50-Fadhila Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Amepewa Na Amejaaliwa Mambo Kadhaa Ambayo Manabii Wengineo Hawakupewa

 

Fadhila Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

 

50-Amepewa Na Amejaaliwa Mambo Kadhaa Ambayo Manabii Wengineo Hawakupewa

Alhidaaya.com

 

 

 

Miongoni mwa mambo ambayo Amejaaliwa na kupewa Nabiy Muhammad  (صلى الله عليه وآله وسلم)  pasi na Manabii wengineo ni:

 

 

1-Kujaaliwa Swafu zake (katika Swalaah za Jamaa) kuwa ni kama Swafu za Malaika.

 

 

2-Amehalalishiwa ghanima (ngawira na mateka ya vita).

 

 

3-Amejaaliwa ardhi kuwa ni twahara. Kwa maana yanapokosekana maji ya kutawadhia Waislamu hufanya Tayammum.

 

 

4-Amejaaliwa ardhi kuwa ni Masjid (Msikiti) kwa maana mtu anaweza kuswali popote katika ardhi madamu ni mahali pasafi; anaweza kuswali njiani, darasani, uwanjani na kadhaalika.

 

 

5-Amepewa Jawaami’ul-Kalim’ (mkusanyiko wa maneno machahe lakini yenye maana pana).

 

 

 

6-Ataruhusiwa Ash-Shafaa’’ah (Uombezi) Siku ya Qiyaamah kuwashufai watu na kuwaingiza Jannah.

 

 

7-Ataruhusiwa kuwaingiza Jannah watu elfu sabiini bila ya kuhesabiwa na bila kuadhibiwa; bonyeza kiungo kifuatacho:

 

24-Fadhila Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Ameruhusiwa Kuingiza Jannah Watu Sabiini Elfu Katika Ummah Wake

 

 

8-Amenusuriwa kwa kutiwa khofu na kizaazaa katika nyoyo za makafiri; kwa maana Allaah (سبحانه وتعالى) Ametia kiwewe na khofu kubwa katika nyoyo za makafiri hadi waogope kupigana vita au wanyon’gonyee na kushindwa kupigana na Waumini.

 

 

9-Ametumwa kwa Ulimwengu wote, kwani Manabii wengineo walitumwa kwa kaumu zao tu.

 

 

Hadiyth zifuatazo zimethibitisha hayo:

 

 

Kunusuriwa Kwa Kiwewe, Kuhalalishiwa Ghanima, Kupewa Ash-Shafaa’ah, Kutumwa Wa Walimwengu Wote:

 

عن جَابِرُ بْنُ عَبْدِ اللَّهِ، أَنَّ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم قَالَ: ((أُعْطِيتُ خَمْسًا لَمْ يُعْطَهُنَّ أَحَدٌ قَبْلِي،  نُصِرْتُ بِالرُّعْبِ مَسِيرَةَ شَهْرٍ، وَجُعِلَتْ لِيَ الأَرْضُ مَسْجِدًا وَطَهُورًا، فَأَيُّمَا رَجُلٍ مِنْ أُمَّتِي أَدْرَكَتْهُ الصَّلاَةُ فَلْيُصَلِّ، وَأُحِلَّتْ لِيَ الْمَغَانِمُ وَلَمْ تَحِلَّ لأَحَدٍ قَبْلِي، وَأُعْطِيتُ الشَّفَاعَةَ، وَكَانَ النَّبِيُّ يُبْعَثُ إِلَى قَوْمِهِ خَاصَّةً، وَبُعِثْتُ إِلَى النَّاسِ عَامَّةً))

Jaabir bin Abdillaah (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Nimepewa mambo matano hakupewa yoyote kabla yangu; Nimenusuriwa na (kutiwa) kiwewe (nyoyoni mwa maadui) kwa mwendo wa mwezi. Na nimefanyiwa ardhi kuwa sehemu ya kufanyia ‘ibaadah na kujitwaharishia, basi mtu mtu yeyote katika ummah wangu akifikiwa na Swalaah, aswali. Na nimehalalishiwa ngawira hazikuwa halali kwa yeyote kabla yangu. Na nimepewa shafaa’ah (maombezi Siku ya Qiyaamah). Na alikuwa Nabiy akitumwa kwa watu wake pekee, lakini mimi nimetumwa kwa watu wote.” [Al-Bukhaariy (5011)]  

 

Kupewa Jawaami’ul-Kalimi, Kunusuriwa Kwa Kiwewe, Kuhalalishiwa Ghanima, Kufanyiwa Ardhi Kuwa Ni Twahara Na Masjid, Kutumwa Kwa Walimwengu Wote, Kufanywa Nabiy Wa Mwisho:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه)  أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ)  قَالَ:  ((فُضِّلْتُ عَلَى الأَنْبِيَاءِ بِسِتٍّ:  أُعْطِيتُ جَوَامِعَ الْكَلِمِ، وَنُصِرْتُ بِالرُّعْبِ، وَأُحِلَّتْ لِيَ الْغَنَائِمُ، وَجُعِلَتْ لِيَ الأَرْضُ طَهُورًا وَمَسْجِدًا، وَأُرْسِلْتُ إِلَى الْخَلْقِ كَافَّةً، وَخُتِمَ بِيَ النَّبِيُّونَ))

Imepokewa kutoka kwa Abu Huraryah (رضي الله عنه)  kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  amesema: ((Nimefadhilishwa juu ya Manabii kwa mambo sita; nimepewa ‘Jawaami’al-Kalimi’  na nimenusuriwa kwa kutiwa kiwewe na khofu (katika nyoyo za maadui) na nimehalalishiwa ghanima  na nimefanyiwa ardhi kuwa kitoharishi na Masjid (mahali pa kuswali), na nimetumwa kwa viumbe wote, na Manabii wamekhitimishwa kwangu))[Muslim]

 

 

Kujaaliwa Swafu Kama Swafu Za Malaikah, Ardhi Kuwa ni Msikiti, Ardhi Kuwa Twahara: 

 

عَنْ حُذَيْفَةَ، قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏ "‏ فُضِّلْنَا عَلَى النَّاسِ بِثَلاَثٍ جُعِلَتْ صُفُوفُنَا كَصُفُوفِ الْمَلاَئِكَةِ وَجُعِلَتْ لَنَا الأَرْضُ كُلُّهَا مَسْجِدًا وَجُعِلَتْ تُرْبَتُهَا لَنَا طَهُورًا إِذَا لَمْ نَجِدِ الْمَاءَ ‏"‏ ‏.‏ وَذَكَرَ خَصْلَةً أُخْرَى ‏.‏

 

Imepokelewa kutoka kwa Hudhayfah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: "Tumefadhilishwa kuliko watu wengine katika mambo matatu: Safu zetu zimefanywa katika safu za Malaika, ardhi yote imefanywa kwetu kuwa Msikiti na mchanga wake umefanywa twahara kwetu ikiwa hakuna maji.” Na akataja fadhila nyengine. [Muslim].

 

Swafu kama za Malaika zimetajwa katika Hadiyth:

 

عَنْ جَابِرِ بْنِ سَمُرَةَ، قَالَ خَرَجَ عَلَيْنَا رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم فَقَالَ ‏"‏ مَا لِي أَرَاكُمْ رَافِعِي أَيْدِيكُمْ كَأَنَّهَا أَذْنَابُ خَيْلٍ شُمْسٍ اسْكُنُوا فِي الصَّلاَةِ ‏"‏ ‏.‏ قَالَ ثُمَّ خَرَجَ عَلَيْنَا فَرَآنَا حَلَقًا فَقَالَ ‏"‏ مَا لِي أَرَاكُمْ عِزِينَ ‏"‏ ‏.‏ قَالَ ثُمَّ خَرَجَ عَلَيْنَا فَقَالَ ‏"‏ أَلاَ تَصُفُّونَ كَمَا تَصُفُّ الْمَلاَئِكَةُ عِنْدَ رَبِّهَا ‏"‏ ‏.‏ فَقُلْنَا يَا رَسُولَ اللَّهِ وَكَيْفَ تَصُفُّ الْمَلاَئِكَةُ عِنْدَ رَبِّهَا قَالَ ‏"‏ يُتِمُّونَ الصُّفُوفَ الأُوَلَ وَيَتَرَاصُّونَ فِي الصَّفِّ ‏"‏ ‏.‏

Imepokelewa toka kwa Jaabir bin Samrah akisema: “Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alitutokea akasema: ((Mbona nawaona mnanyanyua mikono yenu kana kwamba ni mikia ya farasi waliochacharika? Tulieni katika Swalaah)). Akasema: Kisha akatutokea akatuona tumejigawa mafungu mafungu akatuambia: ((Kwa nini msipange safu kama wanavyopanga safu Malaika mbele ya Rabb wao?)) Tukasema: Ee Rasuli wa Allaah! Ni vipi Malaika wanapanga safu mbele ya Rabb wao? Akasema: ((Wanaikamilisha safu ya kwanza na wanazinyoosha safu zao)). [Muslim, Abuu Daawuwd (661), An-Nasaaiy (2/92), Ibn Maajah (992)].

 

 

 

 

Share