03-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Zakaah: Fadhila Na Faida Za Kutoa Zakaah

 

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Zakaah 

 

03-Fadhila Na Faida Za Kutoa Zakaah

 

Alhidaaya.com

 

 

1- Zakaah ni kati ya sifa za watu wema wa Peponi. Allaah Anasema:

 

((إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ • آخِذِينَ مَا آتَاهُمْ رَبُّهُمْ ۚ إِنَّهُمْ كَانُوا قَبْلَ ذَٰلِكَ مُحْسِنِين• كَانُوا قَلِيلًا مِّنَ اللَّيْلِ مَا يَهْجَعُونَ • وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُونَ • وَفِي أَمْوَالِهِمْ حَقٌّ لِّلسَّائِلِ وَالْمَحْرُومِ))

((Hakika wenye taqwa watakuwa katika Jannaat na chemchemu • Wakichukua yale Atakayowapa Rabb wao • Hakika wao walikuwa kabla ya hapo ni wahisani • Walikuwa kidogo tu katika usiku wakilala kwa raha •  Na kabla ya Alfajiri wakiomba maghfirah • Na katika mali zao kuna haki maalumu kwa mwenye kuomba na asiyeomba)). [Adh-Dhaariyaat (51:15-19)]

 

 

 

2- Zakaah ni miongoni mwa sifa za Waumini wenye kustahiki kuzipata Rahmah za Allaah. Allaah Anasema:

 

((وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَيُطِيعُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ أُولَـٰئِكَ سَيَرْحَمُهُمُ اللَّـهُ ۗ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ))

((Na Waumini wanaume na Waumini wanawake ni marafiki wandani wao kwa wao, wanaamrisha mema na wanakataza munkari na wanasimamisha Swalaah na wanatoa Zakaah na wanamtii Allaah na Rasuli Wake. Hao Allaah Atawarehemu. Hakika Allaah ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote)). [At Tawbah (9:71]

 

 

3- Allaah Huikuza na kuitunza kwa mtoaji wake. Anasema:

 

((لَّيْسَ عَلَيْكَ هُدَاهُمْ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَهْدِي مَن يَشَاءُ ۗ وَمَا تُنفِقُوا مِنْ خَيْرٍ فَلِأَنفُسِكُمْ ۚ وَمَا تُنفِقُونَ إِلَّا ابْتِغَاءَ وَجْهِ اللَّـهِ ۚوَمَا تُنفِقُوا مِنْ خَيْرٍ يُوَفَّ إِلَيْكُمْ وَأَنتُمْ لَا تُظْلَمُونَ))

((Si juu yako kuwahidi, lakini Allaah Humhidi Amtakaye. Na chochote cha khayr mtoacho, basi ni kwa ajili ya nafsi zenu. Na hamtoi ila kutaka Wajhi wa Allaah. Na chochote mtoacho katika khayr mtalipwa kamilifu nanyi hamtodhulumiwa)). [Al-Baqarah (2:276)]

 

Na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam amesema:

((من تصدق بعدل تمرة من كسب طيب - ولا يقبل الله إلا الطيب - فإن الله يتقبلها بيمينه ثم يربيها لصاحبها، كما يربي أحدكم فلوه حتى تكون مثل الجبل))

 ((Mwenye kutoa swadaqah ya thamani ya tende moja ya chumo safi la halali – na Allaah Hakubali isipokuwa kilicho safi –Allaah Huipokea kwa Mkono Wake wa kuume, kisha Huilea kwa mtoaji wake kama mmoja wenu anavyomtunza farasi wake mchanga mpaka inakuwa mithili ya mlima)). [Hadiyth Swahiyh: Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1410) na Muslim (1014)]

 

 

4- Allaah Mtukufu Atamwekea kivuli mtoaji kimkinge na joto la Siku ya Qiyaamah. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((سبعة يظلهم الله في ظله يوم لا ظل إلا ظله ... ورجل تصدق بصدقة فأخفاها حتى لا تعلم شماله ما أنفقت يمينه...))

((Watu saba Allaah Atawaweka katika Kivuli Chake siku ambayo hakuna kivuli isipokuwa Kivuli Chake……na mtu aliyetoa swadaqah akaificha kiasi cha kushoto kwake kutojua kilichotolewa na kuume kwake…)). [Hadiyth Swahiyh: Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (660) na Muslim (1031)]

 

 

5- Zakaah huitakasa mali, huistawisha na humfungulia mtoaji wake milango zaidi ya rizki. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((ما نقصت صدقة من مال...))

((Swadaqah haipunguzi chochote katika mali…)). [Hadiyth Swahiyh: Imekharijiwa na Muslim (2588)]

 

 

6- Zakaah ni sababu ya kushuka kheri na barakah, na kuizuia ni sababu ya kuzuilika kheri hizo. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

((وما منع قوم زكاة أموالهم إلا منعوا القطر من السماء، ولولا البهائم لم يمطروا))

((Na watu hawazuilii Zakaah za mali zao, ila hunyimwa mvua toka mbinguni, na lau si wanyama, basi wasingelipata mvua)). [Ibn Maajah (4019) na wengineo. Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Asw-Swahiyhah (105)]

 

 

7- Zakaah hufuta makosa na madhambi. Katika Hadiyth ya Mu’aadh bin Jabal, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((..والصدقة تطفئ الخطيئة كما يطفئ الماء النار))

((…na swadaqah huzima makosa kama maji yanavyozima moto)). [At-Tirmidhiy (609), An-Nasaaiy  katika Al-Kubraa (11394), Ibn Maajah (3973) na Ahmad (5/531). Ina uwezekano wa kufanywa Hadiyth Hasan]

 

 

8- Ni dalili ya ukweli wa iymaan ya mtoaji, kwa kuwa nafsi zinapenda mali, na kipendwacho hakitolewi ila kwa ajili ya kukitaka mfano wake au zaidi yake, bali hili ndilo litafutwalo zaidi. Na kwa ajili hiyo, Zakaah imeitwa swadaqah, kwa kuwa inaonyesha ukweli wa mtoaji wake katika kuzitafuta Radhi za Allaah ‘Azza wa Jalla. [Ash-Sharhu Al-Mumti’u]

 

 

9- Huitakasa tabia ya mtoaji, na hukikunjua kifua chake. Zakaah humwopoa mtoaji wake toka kwenye kundi la mabakhili na kumwingiza katika kundi la wakarimu, na hukikunjua kifua chake. Mtu anapotoa mali yake - kwa roho safi na ukwasi – basi huhisi ukunjufu ndani ya nafsi yake.  [Angalia Zaad Al-Ma’aad cha Ibn Al-Qayyim (2/25)]

 

 

10- Huilinda na kuikinga mali kutokana na tamaa na uchu wa watu masikini na isifikiwe na mikono ya wahalifu.

 

 

11- Ni msaada kwa mafukara na wahitaji. Huwarejesha kuanza tena kazi na shughuli zao kama walikuwa wenye uwezo wakakwama, au huwasaidia kujijengea mazingira bora ya kuishi kama walikuwa hawajiwezi. Na hapa Zakaah inaikinga jamii kutokana na tatizo la umasikini, na huilinda dola isilemewe na majukumu zaidi na utendaji wake kuwa wa kusuasua. [Al–Fiqhu Al- Islaamiy Waadillatuh (2/732]

 

 

12- Ni mchango wa wajibu wa kujitolea wa Muislamu kwa jamii yake, na msaada kwa Dola Ya Kiislamu wakati wa dharura, kutayarisha majeshi, kukabiliana na uadui na kuwawezesha masikini wafikie upeo wa kujitosheleza. [Angalia iliyotangulia]

 

 

13- Ni shukrani kwa neema ya mali. [Adh-Dhakhiyrah cha Al-Quraafiy (3/7]

 

 

 

 

Share