06-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swiyaam: Jambo Gani Kunakuwa Wajibu Kufunga Ramadhwaan?

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swiyaam

 

06-Ni Kwa Jambo Gani Kunakuwa Wajibu Kufunga Ramadhwaan?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Ni waajib kufunga Ramadhwaan kwa kuthibiti mwezi, nao huthibiti kwa moja ya mawili:

 

1- Kuona Mwezi Mwandamo Wa Ramadhwaan

Allaah Ta’aalaa Anasema:

((فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ))

((Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi, na aufunge)). [Al-Baqarah (2:185)]

 

Na toka kwa Ibn ‘Umar kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

((إذا رأيتموه فصوموا، وإذا رأيتموه فأفطروا، فإن غم عليكم فاقدروا له))

((Mkiuona basi fungeni, na mkiuona basi fungueni. Na kama mawingu yatawakingeni, basi ukadirieni [kutimia siku 30])). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1900) na Muslim (1080)]

 

Na toka kwa Ibn ‘Umar pia kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

((الشهر تسع وعشرون ليلة، فلا تصوموا حتى تروه، فإن غم عليكم فأكملوا العدة ثلاثين))

((Mwezi ni masiku 29, basi msifunge mpaka muuone. Na kama mawingu yatawakingeni, basi kamilisheni hisabu thalathini)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1907)]

 

Kuthibitisha Mwezi Mwandamo (Mbalamwezi) ni kwa kuuona na si kwa hisabu [za kifalaki]

 

Njia ya kuthibitisha Mwezi Mwandamo ni kwa kuuona na si kwa njia nyingine, na haiswihi kuainisha mahala pa kuonekana kwake kwa hesabu (za kifalaki). Sisi tunajua kwa njia ya lazima kupitia Diyn yetu ya Uislamu kuwa kuangalia ndiko kunakotumika kuutafuta Mwezi Mwandamo wa Swawm ya Ramadhwaan na Mwezi wa Hajji (Dhul Hijjah), na pia kwa eda, au kiapo cha kutomwingilia mke, au ahkaam nyinginezo zenye mafungamano na mwezi, na haijuzu kwa habari ya hesabu za mtaalamu wa falaki. Zipo Hadiyth lukuki za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) zinazogusia hili. Kati yake ni neno lake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

((إنا أمة أمية لا نكتب ولا نحسب، الشهر هكذا وهكذا))

((Sisi ni umma usio jua kusoma na kuandika, hatuandiki wala hatuhesabu. Mwezi ni hivi na hivi)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1913), Muslim (1080) na wengineo]

 

Yaani, mara unakuwa siku 29 na mara nyingine unakuwa siku 30. Waislamu wote wamekubaliana juu ya hilo. Hakuna asilani makhitalifiano ya kale wala ya sasa yanayojulikana kuhusiana na jambo hili. Isipokuwa hivi leo, baada ya kupita miaka 300 ya utulivu wa makubaliano hayo,  wamedhihiri wanaojinasibisha na taaluma ya Fiqh ambao wamejuzisha kutumia hesabu za kifalaki. Ni jambo la ajabu ambalo limeshatanguliwa na Ijma’a inayopingana nalo. [Angalia Majmuw’u Al-Fataawaa (25/113, 132, 146), Haashiyatu Ibn ‘Aabidiyna (2/393), Al-Majmuw’u (6/279) na Bidaayatul Mujtahid (1/423)]

 

Kuona Mwezi Mwandamo wa Ramadhwaan kunathibiti kwa ushahidi wa mtu mwadilifu aliyeuona

 

Anapouona mtu mmoja mwadilifu anayeaminiwa Mwezi Mwandamo wa Ramadhwaan, basi taarifa yake itakubaliwa na itafanyiwa kazi kwa mujibu wa ‘Ulamaa wengi kama Abu Haniyfah, Ash-Shaafi’iy, Ahmad na Ahlu Adh-Dhwaahir.  Ibn Al-Mundhir ameukhitari msimamo huu.

 

Ama Maalik, Al-Layth, Al-Awzaa’iy, Ath-Thawriy na Ash-Shaafi’iy katika kauli yake nyingine, wameshurutisha wauone watu wawili waadilifu wakilifananisha hilo na utoaji ushahidi (ambao unahitaji mashahidi wawili).

 

Kauli ya kwanza (ya kutosha kuuona mtu mmoja) ndiyo yenye nguvu zaidi, kwa kuwa kumfananisha mwenye kuuona na msimulizi wa Hadiyth ni sawa zaidi kuliko kumfananisha na mtoa ushahidi. Katika sharia inajuzu kukubali habari ya mtu mmoja, kisha inashadidia zaidi kwenye mali na haki za watu kinyume na inavyoshadidia katika habari za kidini.

 

Kutosheka na taarifa ya mtu mmoja kunatolewa dalili na Hadiyth ya Ibn ‘Umar aliyesema: ((Watu walikusanyika kuangalia Mwezi Mwandamo, nami nikauona. Nikampa taarifa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam), akafunga (siku ya pili) na akaamuru watu waufunge)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2342) Ad-Daaramiy (2/4) na Ibn Hibaan (3447). Angalia Al-Irwaa (908)]

 

Taarifa kuhusu hili inakubaliwa kwa ngazi sawa toka kwa mwanamume au mwanamke katika kauli mbili sahihi za ‘Ulamaa. [Ni madhehebu ya Mahanbali kama ilivyo katika Sharhu Al-Muntahaa (1/440) na Ibn Hazm katika Al-Muhallaa (6/350)]

 

Ama Mwezi Mwandamo Wa Shawwaal 

 

Fuqahaa wameitafikiana kuwa ushahidi wa mtu mmoja hautoshi katika kuthibitisha Mwezi Mwandamo wa Shawwaal, bali unaokubaliwa ni ushahidi wa watu wawili waadilifu. Ash-Shawkaaniy ameliunga hili mkono, na Ibn Rushdiy anaonyesha kama anaegemea huko. Lakini Abu Thawr na Ibn Hazm wamelikhalifu hilo wakisema kuwa ushahidi wa mtu mmoja unatosha, kwa kuwa ushahidi ni ule ule wa sehemu mbili za Mwezi wa Ramadhwaan, mwanzo wake wa kuingia na kutoka kwake.

 

Ninasema: “Hoja ya Jumhuri ni Hadiyth ya ‘Abdul Rahmaan bin Zayd bin Al-Khattwaab ya kuwa Swahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) walimweleza kuwa (Rasuli) kasema:

((صوموا لرؤيته، وأفطروا لرؤيته، وانسكوا لها، فإن غم عليكم فأكملوا ثلاثين، فإن شهد شاهدان فصوموا وأفطروا))

((Fungeni kwa kuuona, na fungueni kwa kuuona, na jikurubisheni kwao [kwa Allaah kwa Swiyaam], na kama mawingu yatawakinga msiuone, basi kamilisheni thelathini. Na kama watashuhudia mashahidi wawili, basi fungeni na fungueni)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na An-Nasaaiy (1/300), na Ahmad (4/321). Angalia Al-Irwaa (909)]

 

Hadiyth hii inadulisha kutokujuzu ushahidi wa mtu mmoja katika kufunga na kufungua. Hivyo funga (kwa ushuhuda wa mtu mmoja) kwa mujibu wa Hadiyth ya Ibn ‘Umar iliyotangulia, inatoka nje (ya duara la kujuzu). Kisha kunabakia kufungua (kumalizika mfungo) ambapo hakuna dalili ya kujuzu kwa ushuhuda wa mtu mmoja. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

Atakayeuona Mwezi Mwandamo peke yake

 

[Al-Badaai’u (2/80), Al-Mudawwanah (1/193), Al-Mubdi’u (3/10), Al-Majmuw’u (6/280), Al-Muhallaa (6/350) na Majmuw’u Al-Fataawaa (25/114)]

 

Atakayeuona Mwezi Mwandamo peke yake na taarifa yake ikakataliwa, basi ‘Ulamaa wana kauli tatu kuhusiana na kufunga kwake na kufungua kwake kwa mujibu wa kuona kwake mwezi.

 

Ya kwanza: Atafunga akiuona Mwezi Mwandamo wa Ramadhwaan, na atafungua kwa siri kwa Mwezi Mwandamo wa Shawwaal ili asikhalifiane na Jamaa. Hii ni kauli ya Ash-Shaafi’iy, riwaya toka kwa Ahmad, na madhehebu ya Ibn Hazm. Ni kwa Neno Lake Ta’aalaa:

((فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ))

((Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi, na aufunge)). [Al-Baqarah (2:185)]

 

Ya pili: Atafunga kwa yeye kuuona, lakini hatofungua isipokuwa pamoja na watu. Ni madhehebu ya Abu Haniyfah, Maalik na mashuhuri toka kwa Ahmad.

 

Ya tatu: Hatofanya lolote kwa kuuona, bali atafunga pamoja na watu na atafungua pamoja nao. Ni riwaya toka kwa Ahmad na limekhitariwa hili na Sheikh wa Uislamu. Ni kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

((صومكم يوم تصومون، وفطركم يوم تفطرون، وأضحاكم يوم تضحون))

((Swawm yenu ni siku mnafunga, na kufungua kwenu ni siku mnafungua, na  Adhwhaa yenu ni siku mnachinja)). [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2324) na wengineo. Angalia Al-Irwaa (905)]

 

Maana ya Hadiyth ni kuwa kufunga na kufungua kunakuwa pamoja na Jamaa.

 

Ninasema: “Lenye nguvu ni kuwa atafunga na kufungua kwa siri kwa mujibu wa yeye alivyouona mwezi kama atapishana na watu. Muhimu Swawm yake isizidi siku 30. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.” 

 

2- Kukamilika Hisabu Ya Sha’abaan Siku Thelathini

 

Kwa kuwa Mwezi Mwandamo haupungui chini ya siku 29 na hauzidi zaidi ya siku 30. Na kama hawakuuona Mwezi Mwandamo usiku wa kuamkia thelathini ya Sha’abaan –anga ikiwa safi bila mawingu au kizuizi chochote cha kuzuia kuona-, basi watakamilisha Sha’abaan siku thelathini na wataamka bila kufunga, ima kwa njia ya waajib au kwa njia ya Sunnah kama tutakavyokuja kufafanua kuhusu kufunga siku ya shaka.

 

Mawingu Au Mfano Wake Yakifunga Watu Wasiweze Kuuona Mwezi Mwandamo Usiku Wa Kuamkia Thalathini Ya Sha’abaan

 

Katika suala hili, ‘Ulamaa wana kauli nyingi. Zilizo mashuhuri zaidi ni nne: [Al-Badaai’i (2/78), Al-Khurshiy (2/238), Al-Majmuw’u (6/269), Al-Inswaaf (2/269), Majmuw’u Al-Fataawaa (25/124) na Zaadul Ma’aadi (2/46-49)]

 

Ya kwanza: Haijuzu kuifunga, si kwa njia ya Waajib wala kwa njia ya Sunnah.

 

Ni madhehebu ya Jumhuri ya ‘Ulamaa na riwaya toka kwa Ahmad. Dalili yao ni:

 

1- Hadiyth ya Ibn ‘Umar kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

((الشهر تسع وعشرون ليلة، فلا تصوموا حتى تروه، فإن غم عليكم فأكملوا العدة ثلاثين))

((Mwezi ni masiku 29, hivyo msifunge mpaka muuone, na kama mawingu yatawatatizeni, basi kamilisheni hisabu thalathini)). [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma kidogo]

 

2- Hadiyth ya Abu Hurayrah ya kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

 

((لا يتقدمن أحدكم رمضان بصوم يوم أو يومين، إلا أن يكون رجل كان يصوم صومه، فليصم ذلك اليوم))

((Asiitangulie kamwe mmoja wenu Ramadhwaan kwa kufunga siku moja au siku mbili, isipokuwa awe mtu alikuwa anafunga Swawm yake, basi na aifunge siku hiyo)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1914) na Muslim (1082)]

 

3- Hadiyth ya ‘Ammaar bin Yaasir amesema:

((من صام اليوم الذي شك فيه فقد عصى ابا القاسم صلى الله عليه وسلم))

((Mwenye kufunga siku ambayo amefanya shaka ndani yake, basi hakika amemwasi Abal Qaasim (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2317), At-Tirmidhiy (681), An-Nasaaiy (4/153) na Ibn Maajah (1645). Angalia Al-Irwaa (961)]

 

4- Ni kuwa kufunga siku hii kwa njia ya hadhari ya kiakiba ni ushadidiaji, uchupaji mipaka na uzushi katika diyn. Kwa kuwa hadhari  inakuwa kwa jambo ambalo asili yake ni waajib. Ama lile ambalo asili yake si waajib, basi hakuna hadhari ya kiakiba katika kuliwajibisha, na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam ashasema:

((هلك المتنطعون))

((Wameangamia washadidiaji wachupao mipaka)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (2670) na Abu Daawuwd (4608) toka Hadiyth ya Ibn Mas’ uwd]

 

Ya pili: Ni lazima kuifunga kwa msingi wa kuwa ni sehemu ya Ramadhwaan

 

Kauli hii ni mashuhuri katika madhehebu ya Hanbali. Pia ni kauli iliyosemwa na kundi katika Swahaba akiwemo ‘Aliy, ‘Aaishah na Ibn ‘Umar pamoja na kundi la Masalaf. Dalili yao ni:

 

1- Kuwa Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) alikuwa unapokuwa usiku wa kuamkia thalathini ya Sha’abaan na mawingu yakazuia kuona au mvua, anaamka akiwa amefunga)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2320) na Ahmad (2/5). Angalia Al-Irwaa (904)]

 

Wamesema: “ Na Ibn ‘Umar ndiye msimulizi wa Hadiyth:

((فإن غم عليكم...))

Hivyo kitendo chake ni tafsiyr ya Hadiyth”.

 

2- Kuwa kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

((فإن غم عليكم فاقدروا له))

.. maana yake ni (ضيقوا له) , yaani ubaneni, na kuibana idadi ni kwa kufanywa Sha’abaan siku ishirini na tisa.

 

3- Kuwa maana ya neno lake:

((فإن غم عليكم فاقدروا له))

((Na kama mawingu yatawakingeni, basi ukadirieni [kutimia siku 30]))..ni kama anga litakuwa safi bila mawingu wala vumbi. Ama katika hali ya kutanda mawingu, hapo hukmu inakuwa nyingine.

 

4- Kuwa Mwezi Mwandamo inawezekana ukawa umetoka lakini umezuiwa na mawingu, hivyo anafunga kiakiba.

 

Ya tatu: Ni kuwa watu wanamfuata Imamu (Kiongozi), akifunga nao watafunga, na asipofunga watakula

 

Ni riwaya toka kwa Ahmad kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

((الفطر يوم يفطر الناس، والأضحى يوم يضحي الناس))

((Kufungua [‘Iyd El Fitwr] ni siku watu wote wanafungua, na [Siku ya ‘Iyd] Adhwhaa ni siku watu wanachinja)). [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh. Imetajwa nyuma kidogo]

 

Ninasema: “Kauli ya Jumhuri ya ‘Ulamaa ya kuzuia kufunga ina nguvu zaidi kutokana na dalili zilizotangulia. Ama kitendo cha Ibn ‘Umar, hakuna ndani yake kinachodulisha kuwa yeye alikuwa akiitakidi uwajibu wake mpaka hili lizingatiwe kuwa ni lenye kufasiri yale aliyoyasimulia. Na linalodulisha hilo ni kuwa lau kama lingekuwa ni waajib, basi angeliwaamuru watu kulitenda japokuwa mkewe na wanawe. Upeo wa tunaloweza kusema kuhusu hili ni kuwa yeye alifunga kwa njia ya Sunnah au kwa njia ya kiakiba. Na hii ndio kauli ya nne, nayo ndiyo ambayo Ibn Taymiyah na Ibn Al-Qayyim wameichagua. Ukiongezea na hayo, imethibiti kupokewa kauli ya Ibn ‘Umar akisema: ”Lau ningelifunga mwaka mzima, basi ningelikula siku ambayo inafanyiwa shaka.” [Isnaad Yake ni Swahiyh. Ameinukulu Ibn Al-Qayyim katika Az Zaad (2/49) toka kwa Hanbal katika Masaail yake kwa Sanad Swahiyh]

 

 

Ninasema: “Kisha kitendo hiki cha Ibn ‘Umar kinakhalifiana na kitendo cha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) ambaye ‘Aaishah amemsimulia aliposema:

 

((كان رسول الله صلى الله عليه وسلم يتحفظ عن شعبان ولا يتحفظ من غيره، ثم يصوم لرؤية رمضان، فإن غم عليه عد ثلاثين يوما ثم صام))

((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa akiuchunga sana [Mwezi wa] Sha’abaan [kwa kuhifadhi na kuyahesabu masiku yake] na hachungi sana miezi mingineyo, kisha anafunga kwa kuonekana Ramadhwaan. Na kama mawingu yatamtinga, huhesabu siku thelathini, kisha hufunga)). [Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2325), Ahmad (6/149) na Al-Bayhaqiy (4/206) na Sanad Yake ni  Muqaarib]

 

Ikibainika katika siku ya shaka kuwa ni Ramadhwaan

Ni kama kuwa yule ambaye ameuona Mwezi Mwandamo hakufika kwa Kadhi (kutoa taarifa) isipokuwa mchana, au watu wakauona mwezi mchana –kabla jua halijapinduka- na mfano wa hivi.

 

1- Awe mtu amefunga siku ya shaka kwa niya ya kuwa ni siku ya Ramadhwaan –kama yalivyo madhehebu ya Hanbal-, huyu swawm yake hiyo itamtosheleza bila makhitilafiano yoyote.

 

2- Awe amefunga siku hii kwa niya ya Sunnah au kwa niya ya kutofungamana na upande wowote. Hapa Jumhuri wanasema kuwa Swawm yake hiyo haimtoshelezi, kwa kuwa ni lazima aainishe niya na aitakidi kuwa anafunga Ramadhwaan. [Al-Khurashiy (2/238), Al-Majmuw’u (6/270), Ar-Rawdhwah (2/353) na Al-Mughniy (3/27)]

 

Abu Haniyfah amesema inamtosheleza –kwa mujibu wa asili yake ya kutoshurutisha niya katika kufunga Ramadhwaan- Na kutosheleza ni riwaya toka kwa Ahmad, nalo ni chaguo la Sheikh wa Uislamu. [Al-Mabsuwtw (3/60) na Al-Mughniy (3/27)]

 

Ninasema: “Kauli ya kwanza ina nguvu zaidi kwa upande wa dalili”.

 

3- Aamke akiwa na niya ya kula, kisha wakati wa mchana –kabla hajala au kunywa chochote- apate habari yakini kuwa Ramadhwaan ishaingia. Hapa Ash-Shaafi’iy amesema: Atakamilisha Swawm yake, lakini lazima ailipe, kwa kuwa hakutia niya usiku. [Fat-hul Maalik Fiy Tartiyb At-Tamhiyd cha Ibn ‘Abdul Barri (5/97).

 

Abu Haniyfah kasema inamtosheleza.

 

4- Aamke akiwa si mwenye kufunga (mlaji), kisha wakati wa mchana apate habari yakini kuwa Ramadhwaan ishaingia baada ya kuwa amekula na kunywa. Huyu ni wajibu kwake ajizuie kula na kunywa mchana wake wote uliosalia bila makhitilafiano yoyote. Na hii ni kutokana na Hadiyth ya Salamah bin Al-Akwa’a aliyesema: ((Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimwamuru mtu mmoja aliyesilimu awatangazie watu aseme: “Aliyekula, basi na afunge siku yake iliyobakia, na ambaye hakuwa amekula, basi na afunge, kwani leo ni Siku ya ‘Aashuwraa)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2007) na Muslim (1129)].

 

Siku hii ilikuwa ni waajib wakati huo. Kisha ni waajib juu yake ailipe siku hii kwa kuwa hakutia niya usiku. Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy na Hanbali. [Al-Ummu (2/95), na Al-Kaafiy cha Ibn Qudaamah (1/350)]

 

Lakini Sheikh wa Uislamu Ibn Taymiyah amesema kuwa haimlazimu kuilipa, kwa kuwa kulipa kunahitajia dalili –na hususan pamoja na kutokuwepo uzembe. [Majmuw’u Al-Fataawaa (25/110), Ash-Sharhu Al-Mumti’u (6/342) na Al-Ikhtiyaaraat (uk. 107)]

 

Ama kutokunuwia, amejibu akisema kuwa niya inaambatana na kulijua jambo, na kwamba Allaah Hamkalifishi mtu kulinuwia jambo ambalo hakulijua, na kulijua jambo hakujatokea isipokuwa wakati wa mchana. Huu ni mwelekeo murua kabisa, lakini la akiba zaidi ni kuilipa. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

Ikiwa Mwezi Mwandamo umeonekana nchi fulani, je ni lazima nchi nyinginezo zifuate?

 

‘Ulamaa wana kauli tatu katika suala hili:

 

Ya kwanza: Watu wa nchi fulani wakiuouna mwezi, ni lazima nchi nyinginezo nazo zifunge bila kuangalia tofauti ya mionekano ya mwezi.

 

Kauli hii ndiyo inayotegemewa kwa Mahanafiy, ni madhehebu ya Maalik na baadhi ya ‘Ulamaa wa Shaafi’iy, na ni mashuhuri kwa Mahanbali. [Haashiyatu Ibn ‘Aabidiyna (2/393), Ash-Sharhul Kabiyr (1/510), Al-Majmuw’u (6/273) na Al-Inswaaf (3/273)]

 

Wamesema:

- Kwa kuwa ni Waislamu wote wanaosemeshwa katika neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

((إذا رأيتموه فصوموا))

((Mnapouona, basi ufungeni)).

 

- Hili li karibu zaidi katika kuungana Waislamu na kuwa wamoja katika neno lao, na pia kutokana na wepesi wa mawasiliano kati ya pande zote za dunia katika wakati wetu wa sasa kwa njia ya satelaiti.

 

Ya pili: Kila nchi – iliyo chini ya mamlaka moja- ina mwezi wake

 

Kauli hii imenukuliwa na Ibn Al-Mundhir toka kwa‘Ikrimah, Al-Qaasim, Saalim na Is-Haaq. [Al-Mughniy (3/289) na Al-Majmuw’u (6/274)]

 

Dalili yao ni:

 

- Hadiyth ya Kurayb – mwachwa huru wa Ibn ‘Abbaas- aliyesema: ((Niliwasili Sham, na Mwezi Mwandamo wa Ramadhwaan ukanidhihirikia nami niko Sham, tukauona Mwezi Mwandamo usiku wa kuamkia Ijumaa. Kisha nikawasili Madiynah mwishoni mwa mwezi, na Ibn ‘Abbaas akaniuliza. Kisha akaukumbuka Mwezi Mwandamo akauliza: Lini muliuona Mwezi Mwandamo? Nikasema: Tuliuona usiku wa kuamkia Ijumaa. Akasema: Wewe uliuona usiku wa kuamkia Ijumaa? Nikasema: Na’am, na watu waliuona, wakafunga, na akafunga Mu’aawiyah. Akasema: Lakini sisi tuliuona usiku wa kuamkia Jumamosi, na bado tunaendelea na Swiyaam mpaka tukamilishe thelathini au tuuone. Nikauliza: Je hutosheki kwa kuuona Mu’aawiyah na kufunga kwake? Akasema: Hapana, hivi ndivyo alivyotuamuru Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1087), Abu Daawuwd (2332), An-Nasaaiy (4/131) na At-Tirmidhiy (693)]

 

- Kauli Yake Ta’aalaa:

((فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ))             

((Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi, na aufunge)). [Al-Baqarah (2:185)]

 

Mafhumu yake ni kuwa ambaye hakuuona hafungi mpaka auone, au akamilishe hesabu ya Sha’abaan.

 

Ya tatu: Ni lazima zifunge nchi ambazo hazitofautiani mwonekano wa mwezi

 

Huu ni mwelekeo sahihi zaidi kwa Mashaafi’iy, ni madhehebu ya baadhi ya ‘Ulamaa wa Kimaalik na Kihanafiy, na ni chaguo la Sheikh wa Uislamu. [Al-Qawaaniynu Al-Fiqhiyyah (103) na vitabu rejea vilivyotangulia]

 

Na hii ndio kauli ya kati na kati (wastani) katika suala hili, kwani miandamo ya mwezi inatofautiana kwa makubaliano ya wataalamu. Na kama miandamo itakuwa sawa kote, basi ni lazima kufunga, na kama inatofautiana, basi si lazima.

 

Ama kauli ya kwanza ya kutozingatia tofauti ya miandamo, kauli hii inakwenda kinyume na lile ambalo limethibiti kiulazima la kutofautiana nyakati. Kwa maana kuwa, ikiwa jua limekuchwa mashariki, basi watu wa magharibi hawawezi kufungua kwa makubaliano ya wote.

 

Ama Hadiyth ya Kurayb, Hadiyth hii inadulisha kuwa wao hawafungui kutokana na kauli ya Kurayb peke yake, -nasi tunaisema- bali mvutano ni kuhusiana na uwajibu wa kuilipa siku ya kwanza, na hili haliko katika Hadiyth. [Al-Mughniy (3/289). Angalia Naylul Awtwaar (4/231)]

 

Kisha hilo halipindukii zaidi ya kuwa ni ufahamu wa Ibn ‘Abbaas wa agizo la Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) la kufunga na kufungua kwa kuuona Mwezi Mwandamo. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

 

 

Share