja baada ya kutekeleza nguzo mbili adhimu kati ya nguzo za Uislamu ambazo ni Hijjah na Swiyaam. Na ndani ya nguzo hizi mbili, Allaah Huwaghufiria mahujaji na wafungaji, na Hueneza Rahma Zake kwa Viumbe Wake wote watiifu.

 

Ama siku za Nayrouz na Marjani, siku hizi zilichaguliwa na watawala wa enzi hizo kutokana na uwastani wa majira ya wakati na hali ya hewa, au kwa faida nyinginezo za mpito. Bila shaka tofauti iko wazi kati ya faida mbili kwa mwenye kulitaamuli hilo”. [Al Fat-hu Ar Rabbaaniy bitartiyb Musnadi Ahmad cha Al-Bannaa (6/119)].

 

· Hukmu Ya Swalaah Ya ‘Iyd Mbili

 

Maulamaa wamekhitalifiana kuhusu hukmu ya Swalaah ya ‘Iyd Mbili katika kauli tatu:

 

Ya kwanza:

 

Ni wajibu kwa kila mtu binafsi (Fardhu ‘Ayn)

 

Ni kauli ya Abu Haniyfah, moja ya kauli za Ash-Shaafi’iy, na riwaya toka kwa Ahmad. Pia ni kauli ya baadhi ya wafuasi wa Maalik, na ni chaguo la Sheikh wa Uislamu. [Al-Badaai-’i (1/273), Ibn ‘Aabidiyn (2/166), Ad-Dusuwqiy (1/396), Al-Inswaaf (2/240), Majmu’u Al-Fataawaa (23/161) na As-Subul Al-Jarraar (1/315)].

 

Dalili zao ni:

 

1- Kauli Yake Ta’alaa:

((فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ))

((Basi swali kwa ajili ya Rabb wako na chinja kwa ajili Yake)). [Al-Kawthar (108:2)]

 

Agizo hapa ni la wajibu.

 

2- Kauli Yake Ta’alaa:

((شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ ۖوَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۗ يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ وَلِتُكْمِلُوا الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُوا اللَّـهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ))

((Mwezi wa Ramadhwaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na Furqaan (upambanuo). Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi na afunge. Na atakayekuwa mgonjwa au safarini basi atimize idadi katika siku nyinginezo. Allaah Anakutakieni mepesi na wala Hakutakieni magumu; na ili mkamilishe idadi na ili mumkabbir Allaah kwa kuwa Amekuongozeni na ili mpate kushukuru)). [Al-Baqarah (2:185)].

 

Agizo la kupiga takbiyr katika ‘Iyd Mbili ni agizo la Swalaah yenye kukusanya takbiyr iliyozoeleka, na takbiyr za ziada kwenye rakaa ya kwanza na ya pili.

 

3- Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwajibika na Swalaah hii katika ‘Iyd Mbili, na hakuiacha katika ‘Iyd yoyote ile, na Makhalifa wake na Waislamu waliendelea na Swalaah hii baada yake.

 

4- Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaamuru watu kutoka kwa ajili ya Swalaah hii hata wanawake, wanawali  na wenye hedhi. (Wenye hedhi aliwaamuru wakae kando na sehemu ya kuswalia). Hata pia alimwamuru asiye na abaya aazime kwa mwenzake. Haya yatakuja kuzungumziwa.

 

5- Swalaah hii ni moja kati ya utambulisho adhimu na bayana wa Uislamu, hivyo imekuwa ni wajibu kama Swalaah ya Ijumaa. Na kwa ajili hiyo, ni lazima kuwapiga vita wenye kukataa katakata kuiswali.

 

6- Swalaah hii inaipomosha Swalaah ya Ijumaa ikiwa zitawafikiana katika siku moja kama ilivyotangulia. Na kisicho wajibu hakiwezi kukipomosha kilicho wajibu.

 

Ya pili:

 

Ni wajibu kwa kutoshelezana (Fardhu Kifaayah)

 

Ikiwa baadhi wataiswali, basi itawapomokea waliobaki. Ni kauli ya Hanbali na baadhi ya Mashaafi’i. [Al-Mughniy (2/304), Kash-Shaaful Qina’a (2/50) na Al-Majmu’u (5/2). An-Nawawiy amedai kwamba kuna Ijma’a ya Maulamaa wote kwamba Swalaah hii si Fardhi ‘Ayn (kila mtu binafsi), lakini hayo yamevunjwa nguvu katika yaliyozungumzwa nyuma].

 

Hoja zao ni dalili zile zile zilizotolewa na kundi la kauli ya kwanza lakini wamesema: “Si lazima kwa kila mtu binafsi kwa kuwa Swalaah haijawekewa adhana. Si wajibu kwa mtu binafsi sawa na Swalaah ya Janazah, na kama ingelikuwa hivyo, basi ingelazimu mtu aisikilize khutbah yake kama khutbah ya Ijumaa.

 

Ya tatu:

 

Ni Sunnah iliyokokotezwa lakini si wajibu. Ni kauli ya Maalik, Ash-Shaafi’iy na wafuasi wao wengi. [Ad-Dusuwqiy (1/396), Jawaahirul Ikliyl (1/101), na Al-Majmu’u (5/2)].

 

Hoja yao ni:

 

1- Neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumwambia bedui wakati alipomtajia Swalaah tano akasema: “Je, kuna jingine zaidi ya hilo juu yangu?” Akasema: ((Hapana, ila ukilifanya la Sunnah)), na mengine yaliyo ndani ya maana hii. [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa nyuma mara nyingi].

 

2- Swalaah hii ni Swalaah yenye rukuu na sijdah na haikuwekewa adhana!! Hivyo si wajibu kisharia kama ilivyo Swalaah ya Dhuhaa.

 

· Kauli Yenye Nguvu

 

Ni kauli ya kwanza kutokana na dalili zake zilizotajwa. Ama kusema kwamba ni Sunnah iliyokokotezwa, kauli hii ni dhaifu. Ama swali la bedui kwa Rasuli, hilo halina hoja, kwa kuwa Rasuli kazitaja Swalaah tano kimahususi ili kuzisisitizia, kuonyesha ulazima wake wa kudumu, na kukariri kwake usiku na mchana. Ama nyinginezo, uwajibu wake ni wa nadra kama Swalaah ya maiti, nadhiri na kadhalika.

 

Ama kusema kwamba Swalaah hii ni Fardhi ya Kutoshelezana, usemi huu haukai sawa. Kisha katika kutoshelezana, hupatikana ndani yake maslaha ya mtu binafsi kwa kufanya wengine kama kuzika maiti, au kupambana na adui. Lakini katika siku ya ‘Iyd, hakuna maslaha maalumu ambayo baadhi ya watu huyafanya wengine wakafaidika, bali Swalaah ya ‘Iyd imetangaziwa mkusanyiko mkubwa zaidi kuliko wa Swalaah ya Ijumaa pale ambapo hata wanawake wameamuriwa kwenda kuihudhuria, lakini hawakuamuriwa kuhudhuria Swalaah ya Ijumaa ingawa ruksa ipo. Rasuli kasema: ((Kuswali majumbani mwenu ni bora zaidi kwenu)). Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

· Wakati Wa Swalaah Ya ‘Iyd Mbili

 

Wakati wa Swalaah ya ‘Iyd huanza baada ya kunyanyuka jua kiasi cha urefu wa mkuki (yaani baada ya kupita wakati wa ukaraha), na humalizika kwa kupinduka jua. Haya ndiyo waliyoyasema Jamhuri (Hanafi, Maalik na Hanbali). [Ibn ‘Aabidyna (1/583), Ad-Dusuuqiy (1/396) na Kash-Shaaful Qina’a (2/50). Ash-Shaafi’iy kajuzisha Swalaah mwanzo wa jua kuchomoza].Imepokelewa toka kwa ‘Abdullah bin Bisr –Swahiba wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) – ya kwamba alitoka pamoja na watu siku ya ‘Iyd el Fitwr au ‘Iyd el Adhw-haa. Akalalamikia imamu kuchelewesha chelewesha na kusema: “Hakika sisi tulikuwa tumeshamaliza saa yetu hii”. Na hiyo ni wakati wa Swalaah ya Adh-dhuhaa. [Hadiyth Swahiyh: Al-Bukhaariy kaitolea maelezo (2/456) na Abu Daawuud kaiunganisha(1135), Ibn Maajah (1317), Al-Haakim (1/295) na Al-Bayhaqiy (3/282)].

 

· Faida

 

Ni bora Swalaah ya ‘Iyd el Adh-haa iswaliwe mwanzoni mwa wakati ili watu wapate nafasi nzuri ya kwenda kuchinja baada ya Swalaah. Ama Swalaah ya ‘Iyd el Fitwr, imesuniwa kuichelewesha kidogo na wakati huu ili watu wawahi kutoa zakaatul fitwr. [Vitabu mama vya fiqh vilivyotangulia].

 

· Hukmu Yake Ikiwa Wakati Wake Umepita

 

Kuna picha tatu za kupita wakati wa Swalaah ya ‘Iyd:  [Al-Badaai-’i (1/276), Ad-Dusuuqiy (1/396-400), Bidaayatul Mujtahid (1/321), Al-Majmu’u (5/27), Al-Mughniy (2/324) na Majma’ul Anhur (1/169)].

 

Ya kwanza:

 

Watu wasijue kwamba ni ‘Iyd ila baada ya kupinduka jua

 

Huu ni udhuru wenye kujuzisha kuichelewesha hadi siku ya pili sawasawa ikiwa ni ‘Iyd el Fitwr au ‘Iyd el Adh-haa. Hili ndilo walilolisema Jamhuri kutokana na Hadiyth ya Abu ‘Umayr bin Anas toka kwa wenzake wengi kati ya Maswahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambao wanashuhudia: “Kwamba wao waliuona mwezi jana, akawaamuru wafungue, na wakipambaukiwa waende kwenye kiwanja chao cha kuswalia”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1157), An-Nasaaiy (3/180) na Ibn Maajah (1653)].

 

Ya pili:

 

Waicheleweshe (wote) Swalaah ya ‘Iyd na wakati wake bila ya udhuru uliotangulia

 

Ikiwa ni ‘Iyd el Fitwr, basi kimsingi itakuwa ishapomoka na haitalipwa. Ama ikiwa ni ‘Iyd el Adh-haa, basi itajuzu kuiakhirisha mpaka siku ya tatu ya kuchinja, kwa maana kwamba itajuzu kuilipa siku ya pili au siku ya tatu kuanzia jua linapopanda mpaka mwanzo wa kupinduka, sawasawa ikiwa kuichelewesha kulikuwa ni kwa udhuru au bila udhuru. Lakini watu wataandamwa na dhana ya kuwa wamefanya vibaya ikiwa walichelewesha bila udhuru.

 

Ya tatu:

 

Iswaliwe katika wakati wake wa siku ya kwanza lakini ikawapita baadhi ya watu

 

Hanafi na Maalik wanasema kwamba haijuzu kisharia kuilipa kwa kuwa ni Swalaah ambayo imewekewa wakati wake maalum na kwa mipaka maalumu. Ni lazima vikamilike vyote ukiwemo wakati. Lakini Ash-Shaafi’iy amejuzisha kuilipa katika wakati wowote aupendao mtu, na kwa namna yoyote, sawasawa akiswali peke yake au kwa jamaa, kwa mujibu wa qaaidah yake ya kuhalalisha kuilipa Sunnah yoyote.

 

Hanbali naye kasema kwamba ni marufuku kuilipa lakini kaongeza: “Atachaguzwa; akitaka ataiswali rakaa nne, ima kwa tasliym moja au kwa tasliym mbili”.

 

Ninasema: “Kauli hii ya Hanbali ni dhaifu, na msingi wake ni kuifananisha na Ijumaa!!”

 

· Lenye Nguvu

 

Ninaloliona katika picha hizi zote tatu ni kwamba mwenye kupitwa na Swalaah ya ‘Iyd kwa udhuru, basi anaweza kuilipa katika siku ya pili. Na kama si kwa udhuru, basi hatoilipa kwa mujibu wa yaliyoelezwa katika mlango wa kulipa Swalaah zilizompita mtu. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

· Mahala Inaposwaliwa

 

Imepokelewa toka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriy (Radhwiya Allaahu Anhu) akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anatoka siku ya Fitwr na Adh-haa kwenda katika kiwanja cha kusalia, na jambo la kwanza analolianza ni Swalaah”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (956), Muslim (889) na An-Nasaaiy (3/187)].

 

Na Sunnah iendeleayo kwa Swalaah ya ‘Iyd mbili, ni kuwa iwe kwenye “Muswallaa”, yaani kwenye jangwa au kiwanja kipana, kwa kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Swalaah moja katika Msikiti wangu huu ni bora kuliko Swalaah 1000 katika misikiti mingineyo isipokuwa Al-Masjid Al-Haraam)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1190) na Muslim (1394)].

 

Lakini pamoja  na fadhla hii kubwa, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitoka na akauacha”. [Al-Madkhal cha Ibn Al-Hajji (2/283)].

 

Isipokuwa kama kutakuwepo udhuru kama mvua [Kuhusiana na hili, kuna Hadiyth Marfu’u ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali nao msikitini waliponyeshewa na mvua, lakini ni Dhwa’iyf], na mfano wake, au baadhi ya watu kushindwa kutoka kwa sababu ya utu uzima au ugonjwa, hapo itakuwa hapana ubaya kuiswalia msikitini.

 

Inapasa ijulikane kwamba lengo la Swalaah ni kujumuika Waislamu mahala pamoja. Haitakikani viwepo viwanja vingi katika maeneo yaliyokaribiana bila haja kama tunavyoshuhudia katika baadhi ya miji ya Kiislamu. “Bali hata baadhi ya viwanja hivi, vimekuwa ni mimbari za kivyama za kusambaratisha umoja wa Waislamu. Walaa hawla walaa quwwata illaa bi Allaah”. [Ahkaamul ‘Iydayn (uk. 24) cha Sheikh ‘Aliy Hasan ‘Abdul Hamiyd, Allaah Amhifadhi].

 

· Faida: Swalaah ya ‘Iyd Makkah

 

Lililo bora ni kuswalia kwenye Al-Masjid Al-Haraam, kwani viongozi wa dini hawakuacha kuendelea kuswalia ‘Iyd mjini Makkah kwenye Al-Masjid Al-Haraam, na hilo ni bora zaidi kuliko kutoka kwenda kuswalia jangwani. [Al-Majmu’u cha An-Nawawiy (5/524)].

 

· Kutoka Kwenda Uwanja Wa Kuswalia Na Adabu Zake

 

1- Ni Sunnah kuoga kabla ya kutoka

 

Imepokelewa toka kwa Naafi’i kwamba Ibn ‘Umar: “Alikuwa anaoga siku ya Fitwr kabla ya kwenda uwanja wa kuswalia”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Maalik (426), na kutoka kwake Ash-Shaafi’iy (73) na ‘Abdul Razzaaq (5754)].

 

‘Aliy bin Abiy Twaalib aliulizwa kuhusiana na kuoga akasema: “ Ni Siku ya Ijumaa, Siku ya Arafah, Siku ya Kuchinja, na Siku ya Fitwr”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ash-Shaafi’iy (114), na kupitia kwake Al-Bayhaqiy (3/278)].

 

2- Kujipamba na kuvaa nguo nzuri

 

Asili ya kupendelewa hili ni Hadiyth ya Ibn ‘Umar aliyesema: “’Umar alilichukua juba la hariri linalouzwa sokoni, akamwendea Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumwambia: Ee Rasuli wa Allaah! Nunua hili ujipambe nalo kwa ‘Iyd na kwa wageni wanaokuja toka nje”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (886), Muslim (2068) na wengineo].

 

Hadiyth. “Kutokana na Hadiyth hii, imejulikana kwamba kujipamba siku ya ‘Iyd ni ada iliyokuwa imezoeleka kwao, na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakulikemea jambo hilo, na kubakia kwake kumetambulika”. [Haashiyat Assandiy ‘Alaa An-Nasaaiy (3/181)].

 

Na imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Alikuwa anavaa burdah jekundu siku ya ‘Iyd”. [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh: Angalia As-Swahiyha (1279)].

 

3- Kula kabla ya kutoka kwenda uwanja wa kuswalia na hasahasa katika ‘Iyd el Fitwr

 

Anas amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa hatoki siku ya Fitwr mpaka ale tende”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (953), At-Tirmidhiy (543), Ibn Maajah (1754) na Ahmad (3/126)].

 

Na Buraydah kasema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa hatoki siku ya Fitwr mpaka ale, na siku ya kuchinja hali mpaka arudi, na hula sehemu ya mnyama wake aliyemchinja”. [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (542), Ibn Maajah (1756) na Ahmad (5/352)].

 

Hikma ya kula kabla ya kutoka kwenda kuswali ‘Iyd el Fitwr ni ili asidhani mwenye kudhani kwamba haifai kula mpaka amalize kuswali ‘Iyd. Na katika ‘Iyd el Adh-haa, huakhirisha kula ili kifungua kinywa chake kiwe kwa mnyama wake aliyemchinja.  [Al Fat-h (2/447), Al-Mughniy (2/371) na Zaad El Maad (1/441)].

 

4- Kupiga takbiyr katika ‘Iyd zote mbili tokea pale anapoanza kutoka nyumbani

 

Allaah Amesema:

(( يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ وَلِتُكْمِلُوا الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُوا اللَّـهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ))

((Allaah Anakutakieni mepesi na wala Hakutakieni magumu; na ili mkamilishe idadi na ili mumkabbir Allaah kwa kuwa Amekuongozeni na ili mpate kushukuru)). [Al-Baqarah (2:185)]

 

Na imetaarifiwa juu ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba yeye: “Alikuwa anatoka siku ya ‘Iyd el Fitwr, na hupiga takbiyr mpaka anapofika uwanja wa kuswalia, na mpaka amalize Swalaah, na anapomaliza Swalaah, huikata takbiyr”. [Mursal, na ina Hadiyth wenza: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abiy Shaybah (1/487). Angalia Asw-Swahiyhah (170)].

 

Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar: “Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anatoka kwenda ‘Iyd mbili pamoja na Al-Fadwl bin ‘Abbaas, ‘Abdullah, Al-‘Abbaas, ‘Aliy, Ja’afar, Al-Hasan, Al-Husayn, Usaamah bin Zayd, Zayd bin Haarithah, na Ayman bin Ummu Ayman (Radhwiya Allaahu Anhuum) huku akiinyanyua sauti yake kwa tahliyl na takbiyr”. [Al Albaaniy kasema ni Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bayhaqiy (3/279). Angalia Al-Irwaa (3/123)].

 

Hivyo basi, kwa mujibu wa makubaliano ya maimamu wanne, inajuzu kwa kila mmoja kupiga takbiyr kwa sauti wakati anapotoka kwenda kuswali ‘Iyd. [Majmu’u Al Fataawaa (24/220)].

 

Lakini, baadhi ya Maulamaa wametanabahisha kwamba haijuzu katika upigaji takbiyr, kujumuika watu wote katika sauti moja kama wanavyofanya watu hivi leo. [Kati ya waliolisema hili ni Al’Allaamah Al-Albaaniy –kama ilivyo kwenye Asw-Swahiyhah (1/121)-, Ibn Baaz na Ibn ‘Uthaymiyn Allaah Awarehemu wote].

 

Ninasema: “Kujuzu mjumuiko huu wa watu katika sauti moja kunaweza kutolewa dalili kwa yale aliyoyatolea maelezo Al-Bukhaariy kwa kulitaja bayana jina la mhusika Ibn ‘Umar kwamba: “Ibn ‘Umar alikuwa anapiga takbiyr katika quba lake huko Mina, watu walioko msikitini wakaweza kumsikia na wao wakapiga takbiyr, na walioko masokoni nao wakapiga takbiyr mpaka Mina yote ikatikisika kwa takbiyr. Na akina mama walikuwa wakipiga takbiyr nyuma ya sauti ya Bin ‘Uthmaan na ‘Umar bin ‘Abdul ‘Aziyz masiku ya tashriyq pamoja na wanaume msikitini. Hivyo, mas-ala ni mahala pa ijtihaad na kuangalia, haitakikani kugombana na kushikana mashati kwa ajili yake”.

 

· Tamko La Takbiyr

 

Hakuna Hadiyth yoyote Marfu’u iliyoripotiwa toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusiana na tamko la takbiyr, lakini imethibiti toka kwa Ibn Mas-’oud ya kwamba yeye alikuwa anasema:

(( الله أكبر الله أكبر، لا إله إلا الله، والله أكبر الله أكبر ولله الحمد)).

[Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abiy Shaybah (2/168)].

 

Na Ibn ‘Abbaas alikuwa anasema: “

(( الله أكبر الله أكبر، الله أكبر ولله الحمد، الله أكبر وأجل، الله أكبر على ما هدانا)).

[Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bayhaqiy (3/315)].

 

Na Salmaan (Radhwiya Allaahu Anhu) alikuwa akisema: “ Pigeni takbiyr:

(( الله أكبر, الله أكبر، الله أكبر  كبيرا)).

[Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bayhaqiy (3/316)].

 

Ama waliyoyaongeza watu wa kawaida na wafuasi wao katika zama hizi kwenye takbiyr katika  tunayoyasikia na kuyajua, hayo yametungwa tu na hayana asili yoyote. Al-Haafidh katika Al Fat-h kasema (2/536): “Hakika pamezushwa katika zama hizi ziada katika hilo isiyo na asili yoyote”.

 

Ninasema: “Katika zama zao ilikuweko (ziada), na sisi hivi leo tuna tungo za mahadhi na nyimbo. Allaahu Atusaidie”.

 

· Faida

 

Wakati wa takbiyr katika ‘Iyd el Adh-haa, unaanzia tokea Alfajiri ya siku ya ‘Arafah hadi mwisho wa masiku ya Tashriyq. Hivi ndivyo walivyofanya Jamhuri ya Salaf, Mafuqahaa wa Maswahaba na Maimamu. [Majmu’u Al-Fataawaa (24/220). Angalia Irwaaul Ghaliyl (3/125)].

Wengine wamesema kuwa wakati wa takbiyr huanza baada ya Swalaah lakini hawana dalili ya kuthibitisha. Al-Bukhaariy (2/461) katoa maelezo kwa kulitaja bayana jina la mhusika Ibn ‘Umar akisema: “Ibn ‘Umar alikuwa anapiga takbiyr Mina katika masiku hayo, na baada ya Swalaah, juu ya tandiko lake, katika  nyumba yake ya mapumziko, katika baraza lake na barabara zote zilizokuwepo wakati huo”.

 

5- Wanawake – hata wenye hedhi- watoke na watoto

 

Imepokelewa toka kwa Ummu ‘Atwiyyah akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alituamuru tuwatoe katika Fitwr na Adh-haa wasichana waliovunja ungo karibuni, wenye hedhi, na wanawali. Ama wenye hedhi, hao watajitenga kando na uwanja wa Swalaah lakini watashuhudia kheri na du’aa ya Waislamu. Nikasema: “Ee Rasuli wa Allaah! Mmoja wetu anaweza kuwa hana jilbabu. Akasema: Basi ukhti yake amvalishe jilbabu lake”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (971) na Muslim (890)].

 

Ni lazima wanawake wawajibike na adabu za kutoka ikiwa ni pamoja na kutojitia manukato na kujikwatua kama inavyojulikana. Ama watoto, Ibn ‘Abbaas aliulizwa: “Je, uliswali ‘Iyd pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)?” Akasema: “Na’am, lau si hadhi yangu kwake, nisingeliweza kuiswali kutokana na utoto wangu”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (977)].

 

Lakini, inatakikana wawe pamoja nao watu wa kuwadhibiti wasicheze na kuruka ruka huku na kule na mfano wa hayo sawasawa kama wataswali au la.

 

6- Kupita njia tofauti wakati wa kwenda kuswali

 

Imepokelewa toka kwa Jaabir bin ‘Abdallah akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapita njia tofauti inapokuwa siku ya ‘Iyd”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (986)].

 

Na imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapotoka kwenda ‘Iyd, hurudi kwa njia nyingine tofauti na ile aliyotokea”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Maajah (1301), Ad-daaramiy (1613), Ahmad (8100), Ibn Khuzaymah (1468), Ibn Hibaan (2815), na Al-Bayhaqiy (3/308). Al-Bukhaariy (943) ameitaja kwa kufuatilia Hadiyth ya Jaabir iliyotangulia –nayo ni kwa njia hiyo hiyo!!- Amesema: “Na Hadiyth ya Jaabir ni Swahiyh zaidi”].

 

Hivyo Maulamaa wengi wamependelea kwenda uwanja wa kuswalia kwa njia na kurudi kwa njia nyingine kwa ajili ya kumwigiza Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

7- Imesuniwa kwenda kwa miguu badala ya kutumia kipando ila kwa dharura

 

Imepokelewa toka kwa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu Anhu) akisema: “Katika Sunnah, utoke kwenda kwenye ‘Iyd kwa miguu”. [Al-Albaaniy kasema ni Hadiyth Hasan. Angalia Swahiyh At-Tirmidhiy (1/164) cha Al-Albaaniy].

 

Kuna udhwa’iyf ndani ya Hadiyth hii lakini ipo Hadiyth yake mwenza ya Ibn ‘Umar isemayo: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anatoka kwenda ‘Iyd kwa miguu na anarudi kwa miguu”. [Al-Albaaniy kasema ni Hadiyth Hasan. Angalia Swahiyh Ibn Maajah (1071) cha Al-Albaaniy].

 

Na hii ni endapo uwanja wa kuswalia upo karibu na haiwi uzito kuufikia kwa miguu. Lakini mtu akihitaji kipando, basi hapana ubaya. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

8- Imesuniwa kwenda mapema

 

Na hii ni baada ya watu kuswali Alfajiri ili kukaa sehemu zao, na waendelee kupiga takbiyr mpaka imamu atoke kwa ajili ya Swalaah. [Angalia Sharhu As-Sunnah cha Al-Baghawiy (4/302)].

 

· Hakuna Sunnah Kabla Ya Swalaah Ya ‘Iyd Wala Baada Yake

 

Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas akisema: “Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali siku ya Fitwr rakaa mbili, hakuswali kabla yake wala baada yake”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (989), At-Tirmidhiy (537), An-Nasaaiy (3/193) na Ibn Maajah (1291)].

 

Ibn Al-‘Arabiy kasema: “Lau kuswali Sunnah kwenye uwanja wa kuswalia kungelifanywa, basi kungelinukuliwa. Na aliyejuzisha, anaona kwamba huo ni wakati huria wa Swalaah, na mwenye kuacha, anaona kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakulifanya, na mwenye kumfuata Rasuli, basi huyo ameongoka”.

 

Al-Haafidh kasema: “Ama kuswali tu Sunnah, hakuna katazo lolote lililothibiti kwa dalili maalum isipokuwa kama hilo litakuwa katika wakati wa karaha ambao uko katika masiku yote. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”. [Fat-hul Baariy (2/552)].

 

Ninasema: “Baadhi ya watukufu wanaona kwamba uwanja wa kuswalia ‘Iyd ni Msikiti. Hivyo mtu anapoingia hapo, asikae mpaka aswali rakaa mbili. Dalili ni Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwazuia wenye hedhi kukaa hapo na kuwaamuru kujitenga kando. [Hili kalisema Al-’Allaamah Ibn ‘Uthaymiyn Allaah Amrehemu].

 

Na hapa kuna mtizamo. Kutolea dalili ya kuzuiwa wenye hedhi kunajibiwa kwa kusema kwamba muradi ni wao kujitenga na Swalaah kama ilivyotangulia katika mlango wa twahara. Isitoshe, ardhi yote ni Msikiti na inajuzu kuswali Sunnah ya maamkizi ya Msikiti wakati mtu anapotaka kuswali kwenye sehemu yoyote ya ardhi!! Alaa kulli haal, lau kama Maswahaba wangelikuwa wanaswali maamkizi kwenye uwanja wa kuswalia ‘Iyd, basi lingenukuliwa hilo kama alivyogusia Ibn Al-‘Arabiy. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi. Lakini, lau watu wataswalia Msikitini, basi hakuna shaka juu ya ruksa ya kuswali rakaa hizo za maamkizi”.

 

· Swalaah Ya ‘Iyd Haina Adhana Wala Iqaamah

 

Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas na Jaabir (Radhwiya Allaahu Anhumaa) wakisema: “Haikuwa ikiadhiniwa siku ya Fitwr wala siku ya Adh-haa”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (960) na Muslim (886)].

 

Imepokelewa toka kwa Jaabir bin Samrah (Radhwiya Allaahu Anhu) akisema: “Niliswali pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ‘Iyd mbili, si mara moja, si mara mbili, bila adhana wala iqaamah”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (887), Abu Daawuud (1148) na At-Tirmidhiy (532)].

 

Ibn Al-Qayyim kasema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapofika sehemu ya kuswalia, anaanza kuswali bila adhana wala iqaamah, wala kusemwa: Aswalaatu Jaami’ah. Na Sunnah, kisifanywe chochote katika hayo”. Na juu ya haya, adhana kwa ajili ya ‘Iyd mbili, ni bid-’a. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

· Namna Ya Kuswali Swalaah Ya ‘Iyd

 

Swalaah ya ‘Iyd ni rakaa mbili. Ni kwa Hadiyth ya ‘Umar (Radhwiya Allaahu Anhu) aliyesema: “Swalaah ya safari ni rakaa mbili, na Swalaah ya Adh-haa ni rakaa mbili, na Swalaah ya Fitwri ni rakaa mbili, kiukamilifu bila kupunguza kwa ulimi wa Nabii wenu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).”[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (3/183) na Ahmad (1/37). Ishatajwa nyuma].

 

Inaswaliwa katika picha ifuatayo:

 

1- Ataianza kwa takbiyrah ya kuhirimia kama zilivyo Swalaah nyinginezo.

 

2- Kisha baada ya takbiyrah ya kuhirimia, atapiga takbiyrah nyingine saba kabla hajaanza kusoma. Haikupokelewa toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba alikuwa ananyanyua mikono yake wakati akipiga takbiyrah za Swalaah ya ‘Iyd, lakini Ibn Al-Qayyim kasema: “Ibn ‘Umar - ingawa ametopea katika kuifuata Sunnah - alikuwa akinyanyua mikono kwa kila takbiyrah”. [Zaad El-Ma’ad (1/441)].

 

Ninasema: “Anayeona kwamba Ibn ‘Umar hafanyi hili ila kwa tawqiyf toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), basi anaweza kunyanyua mikono yake, na kama si hivyo, basi bora ya uongofu, ni uongofu wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”.

 

3- Haikupokelewa toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) dhikr maalumu wakati anaponyamaza baina ya takbiyrah hizi, lakini Ibn Mas-’oud kasema: “ Baina ya kila takbiyrah mbili ni Himdi kwa Allaah ‘Azza wa Jalla na Sifa kwa Allaah”. [Isnadi yake ni Hasan. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bayhaqiy (3/291)].

 

4- Kisha ataanza kusoma Al-Faatihahh – baada ya takbiyrah 7- halafu Suwrah. Imesuniwa asome ق والقرآن المجيد katika rakaa ya kwanza, na katika rakaa ya pili asome اقتربت الساعة وانشق القمر kama ilivyothibiti toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (891), An-Nasaaiy katika Al-Kubraa (11550), At-Tirmidhiy (534), na Ibn Maajah (1282)].

 

Na huenda alisoma kwenye rakaa mbili سبح اسم ربك الأعلى na هل أتاك حديث الغاشية

 

[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (878), na nyingine toka kwa An-Nu’umaan bin Bashiyr. Imetajwa nyuma kidogo].

 

5- Na baada ya kisomo, atayafanya mengineyo ya rakaa katika umbile lake la kawaida.

 

6- Atapiga takbiyrah ya kusimama kwenda rakaa ya pili.

 

7- Halafu atapiga baada yake takbiyrah tano kwa namna iliyotangulia katika rakaa ya kwanza.

 

8- Atasoma Al-Faatihahh na Suwrah tuliyoieleza.

 

9- Kisha ataikamilisha Swalaah yake na kutoa tasliym.

 

Hii ni kauli ya Maulamaa wengi katika Maswahaba na kisha waliokuja baada yao kuhusu sifa ya Swalaah ya ‘Iyd mbili. Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu Anha): “Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akipiga takbiyrah katika Fitwr na Adh-haa; takbiyrah saba katika rakaa ya kwanza, na tano katika rakaa ya pili, mbali na takbiyrah mbili za rukuu”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1150), Ibn Maajah (1280) na Ahmad (6/70)].

 

Imepokelewa na ‘Amri bin Shu’ayb toka kwa baba yake toka kwa babu yake akisema: “ Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipiga takbiyrah ya ‘Iyd: saba katika rakaa ya kwanza, kisha akasoma, halafu akasoma, kisha akapiga takbiyrah wakarukuu, halafu akasujudu, kisha akasimama akapiga takbiyrah tano, halafu akasoma, kisha akapiga takbiyrah akarukuu, halafu akasujudu”. [Al-Albaaniy kasema ni Hadiyth Hasan. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1152) na Ibn Maajah (1278). Angalia Al-Irwaa (3/108-112)].

 

· Khutbah Ni Baada Ya Swalaah, Na Mtu Ana Ruksa Ya Kuondoka Baada Ya Swalaah Au Kubaki Akaisikiliza

 

Ni Sunnah kwa imamu akhutubu khutbah moja tu baada ya Swalaah – na si khutbah mbili – [Yaliyosimuliwa ya kuwa zilikuwa ni khutbah mbili, ni Dhwa’iyf mno. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi] …kwa kusimama chini na si juu ya mimbari. Hivi ndivyo alivyofanya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Makhalifa Waongofu baada yake.

 

1- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaah Anhu) akisema: “Nilihudhuria ‘Iyd pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Abu Bakr, ‘Umar na ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu Anhum). Wote hao walikuwa wanaswali kabla ya khutbah”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (962) na Muslim (884)].

 

2- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar: “Kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Abu Bakr na ‘Umar, walikuwa wakiswali ‘Iyd mbili kabla ya khutbah”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (963) na Muslim (888)].

 

3- Imepokelewa toka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriy akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anatoka siku ya ‘Iyd na Adh-haa kwenda uwanja wa kuswalia. La kwanza analoanza nalo ni Swalaah, kisha huondoka pale aliposwalishia, akasimama kuwaelekea watu – na watu wamekaa kwenye safu zao - kisha akawapa mawaidha, akawausia na akawaamuru. Na kama anataka kuamuru kikosi kiende sehemu fulani basi hukiamuru, au kuamuru jambo lolote huamuru, kisha huondoka”. Abu Sa’iyd kasema: “Watu waliendelea na hayo mpaka nilipotoka na Marwaan – naye ni Gavana wa Madiynah - kwenda kwenye Adh-haa au Fitwr. Tulipofika sehemu ya kuswalia, tulishtukizwa kuona mimbari iliyotengenezwa na Kuthayr bin As-Swalt, naye Marwaan ghafla akataka kuipanda kabla ya Swalaah. Nikaikamata nguo yake nikamvuta, naye akanivuta, akapanda na kukhutubu kabla ya Swalaah. Nikamwambia: Mmebadili, Wallaahi. Akasema: Ee Abu Sa’iyd! Unayoyajua hayapo tena. Nikasema: Ninayoyajua Wallaah ni bora zaidi kuliko nisiyoyajua. Akasema: Hakika watu hawakuwa wakikaa kutusikiliza baada ya Swalaah, nami nikaifanya kabla ya Swalaah”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (956) na Muslim (889)].

 

Kusikiliza khutbah hii si lazima, na imesuniwa kwa imamu awakhiyarishe waliohudhuria baina ya kusikiliza au kuondoka ikiwa ni kukiiga kitendo cha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Imepokelewa toka kwa ‘Abdullah bin As Saaib akisema: “ Nilihudhuria ‘Iyd pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alipomaliza Swalaah alisema: ((Hakika sisi tunakhutubu. Basi anayetaka kukaa asikilize khutbah akae, na anayetaka kuondoka, basi aondoke”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1155), An-Nasaaiy (3/185) na Ibn Maajah (1290)].

 

· Faida

 

Khutbah ya ‘Iyd ni kama khutbah nyinginezo. Hufunguliwa kwa Himdi, na Kumsifu Allaah Mtukufu. Hakuna Hadiyth Swahiyh inayoelezea kwamba inafunguliwa kwa takbiyrah.

 

· Je, Watu Hupongezana Kwa ‘Iyd?

 

Sheikh wa Uislamu amesema kwenye Al-Fataawaa (24/253): “Ama kupongezana siku ya ‘Iyd kwa kuambiana wakati wanapokutana baada ya Swalaah ya ‘Iyd: “Taqabbala Allaahu minnaa waminkum” au “Ahaala ‘alayka”, na mfano wa hayo, hili limesimuliwa toka kwa baadhi ya Maswahaba ya kwamba walikuwa wakilifanya. [Al-Haafidh kasema kwenye Al-Fat-h: (2/517): “Tumesimulia katika Al-Mahaamaliyyaat kwa isnadi Hasan toka kwa Jubayr bin Nafiyr akisema: Maswahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa wanapokutana siku ya ‘Iyd huambiana: “Taqabbala Allaahu minnaa wa minka”. Ibn Qudaamah amenukulu kwenye Al-Mughniy (2/259) mfano wake toka kwa Abu Umaamah na wengineo katika Maswahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na amenukulu toka kwa Ahmad akiisifia vizuri Hadiyth ya Abu Umaamah. Angalia Tamaam Al-Minnah uk. 354-356].

 

Maimamu kama Ahmad na wengineo wameliruhusu lakini Ahmad kasema: Mimi sianzi kumpongeza mtu, na ikiwa mtu atanianza, basi ninamjibu. Na hii ni kwa vile kujibu maamkizi ni wajibu, ama kuanza pongezi, hili ni jambo ambalo halikuamuriwa na pia si jambo ambalo limekatazwa. Basi mwenye kulifanya ana kiigizo, na mwenye kuliacha basi ana kiigizo. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.

 

“Na hakuna shaka kwamba pongezi hizi ni katika akhlaqi njema, ni picha nzuri ya kijamii kati ya Waislamu, zina athari nzuri katika kuimarisha mahusiano na mtangamano, na kueneza roho ya mapenzi kati ya Waislamu. Linaloweza kusemwa kwa uchache kuhusiana na hili ni umpongeze anayekupongeza, na unyamaze kama atanyamaza”. [Waqafaatun Lis Swaaimiyna cha Sheikh Salmaan Al-‘Awdah (uk.99) akikizungumzia kitabu cha Ahkaamul ‘Iydayn cha Hishaam Al-Burghush (uk. 57)].

 

 

 

Share