029-Asbaabun-Nuzuwl: Al-‘Ankabuwt Aayah 10: وَمِنَ النَّاسِ مَن يَقُولُ آمَنَّا بِاللَّـهِ فَإِذَا أُوذِيَ فِي اللَّـهِ

أسْبابُ النُّزُول

Asbaabun-Nuzuwl

(Sababu Za Kuteremshwa Suwrah Na Aayaat Za Qur-aan)

 

Imekusanywa na: Alhidaaya.com

 

029-Asbaabun-Nuzuwl Al-‘Ankabuwt: Aayah 10

 

 

 

Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى)

 

 وَمِنَ النَّاسِ مَن يَقُولُ آمَنَّا بِاللَّـهِ فَإِذَا أُوذِيَ فِي اللَّـهِ جَعَلَ فِتْنَةَ النَّاسِ كَعَذَابِ اللَّـهِ وَلَئِن جَاءَ نَصْرٌ مِّن رَّبِّكَ لَيَقُولُنَّ إِنَّا كُنَّا مَعَكُمْ ۚ أَوَلَيْسَ اللَّـهُ بِأَعْلَمَ بِمَا فِي صُدُورِ الْعَالَمِينَ ﴿١٠﴾ وَلَيَعْلَمَنَّ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَلَيَعْلَمَنَّ الْمُنَافِقِينَ ﴿١١﴾

 Na miongoni mwa watu wako wasemao: Tumemwamini Allaah; lakini wanapoudhiwa kwa ajili ya Allaah, hufanya fitnah za watu kama kwamba ni adhabu ya Allaah. Na inapowajia nusura kutoka kwa Rabb wako husema: Hakika sisi tulikuwa pamoja nanyi. Je, kwani Allaah Hayajui yale yaliyomo katika vifua vya walimwengu? Na bila shaka Allaah Atatambulisha wale walioamini, na bila shaka Atawatambulisha wanafiki. [Al-‘Anakbuwt: (29 :10, 11)]

 

 

Sababun-Nuzuwl: 

 

قَالَ مُجَاهِدٌ: نَزَلَتْ فِي أُنَاسٍ كَانُوا يُؤْمِنُونَ بِأَلْسِنَتِهِمْ، فَإِذَا أَصَابَهُمْ بَلَاءٌ من اللَّه أو مصيبة فِي أَنْفُسِهِمُ، افْتَتَنُوا.

Mujaahid amesema: “Iliteremshwa kuwazungumzia watu ambao walikuwa wanaamini kwa ndimi zao tu (na si kwa nyoyo zao), na wanapopatwa na mtihani toka kwa Allaah, au msiba katika nafsi zao, basi hufitinika (hutetereka wakaacha iymaan yao)”.

 وَقَالَ الضَّحَّاكُ: نَزَلَتْ فِي أُنَاسٍ مِنَ الْمُنَافِقِينَ بِمَكَّةَ كَانُوا يُؤْمِنُونَ، فَإِذَا أُوذُوا رَجَعُوا إِلَى الشِّرْكِ.

 

Adh-Dhwahhaak amesema: “Iliteremka kuwazungumzia watu katika wanafiki wa Makkah ambao walikuwa wameamini. Na wanaposumbuliwa na kutaabishwa, basi wanarejea katika shirki”.

 وَقَالَ عِكْرِمَةُ عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ: نَزَلَتْ فِي الْمُؤْمِنِينَ الَّذِينَ أَخْرَجَهُمُ الْمُشْرِكُونَ إِلَى بَدْرٍ فَارْتَدُّوا، وَهُمُ الَّذِينَ نَزَلَتْ فِيهِمْ:  ((إِنَّ الَّذِينَ تَوَفَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ ظَالِمِي أَنْفُسِهِمْ )) الْآيَةَ.

‘Ikrimah amesema akipokea toka kwa Ibn ‘Abbaas: “Iliteremka kuwazungumzia Waumini ambao washirikina waliwatoa kwa nguvu kwenda (Vita vya) Badr, wakaritadi. Na hao ndio walioteremshiwa Aayah:

 

 

إِنَّ الَّذِينَ تَوَفَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ ظَالِمِي أَنفُسِهِمْ قَالُوا فِيمَ كُنتُمْ ۖ قَالُوا كُنَّا مُسْتَضْعَفِينَ فِي الْأَرْضِ ۚ قَالُوا أَلَمْ تَكُنْ أَرْضُ اللَّـهِ وَاسِعَةً فَتُهَاجِرُوا فِيهَا ۚ فَأُولَـٰئِكَ مَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا ﴿٩٧﴾

Hakika wale ambao Malaika wamewafisha, hali wamejidhulumu nafsi zao; (Malaika) watawaambia: Mlikuwa katika hali gani? Watasema: Tulikuwa tukikandamizwa katika ardhi.  (Malaika) Watasema: Je, kwani ardhi ya Allaah haikuwa ya wasaa mkahajiri? Basi hao makazi yao yatakuwa ni Jahannam, na uovu ulioje mahali pa kuishia. [An-Nisaa (4:97)]

 

 

Na [katika Tafsiyr Zaadul-Masiyr Fiy ‘Ilmi At-Tafsiyr], Ibn Al-Jawziy ameandika:

 

 

“Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَقُولُ آمَنَّا بِاللَّـهِ فَإِذَا أُوذِيَ فِي اللَّـهِ جَعَلَ فِتْنَةَ النَّاسِ كَعَذَابِ اللَّـهِ وَلَئِن جَاءَ نَصْرٌ مِّن رَّبِّكَ لَيَقُولُنَّ إِنَّا كُنَّا مَعَكُمْ ۚ أَوَلَيْسَ اللَّـهُ بِأَعْلَمَ بِمَا فِي صُدُورِ الْعَالَمِينَ

Na miongoni mwa watu wako wasemao: Tumemwamini Allaah; lakini wanapoudhiwa kwa ajili ya Allaah, hufanya fitnah za watu kama kwamba ni adhabu ya Allaah. Na inapowajia nusura kutoka kwa Rabb wako husema: Hakika sisi tulikuwa pamoja nanyi. Je, kwani Allaah Hayajui yale yaliyomo katika vifua vya walimwengu?. [Al-‘Ankabuwt (29 :10)]

 

 

[Mufassiruwna] Wamekhitalifiana katika kauli nne kuhusu nani Aayah hii iliteremka kumzungumzia:

 

 

Ya kwanza:

 

Iliteremka kuwazungumzia Waumini ambao washirikina waliwatoa kwenda Badr, wakaritadi. Imesimuliwa na ‘Ikrimah toka kwa Ibn ‘Abbaas.

 

 

Ya pili:

 

Iliteremka kuwazungumzia watu waliokuwa wakiamini kwa ndimi zao, na wanapopatwa na mtihani toka kwa Allaah au msiba kwenye nafsi zao na mali zao, basi hufitinika. Ni kauli ya Mujaahid.

 

 

Ya tatu:

 

Iliteremka kuwazungumzia watu katika wanafiki mjini Makkah. Walikuwa wameamini, lakini wanaposumbuliwa na kutaabishwa, na ukawasibu msukosuko toka kwa washirikina, basi hurejea katika shirki. Ni kauli ya Adh-Dhwahhaak.

 

 

Ya nne:

 

Iliteremka kumzungumzia ‘Ayyaash bin Abiy Rabiy‘ah. Alikuwa amesilimu, akajihofia nafsi yake kutokana na jamaa zake na watu wake. Akatoroka Makkah kwenda Madiynah, na hiyo ilikuwa kabla Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) hajakwenda Madiynah. Mama yake akapata mfadhaiko mkubwa, akawaambia nduguze (‘Ayyaash kwa mama) Abu Jahl bin Hishaam na Al-Haarith bin Hishaam: Wa-Allaahi, siingii nyumbani, wala sili chakula, wala sinywi chochote mpaka mje naye kwangu. Wakatoka kumtafuta mpaka wakampata. Wakashikilia kumshawishi na kumrai mpaka akakubali kuwafuata kurudi Makkah hadi kwa mama yake. Alipofika, mama yake alimfunga na kumwambia: Wa-Allaahi, sikufungui kamba nilizokufunga mpaka umkatae Muhammad. Akaanza kumchapa mijeledi na kumtesa mpaka akamkufuru Muhammad baada ya kushindwa kuhimili kipigo na mateso. Ndipo Aayah hii ikateremka kumzungumzia ‘Ayyaash. Kisha baadaye alihajiri na akaujenga vyema Uislamu wake.

 

Hii ni kauli ya Ibn As-Saaib na Muqaatil. Na katika riwaayah toka kwa Muqaatil ni kuwa nduguze wawili walimpiga mijeledi mia mbili wakati walipokuwa njiani kurejea naye Makkah, akaiacha Dini ya Muhammad, na hapo ikateremka Aayah hii.”

 

Katika Tafsiyr yake, At-Twabariy ameandika:

 

Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَقُولُ آمَنَّا بِاللَّـهِ فَإِذَا أُوذِيَ فِي اللَّـهِ جَعَلَ فِتْنَةَ النَّاسِ كَعَذَابِ اللَّـهِ وَلَئِن جَاءَ نَصْرٌ مِّن رَّبِّكَ لَيَقُولُنَّ إِنَّا كُنَّا مَعَكُمْ ۚ أَوَلَيْسَ اللَّـهُ بِأَعْلَمَ بِمَا فِي صُدُورِ الْعَالَمِينَ ﴿١٠﴾ وَلَيَعْلَمَنَّ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَلَيَعْلَمَنَّ الْمُنَافِقِينَ ﴿١١﴾

Na miongoni mwa watu wako wasemao: Tumemwamini Allaah; lakini wanapoudhiwa kwa ajili ya Allaah, hufanya fitnah za watu kama kwamba ni adhabu ya Allaah. Na inapowajia nusura kutoka kwa Rabb wako husema: Hakika sisi tulikuwa pamoja nanyi. Je, kwani Allaah Hayajui yale yaliyomo katika vifua vya walimwengu? Na bila shaka Allaah Atatambulisha wale walioamini, na bila shaka Atawatambulisha wanafiki. [Al-‘Ankabuwt (29 :10)]

 

 

Iliteremka kuwazungumzia wanafiki ambao walikuwa wanadai kuwa wao wamemwamini Allaah.

 

"فَإِذَا أُوذِيَ فِي اللَّـهِ جَعَلَ فِتْنَةَ النَّاسِ"

yaani maudhi yao.

 

"كَعَذَابِ اللَّـهِ"

 

huko Aakhirah, akaritadi na kuiacha iymaan yake.

 

Mujaahid amesema: “Iliteremka kuwazungumzia watu ambao walikuwa wanaamini kwa ndimi zao, na wanapopata mtihani kutoka kwa Allaah, au msiba katika nafsi zao, basi hutetereka”.

 

Adh-Dhwahhaak amesema: “Iliteremka kuwazungumzia watu katika wanafiki wa Makkah ambao walikuwa wameamini, lakini wanapoudhiwa wanarejea katika shirki”.

 

‘Ikrimah amesema: “Watu walikuwa wamesilimu, washirikina wakawalazimisha watoke pamoja nao kwenda Badr (ili kuongeza wingi wa idadi ya wapiganaji na hivyo kuzusha hofu kwa Maswahaba), na baadhi yao (Waislamu waliolazimishwa) wakauawa. Na hapo Allaah (سبحانه وتعالى)   Akateremsha:

 

إِنَّ الَّذِينَ تَوَفَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ ظَالِمِي أَنفُسِهِمْ قَالُوا فِيمَ كُنتُمْ ۖ قَالُوا كُنَّا مُسْتَضْعَفِينَ فِي الْأَرْضِ ۚ قَالُوا أَلَمْ تَكُنْ أَرْضُ اللَّـهِ وَاسِعَةً فَتُهَاجِرُوا فِيهَا ۚ فَأُولَـٰئِكَ مَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا ﴿٩٧﴾

Hakika wale ambao Malaika wamewafisha, hali wamejidhulumu nafsi zao; (Malaika) watawaambia: Mlikuwa katika hali gani? Watasema: Tulikuwa tukikandamizwa katika ardhi.  (Malaika) Watasema: Je, kwani ardhi ya Allaah haikuwa ya wasaa mkahajiri? Basi hao makazi yao yatakuwa ni Jahannam, na uovu ulioje mahali pa kuishia. [An-Nisaa (4:97)]

 

Waislamu walioko Madiynah wakawaandikia Waislamu waliobakia Makkah Aayah hii (kuwajulisha kuwa hawana tena udhuru wa kubakia Makkah), nao wakatoka. Lakini washirikina waliwaandama wakawataabisha, na baadhi ya Waislamu walifitinika. Aayah hii ikateremka kuwazungumzia.”

 

Imesemwa: “Iliteremka kumzungumzia ‘Ayyaash bin Abiy Rabiy’ah. Alisilimu na akahajiri, kisha akaudhiwa, akapigwa na akaritadi. Abu Jahl na Al-Harth ambao walikuwa ni ndugu zake kwa mama, ndio waliomtesa. Ibn ‘Abbaas amesema: Kisha aliishi baada ya hapo kwa miaka kadhaa, na akawa Muislamu safi.”

 

 

 

Share