28-Imaam Ibn 'Uthaymiyn: Mwanamke Kapata Ajali Akiwa Na Mimba Changa Akatokwa Damu Nyingi Je Afungulie Swawm

 

 

Fataawaa Mas-ala 60 Kuhusu Hedhi Na Nifaas

 

28-Mwanamke Kapata Ajali Akiwa Na Mimba Changa

Akatokwa Damu Nyingi Je Afungulie Swawm

 

Imaam Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu-Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Mwanamke kapata ajali na alikuwa na mimba katika miezi ya mwanzo na mimba ikatoka baada ya kutoka damu nyingi. Je yapasa afungulie Swawm yake au aendelee na Swawm? Na je akifungua atakuwa ana madhambi yoyote?

 

 

 

JIBU:

 

Tunajibu kwa kusema kuwa mwenye mimba hawi na hedhi kama alivyosema Imaam Ahmad: “Wanawake wenye mimba wanafahamika kwa kukatika kwa hedhi.” Na hedhi kama walivyosema ‘Ulamaa imeumbwa na Allaah (Tabaaraka wa Ta’aalaa) kwa hekima: Chakula cha kichanga katika tumbo la mamake, na mimba ikianza hedhi hukatika; lakini baadhi ya wanawake inaweza kuendelea hedhi yake kama ilivyokuwa kabla ya mimba, kwa hili inahukumiwa kuwa hedhi yake ni sahihi; kwa sababu kwani hedhi iliendelea na haikuathiriwa na mimba, kwa hali hiyo hedhi hii inakuwa ni kizuizi kwa kila chenye kuzuia hedhi isipokuwa mimba inapaswa kwa kila chenye kupaswa na hudondoka kwa kila chenye kudondoshwa. Matokeo yake ni kuwa damu inayotoka kwa mwenye mimba zipo aina mbili:

 

 

Aina ya kwanza: Aina ambayo inahukumiwa kuwa ni hedhi ambayo inaendelea kama vile ilivyokuwa kabla ya mimba. Kwa maana hiyo kuwa mimba haikuuathiri basi itakuwa ni hedhi.

 

 

Aina ya pili: Ni damu inayotoka kwa mwenye mimba na kuchuruzika ima ni kwa sababu ya ajali, au kubeba kitu, au kuangukia kitu na mfano wa hayo. Damu hii sio damu ya hedhi bali ni damu ya ‘Irq   (damu ya Istihaadhwah). Kwa hili halimzuii na Swalaah wala Swawm bali yeye ataingia katika hukmu ya watu waliotoharika.

 

Ama ikitokea kwenye ajali mtoto akatoka au mimba tumboni ikidondoka basi ni kama walivyosema ‘Ulamaa akitoka na kubainika kuwa mwana Aadam keshaumbwa, basi damu yake baada ya kutoka itakuwa ni nifaas na hapo ataacha Swalaah na Swawm na atajitenga mbali na mumewe hadi atoharike. Na kama kichanga kitatoka kabla hajaumbwa basi haizingatiwi kuwa ni damu ya nifaas, bali ni damu chafu ambayo haimkatazi na Swalaah wala Swiyaam wala yasiyokuwa hayo.

 

‘Ulamaa wamesema: “Na muda mchache wa kuumbwa kichanga tumboni ni siku themanini na moja; kwani kichanga katika tumbo la mamake kama alivyosema ‘Abdullah bin Mas’uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alituhadithia naye ni mkweli wa kusadikishwa kasema:

 

(إِنَّ أَحَدَكُمْ يُجْمَعُ خَلْقُهُ فِي بَطْنِ أُمِّهِ أَرْبَعِينَ يَوْمًا نُطْفَةً، ثُمَّ يَكُونُ عَلَقَةً مِثْلَ ذَلِكَ، ثُمَّ يَكُونُ مُضْغَةً مِثْلَ ذَلِكَ، ثُمَّ يُرْسَلُ إلَيْهِ الْمَلَكُ فَيَنْفُخُ فِيهِ الرُّوحَ، وَيُؤْمَرُ بِأَرْبَعِ كَلِمَاتٍ: بِكَتْبِ رِزْقِهِ، وَأَجَلِهِ، وَعَمَلِهِ، وَشَقِيٍّ أَمْ سَعِيدٍ  رواه البخاري ومسلم

Kutoka kwa Abuu 'Abdir-Rahmaan 'Abdillaah bin Mas-‘uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: “Ametusimulia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye ni mkweli mwenye kuaminiwa: “Hakika kila mmoja wenu hukusanywa umbo lake katika tumbo la mama yake siku arubaini akiwa ni mkusanyiko wa mbegu (za uzazi za mama na baba), kisha arubaini zifuatazo huwa ni donge la damu, kisha arubaini zijazo huwa pande la nyama, kisha Allaah Humtuma Malaika kwake na kumpulizia roho (yake).  Na (Malaika huyo) anaamrishwa maneno manne; Kuandika rizki yake, ajali yake (umri atakaoishi duniani), amali zake, mtu muovu au mwema. [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

Hawezi kuumbwa kabla ya hapo na mara nyingi uumbaji hauonekani kabla ya siku tisiini kama walivyosema baadhi ya ‘Ulamaa.

 

Share