04-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Zakaah: Hukmu Ya Kuzuia Zakaah Na Adhabu Kwa Asiyetoa

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Zakaah 

 

04-Hukmu Ya Kuzuia Zakaah Na Adhabu Kwa Asiyetoa

 

Alhidaaya.com

 

 

 

1- ‘Ulamaa wote wamekubaliana kuwa mwenye kukataa uwajibu wa Zakaah na akakanusha ufaradhi wake, basi huyo ni kafiri kwa Ijma’a. Kwa kuwa mtu huyo anaikadhibisha Qur-aan na Sunnah na anakanusha jambo ambalo linajulikana na wote katika diyn. [Al-Mughniy (2/572) na Al-Majmuw’u (5/334)]

 

 

2- Ama mwenye kukubali kuwa ni waajib lakini akakataa kutoa:

 

(a) Imesimuliwa toka kwa Ahmad kuwa amesema: “Mwenye kuacha kutoa kwa ubakhili wake, basi atakufurishwa kama mwenye kuacha Swalaah kwa uvivu”. Baadhi ya wafuasi wa Hanbali wameitilia nguvu riwaya hii. [Ash-Sharhu Al Kabiyr (3/43), Al-Mubdi’u (1/308) na Ash-Sharhu Al-Mumti’u].

 

Wameitolea dalili kwa Kauli Yake Ta’aalaa:

 

((فَإِن تَابُوا وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ فَإِخْوَانُكُمْ فِي الدِّينِ ۗ وَنُفَصِّلُ الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ))

((Wakitubu, na wakasimamisha Swalaah, na wakatoa Zakaah; basi ni ndugu zenu katika Dini. Na Tunafasili waziwazi Aayaat kwa watu wanaojua)). [At-Tawbah (9:11)]

 

 

Wamesema: “Udugu katika diyn haufutiki isipokuwa kama mtu atatoka kwenye diyn. Na Allaah Ameratibu uthibitisho wa udugu juu ya sifa hizi tatu: Kutubia na kuacha shirk, kusimamisha Swalaah na kutoa Zakaah”.

 

(b) Lakini Jumhuri ya ‘Ulamaa wanasema kuwa asiyetoa Zakaah kutokana na ubakhili wake tu na hapingi au kukataa kuwa ni waajib, basi huyo anafanya dhambi kubwa kati ya madhambi makubwa angamizi na kosa baya kabisa, na anaingia ndani ya duara la makamio makali ya kukabiliwa na adhabu kali Siku ya Qiyaamah. Na madhali anakiri na kukubali uwajibu wa kutoa Zakaah, basi hatoki nje ya diyn kwa kutoitoa.

 

Mwelekeo huu ndio sahihi. Unatiliwa nguvu na Hadiyth ya Abu Hurayrah ya kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomtaja mzuiaji Zakaah ya dhahabu na fedha (silva), na akaelezea adhabu yake, alisema baada ya hapo:

((ثم يرى سبيله إما إلى الجنة وإما إلى النار))

((Kisha ataonyeshwa njia yake, ima kwenda Peponi au ima kwenda Motoni)). [Hadiyth Swahiyh: Imekharijiwa na Muslim (987)]

Na kama ni kafiri, basi hawezi kuwa na njia ya kuelekea Peponi. Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.

 

 

Ama adhabu ya mzuiaji Zakaah hapa duniani, adhabu hiyo inakuwa ya kiqadari na kisharia. Ya kiqadari ni Allaah Ta’aalaa kumwonja kila mwenye kuifanyia ubakhili Haki ya Allaah na haki ya masikini katika mali yake kwa baa la njaa na ukame kama anavyosema Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

((وما منع قوم الزكاة إلا ابتلاهم الله بالسنين))

((Na watu hawazuii Zakaah isipokuwa Allaah Huwaonja kwa ukame)). [Imekharijiwa na At-Twabaraaniy katika Al-Awsatw (4577), Al-Haakim (2/136) na Al-Bayhaqiy (3/346). Al-Albaaniy kasema ni Hadiyth Hasan]

 

Na katika riwaya:

((إلا حبس عنهم القطر))

((Isipokuwa Huwafungia mvua)).

 

Ama adhabu ya kisharia:

 

 

(a) Ikiwa mzuiaji Zakaah yuko ndani ya mamlaka na udhibiti wa mtawala, basi Zakaah itachukuliwa kutoka kwake kwa nguvu kutokana na neno la Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii sallam):

 

((أمرت أن أقاتل الناس حتى يقولوا: لا إله إلا الله محمد رسول الله، فإذا قالوها، عصموا مني دماءهم وأموالهم إلا بحقها وحسابهم على الله))

((Nimeamuriwa kuwapiga watu vita mpaka watamke: Laailaaha illa Allaahu Muhammadun Rasuwlul Laah. Wakilisema hilo, watazikinga damu zao na mali zao kutokana nami ila kwa haki yake na hisabu yao iko juu ya Allaah)).

 

Na kati ya haki zake ni Zakaah. Abu Bakri (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alisema mbele ya kadamnasi ya Maswahaba:

 

((الزَّكَاةَ حَقُّ الْمَالِ، وَاَللَّهِ لَوْ مَنَعُونِي عَنَاقًا كَانُوا يُؤَدُّونَهَا إلَى رَسُولِ اللَّهِ - صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ - لَقَاتَلْتُهُمْ عَلَى مَنْعِهَا))

((Zakaah ni haki ya mali. Wa-Allaahi, lau watazuia kunipa mimi kondoo mchanga waliyekuwa wakimtoa kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam), basi nitapambana nao kivita kwa kuzuia…..)). [Hadiyth Swahiyh: Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1399) na Muslim (20)

 

Na Jumhuri wanasema ikichukuliwa Zakaah kwa nguvu kwa aliyegoma kutoa, basi hakichukuliwi kingine cha ziada katika mali yake. Wanatolea dalili Hadiyth: ((Hakuna katika mali haki nyingine zaidi ya Zakaah)). [Ibn Maajah (1789) kwa Sanad Dhwa’iyf]

 

Ama Ash-Shaafi’iy katika madhehebu yake ya kale, Is-haaq na baadhi ya Maswahiba wa Ahmad, wanasema itachukuliwa Zakaah pamoja na nusu ya mali yake kama adhabu kwake. [Naylul Awtwaar (4/147), na Al-Mawsuw’atu Al-Fiqhiyyah (23/231).

 

Wametoa dalili kwa Hadiyth isemayo:

((ومن منعها فإنا آخذوها وشطر ماله))

((Na mwenye kuizuia, basi sisi ni wenye kuichukua pamoja na nusu ya mali yake)). [Abu Daawuwd (1560), An-Nasaaiy (5/15-17) na Ahmad kwa Sanad Hasan]

 

Waliotangulia wamejibu wakisema kuwa Hadiyth hii ni Mansuwkh, na kuongeza kuwa dai la naskh halikubaliwi kama tarehe na historia havijulikani.

(b) Kama mgomaji kutoa Zakaah yuko nje ya mamlaka na udhibiti wa mtawala, basi ni lazima apambane naye kivita, kwa kuwa Maswahaba walipambana kivita na waliokataa kutoa Zakaah.

 

Ama adhabu ya anayekataa kutoa Zakaah huko aakhirah, kuna Aayaat na Hadiyth kadhaa zilizozungumzia hilo. Kati yake ni:

 

1- Neno Lake Ta’aalaa:

 

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ كَثِيرًا مِّنَ الْأَحْبَارِ وَالرُّهْبَانِ لَيَأْكُلُونَ أَمْوَالَ النَّاسِ بِالْبَاطِلِ وَيَصُدُّونَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ۗ وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلَا يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ •  يَوْمَ يُحْمَىٰ عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَىٰ بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنُوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ ۖ هَـٰذَا مَا كَنَزْتُمْ لِأَنفُسِكُمْ فَذُوقُوا مَا كُنتُمْ تَكْنِزُونَ))

((Enyi walioamini! Hakika wengi katika Wanachuoni Marabai wa dini (zao) na Wamonaki wanakula mali za watu kwa batili, na wanazuia Njia ya Allaah. Na wale wanaorundika dhahabu na fedha [silva] na wala hawazitoi katika Njia ya Allaah, basi wabashirie adhabu iumizayo • Siku zitakapopashwa katika Jahannam, na kwazo vikachomwa moto vipaji vyao, na mbavu zao, na migongo yao (wakiambiwa): “Haya ndiyo mliyoyarundika kwa ajili ya nafsi zenu. Basi onjeni yale mliyokuwa mkiyarundika)). [At-Tawbah (9:34 na 35)]

 

 

2- Toka kwa Abu Hurayrah kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((مَنْ آتَاهُ اللَّهُ مَالاً فَلَمْ يُؤَدِّ زَكَاتَهُ، مُثِّلَ لَهُ يوم القيامة شُجَاعًا أَقْرَعَ، لَهُ زَبِيبَتَانِ يُطَوَّقُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ، ثم يَأْخُذُ بِلِهْزِمَتَيْهِ ـ يَعْنِي شِدْقَيْهِ ـ ثم يَقُولُ أَنَا كنزك أنا مَالُكَ)) ‏.‏ ثُمَّ تَلاَ هَذِهِ الآيَةَ ‏{‏وَلاَ يَحْسِبَنَّ الَّذِينَ يَبْخَلُونَ بِمَا آتَاهُمُ اللَّهُ مِنْ فَضْلِهِ هُوَ خَيْرًا لَّهُم ۖ ... بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ))

((Mtu ambaye Allaah Amempa mali naye asiitolee Zakaah yake, basi ataundiwa kwa mali hiyo Siku ya Qiyaamah mfano wa joka lenye kichwa cheupe (upara), lina mabaka meusi juu ya macho yake, litamviringa Siku ya Qiyaamah.   Kisha litambana kwa taya zake mbili liseme: Mimi ni hazina ya mali yako, mimi mali yako. Kisha akasoma Aayah hii:

 

((وَلَا يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ يَبْخَلُونَ بِمَا آتَاهُمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ هُوَ خَيْرًا لَّهُم ۖ بَلْ هُوَ شَرٌّ لَّهُمْ ۖ سَيُطَوَّقُونَ مَا بَخِلُوا بِهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ وَلِلَّـهِ مِيرَاثُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۗ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ))

((Wala wasidhani kabisa wale wanaofanya ubakhili kwa yale Aliyowapa Allaah katika fadhila Zake kwamba hayo ni khayr kwao, bali ni shari kwao. Watafungwa kongwa yale waliyoyafanyia ubakhili Siku ya Qiyaamah. Na ni Wake Allaah Pekee urithi wa mbingu na ardhi. Na Allaah kwa yale myatendayo ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika)). [Al-Bukhaariy (1403)]

 

 

3- Toka kwa Abu Hurayrah amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakuna yeyote mwenye hazina ya mali ambayo haitolei Zakaah, isipokuwa atapashiwa moto kwenye moto wa Jahannam, kisha ifanywe vipande vipana [vya metali], achomwe navyo mbavu zake na kipaji chake mpaka pale Allaah Atakapohukumu kati ya Waja Wake katika siku ambayo urefu wake ni miaka elfu khamsini. Halafu ataonyeshwa njia yake, ima ya kwenda Peponi, au ya kwenda motoni. Na hakuna yeyote mwenye kumiliki ngamia na asiwatolee Zakaah yake, isipokuwa atatandazwa kifudifudi mbele yao kwenye ardhi pana tambarare, wakiwa wakubwa kama walivyokuwa, watamkanyaga, kila wanapomaliza kumkanyaga wa mwisho wao, wa mwanzo wao watarejeshwa kumkanyaga tena mpaka Allaah Atakapohukumu baina ya Waja Wake katika siku ambayo urefu wake ni miaka elfu khamsini. Halafu ataonyeshwa njia yake, ima ya kwenda Peponi, au ya kwenda motoni. Na hakuna yeyote mwenye kumiliki mbuzi na kondoo na asiwatolee Zakaah yake, isipokuwa atatandazwa kifudifudi mbele yao kwenye ardhi pana tambarare, wakiwa wakubwa kama walivyokuwa, watamkanyaga kwa kwato zao, na watampiga kwa pembe zao, hakuna kati yao mwenye pembe zilizopinda wala asiye na pembe, kila wanapomaliza kumkanyaga wa mwisho wao, wa mwanzo wao watarejeshwa kumkanyaga tena mpaka Allaah Atakapohukumu kati ya Waja Wake katika siku ambayo urefu wake ni miaka elfu khamsini katika mnayohesabu. Halafu ataonyeshwa njia yake, ima ya kwenda Peponi, au ya kwenda motoni…)). [Muslim (987) na Abu Daawuwd (1642)]

 

 

 

 

Share